Habari
ZIARA YA MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN MIKOA YA LINDI NA MTWARA
ZIARA YA MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN MKOANI MTWARA
Rais Samia alizindua Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini iliyojengwa eneo la Mitengo Mikindani itatoa huduma mbali mbali za kibingwa imejengwa kwa gharama ya shs bilioni 15.8 itahudumia kanda ya kusini na nchi za Jirani zinazopakana.
Hospitali hiyo ina vifaa vya kisasa, ikiwemo mashine za MRI na CT – SCANA. Huduma za kuchuja damu, yaani Dialysis, zitaanzishwa hivi karibuni.
Rais Samia amekabidhi magari matatu ya kubebea wagonjwa (ambulance) ambayo ni mini ICU.
Rais Samia pia alizindua Chujio la maji lililopo Mangamba. Mradi umegharimu shs bilioni 3.4 na utanufaisha wananchi 141,000 na ina uwezo wa kutibu maji kiasi cha cubic mita 12.5.
Rais Samia amekagua ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege kilichogharimu shilingi bilioni 281.55. Kiwanja hiki kimekamilika kwa asilimia 98, kina uwezo wa kuhudumia ndege kubwa za ndani na nje ya nchi zenye ukubwa wa Boeing 787-8 (Dreamliner).
Rais Samia pia amezindua barabara ya Mnivata - Mtwara (km 50) katika eneo la Naliendele. Kipande hiki cha barabara ni sehemu ya barabra ya Mtwara – Newala – Masasi yenye kilomita 210 ambayo imejengwa kimkakati ili kuyaunganisha maeneo yanayozalisha korosho kwa wingi katika wilaya za Tandahimba na Newala. Barabara hii itarahisisha usafirishaji wa korosho kutoka kwa wakulima hadi kwenye masoko ya ndani na nje kupitia Bandari na Kiwanja cha Ndege cha Mtwara.
Katika siku hiyo ya kwanza ya ziara, Rais Samia amekagua shughuli za uimarishwaji wa bandari ambapo eneo la mita za mraba 75,000 limeshatengwa kwa ajili ya kupitisha korosho na nafaka zingine.uimarishwaji wa Bandari ya Mtwara itasaidia kupunguza msongamano katika bandari ya Dar es Salaam lakini itachangia kukua kwa biashara katika ukanda wa kusini.
Akihutubia katika mkutano wa hadhara, Rais Samia alikemea tabia ya wafanya biashara kusafirisha korosho kwa njia ya barabara na kuzichakachua ili wapate faida kubwa hivyo aliwataka wafanyabiashara watakaosafirisha kwa njia ya malori kupata kibali maalum kutoka kwa Mkuu wa Mkoa.
Siku ya pili ya tarehe 16 Septemba, 2023 Rais Samia aliendelea na ziara yake katika mkoa wa Mtwara ambapo akielekea Tandahimba, Rais Samia alisimama njiani na kuzungumza na wananchi wa Kijiji cha Nanguruwe, Nanyamba ambapo aliwataka wananchi kuweka jitihada katika kilimo cha ufuta na mbaazi kwa kuwa serikali imeshatafuta soko la zao la mbaazi kwa kuweka mikataba nan chi wanunuzi.
Alieleza kuwa serikali imeamua kujenga shule kubwa ya wasichana katika kila mkoa. Rais Samia aliwataka wazazi wa mkoa wa Mtwara kuwaacha wasichana kupata fursa ya kusoma badala ya kuendekeza mil ana desturi za mkoa huo zinazolazimu kukatisha masomo ya m oto wa kike na kuolewa.
Rais Samia pia aliwataka wananchi kuacha tabia ya kucheza ngoma mara wanapopata fedha za mavuno ya mazao yao ya korosho. Aliwataka wakulima kuweka fedha zao akiba katika benki ili kujijengea uwezo siku za usoni waweze kujitegemea kununua pembejeo za kilimo pindi serikali itakapositisha kutoa ruzuku kwa wakulima.
Rais Samia alihutubia katika uwanja wa Majaliwa uliopo Wilaya ya Tandahimba na kuwataka Madiwani , Wakuu wa wilaya pamoja na kamati za Siasa wa Halmashauri ya Tandahimba kusimamia vizuri fedha za maendeleo zinazotolewa na Serikali.
