Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tovuti Rasmi ya Rais

Hotuba

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE HAFLA YA KUKARIBISHA MWAKA MPYA ALIYOIANDAA KWA AJILI YA MABALOZI NA WAKUU WA MASHIRIKA YA KIMATAIFA IKULU, DAR ES SALAAM, TAREHE 21 JANUARI, 2020


    HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE

HAFLA YA KUKARIBISHA MWAKA MPYA ALIYOIANDAA KWA AJILI YA MABALOZI NA WAKUU WA MASHIRIKA YA KIMATAIFA

IKULU, DAR ES SALAAM, TAREHE 21 JANUARI, 2020

 

Mheshimiwa Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo

ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki;

 

Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro, Naibu Waziri wa Mambo

 ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki;

 

Mheshimiwa Ahamada Fakih, Balozi wa Muungano wa Visiwa

vya Comoro na Kiongozi wa Mabalozi nchini;

 

Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi

za Kimataifa;

 

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:

Dunia, kwa sababu ya utandawazi, mageuzi mbalimbali pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia; imekuwa imekuwa kila karne, kila muongo, mwaka, siku na kila dakika ikishuhudia mabadiliko mengi makubwa yakitokea. Na mabadiliko hayo yanazigusa nyanja zote: siasa, uchumi, ulinzi na usalama, jamii, utamaduni, diplomasia, na kadhalika. 

 

Lakini, pamoja na mabadiliko hayo makubwa ambayo yamekuwa yakitokea duniani, yapo baadhi ya mambo ambayo yameendelea kudumu.  Hayajabadilika. Na mojawapo ya mambo hayo ni suala la kutakiana heri ya mwaka mpya. Kila mwaka mpya unapoanza, imekuwa ni utamaduni uliojengeka duniani kote kwa watu kutakiana heri. Hivyo basi, nami napenda nitumie fursa hii, kwa niaba ya Serikali pamoja na Watanzania wote, kuwatakia Heri ya Mwaka Mpya wa 2020, ninyi Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa, familia pamoja na watumishi wenu.  Aidha, kupitia kwenu, naomba salamu zangu za Heri ya Mwaka Mpya ziwafikie Wakuu wa Nchi, Serikali na Mashirika yote ambayo mnayawakilisha vizuri hapa nchini.

Natambua kuwa kwa baadhi yeu hapa hii ni mara yao ya kwanza kwenu kushiriki hafla ya namna hii hapa nchini. Hivyo basi, napenda niwakaribishe hapa Ikulu lakini pia nchini kwetu kwa ujumla. Kama ambavyo naamini mpaka sasa mmeshuhudia wenyewe, nchi yetu ni tulivu, ina amani, na watu wake ni wakarimu sana.  Zaidi ya hapo, najua mnajua kwamba, nchi yetu ina vivutio vingi vya utalii, ikiwemo mbuga za wanyama, uoto mzuri wa asili (misitu, milima, mabonde, maporomoko), maeneo ya kihistoria na halikadhali fukwe nzuri za Bahari na Maziwa. Nawahimiza kutembelea vivutio hivyo ili kujionea uzuri wa Tanzania.

 

 

Waheshimiwa Mabalozi;

Wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa;

Mwaka 2020 una umuhimu wa pekee sana kwa Tanzania. Mwaka huu Serikali ya Awamu ya Tano ya nchi yetu ambayo Watanzania waliniamini na kunipa ridhaa ya kuongoza, itatimiza miaka mitano na hivyo kuhitimisha muhula wake wa kwanza. Aidha, mwezi Oktoba, nchi yetu itafanya Uchaguzi wake Mkuu. Kwa sababu hiyo, Salamu zangu za Mwaka Mpya kwenu kwa Mwaka huu, mbali na kufanya tahmini ya mwaka uliopita na kueleza mikakati ya mwaka tuliouanza kama ilivyo kawaida, zitagusia pia tathmini yangu ya miaka takriban minne na ushee, ambayo Serikali hii imekuwepo madarakani.

