Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

RAIS SAMIA ATAKA WAAFRIKA KUENDELEZA UMOJA BAADA YA UHURU WA KISIASA


RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa mataifa ya Afrika kushikamana kwa dhati katika kusukuma mbele maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiakili, akisema hatua ya kwanza ya ukombozi wa kisiasa sasa inahitaji kuendelezwa kwa mageuzi ya kifikra na kijumla.

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Jamhuri ya Msumbiji, Rais Dkt. Samia alisema kuwa bara la Afrika limepiga hatua kubwa katika kutafuta uhuru wa kisiasa, lakini mafanikio hayo hayatoshi pasipo kuwa na umoja wa kitaifa, mshikamano wa kikanda na mwelekeo wa pamoja wa kiuchumi.

“Bara letu limefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika hatua ya kwanza ya ukombozi, yaani uhuru wa kisiasa. Tunapaswa kushirikiana kufanikisha hatua nyingine ya mageuzi ya kifikra na kutafuta uhuru wa kiuchumi,” alisema Rais Dkt. Samia.

Akitolea mfano wa Mwenge wa Uhuru uliotembezwa nchini Msumbiji, Rais Dkt. Samia alisema hatua kama hizo zinaimarisha mshikamano na kuamsha ari ya kizalendo na matumaini kwa wananchi.

“Uwepo wa Mwenge wa Uhuru hapa unaonesha dhamira ya kuwajenga raia wenye mshikamano na imani kwa nchi yao,” alieleza.

Kadhalika, Rais Dkt. Samia alisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana ikiwa wananchi hawataweka mbele maslahi ya Taifa, kulinda rasilimali na kuwa tayari kujituma kwa ajili ya kizazi kijacho.

Akigusia usawa wa kijinsia, Rais Dkt. Samia alisema kuwa kumuinua mwanamke ni sharti la mafanikio ya mapinduzi ya kweli ya maendeleo.

“Ukombozi wa mwanamke ni kiini cha kuleta mapinduzi na ni sharti la msingi la kufanikiwa kwa mapinduzi yenyewe,” alisisitiza , akinukuu maneno ya Hayati Samora Machel.

Rais Dkt. Samia pia alikumbusha kuwa mshikamano wa Waafrika haupaswi kuishia kwenye historia ya ukombozi, bali uendelee katika kushirikiana kwenye biashara, elimu, afya, na usalama wa kikanda.

“Maadhimisho haya yawe chachu ya kuendeleza ushirikiano na mshikamano baina ya Waafrika wakati tunapopigania maendeleo endelevu na ustawi wa jamii zetu,” alihitimisha.