Ziara ya Rais Samia iliendelea kwa kufanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa Sabasaba Newala ambapo Rais Samia alipokea taarifa za:
- Ujenzi wa Hospitali za Halmashauri ya Wilaya ya Newala- Mchemo ambao hadi sasa umeshapokea bilioni 2.85
Alielezwa kuwa Jengo la EMD limeshakamilika kwa asilimia 100. Mradi kamili wa Hospitali unatarajia kukamilika mwezi Desemba mwaka huu.
- Ujenzi wa Mradi wa Maji Makonde
Alielezwa kuwa Mradi huu utahusisha kujenga visima, machujio na matenki makubwa eneo la Mitema hivyo kuwezesha kutoa maji lita milioni 26 badala ya milioni 10 ya hivi sasa.
-
- Matenki yatajengwa eneo la Nambunga lenye uwezo wa lita milioni 6 pamoja na common booster station ili iweze kusukuma maji kufika Nambunga.
- Eneo la Nanda litajengwa tank la lita milioni 3
- Eneo la Mtavala lita milioni 3
- Eneo la Nyundo tenki la lita milioni 1
Mradi huu wa maji wa Makonde utahudumia kata 93. Utekelezaji wa mradi umeshaanza na umefikia asilimia 15 na utakapokamilika utaweza kuhudumia wanachi wote wa wilaya ya Newala kwa makadirio ya wakazi 839,000
- Jengo la Utawala Halmashauri ya Wilaya ya Newala
Kwamba, linajengwa katika kata ya Muungano, Kijiji cha Mmovo ambapo mradi huu ilianza rasmi ujenzi. Gharama za mradi huu ni shilingi bilioni 3.64 na mradi umeshafikia asilimia 96.3
Baadae Rasi Samia alielekea Wilayani Masasi ambapo aliweka jiwe la Msingi kwenye jengo la Utawala Halmashauri ya Wilaya ya Masasi lililogharimu shilingi bilioni 2.66. Rais Samia ameitaka halmashauri hiyo kubuni mbinu za kukusanya mapato ili iweze kujiendesha.
Aliwataka pia wananchi kuandaa mashamba yao ya mikorosho kwa namna inayostahiki ili waweze kupata mavuno mazuri. Rais Samia pia aliwataka wananchi kuongeza jitihada katika kilimo cha mbaazi na ufuta
Rais Samia alidhuru kaburi la aliyekuwa Rais wa Awamu ya 3 Hayati Benjamin Willium Mkapa lililopo katika Kijiji cha Lupaso na kisha kuzungumza na wananchi wa kijijini hapo.
Siku ya 3 Rais Samia aliendelea na ziara yake mkoani Mtwara kwa kukagua na kuweka jiwe la msingi kwenye ghala la kuhifadhia mazao lililopo Mangaka Wilaya ya Nanyumbu ikiwa ni moja kati ya maghala 14 yaliyojengwa nchi nzima (12 bara na 2 Zanzibar).
Mradi huu umejengwa chini ya udhamini wa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo pamoja na African Development Bank (AfDB) una thamani ya shilingi bilioni 78.9. ghala hili lina uwezo wa kuhifadhi tani 1000 za mazao. Mradi wa kujenga maghala nchini unahusisha:
- Ujenzi wa miundo mbinu
- Utoaji elimu juu ya udhibiti wa sumu kuvu
- Kuimarisha taasisi za udhibiti na utafiti
Maghala hayo yana sehemu tatu ambayo ni ghala la kuhifadhia, maabara ya kupima sumu kuvu na sehemu ya kukaushia ikiwa mkulima amepeleka mazao ambayo hayajakauka.
Akizungumza na wananchi wa Nanyumbu katika eneo la round about ya Mangaka aliwasisitiza waaandae mashamba kwa ajili ya kilimo cha mbaazi na ufuta ili waweze kuinua hali ya uchumi
Akihitimisha ziara yake Mkoani Mtwara, Rais Samia alifanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa masasi Mji Rais Samia kwa sasa mkandarasi yuko kazini kuiunganisha Wilaya ya Masasi kwenye gridi ya Taifa kutokea mkoani Ruvuma ambao utakamilika baada ya miezi 18. Pia yupo Mkandarasi ambae anatoa umeme Ruangwa kupitia Nangugwa ambapo Mradi huo utakamilika ifikapo Disemba mwaka huu.
Ilielezwa kuwa Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Masasi – Nachingwea – Liwale yenye kilomita 175 ambayo tayari imeshasainiwa Mkataba, inasubiri malipo ya awai ianze kujengwa.
