Wasifu
MHE. DKT. SAMIA SULUHU HASSAN
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa TanzaniaMAISHA YAKE
Mhe. Samia Suluhu Hassan alizaliwa Januari 27, 1960 katika Kijiji cha Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja. Ameolewa na Bw. Hafidh Ameir na wamejaaliwa watoto wanne, watatu wa kiume na mmoja wa kike.
ELIMU NA MAFUNZO
Mhe. Samia Suluhu Hassan alipata elimu ya msingi katika shule mbalimbali, zikiwemo Shule ya Msingi Chwaka iliyoko Unguja kuanzia 1966 hadi 1968, Shule ya Msingi Ziwani mwaka 1970 na Shule ya Msingi Mahonda mwaka 1972. Baada ya hapo, alijiunga na Shule ya Sekondari ya Ng’ambo kwa ajili ya masomo ya Kidato cha Kwanza hadi cha tatu, na Shule ya Sekondari Lumumba kwa ajili ya Kidato cha Nne kati ya mwaka 1973 hadi 1976.
Mwaka 1983, alipata Astashada katika Mafunzo ya Takwimu kutoka Chuo cha Uchumi, Zanzibar. Baada ya kufanya kazi kwa kipindi kifupi kwenye Wizara ya Mipango na Maendeleo, mwaka 1983 hadi 1986, alijiunga na Chuo cha Maendeleo ya Uongozi Mzumbe (IDM) kwa ajili ya masomo ya juu katika Utawala wa Umma. Aidha, alipata mafunzo mbalimbali katika Taasisi ya Chuo cha Utawala wa Umma Lahore, Pakistan 1987, Taasisi ya Eastern and Southern African Management Institute (ESAMI) 1991, na Taasisi ya Uongozi ya Hyderabad India 1998 kwa ajili ya Astashahada ya Utawala. Baada ya hapo, alijiunga na Chuo Kikuu cha Manchester kilichopo Uingereza kwa ajili ya masomo ya Juu ya Uchumi. Vilevile, alipata Shahada ya Uzamili ya Maendeleo ya Jamii kupitia programu ya pamoja kati ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Chuo Kikuu cha Southern New Hampshire, Marekani.
UZOEFU NDANI YA SERIKALI
Mhe. Samia Suluhu Hassan ni Rais wa sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Aliapishwa Machi 19, 2021 kufuatia kifo cha ghafla cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Ndugu Samia ni mwanamke wa kwanza nchini kushika nafasi za Makamu wa Rais na hatimaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nyadhifa nyingine alizoshika ndani ya Serikali ni; Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia mambo ya Muungano 2010/2015; Waziri wa Utalii, Biashara na Uwekezaji katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar 2005/2010 na Waziri wa Kazi, Vijana, Ajira, Maendeleo ya Wanawake, na Watoto, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 2000/2005. Mwaka 2014, alihudumu kama Makamu Mwenyekiti wa Bunge lililojadili Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kuandaa rasimu ya Katiba mpya ya Tanzania. Mwaka 1987 hadi 1988, alikuwa Afisa Mipango Rasilimali Watu na Mwaka 1977 hadi 1983, Karani Masijala.
UZOEFU NDANI YA CHAMA CHA MAPINDUZI
Mhe. Samia Suluhu Hassan aliingia katika siasa kama mwanachama wa CCM tarehe 10 Juni, 1987. Aliingia katika siasa za uchaguzi mwaka 2000 katika nafasi ya Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Zanzibar kama Mwakilishi wa Viti Maalum vya Wanawake hadi mwaka 2010. Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, aligombea na kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwakilisha jimbo la Makunduchi, Zanzibar.
Mwaka 2002, alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi, na vile vile, kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi; nyadhifa ambazo ameendelea kuzifanyia kazi hadi leo. Ndugu Samia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja; na alikuwa Mjumbe wa Kamati za Siasa Mkoa na Wilaya ya Kusini Unguja.
Kwa upande wa Jumuiya za Chama cha Mapinduzi, Ndugu Samia ni mwanachama wa Jumuiya ya Wanawake wa Tanzania (UWT) kuanzia mwaka 1996 hadi leo. Aidha, ameshiriki katika kuandika Ilani ya Chama cha Mapinduzi mara nne mfululizo kuanzia 2005/2010, 2010/2015, 2015/2020 na 2020/2025.
UZOEFU KATIKA TAASISI NYINGINE
Mwaka 2016, Mhe. Samia aliteuliwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Ban Ki Moon, kuwa Mjumbe wa Jopo la Umoja wa Mataifa kuhusu Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi, akiwakilisha Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika kati ya mwaka 2016 na 2017. Katika kipindi cha ujumbe wake, aliwasilisha mambo 27 kwenye Jopo hilo, ambayo Serikali ya Tanzania ilibainisha kama hatua za kimkakati kwa ajili ya kuweka mfumo endelevu wa kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi.
Miongoni mwa matokeo ya kazi zake ni kusimamia uanzishwaji wa majukwaa ya uchumi ya wanawake nchini kwa lengo la kuwaunganisha wanawake wafanyabiashara wadogo na wakati kwenye masoko, hasa wanawake wanaoishi mipakani, kuwaunganisha na mikopo nafuu na kuhimiza mafunzo ya ujasiriamali; na kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kuanzisha kampeni ya kuongeza uwajibikaji katika kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto, maarufu kama “Jiongeze Tuwavushe Salama”.
Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (World Food Programme) mwaka 1988 hadi 1997. Vile vile, amefanya kazi katika Kamati, Bodi na Taasisi mbalimbali kama vile; Mjumbe wa Kamati ya Msamaha wa Wafungwa (Parole Committee) ya Zanzibar (2001- 2010), Mlezi wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Zanzibar (1997-2000), Mjumbe wa Bodi ya Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote – EOTF (1996-2000), Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Taasisi zisizo za Kiserikali Zanzibar (ANGOZA) 1995-2000, Mwanachama wa Lions Club Zanzibar (1991-1998), Mjumbe wa Kamati ya Uundaji wa Sera ya Elimu Zanzibar (1996) na Mwanachama Mwanzilishi wa Taasisi ya Kuchochea Maendeleo ya Wanawake Zanzibar (1991-1994).