Habari
ZANZIBAR YAKUMBUKWA KIINI CHA ARI YA UKOMBOZI COMORO

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Visiwa vya Zanzibar vilikuwa kitovu cha ari ya ukombozi wa Comoro kutokana na mchango wa wanadiaspora wa Comoro waliokuwa wakiishi visiwani humo kabla ya uhuru wa taifa lao.
Akizungumza mjini Moroni katika maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Comoro, Rais Samia alikumbusha namna harakati za kisiasa za ukombozi wa bara la Afrika zilivyowasha moto wa hamasa kwa vijana na wazee wa Comoro waliokuwa Zanzibar, Tanganyika na Kenya.
“Vuguvugu la uhuru wa Afrika lilikuza ari ya mapambano hata kwa Wacomoro waliokuwa Zanzibar. Wengi walishiriki kwa njia ya mijadala, uandishi na uhamasishaji. Tuliwapokea kama ndugu,” alisema Rais Dkt. Samia.
Vilevile, aliwakumbusha wananchi wa Comoro kuhusu mchango wa wanawake waliokuwa sehemu ya harakati hizo, wakiwemo Bi Sakina Ibrahim, Rabiata Mohamed, na Hadidja Sabil ambao walifungwa kwa kushiriki maandamano na mikutano ya kisiasa.
Aidha, Rais Dkt. Samia alitoa wito kwa kizazi kipya kuwaenzi mashujaa hao kwa kulinda amani na kudumisha misingi waliyoipigania ya usawa, haki na utu.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia alisema, “Tanzania na Comoro ni familia moja ya kihistoria. Visiwa vyetu vimeunganishwa na bahari lakini mioyo yetu imeunganishwa na mapambano, maadili na urafiki wa kweli.”