Aidha, Serikali imetenga bilioni 1.3 kwa ajili ya kuweka taa za barabarani katika maeneo ya Nangaka, Masasi na Nanyumbu ambazo ujenzi utaanza mara moja.
Rais Samia alisema Serikali itajenga kongani ya viwanda katika eneo la Maranje Wilayani Nanyumbu ili kiwe kituo cha kubangua korosho zote za Mtwara. Amesema lengo la kujenga viwanda hivyo ni kuongeza thamani ya korosho na kuongeza mnyororo wa thamani kwa kuuza maganda ya korosho ambayo yatatumika kutengenezea mafuta.
Rais Samia alitoa wito kwa wakulima wa Mtwara kuacha kuandaa mashamba kwa njia ya kuchoma moto kwani kufanya hivyo kunaharibu mazingira na mikorosho yenyewe na hivyo kuisababishia isitoe matunda ya kutosha.
Kuhusu Migogoro ya wakulima na wafugaji, Rais Samia aliziagiza kamati za ulinzi na usalama za mikoa nchini kuishughulikia na kuipa kipaumbele migogoro hiyo. Rais Samia aliwaeleza wananchi kuwa Serikali italishughulikia katika ngazi ya taifa kwa kuandaa mkakati ambao utatatua changamoto hiyo.
Rais Samia alisisitiza juu ya mila na desturi za wananchi wa Mtwara pindi wanapopata fedha waache kuwacheza wasichana katika umri mdogo na kuwaozesha na hivyo kuwasababishia ujauzito katika umri mdogo.
Ameitaka halmashauri ya Wilaya ya Masasi kutumia asilimia 40 ya mapato na kuielekeza katika shughuli za maendeleo ikiwemo kujenga jengo la kuhifadhia X-Ray ili ianze kuhudumia wananchi badala ya kusubiri fedha kutoka Serikali Kuu.
Rais Samia aliwataka viongozi wa halmashauri hiyo kuacha kuwanyonya wakulima kwa kuwakata fedha za mauzo na kuzipeleka katika mifuko ya maendeleo ambayo haijulikani, haipo kisheria na haifanyiwi ukaguzi.
Rais Samia alihitimisha Ziara yake Mkoani Mtwara na kuaza mkoani Lindi na kuanzaia katika Halmashauri ya Wilaya ya Liwale ambayo imezungukwa na hifadhi ya Selous na Nyerere.
Rais Samia alieleza kuwa Wilaya ya Liwale ndio inayoongoza kutoa ikolojia ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi hivyo kwa mchango huo serikali imeamua kuitazama kwa jicho la pekee.
Aliongeza kuwa Liwale pia inazalisha misitu ya asili ikiwemo mninga ambapo asilimia kubwa ya mapato yake yanatokana na mazao ya mninga. Licha ya kuwa wananchi wa Liwale wanaruhusiwa kuvuna miti kisheria, Rais Samia aliwaisisitiza wananchi hao kupanda miti kwa wingi ili kuendelea kunufaika na rasilimali hiyo na kurithisha vizazi vijavyo.
Hali kadhalika, Rais Samia amesema program ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) itapelekwa Liwale katika ufugaji wa nyuki kwa ajili ya asali ili vijana waweze kufaidika na program hiyo kwa kujiajiri.
Aliwataka wananchi kulima kwa kiasi kikubwa mazao ya alizeti, korosho, mbaazi na ufuta kwa kuwa serikali inafanya mpango wa kuwatafutia soko. Program ya BBT itawashirikisha vijana pia katika kilimo cha mazao hayo.
Rais Samia pia amewataka wawekezaji Wilayani Liwale kutvumilia hali ya changamoto ya umeme kwa kuwa serikali inakwenda kuitatua changamoto hiyo kwani nayo ipo katika mpango wa kuunganishwa na gridi ya Taifa kutokea mkoani Ruvuma.
Akiwa Liwale, Rais Samia ameeleza kuwa Serikali itashughulikia changamoto ya ndovu katika ngazi ya kitaifa kwa haraka ili kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi za kila siku.
Amesema Serikali imetoa fedha ili barabara iweze kujengwa na kupitika hasa barabara muhimu ya Nangurukuru kwenda Liwale yenye jumla ya KM 230 ambapo fedha ya kujenga km 72 za awali zimeshatolewa. Rais Samia amesema kila mwaka wa bajeti Serikali itatoa fedha ili kuifanya barabara hiyo ikamilike.