 

Mtakumbuka kuwa Serikali hii iliingia madarakani mwezi Novemba 2015. Na kama ilivyo kwa Serikali nyingi duniani, wakati wa kampeni za kuingia madarakani, kupitia Ilani yake ya Uchaguzi, tuliahidi mambo mengi kwa wananchi. Aidha, mtakumbuka kuwa, mwaka huo wa 2015 mwanzoni, Umoja wa Afrika ulipitisha Agenda yake ya Mandeleo ya Miaka 50 ijayo hadi mwaka 2063 (yaani the African Union Agenda 2063). Na mtakumbuka pia kuwa, miezi miwili tu kabla ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani, yaani mwezi Septemba 2015, Umoja wa Mataifa nao ulipitisha Agenda yake ya Maendeleo Endelevu ya Mwaka 2030 (Agenda 2030 for Sustainable Development Goals – SDGs).

 

Hivyo basi, mara tu baada ya kuingia madarakani, Serikali, kwa kutumia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025, Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa Mwaka 2015 – 2020; mipango ya kimataifa niliyoitaja pamoja na mingine ya kikanda, ikiwemo ya SADC na EAC; iliandaa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka mitano 2016/2017 – 2020/2021. Dhima kuu ya Mpango huu ni kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu. Aidha, malengo ya Mpango huu ni kuhakikisha rasilimali na fursa za nchi zinatumika vizuri ili kujenga uchumi wa viwanda na kupunguza umasikini. Malengo mengine mahsusi ni kuimarisha kasi ya ukuaji mpana wa uchumi kwa manufaa walio wengi, kuongeza kasi ya kupunguza umaskini, kuongeza fursa ya ajira kwa wote, kuongeza upatikanaji na ubora wa huduma za jamii na kuongeza mauzo nje kwa bidhaa za viwandani.

Waheshimiwa Mabalozi;

Wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa;

Mabibi na Mabwana;

Ninayo furaha kueleza kuwa utekelezaji wa Mpango wetu wa Taifa wa Maendeleo unaendelea vizuri. Na kusema kweli, kupitia Mpango huo, nchi yetu imepata mafanikio makubwa sana. Kwa haraka haraka, naomba mniruhusu nitaje baadhi ya mafanikio yaliyopatikana.

 

Kwanza kabisa, tumeweza kulinda na kudumisha amani na usalama wa nchi yetu. Kama mjuavyo, moja ya sifa ambayo nchi yetu imejijengea duniani tangu kupata uhuru wake mwaka 1961, ni kudumisha amani na utulivu. Hivyo basi, Serikali ya Awamu ya Tano nayo imelipa umuhimu mkubwa suala la amani na usalama. Zaidi ya hapo, tumeweza kuimarisha Muungano wetu, ambapo mwezi Aprili mwaka huu utatimiza miaka 56. Napenda kutumia fursa hii kuvipongeza vyombo vyetu vyote vya ulinzi na usalama, viongozi wetu wa dini pamoja na Watanzania kwa ujumla kwa kuendelea kutunza na kudumisha amani nchini. Aidha, nawashukuru ninyi Waheshimiwa Mabalozi pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa kwa kuendelea kushirikiana nasi vizuri katika kulinda na kudumisha amani ya nchi yetu. Ahsanteni sana.

Waheshimiwa Mabalozi;

Wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa;

         Kutokana na kuweza kudumisha amani, nchi yetu imeweza, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kupata mafanikio mengi makubwa ya kiuchumi. Kwa wastani, tangu Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani, uchumi wetu unakua kwa asilimia 7. Tumeweza pia kudhibiti mfumko wa bei, ambapo katika kipindi cha miaka minne iliyopita mfumko wa bei kwa wastani kwa mwaka umekuwa chini ya asilimia 5. Mwaka jana, 2019, mfumko wa bei ulikuwa asilimia 3.5. Akiba ya fedha za kigeni nayo imeimarika, kutoka Dola za Marekani bilioni 4.123 mwaka 2015 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 5.579, kiasi ambacho kinatosheleza kuagiza bidhaa na huduma kwa kipindi kisichopungua miezi 6.3.

 

Mafanikio mengine ya kiuchumi yamepatikana katika ukusanyaji mapato, hususan mapato ya kodi ambayo yameongezeka kutoka wastani wa shilingi bilioni 850 kwa mwezi mwaka 2015 hadi kufikia shilingi trilioni 1.5 hivi sasa, ambapo mwezi Disemba 2019 zilikusanywa shilingi trilioni 1.9. Aidha, katika kipindi cha miaka minne iliyopita, nchi yetu imeweza kuvutia uwekezaji wa zaidi ya Dola za Marekani bilioni 13, sawa na shilingi trilioni 30, na kutengeneza ajira zaidi ya laki moja.

