Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

SAMIA AWAENZI WAASISI WA UHURU WA AFRIKA


RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema urithi wa mapambano ya ukombozi wa Tanzania na Msumbiji hautakamilika bila kuwatambua waasisi wa mataifa ya hayo waliounganisha watu wao kwa misingi ya undugu, mshikamano na imani ya uhuru wa kweli.

Akizungumza katika Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Jamhuri ya Msumbiji, Rais Dkt. Samia aliwakumbuka kwa heshima ya kipekee Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Hayati Dkt. Eduardo Mondlane na Hayati Samora Machel, akisema walijenga msingi imara wa mshikamano wa sio tu nchi zao, bali bara la Afrika kwa ujumla.

Rais Dkt. Samia alifafanua kuwa waasisi hao waliongoza harakati za ukombozi kwa kujitolea kwao, wakiamini kuwa hakuna Mwafrika aliye huru wakati mwingine anatumikishwa.

“Mmakonde anayeishi kaskazini mwa Ruvuma hana tofauti na yule wa kusini. Kumnyima uhuru mmoja ni kuwanyima wote,” alisema Rais Dkt. Samia akinukuu kauli ya Hayati Mwalimu Nyerere.

Aidha, Rais Dkt. Samia alieleza kuwa kazi ya ukombozi iliyofanywa na viongozi hao haikuwa ya maneno tu, bali ya vitendo vilivyozaa umoja wa dhati, akiongeza kuwa urithi wa waasisi hao ni kielelezo cha kazi inayopaswa kuendelezwa na kizazi cha sasa kwa misingi ya  mshikamano, uzalendo na maamuzi ya kishujaa kwa maslahi ya taifa.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia pia alipongeza jitihada za Msumbiji, hata baada ya uhuru, za kusaidia mataifa mengine ya Kusini mwa Afrika kupata uhuru wao.

“Msumbiji ilisaidia Zimbabwe, Afrika Kusini na Namibia kupata uhuru. Huu ndio moyo wa mapambano ulioachwa na waasisi wetu,” alisema Rais Dkt. Samia.

Rais Dkt. Samia alitoa rai kwa kizazi cha sasa kuenzi na kuendeleza maono ya viongozi wa kwanza walioweka misingi ya ukombozi, mshikamano na maendeleo ya kweli ya bara la Afrika.