Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

“TUMIENI MAGEUZI KUFUNGUA MILANGO YA HISA,” SAMIA AZIAGIZA TAASISI


RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa mashirika ya umma kuongeza ubunifu katika kutafuta mitaji, akizitaka taasisi hizo kuchangamkia fursa za soko la hisa kama njia ya kujiimarisha na kuongeza tija ya kiuchumi.

Akizungumza katika hafla ya Siku ya Gawio iliyofanyika Ikulu Dar es Salaam tarehe 10 Juni, 2025, Rais Dkt. Samia alisema pamoja na Serikali kuongeza uwekezaji kwa zaidi ya asilimia 32 na kufikia Shilingi trilioni 86.29, bado changamoto ya upatikanaji wa mitaji imeendelea kuwa kikwazo kwa taasisi nyingi.

“Mageuzi ni pamoja na kuwa wabunifu; tusisubiri kila changamoto itatuliwe na Serikali,” alisema Rais Dkt. Samia.

Katika kuelekea suluhisho endelevu, Rais Dkt. Samia alitoa maagizo mahsusi kwa Msajili wa Hazina kufanya utafiti na kutoa mapendekezo ya mashirika yanayoweza kujiorodhesha kwenye soko la hisa katika kipindi kifupi, cha kati na cha muda mrefu.

“Hatua hii sio tu itasaidia kupata mitaji, bali pia itawezesha wananchi kuwa sehemu ya umiliki wa mashirika na rasilimali zao,” alisisitiza.

Aidha, aliwataka viongozi wa mashirika hayo kuwa tayari kupokea na kuendesha mageuzi yanayohitajika ili kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya kisekta.

Kwa mujibu wa Rais Dkt. Samia, ubunifu katika utafutaji wa mitaji utasaidia taasisi kujitegemea zaidi, kuimarisha huduma na kupunguza utegemezi kwa bajeti ya serikali.

Kauli hiyo ya Rais imekuja wakati taasisi nyingi za umma zikiwa tayari zimeanza kuonyesha mwelekeo chanya, baadhi zikiondoka kwenye utegemezi wa ruzuku za mishahara na sasa kujitegemea, ikiwa ni matokeo ya maboresho ya kiutendaji yanayofanyika ndani ya mashirika hayo.