Habari
RAIS SAMIA: UCHAGUZI OKTOBA UWE WA AMANI, HOJA NA SERA

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, katika mazingira ya amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa.
Akihutubia katika Kongamano la Amani lililoandaliwa na Umoja wa Maimamu Tanzania (UMATA) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Maridhiano na Amani jijini Dar es Salaam leo, Rais Dkt. Samia alisema demokrasia ya vyama vingi inahitaji kujengwa juu ya msingi wa heshima na maridhiano ya pamoja.
“Kampeni za uchaguzi ni hoja na sera, siyo ugomvi. Ni wajibu wetu kama viongozi kuhubiri mshikamano na kuepusha lugha inayoweza kuchochea vurugu,” alisema Rais Dkt. Samia.
Alifafanua kuwa, tofauti na hali ilivyo katika mataifa mbalimbali duniani ambako kipindi cha uchaguzi huzua msuguano wa kisiasa, Tanzania imejijengea utamaduni wa kutunza amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Halikadhalika, alisisitiza umuhimu wa viongozi wa kisiasa kutanguliza mbele maslahi ya taifa badala ya maslahi binafsi.
“Tanzania ni kubwa kuliko sisi sote. Kuna maisha baada ya uchaguzi, na tunapaswa kulinda misingi ya taifa letu bila kuyumbishwa na tofauti za kisiasa,” alisema.
Vilevile, alitoa rai kwa wagombea wote wa kisiasa na wafuasi wao kujiepusha na migongano isiyo na tija, na badala yake washindane kwa sera zinazolenga kuwaletea wananchi maendeleo.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia alieleza kukamilika kwa maandalizi ya uchaguzi na kubainisha kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vitahakikisha mazingira salama na ya uwazi katika zoezi zima la kupiga kura.
“Kwa kuwa kila chama kitakuwa na mawakala wake, na kutakuwepo waangalizi wa kikanda, tuna hakika mchakato wa uchaguzi utakuwa wa wazi, huru na wa haki,” alisema.
Aidha, Rais Dkt. Samia aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura. “Uchaguzi ni nafasi ya wananchi kuchagua viongozi wanaowataka. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kushiriki na kuamua mustakabali wa taifa,” aliongeza.
Vilevile, alitambua mchango wa viongozi wa dini katika kudumisha amani na utulivu wa kitaifa, na kuongeza kuwa mshikamano wa kidini ni nguzo ya kuimarisha utulivu wa kitaifa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Rais Dkt. Samia amewasihi Watanzania waendelee kushirikiana, kudumisha mshikamano na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuharibu taswira ya taifa katika macho ya dunia.