Habari
ADESINA: SAMIA ANAIJENGA AFRIKA KUPITIA TANZANIA

RAIS wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina, amesema uongozi thabiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan umeiwezesha Tanzania kusimama kama kitovu cha miundombinu ya kisasa na ya kimkakati kwa Afrika Mashariki na Kati.
Akihutubia wananchi wa Nala, katika ziara yake ya kutembelea miradi ya maendeleo jijini Dodoma, Dkt. Adesina alisema Benki hiyo imeridhishwa na kasi, ubora na uthubutu wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kutekeleza miradi mikubwa inayolenga kuunganisha Tanzania na nchi jirani kwa njia ya kisasa ya reli, barabara na anga.
“Tunashuhudia sio tu reli, barabara na viwanja vya ndege, bali tunaona Tanzania ikigeuka kuwa mhimili wa usafirishaji, biashara na maendeleo ya kikanda. Haya yote ni matokeo ya uongozi wa maono wa Rais Dkt. Samia,” alisema Dkt. Adesina.
Alieleza kuwa AfDB imewekeza zaidi ya dola bilioni 2 (zaidi ya Shilingi Trilioni 6) katika miradi saba ya miundombinu nchini Tanzania, ukiwemo mradi wa reli ya kisasa ya SGR unaounganisha bandari ya Dar es Salaam na nchi zisizo na bandari kama Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
“SGR ni mradi wa kimkakati unaotekelezwa kwa ushirikiano wa karibu na Serikali ya Tanzania. Tayari tumeshatoa zaidi ya Dola Milioni 85, huku tukiongoza jitihada za kupata Dola Bilioni 1 zaidi kupitia ushirikiano na taasisi za fedha duniani,” alifafanua.
Aidha, Dkt. Adesina aliipongeza Serikali kwa utekelezaji wa mradi wa barabara ya mzunguko ya jiji la Dodoma (Dodoma outer ring road) ambao umefikia asilimia 82 ya utekelezaji na utakuwa kichocheo cha ukuaji wa mji mkuu wa nchi.
“Mradi huu utapunguza msongamano, kurahisisha huduma na kuimarisha muunganiko wa kikanda kupitia mtandao wa barabara za Afrika (Trans-African highways network) na ukanda wa kati (the central corridor). Ni kielelezo cha mji mkuu unaojengwa kwa maono ya mbali,” aliongeza Dkt. Adesina.
Kadhalika, Dkt. Adesina alisema kuwa AfDB itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha miundombinu bora inafikiwa kwa ajili ya kufanikisha Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika.