Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

Hotuba ya Rais Kikwete kwa wananchi wa Wilaya ya Muheza


Rais Jakaya Mrisho Kikwete amewaeleza wananchi wa Muheza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Jitegemee jana tarehe 26 Machi, 2014 kuwa, Serikali imekubali kimsingi kuyachukua mashamba manane  (8) kati ya 11 ya Mkonge Wilayani Muheza ambayo yametelekezwa, ili kuyagawa upya kwa Wananchi ambao wana tatizo la Ardhi Wilayani humo.

"Tumeshakubali kimsingi kuyachukua mashamba hayo kulingana na taratibu za Serikali na kisha kuyagawa upya kwa Wananchi ili kupunguza tatizo la Ardhi hapa Muheza" Rais amewaambia wananchi waliofika kwenye mkutano huo wa hadhara kumsikiliza.

Mashamba ya Mkonge Mkoani Tanga yamekuwa na tatizo la kutelekezwa ama kutoendelezwa kabisa hivyo kusababisha Wananchi kuyavamia na kuzua migogoro mingi Mkoani Tanga.

Wilaya ya Muheza ina jumla ya Mashamba kumi na moja (11) na kati ya hayo Serikali imefanya taratibu za kuyarudisha mikononi mwake kwa ajili ya kuyagawa kwa Wananchi.

Suala la upungufu wa Ardhi na maombi kwa Serikali kuyagawa Mashamba hayo kwa Wananchi ili waweze kuyatumia kwa shughuli za kilimo, imekuwa moja ya kilio kikubwa katika Wilaya zote ambazo Rais amefanya ziara Mkoani Tanga ambazo ni Handeni, Korogwe, Muheza na Tanga.

Mashamba mengine yapo katika Wilaya za Handeni, ambako Mashamba yapo mawili (2),  Korogwe mashamba manne (4), na Tanga mashamba manne (4).

Wilaya zingine ambazo nazo zina tatizo hili na ambazo Rais atatembelea baadaye ni Mkinga ambako kuna mashamba matatu (3), Pangani shamba moja (1) na Lushoto shamba moja (1).

Katika ziara yake Wilayani Muheza Mhe. Rais amefungua soko kubwa la kuuzia vyakula mbalimbali na matunda la Michungwani, kukagua ujenzi wa Maabara na ukarabati wa madarasa na nyumba za Walimu katika shule ya Sekondari Pongwe.

Rais pia amezindua mradi wa Maji katika Kijiji cha Kwemhosi mradi ambao unalenga kupunguza uhaba wa maji katika vijiji 10 kupitia mpango wa Water Sector Development Program (WSDP)

Mradi huu umekamilika katika vijiji 8 na tayari vijiji 6 vimeanza kufaidika ambapo hadi kukamilika utakuwa na uwezo wa kutoa lita 90,000 za Maji kwa siku na kuhudumia jumla ya wakazi 1,604.

Katika mkutano wa hadhara pia Rais amekabidhi Mizinga 133 ya kufugia Nyuki na Mtambo wa kuchimbia visima vya maji.

Rais anaendelea na ziara yake ambapo tarehe 27Machi,2014 atakuwa Wilayani Tanga.

Imetolewa na;

 Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais  Msaidizi,
Tanga.


26 Machi,2014