Habari
TISEZA: MWAROBAINI MPYA WA UWEKEZAJI NCHINI

SERIKALI imesisitiza dhamira yake ya kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini kupitia Mamlaka mpya ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA) kama injini muhimu katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati nchini.
Hayo yamesemwa leo na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC), Ubungo, Dar es Salaam, kilichojengwa kwa ubia kati ya mwekezaji kutoka China na Serikali ya Tanzania.
Rais Dkt. Samia akibainisha kuwa lengo la mamlaka hiyo mpya ni kuunganisha na kuleta pamoja huduma zote muhimu za uwekezaji ili kuondoa urasimu na kucheleweshwa kwa miradi nchini.
“Tumeunda Mamlaka mpya ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA) ili kuimarisha dhana ya ‘One-Stop Centre’ ya wawekezaji wote wanahudumiwa na taasisi hii kwa ufanisi mkubwa,” alisema Rais Dkt. Samia.
Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa Tanzania ni eneo salama na lenye amani, hali inayovutia wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza kwa kujiamini, na kuongeza kuwa miradi kama EACLC ni ushahidi wa matokeo chanya yanayotokana na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na sekta binafsi.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kujenga mazingira wezeshi yatakayovutia wawekezaji nchini na kutoa rai kwa wawekezaji wapya kutumia nafasi hii kuanzisha miradi inayoongeza thamani ya bidhaa za Tanzania na kuimarisha ushiriki wa nchi katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Rais Dkt. Samia pia ametoa pongezi kwa wadau wote waliotekeleza mradi huo, akiwemo mwekezaji wa kituo hicho, na kueleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kutekeleza miradi mingine ya kimkakati itakayochochea ukuaji wa uchumi.