Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Habari

MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AFANYA ZIARA YA KISERIKALI NCHINI MISRI KUANZIA TAREHE 10-12 NOVEMBA, 2021


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amefanya Ziara ya Kiserikali ya siku tatu kuanzia tarehe 10-12 Novemba, 2021.

Mapema alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Cairo, Mhe. Rais Samia amepokelewa na Waziri wa Nchi anaeshughulikia Uhamiaji na Wamisri Waishio Nje, Mhe. Nabila Makram.

Mara baada ya kuwasili Ikulu mjini Cairo, Mhe. Rais Samia amefanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mhe. Abdel Fattah Al-Sis na kuzungumza na waandishi wa habari ambapo mazungumzo hayo yamezungumzia maeneo kadhaa ya ushirikiano wa pamoja katika nyanja za elimu, nishati, michezo, ulinzi na ushirikiano wa kijeshi pamoja na umuhimu wa kuendeleza Tume ya Pamoja ya Ushirikiano iliyoanzishwa mwaka 1989.

Akiwa nchini humo, Mhe. Rais Samia ametembelea mji mpya wa Serikali wa Cairo (New Cairo Administrative City) ambapo Serikali ya Misri ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha kuhamisha Makao Makuu ya Serikali katika mji mpya. Katika mji huo mpya inatarajiwa Wizara, Taasisi za Serikali, Bunge, Mahakama, Balozi za nje zenye uwakilishi nchini Misri ikiwemo Tanzania na nyinginezo kuhamia kwenye eneo hilo ambalo pia litakapokamilika linatarajiwa kuwa na watu takribani milioni 6.5.

Aidha, Mhe. Rais Samia ametembelea eneo la viwanda la Kampuni ya Elsewedy ambao ni miongoni mwa wawekezaji wakubwa nchini Misri wanaokusudia kujenga eneo la uwekezaji viwanda nchini Tanzania.

Kampuni ya Elsewedy pia ndio mkandarasi mkuu wa mradi wa Bwawa la Kufua Umeme wa Maji la Julius Nyerere kwenye mto Rufiji.

 

Mhe. Rais Samia pia ametembelea Taasisi ya uwekezaji na biashara huria (General Authority for Investment and Free Zones) ambayo ni Mamlaka Maalum iliyo chini ya Wizara ya Uwekezaji yenye dhamana ya biashara na kutoa motisha maalum kwa wawekezaji kwenye maeneo husika na pia utoaji vibali vya biashara na uwekezaji nchini Misri.

 

Katika Taasisi hiyo, Mhe. Rais Samia amekutana na Wawekezaji mbalimbali na kutumia fursa hiyo kutoa wito kwa wawekezaji hao wa Misri kuja Tanzania kutumia fursa za uwekezaji zilizopo katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kilimo, madini, nishati ya umeme, elimu na nyinginezo.

Mhe. Rais Samia ameshuhudia utiaji sani wa hati za Makubaliano kati ya Tanzania na Misri katika kukuza uwekezaji kwa nchi hizo mbili.