Rais Samia amesikitishwa na tabia ya wazazi ya kutokupeleka watoto shule licha ya jitihada ya serikali ya kutoa elimu bila malipo hivyo kuwataka kuacha tabia hiyo na kuwaacha Watoto waendelee na masomo hasa ya sekondari pindi wanapofaulu darasa la saba badala ya kuwaoza watoto wa kike.
Akiendelea na ziara yake katika wilaya ya Nachingwea, Rais Samia aliwataka wananchi wazidishe juhudi katika kilimo cha mazao ya korosho, ufuta na mbaazi
Tarehe 18 Septemba, Rais Samia aliendelea na ziara yake katika Wilaya ya Ruangwa ambapo alizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Kilimahewa ambapo wananchi walieelezwa kuwa Wilaya hiyo haina changamoto kubwa zinazowakabili.
Alisema Mradi mkubwa wa LNG ambao utawanufaisha wananchi wa mkoa wa Lindi uko katika majadiliano kati ya serikali na muwekezaji. Serikali itajenga kiwanda cha kubangua korosho cha ukubwa wa kati mkoani Lindi kwa lengo la kuwawezesha wananchi kuzalisha mafuta kwa kutumia maganda ya korosho ili waweze kupata faida zaidi na kuifanya Lindi ifunguke kiuchumi.
Rais Samia alisema serikali itaendeleza utafiti zaidi katika sekta ya madini ili kujua kiasi cha dhahabu kilichopo na kuwapanga wachimbaji wadogo wadogo ili wachimbe kitaalamu.
Rais Samia aliendelea na ziara yake katika mkoa wa Lindi kwa kuweka jiwe la msingi barabara ya Ruangwa Nanganga yenye urefu wa KM 53.2 ambayo ni sehemu ya barabara ya Nachingwea – Ruangwa – Nangwangwa yenye urefu wa kilomita 106 kiwango cha lami.
Barabara hiyo inayojengwa na mkandarasi China 15 Group kwa thamani ya shilingi bilioni 50.3. barabara hiyo inasimamiwa na TEKU wa TANROAD na imeshakamilika kwa asilimia 71.
Rais Samia amewataka wakandarasi kwenda kwa kazi ili kumaliza mradi huo kwa wakati.
Akiwa njiani kuelekea Wilaya ya Mtama, Rais Samia alisimama na kuzungumza na wanakijiji wa Nangungu na Nandalaga.
Rais Samia aliendelea na ziara yake kwa kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa jengo la Halmashauri linalojengwa na Mkandarasi SUMA JKT Construction Ltd. Jengo hilo lina gharama ya shilingi bilioni 3.3 ambazo zinatolewa na serikali. Mrradi huo ulioanza Novemba 2021 unatarajiwa kukamilika Novemba 2023. Hadi hivi sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 70.
Akiwa Mtama Rais Samia pia alizungumza na wananchi na kuwasisitiza kutunza amani na utulivu katika maeneo yao.
Kupanda bei kwa korosho na kuwaeleza kuwa msimu wa mwakani wakulima watauza korosho iliyoongezwa thamani hivyo kuwataka wananchi kuongeza kasi ya kutanua mashamba na kulima kwa kiwango kikubwa (large scale farming) hasa mashamba ya mbaazi.
Tarehe 19 Septemba, 2023 rais Samia aliendelea na ziara yake katika wilaya ya Kilwa Masoko ambapo Jiwe la Msingi kwa ajili ya Ujenzi wa Bandari kubwa ya uvuvi inayotarajiwa kukamilika Februari 2025 kwa gharama ya shilingi bilioni 266 na kutoa ajira zaidi ya 30,000.
Rais Samia pia alizindua Awamu ya Kwanza ya ugawaji wa boti za kisasa, ambapo jumla ya boti 160 za mkopo wa masharti nafuu zitagawiwa kote nchini kwa ajili ya uvuvi (boti 131) na kilimo cha mwani (boti 21). Kupitia mpango huu, serikali inatarajia kutengeneza ajira za moja kwa moja zipatazo 3,295.
Rais Samia alikabidhi boti 34 ili ziendelee kuimarisha shughuli za uvuvi na kilimo cha mwami katika pwani ya Kilwa Masoko ambazo zitaongeza kipato cha jamii kwa ujumla.
Alieleza kuwa lengo la serikali ni kuifanya Lindi kuwa kitovu cha uchumi wa buluu kwa ukanda wa kusini.