Biashara yetu ya nje nayo imeongezeka kutoka shilingi trilioni 11.5 mwaka 2015 hadi kufikia shilingi trilioni 16.6 mwaka 2018. Ukuaji huu umechagizwa zaidi na kuimarika kwa shughuli kuu za kiuchumi na uzalisha nchini, ikiwemo kilimo, ujenzi, viwanda, madini na utalii. Mathalan, kwenye kilimo, uzalishaji wa mazao ya biashara umeongezeka kutoka tani 796,512 mwaka 2015/16 hadi tani milioni 1,141,774 mwaka 2019 sawa na ongezeko la asilimia 43.3. Sekta ya viwanda pia imeendelea kukua, ambapo kati ya mwaka 2015 hadi sasa viwanda vipya 4,877 vimejengwa.

 

Vilevile, baada ya mwaka 2017 kufanya marekebisho ya sheria ili kuongeza uwazi katika biashara ya madini pamoja na kuimarisha usimamizi, makusanya ya Serikali na mchango wa sekta hiyo umeanza kuongezeka. Mathalan, mauzo ya dhahabu nje ya nchi yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.469 mwaka 2017/2018 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 1.743 mwaka 2018/2019. Aidha, mapato ya Serikali kutokana na madini yameongezeka kutoka shilingi bilioni 168 mwaka 2014/2015 hadi shilingi bilioni 346 mwaka 2018/2019. Kwa upande wa utalii, idadi ya watalii imeongezeka kutoka milioni 1.1 mwaka 2015 hadi kufikia watalii milioni 1.5 mwaka 2018. Aidha, mapato ya utalii yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.9 mwaka 2015 hadi Dola za Marekani bilioni 2.488 mwaka 2018.

Waheshimiwa Mabalozi;

Wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa;

Kwa sababu ya kukua kwa uchumi, nchi yetu imeweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, hususan katika sekta ya miundombinu. Najua mnafahamu kuhusu ujenzi wa reli ya kisasa unaoendelea kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma pamoja na ujenzi wa Bwawa kubwa la kuzalisha umeme, Megawati 2,100, katika Bonde la Mto Rufiji. Tumejenga pia barabara takriban kilometa 2,500; barabara nyingine zaidi ya kilometa 2,400 zinaendelea kujengwa; na wakati huo huo kuna kilometa 7,087 ambazo zipo kwenye hatua mbalimbali za maandalizi. Tumekamilisha ujenzi wa madaraja makubwa yapatayo 8, likiwepo Daraja la Magufuli katika Mto Kilombero lenye urefu wa meta 384; na ujenzi wa madaraja mengine unaendelea, likiwemo Daraja la Kigongo - Busisi lenye urefu wa kilometa 3.2, Daraja la Salender lenye urefu wa kilometa 1.1 pamoja na Daraja la Wami lenye urefu wa meta 513.5.

 

Tumefufua pia reli yetu ya kati kutokea Dar es Salaam – Tanga hadi Moshi ambayo ilikuwa haitoi huduma kwa zaidi ya miaka 20. Kwa upande wa usafiri wa maji, tunafanya upanuzi wa Bandari zetu kuu za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga; na wenzetu kule Zanzibar wapo kwenye hatua mbalimbali za ujenzi wa Bandari Mangapwani na Mpigaduri na wamenunua meli kubwa mbili, ambazo zinatoa huduma katika Bandari ya Hindi. Tupo pia kwenye hatua mbalimbali za ujenzi na ukarabati wa meli takriban 7 kwa ajili ya kutoa huduma katika Maziwa yetu Makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa na pia kuboresha Bandari zake. Kuhusu usafiri wa anga, tayari tumekamilisha ujenzi wa Jengo jipya la Abiria (Terminal III) katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere na tunaendelea na upanuzi wa Uwanja wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume kule Zazibar pamoja na viwanja vingine 11. Aidha, ujenzi rada 4 (Dar es Salaam, Kilimanjaro, Songwe na Mwanza) unaendelea na pia tumefufua Shirika letu la Ndege (ATCL) kwa kununua ndege mpya 11, ambapo 8 tayari zimewasili. Hatua hizi zimewezesha kuongezeka kwa idadi ya wasafiri wa anga nchini kutoka wasafiri milioni 4.8 mwaka 2015 hadi wasafiri milioni 5.8 mwaka 2018. Bila shaka, mwaka jana (2019) watakuwa wameongezeka zaidi.

