Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

EACLC KUIPAISHA TANZANIA KIBIASHARA


RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kukamilika kwa Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) kutapunguza muda wa kushughulikia mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kutoka wastani wa siku saba hadi chini ya siku tatu, hatua itakayoongeza ushindani wa bandari hiyo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa kituo hicho kilichopo Ubungo, Dar es Salaam, Rais Dkt. Samia amesema mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara kwa Afrika Mashariki na Kati, sambamba na miradi mingine ya kimkakati ya Bandari Kavu ya Kwala na kuanza kwa safari za mizigo za treni ya umeme ya SGR aliyoizindua jana mkoani Pwani.

Rais Dkt. Samia amsesema kituo hicho kinalenga kutatua changamoto za biashara na usafirishaji kwa muda mrefu zikiwemo ucheleweshaji wa mizigo, gharama kubwa za uendeshaji na ukosefu wa miundombinu rafiki kwa wafanyabiashara.

“Kupitia kituo hiki, wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi wataweza kufanikisha shughuli zao kwa urahisi zaidi, ufanisi mkubwa na kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kidigitali,” alisema Rais Dkt. Samia.

Kituo hicho chenye maghala ya kisasa, huduma za usafirishaji na ofisi za biashara katika eneo moja kinatazamiwa kupunguza gharama za usafirishaji na kufanya bidhaa za Tanzania kuwa na ushindani zaidi katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Halikadhalika, Rais Dkt. Samia amesema mradi huo utachochea mauzo ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi na kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni, huku ukiongeza mapato ya Serikali Kuu na makusanyo ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.

“Tunatarajia mradi huu utakuza Biashara ya Kikanda; utaweza kuhudumia wafanyabiashara kutoka nchi zote wanachama wa EAC, COMESA na SADC, na kusaidia kufanikisha ndoto ya soko la pamoja la Afrika – AfCFTA,” alisema.

Ameongeza kuwa matumizi ya mifumo ya kisasa ya kidijitali katika usimamizi wa maghala, ufuatiliaji wa mizigo na usafirishaji yataleta ufanisi wa hali ya juu, sambamba na jitihada za kujenga uchumi unaotegemea maarifa na teknolojia.