Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

RAIS SAMIA: UDUGU WETU NA COMORO SI WA MKATABA, BALI DAMU


RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema uhusiano wa Tanzania na Comoro umejengwa juu ya msingi wa damu, ujamaa na historia ya pamoja, si kwa mikataba tu ya kidiplomasia.

Akizungumza katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Visiwa vya Comoro yaliyofanyika tarehe 06 Julai, 2025, katika Uwanja wa Malouzini Omnisport, mjini Moroni, Rais Dkt. Samia alisema, “Tanzania itaendelea kuwa bega kwa bega na Comoro katika nyakati nzuri na ngumu. Udugu wetu si wa mikataba tu bali ni wa historia, lugha, na mapambano ya pamoja.”

Rais Dkt. Samia alisema Tanzania ilikuwa sehemu ya harakati za ukombozi wa Comoro tangu mwaka 1962 kupitia ofisi ya chama cha ukombozi nchini umo cha MONALICO iliyoundwa na wanadiaspora wa Comoro mjini Dar es Salaam. Harakati hizo ziliungwa mkono kwa misaada ya kisiasa, vyombo vya habari na hifadhi kwa wapigania uhuru.

Aidha, alisema mafanikio ya Comoro katika kipindi cha nusu karne ni ushahidi wa ujasiri wa watu wake.

“Comoro imepiga hatua katika uchumi, huduma za jamii, miundombinu na utalii. Nawapongeza kwa mafanikio hayo,” alibainisha Rais Dkt. Samia.

Sherehe hizo zilihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wakiwemo wa kutoka nchi za Burundi, Mauritius, Ethiopia, Senegal na Madagascar na China.

Katika hotuba yake, Rais Dkt. Samia pia alisisitiza kuwa uhuru wa kisiasa haukamiliki pasipo uhuru wa kiuchumi, akisisitiza kuwa Afrika mpya ya leo inapaswa kujengwa na watu wake kupitia rasilimali zao.