Habari
SAMIA ANG’ARA TUZO ZA MAGEUZI SEKTA YA MAJI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekabidhiwa rasmi Tuzo ya Presidential Global Water Changemakers 2025 kwa uongozi wake mahiri na mchango mkubwa katika kuimarisha sekta ya maji nchini.
Tuzo hiyo, iliyopokelewa mwezi Agosti mwaka huu mjini Cape Town, Afrika Kusini, na Balozi wa Tanzania nchini humo, Balozi James Bwana, kwa niaba ya Rais Dkt. Samia, imewasilishwa kwake leo tarehe 26 Oktoba 2025 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Kombo, katika hafla iliyofanyika Ikulu Tunguu, Zanzibar.
Heshima hiyo ya kimataifa imetolewa kwa kutambua uongozi wa Rais Dkt. Samia katika kuongoza mageuzi makubwa ya kitaifa na kikanda kwenye sekta ya maji, ikiwemo juhudi za kukabiliana na changamoto za maji na mabadiliko ya tabianchi kupitia miradi ya kimkakati na ushirikiano wa kifedha.
Waziri Kombo alisema tuzo hiyo ni uthibitisho wa nafasi ya kipekee ya Rais Dkt. Samia katika kusukuma mbele ajenda za maendeleo endelevu.
“Tuzo hii imetambua nafasi ya kipekee ya Rais katika kuongoza juhudi za kitaifa na bara la Afrika zenye lengo la kukabiliana na changamoto za maji na mabadiliko ya tabianchi,” alisema na kuongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita “imeleta mageuzi makubwa katika sekta ya maji kupitia miradi inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma, kuimarisha uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi na usawa wa huduma kwa Watanzania wote.”
“Uongozi wa Rais Dkt. Samia umeiwezesha Tanzania kutambulika kimataifa katika sekta ya maji na kuwa mfano wa kuigwa kwa nchi nyingine barani Afrika,” aliongeza Waziri Kombo, akibainisha kuwa dhamira hiyo inaakisi sera jumuishi na uongozi unaoweka ustawi wa wananchi mbele.
Hafla ya utoaji wa tuzo hiyo ilifanyika Agosti mwaka huu mjini Cape Town, Afrika Kusini katika mkutano wa G20 AU – AIP Africa Water Investment Summit na kuwasilishwa na Mfalme Mswati III wa Eswatini na Rais Duma Boko wa Botswana, kwa niaba ya waandaaji ambao ni Global Water Partnership (GWP), Korea Water Resources Corporation (K-Water), World Bank Group na Continental Africa Water Investment Programme (AIP).
Tanzania imepiga hatua kubwa katika upatikanaji wa huduma ya maji, ambapo hadi Desemba 2024, upatikanaji wa maji vijijini umeongezeka kutoka asilimia 70.1 mwaka 2020 hadi asilimia 83, huku miradi 2,352 ikiwa imekamilika na mingine 912 ikiendelea kutekelezwa.
Kwa upande wa mijini, upatikanaji umefikia wastani wa asilimia 91.6, na kukamilika kwa miradi mikubwa kama Same–Mwanga–Korogwe, Mugango–Kiabakari–Butiama, na Bunda, kunatarajiwa kuongeza kiwango hicho hadi zaidi ya asilimia 95.
Mafanikio haya yanadhihirisha dhamira ya Serikali chini ya Rais Dkt. Samia katika kuhakikisha huduma ya maji safi inawafikia Watanzania wote.




