Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Wasifu

Mwl. JULIUS KAMBARAGE NYERERE
Mwl. JULIUS KAMBARAGE NYERERE
Baba wa Taifa

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Kwanza wa Tanzania alizaliwa tarehe 13 Aprili, mwaka 1922 katika kijiji cha Butiama, Wilaya ya Musoma katika Mkoa wa Mara. Alikuwa mtoto wa Chifu Nyerere Burito na Bibi Christina Mugaya Wanyang’ombe. 

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na viongozi wenzake wa awamu ya kwanza walielekeza juhudi zao katika kuwaunganisha Watanzania na kuweka misingi imara ya kuijenga taifa; kudumisha uhuru na amani na kuweka itikadi na sera za kukabili ujinga, umaskini na maradhi. Aidha, awamu hii iliweka misingi madhubuti ya uhusiano wa nje ikiwa ni pamoja na sera ya kutofungamana na siasa za upande wowote, msisitizo katika ukombozi wa Bara la Afrika na mapambano dhidi ya ubeberu na vibaraka wao. Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Azimio la Arusha lililosisitiza siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, na kuundwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni matunda ya uongozi wa awamu ya kwanza. Mwalijmu Julius Kambarage Nyerere alifariki dunia katika hospitali ya Mtakatifu Thomas iliyoko mjini London, Uingereza tarehe 14 Oktoba, 1999. Kutokana na mchango wake mkubwa kama muasisi wa Taifa hili, Mwalimu Nyerere ataendelea kukumbukwa kuwa Baba wa Taifa.

 

Kazi

Uwezo wa kujieleza na uadilifu vilimsaidia Nyerere kutimiza lengo la TANU la kuipatia nchi uhuru bila vita wala kumwaga damu.Ushirikiano wa Gavana wa Kiingereza Sir Richard Turnbull ulikuwa pia jambo lililochangia kwenye kupata uhuru. Nyerere aliingia
Baraza la kikoloni la kutunga sheria 1958, na alichaguliwa Waziri Kiongozi 1960. Mwaka 1961, Tanganyika ilipewa uhuru wa madaraka ya ndani na Nyerere akawa Waziri Mkuu wa kwanza Desemba 9, 1961. Mwaka mmoja badae, Nyerere alichaguliwa Rais wa Tanganyika ilipokuwa Jamhuri. Nyerere aliwezesha muungano kati ya visiwa vya Zanzibar na Tanganyika kuwa Tanzania, baada ya Mapinduzi ya 1964 yaliyomtoa madarakani Jamshid bin Abdullah, Sultani wa Zanzibar.

 

Elimu

Mwalimu Julius  Kambarage Nyerere alipata elimu ya msingi katika shule ya Mwisenge iliyoko katika Manispaa ya Musoma na baadaye akaendelea na masomo katika shule ya Tabora.

Alisomea shahada ya Ualimu katika Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda mwaka 1943-45 na mwaka 1952 alihitimu shahada ya uzamili katika masomo ya Historian a Uchumi Edinburgh, Uingereza.

 

Nyadhifa nyengine

1954 - Mwanachama Muasisi wa TANU

1958-1960 - Mbunge wa Bunge la Sheria kwenye uchaguzi wa kwanza ambao waafrika waliruhusiwa kupiga kura

1958 - Kiongozi wa Upinzani Bungeni

1960 - Waziri Kiongozi wa Serikali ya ndani

1961 - Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali Huru ya Tanganyika

1962 - Alichaguliwa kuwa Rais Tanganyika ilipokuwa Jamhuri

1963-1970 - Mkuu wa Chuo cha Afrika MAshariki

1964-1985 - Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

1970-1985 - Mkuu wa Chuo cha Dar-es-Salaam

1977-1990 - Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi

1984-1985 - Mkuu wa Chuo cha Kilimo, Sokoine

1985 - Alijiuzulu Urais

1976 - Tuzo ya Nehru kwa maelewano ya kimataifa

1982 - Tuzo ya Ulimwengu wa tatu

1983 - Medali ya Nansen huduma iliyotukuka kwa wakimbizi

1987 - Tuzo ya amani ya Lenin

1992 - Tuzo ya kimataifa ya Simón Bolívar