Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

SERIKALI KUGHARAMIA CHANJO, UTAMBUZI MIFUGO NCHINI


SERIKALI itaendelea kubeba gharama za msingi kwa ajili ya chanjo na utambuzi wa mifugo kama hatua ya kumlinda mfugaji mdogo dhidi ya gharama za utunzaji na hatari za magonjwa ya mifugo.

Hayo yamebainishwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo tarehe 16 Juni, 2025, wilayani Bariadi, mkoani Simiyu.

 “Chanjo na utambuzi si hiari, ni wajibu wa kila mmoja wetu. Serikali imeamua kubeba sehemu kubwa ya gharama hizi ili kumuwezesha mfugaji wa kawaida kufikia huduma hizi muhimu,” alisema Rais Dkt. Samia

Rais Dkt. Samia aliongeza kuwa Serikali tayari imeanza kugawa vifaa vya kampeni hiyo kwa halmashauri zote nchini ikiwa ni pamoja na hereni za mifugo, friji za kuhifadhia chanjo, vifaa vya usajili na sare kwa maafisa ugani.

Hali kadhalika, Rais Dkt. Samia alisisitiza kuwa kampeni hiyo inalenga kumuwezesha mfugaji kuwa na mifugo yenye afya, inayotambulika kisheria na yenye thamani sokoni.

Kwa upande wa ufuatiliaji, Rais Dkt. Samia alielekeza: “Nataka kuona viongozi wa mikoa, wilaya na halmashauri wanasimamia kwa karibu matumizi ya vifaa vilivyogawiwa. Hii si kampeni ya msimu, bali ni msingi wa kuijenga sekta hii.”

Pia alibainisha kuwa uwepo wa kanzidata ya kitaifa ya mifugo na kilimo utasaidia kupanga kwa ufanisi mahitaji ya huduma na kufanya maamuzi ya kisera kwa kutumia takwimu sahihi.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia alitembelea mabanda ya maonesho ya teknolojia na huduma za mifugo ikiwemo huduma za uzalishaji chanjo zinazofanyika hapa nchini.