Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

Katibu mkuu Umoja wa Mataifa ampongeza Rais Jakaya Mrisho Kikwete


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesifu jitihada za Rais Jakaya Mrisho Kikwete na

mchango wake mkubwa katika kupigania Afya ya Mama na Mtoto.

Bw. Ban Ki Moon ametoa pongezi hizo tarehe 30 Mei,2014 wakati alipokuwa

akizungumzia  juhudi za kumuokoa Mama na Mtoto baada ya Mwaka 2015, mwishoni

mwa mkutano wa siku 3 kuhusu Afya ya Mama na Mtoto kama ilivoainishwa katika

Malengo ya Milenia .

Rais Kikwete na Waziri Mkuu wa Canada Bw. Stephen Harper, kwa  miaka minne  

wamekuwa Wenyeviti Wenza wa Kamisheni ya Habari na Uwajibikaji katika masuala

ya Afya ya Mama na Mtoto , ambayo imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha vifo vya

Watoto wachanga na Mama wajawazito vinapunguzwa  kwa nusu ifikapo Mwaka 2015.

"Napenda kumpongeza Rais Kikwete kwa mchango wake mkubwa katika jitihada hizi za

kupunguza vifo vya Watoto na akina Mama. Rais Kikwete na Waziri Harper wamedhihirisha

uongozi katika kukuza Afya ya Mama na Mtoto, nawapongeza sana " Bw. Ban Ki Moon

amesisitiza na kuwaomba viongozi wengine kuiga mfano wa Canada wa kuchangia

zaidi katika jitihada hizi.

Pamoja na mafanikio hayo, Rais Kikwete amesema bado jitihada zinahitajika katika

kuhakikisha mafanikio haya yanaimarishwa zaidi na kwamba hayapotei .

“Bado tunahitaji wataalamu wa Afya wenye ujuzi , vifaa na teknolojia ya kisasa" Amesema

na kuongeza kuwa bado zinahitajika juhudi za pamoja katika kusimamia mafanikio

yaliyokwisha kupatikana.

Bw.Ban Ki Moon pia amesema Afya ya Mama na Mtoto ni ajenda muhimu kupigania

hata baada ya Mwaka 2015 kwani ni muhimu kwa maendeleo.

Rais Kikwete pia amehudhuria chakuala cha jioni kilichoandaliwa na wafanya biashara

wa Canada na Tanzania ambapo ameelezea umuhimu wa biashara na uwekezaji nchini

kwa madhumuni ya kukuza uchumi wa Tanzania.

Rais amesema Tanzania inahitaji vitega uchumi zaidi kutoka Canada na hivyo

kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Canada kuja kuwekeza Tanzania.

Rais Kikwete anatarajia kuondoka Toronto leo tarehe 31 Mei, kurejea Dar es Salaam,

kupitia Marekani.

Imetolewa na;

Premi Kibanga,

Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,

Toronto – Canada.

31 Mei, 2014