Habari
MIRADI YA SAMIA YAANDIKA SURA MPYA MAKAO MAKUU DODOMA

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amepongezwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa uongozi wake thabiti unaoleta mageuzi ya kimkakati katika miundombinu ya nchi, hatua inayobadilisha sura ya mji mkuu wa Dodoma na mustakabali wa taifa kiuchumi, kijamii na kidiplomasia.
Pongezi hizo zimetolewa na Rais wa benki hiyo, Dkt. Akinwumi Adesina, alipotembelea miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo barabara za kisasa, reli ya SGR na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma.
Dkt. Adesina alisema Tanzania ni mfano wa mafanikio ya maendeleo ya Afrika ya kisasa yanayozingatia ujumuishaji wa kikanda.
“Leo hii tumeshuhudia Dodoma ikipambwa na barabara za kisasa, uwanja mpya wa ndege wa kimataifa, na reli ya SGR. Haya ni mafanikio makubwa yanayochagizwa na uongozi thabiti wa Rais Dkt. Samia,” alisema Dkt. Adesina.
Aliongeza pia ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato utakaokamilika mwishoni mwa mwaka ujao utaiwezesha Dodoma kuwa kitovu cha anga, biashara, diplomasia na utalii.
“Msalato ni mradi wa mfano. Tumetoa zaidi ya dola milioni 198 kwa ujenzi wake. Uwanja huu utaiunganisha Dodoma na dunia, na kuifanya kuwa jiji lenye ushawishi wa kimataifa,” alieleza.
Kwa upande wa barabara ya mzunguko ya Dodoma yenye urefu wa kilomita 112.3, Dkt. Adesina alisema mradi huo ni wa kimkakati kwa ukuaji wa mji mkuu na maendeleo ya watu wake.
“Ni mradi unaozunguka mji mkuu kwa lengo la kupunguza presha ya mijini, kuboresha mipango miji na kutoa fursa mpya za kiuchumi. Ni sehemu ya kuijenga Dodoma kama jiji la kisasa lenye miundombinu thabiti,” aliongeza Dkt. Adesina.
Rais huyo wa AfDB anayekaribia kumaliza wakati wake, alihitimisha kwa kuipongeza Serikali kwa kuonesha dhamira ya dhati ya kushirikiana na Afrika nzima katika kufanikisha maendeleo shirikishi kupitia miundombinu yenye tija kwa vizazi vya sasa na vijavyo.