Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

BIOSUSTAIN YAFUNGUA MILANGO YA AJIRA NA UWEKEZAJI MPYA MEATU


RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi kiwanda cha kuchakata pamba cha Biosustain Tanzania Ltd kilichopo Wilaya ya Meatu, na kusisitiza dhamira ya Serikali kuimarisha mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na wananchi wa Meatu tarehe 17 Juni, 2025, Rais Dkt. Samia amesema uzinduzi wa kiwanda hicho ni ishara ya mwelekeo chanya wa Tanzania kuelekea uchumi wa viwanda unaotegemea malighafi zinazozalishwa na wananchi, hususan katika sekta ya kilimo.

“Tunaweka msingi imara wa Tanzania ya viwanda,” amesema Rais Dkt. Samia, akiongeza kuwa Serikali inaendelea na jitihada za kuvutia viwanda katika wilaya ya Meatu na mkoa wa Simiyu kwa ujumla ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi ya mkoa huo.

Niwahakikishie wawekezaji wa viwanda, kikiwemo kiwanda cha pamba cha Biosustain, kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira bora kwa ajili ya kukuza viwanda vya ndani,” alisema Rais Dkt. Samia.

Kiwanda cha Biosustain kinatarajiwa kupanua shughuli zake kwa kuanzisha kiwanda kingine cha uzalishaji wa mafuta ya mbegu za pamba na alizeti chenye thamani ya Shilingi Bilioni 12, hatua ambayo itazidisha ajira na kukuza soko la mazao ya wakulima wa mkoa wa Simiyu.

Katika kuhakikisha uwekezaji unaendelea kuimarika, Rais Dkt. Samia amesema Serikali imekuwa ikitenga maeneo maalum kwa ajili ya viwanda na biashara, na kusisitiza kuwa Mkoa wa Simiyu uko mstari wa mbele katika utekelezaji wa mkakati huo. Pia amepongeza Halmashauri ya Meatu kwa kuwa na mpango wa viwanda unaolenga kutoa ajira kwa vijana na wanawake.

Aidha, Rais Samia ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuzalisha pamba kwa wingi, kwa kuwa soko lipo na Serikali itaendelea kulinda bei kwa kuhakikisha kunakuwa na uwazi na ushindani wa haki katika ununuzi wa pamba kutoka kwa wakulima.

Nitoe rai kwa wananchi kuendelea kuzalisha pamba na mazao mengine ili kuendelea kuvilisha viwanda vilivyopo na kuzidi kuvutia viwanda vingine.

Kiwanda hicho kinatajwa kuwa sehemu muhimu ya mnyororo wa thamani wa pamba mkoani Simiyu, ambacho tayari kimezalisha ajira 375 za kudumu na ajira 830 za msimu.