Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 28 Julai, 2021 amezindua utolewaji wa chanjo ya UVIKO 19 na kuongoza Watanzania kupata chanjo hiyo katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kabla ya kuanza zoezi hilo, Mhe. Rais Samia amewatoa hofu Watanzania kuwa chanjo hiyo ni salama na yeye kama Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama asingejitoa mwenyewe kujipeleka kwenye hatari huku akijua kuwa ana majukumu makubwa yanayomtegemea.
“ Nimekubali kwa hiyari yangu kuchanja nikijua ndani ya mwili wangu nina chanjo kadhaa ambazo nimeishi nazo kwa miaka 61 sasa, tangu tumezaliwa tumepata chanjo zisizopungua tano na hii ya sita na nyingine nilizochanja nikiwa nasafiri, hivyo sioni hatari ya chanjo hii baada ya wanasayansi kujiridhisha na zimekuja nchini na wanasayansi wetu nchini wamejiridhisha mimi niko tayari kuchanja” amesema Mhe. Rais Samia.
Mhe. Rais Samia amewaomba Watanzania kwa hiyari yao kushiriki katika zoezi hilo la chanjo hiyo ya UVIKO 19 ila waendelee kujihadhari na ugonjwa huo.
Aidha, Mhe. Rais Samia amesema kama hujaguswa na maradhi hayo ya UVIKO 19 au watu wako wa karibu unaweza kubeza chanjo ila walioguswa wanatamani kupata chanjo hiyo kwa haraka iwezekanavyo.
Amesema amekuwa akipokea jumbe mbalimbali za simu kutoka kwa baadhi ya Watanzania wakimuuliza jinsi ya kupata chanjo hizo ambapo amesema kwa sasa Serikali inaendelea kuratibu upatikanaji wa chanjo za kutosha ili kuwezesha wananchi wengi kupata chanjo hizo.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewataka wananchi kuwapuuza wale wote wanaopotosha kuhusu chanjo hizo za UVIKO 19 na kusisitiza kuwa ni salama kwa afya baada ya wataalam wetu nchini kujiridhisha kabla ya kuamua kufanyika kwa zoezi hilo.
Mhe. Dkt. Gwajima amewaomba viongozi wa dini, siasa na viongozi wengine katika makundi mbalimbali na Watanzania kwa ujumla kupokea chanjo hiyo kwa kuwa ni silaha ya kisasa katika kukabiliana na UVIKO 19.
Mhe. Waziri Dkt. Gwajima amebainisha kuwa nchi ambazo zimefanya zoezi kama hili la uchanjaji zimepata matokeo mazuri ikiwemo kupunguza maambukizi, kupunguza idadi ya wagonjwa wanaohitaji kulazwa pamoja na kupunguza vifo vitokanavyo na UVIKO 19.
Wakati huohuo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan amepokea miradi iliyofadhiliwa na kujengwa na Serikali ya Ujerumani kupitia Jeshi la nchi hiyo (GAFTAG) kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika hafla iliyofanyika katika Hospitali ya Jeshi Lugalo Jijini Dar es Salaam.
Katika hafla hiyo, Mhe. Rais Samia na Amiri Jeshi Mkuu amesema miongoni mwa miradi iliyokabidhiwa leo ni Idara ya Magonjwa ya Kuambukiza (Infectious Disease Department) ambapo amesema msaada huo umekuja katika kipindi sahihi na muda muafaka kutokana na Dunia ikiwa ni pamoja na Tanzania kukabiliwa na mlipuko wa magonjwa mengi ya kuambukiza, ikiwemo UKIMWI, Kifua Kikuu, Malaria, Ebola pamoja na UVIKO 19.
Mhe. Rais Samia amesema ujenzi wa Idara hiyo utaongeza uwezo wa nchi wa kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza ambapo pia inaendana na dhamira ya Serikali ya kuimarisha na kuboresha huduma za afya nchini pamoja na dhana ya utalii wa kitabibu.
Aidha, Mhe. Rais Samia amesema miradi iliyokabidhiwa ni muendelezo wa miradi mingi ambayo Serikali ya Ujerumani imefadhili nchini tangu mwaka 1961 kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Chuo cha Sayansi ya Tiba cha Jeshi (Military College of Medical Science), Hospitali ya Jeshi Kanda ya Arusha, Idara ya Dharura ya Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo, Ujenzi wa Mabweni ya wanafunzi katika Hospitali ya Kanda Bububu Zanzibar pamoja na ujenzi wa Karakana ya kisasa ya kutengeneza Magari ya Jeshi.
Mhe. Rais ameihakikishia Serikali ya Ujerumani kuwa Tanzania itaendelea kuenzi na kukuza zaidi uhusiano wa kirafiki na kihistoria kati ya mataifa haya mawili na kulitaka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kutunza miradi hiyo ili iendelee kutoa huduma kama ilivyokusudiwa.
Vilevile, Mhe. Rais Samia ameipongeza JWTZ kwa kazi nzuri ya kulinda mipaka ya nchi na kuiwakilisha vyema nchi kimataifa kwenye misheni mbalimbali za kulinda amani.
Hafla ya makabidhiano ya miradi mbalimbali iliyofadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kwa Jeshi la Tanzania imehudhuriwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo, Mhe. Balozi wa Ujerumani nchini Bibi Regine Hess, Mkuu wa Kikundi Maalum cha Ushauri wa Kijeshi kwa Tanzania (GEFTAG) Luteni Kanali Thomas Nalbach, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii ,Jinsia , Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali.