Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

SAMIA AANDIKA REKODI MAGEUZI DEMOKRASIA NCHINI


RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ya Awamu ya Sita imefanikiwa kuweka msingi thabiti wa mageuzi ya kisiasa na demokrasia kwa kufungua fursa za kisiasa, kuruhusu uhuru wa mikutano ya hadhara, na kuanzisha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania.

Akilihutubia Bunge la 12 kwa mara ya mwisho leo jijini Dodoma, Rais Dkt. Samia amesema hatua hizo ni sehemu ya utekelezaji wa falsafa ya R4 inayojumuisha mageuzi, maridhiano, ustahimilivu na ujenzi mpya wa taifa.

“Tuliona ni muhimu kujenga maelewano na kuondoa misuguano ya kisiasa ili taifa liweze kuungana katika ajenda ya maendeleo. Tulikubaliana na wadau na kuchukua hatua madhubuti, ikiwemo kuondoa zuio la mikutano ya hadhara,” alisema Rais Dkt. Samia.

Aidha, Rais Dkt. Samia amesema hatua ya Serikali kuboresha sheria muhimu, zikiwemo Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka 2024, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, na Sheria ya Vyama vya Siasa, imejibu kilio cha muda mrefu cha vyama vya siasa na asasi za kiraia kuhusu uhuru na usawa wa kisiasa.

Akizungumza kuhusu ruzuku kwa vyama, Rais Dkt. Samia alisema Serikali imetoa Shilingi Bilioni 87.8 hadi kufikia Juni 2025 kwa vyama vinavyostahili, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha utendaji wao. Aidha, Baraza la Vyama vya Siasa limefanya mikutano sita na kutoa mapendekezo yaliyofanyiwa kazi na Serikali.

Rais Dkt. Samia pia ametangaza kuwa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2025 uko katika hatua ya mwisho na kwamba Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi itatangaza rasmi tarehe ya uchaguzi huo muda si mrefu baada ya kukamilika kwa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

“Kila hatua tuliyochukua imekuwa ya mashauriano. Na tumeamua kuwa uchaguzi huu uendeshwe kwa uhuru, haki, amani na kwa kushirikisha wadau wote,” amesema Rais Dkt. Samia.

Katika hotuba yake, Rais Dkt. pia ameeleza kuwa pamoja na mafanikio hayo, mchakato wa Katiba Mpya umeahirishwa hadi kipindi kijacho cha miaka mitano, kama mojawapo ya ahadi za Ilani ya Chama cha Mapnduzi kwa mwaka 2025–2030.

Kwa mujibu wa Rais Samia, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa mageuzi haya yanakuwa ya kudumu, yanayolinda maridhiano ya kitaifa na kulinda ustawi wa demokrasia ya Tanzania kwa vizazi vijavyo.