Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

SERIKALI KUENDELEZA USHIRIKIANO NA TAASISI ZA DINI


RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za kidini nchini ili kuhakikisha zinatimiza wajibu wao katika kuimarisha amani, maadili na maendeleo ya kijamii.

Akizungumza katika uzinduzi wa Kanisa la Calvary Assemblies of God (Arise and Shine) lililopo Kawe jijini Dar es Salaam, tarehe 05 Julai, 2025, Rais Dkt. Samia alisema Serikali haitayumba katika kuendelea kutoa misamaha ya kodi kwa taasisi za kidini zinazotoa huduma zisizo za kibiashara.

“Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa taasisi za kidini katika kujenga jamii yenye maadili. Tutaendelea kushirikiana nanyi katika kuhakikisha taifa letu linadumu katika amani na mshikamano,” alisema Rais Dkt. Samia.

Rais Dkt. Samia pia alibainisha kuwa mchango wa taasisi hizo hauishii katika maeneo ya kiroho pekee, bali pia umejikita katika shughuli za kijamii kama elimu, afya na utunzaji wa watoto yatima.

Katika hatua nyingine, alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inatambua mchango huo kama sehemu ya maendeleo ya taifa.