Rais Samia aliendelea na ziara yake katika mkoa wa Lindi kwa kuweka jiwe la msingi kwenye shule ya sekondari ya wasichana Lindi, Kijiji cha kilangala ikiwa ni moja kati ya shule 10 zinazojengwa chini ya Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP). Mradi unagharimu bilioni 106 hadi ukamilike nchi nzima.
Majengo hayo yamejengwa kwa mafundi wa kijamii (force account). Kwa awamu ya kwanza Ujenzi wa shule huo umeshakamilisha bweni moja kwa asilimia 100 na mabweni manne kwa asilimia 90 ambapo bweni moja lina uwezo wa kubeba wanafunzi 120.
Awamu ya pili yatajengwa mabweni manne yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 80 kila bweni.
Ujenzi utakapokamilika itakuwa na uwezo wa kuwa na wanafunzi 920 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita.
Awamu ya kwanza madarasa manne, madarsa imekamilisha madarasa 12 kwa asilimia 100 na hivi sasa yanajengwa madarasa mengine 10,
Rais Samia aliendelea na ziara yake kwa kuweka Jiwe la Msingi Hospitali ya Mkoa ya Rufaa, Kijiji cha Mitwero na kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara.
Akizungumza katika mkutano huo, Rais Samia amesema Lindi ni miongoni mwa mikoa kumi na moja (11) iliyoingizwa kwenye Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) nchini kwa kushirikiana na IFAD, ambayo itagharimu Dola za Marekani milioni 77.42. Kupitia Programu hii, kitajengwa Kiwanda cha Kuchakata Samaki Kata ya Masoko pamoja na vichanja vya kukaushia dagaa na mazao mengine ya uvuvi katika maeneo mbalimbali.
Rais Samia alieleza kuhusu fursa kubwa ya uzalishaji wa gesi asilia mkoani Lindi na kwamba Serikali imeamua kutekeleza Mradi uliokuwa umekwama kwa muda mrefu wa Kuchakata Gesi Asilia (yaani LNG). Mradi huu utakuwa kichocheo kikubwa cha uchumi na biashara wakati wa utekelezaji, ambapo inakadiriwa zitazalishwa zaidi ya ajira elfu kumi (10,000) na wakati wa uendeshaji ambapo kutakuwa na ajira 600 za moja kwa moja.
Rais Samia aliitaka Wizara ya Madini iwahamasishe na kuwawezesha vijana kuingia kwenye uchimbaji mdogo wa madini mkoani humo kwa kuwa yapo majadiliano yanaendelea kati ya Serikali na baadhi ya makampuni kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya kinywe (graphite).
Rais Samia alieleza vijana wa Lindi wanaweza kutengeneza ajira kupitia utalii katika Mbuga za Wanyama za Selous na Nyerere pamoja na Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara kwa kuwa Lindi ni Mkoa pekee nchini wenye maeneo mawili (02) yaliyotambuliwa na UNESCO kuwa urithi wa dunia, ambayo ni Hifadhi ya Selous na Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara.
Aidha, Rais Samia alihitimisha ziara yake katika mkoa wa Lindi kwa kuzungumza na wananchi wa Somanga Wilaya ya Kilwa pamoja na wananchi wa Ikwiriri wilaya ya Rufiji na Kibiti akiwa njiani kuelekea Mkuranga Wilaya ya pwani
Rais Samia amehitimisha ziara yake mikoa ya kusini ambapo akiwa njiani kurejea jijini Dar es Salaam amezungumza na wananchi wa Somanga, Ikwiriri na Mkuranga na kuwaeleza nia ya serikali ya kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo alizindua kiwanda cha kutengeneza vioo cha Sapphire Float Glass Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
Mradi wa kiwanda hiki umegharimu dola za Marekani milioni 311.14 (sawa na shilingi bilioni 745.74);
Rais Samia amesema serikali inaendelea kuwekeza kwenye mifumo ya utoaji huduma ili kupunguza urasimu na kutekeleza hatua za kiuchumi ambazo zimepokelewa vyema na wadau wa maendeleo.
Amesema Serikali inatarajia kuzindua Mfumo wa kielektroniki wa kuhudumia wawekezaji (Tanzania Electronic Investment Window) ambao utaunganisha taasisi 12 za serikali zinazotoa huduma kwa wawekezaji.
Wawekezaji watakaotaka kuwekeza nchini watapewa msaada katika mchakato wa usajili wa kampuni, upatikanaji wa ardhi, vibali na leseni kupitia dirisha moja la huduma ndani ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).