 

Tunaendelea pia kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme nchini. Mbali na kutekeleza mradi mkubwa wa kufua umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, tunaendelea na miradi mingine kwa kutumia vyanzo mbalimbali ikiwemo maji, gesi asilia, jua, upepo, n.k. Aidha, tumekamilisha miradi mikubwa ya kusafirisha umeme, ikiwemo Mradi wa  Iringa – Shinyanga; Makambako – Songea; Lindi – Mtwara; n.k.; pamoja na kuendelea  na Mradi wa Kupeleka Umeme Vijiji, ambapo tumeweza kuongeza idadi ya vijiji vilivyofikishiwa umeme kutoka 2,018 mwaka 2015 hadi kufikia vijiji 8,587 hivi sasa. 

Sambamba na kujenga miundombinu, kutokana na kuimarika kwa uchumi wetu, tumeweza kupanua wigo na kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu za jamii, hususan afya, elimu na maji. Kwenye afya, tumejenga na kukarabati miundombinu ya kutolea huduma za afya, ikiwemo vituo vya afya 352 na hospitali za wilaya 69. Aidha, tumeajiri watumishi wa afya wapatao 8,000; tumeongeza bajeti ya dawa na vifaa tiba na kuimarisha huduma za kibingwa, hususan za magonjwa ya moyo, mifupa/mishipa, figo na kansa. Hii imetusaidia kupunguza kupeleka wagonjwa nje ya nchi.

 

Kuhusu elimu, kama mnavyofahamu, Serikali inaendelea kutoa elimu ya msingi hadi sekondari bila malipo, ambapo mpaka sasa tumetumia zaidi ya shilingi trilioni 1 kugharamia. Tumeongeza pia bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kutoka shilingi bilioni 341 mwaka 2014/2015 hadi shilingi bilioni 450 mwaka huu wa Fedha 2019/2020. Hatua hizi zimeongeza udahili kwenye shule za msingi, sekondari pamoja na vyuo vikuu. Zaidi ya hapo, tumejenga miundombinu mbalimbali, ikiwemo madarasa, kumbi za mihadhara, maabara, maktaba, mabweni, hosteli, mabwalo ya chakula, nyumba za watumishi na ofisi. Kwa upande wa sekta ya maji, katika kipindi cha miaka minne iliyopita, tumetekeleza miradi ya maji yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 3. Hii imewezesha hali ya upatikanaji nchini kuimarika kutoka asilimia 56 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 71 hivi sasa (ambapo mijini ni asilimia 84 na vijijini asilimia 64).

 

Mafanikio mengine tuliyoyapata katika kipindi cha miaka minne iliyopita ni kuongeza mapambano dhidi ya rushwa; kuhamishia Makao Makuu ya Nchi yetu Jijini Dodoma na pia kufanya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ulio huru na haki mwaka jana.

 

Waheshimiwa Mabalozi;

Waheshimiwa Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;

Katika nyanja za kimataifa, kama mnavyofahamu, nchi yetu tangu ipate uhuru wake mwaka 1961, imekuwa mstari wa mbele katika masuala ya kimataifa. Hivyo basi, katika kipindi cha miaka cha miaka minne iliyopita, tukiongozwa na Sera yetu ya Mambo ya Nje inayoweka mkazo Diplomasia ya Uchumi, tumeweza kuimarisha uhusiano wetu na nchi mbalimbali pamoja na taasisi mbalimbali za kimataifa. Mimi pamoja na viongozi wenzangu tumeweza kufanya ziara kwenye nchi mbalimbali na kushiriki katika mikutano ya kimataifa. Mathalan, mwaka jana, binafsi nilitembelea nchi za Afrika Kusini, Namibia na Zimbabwe. Aidha, katika kipindi hicho viongozi mbalimbali wa nchi na taasisi za kimataifa walitembelea nchi yetu. Katika kipindi cha miaka minne iliyopita tumeweza kufungua Balozi mpya 7 (Algeria, Cuba, Israel, Korea, Qatar, Namibia na Uturuki).

 

 Mtakumbuka pia kuwa wakati Serikali ninayoingoza ikiingia madarakani, nchi yetu ilikuwa Mwenyekiti wa EAC; jukumu ambalo tulipaswa kulikabidhi mwezi Februari 2016. Hata hivyo, Wakuu wa Nchi wa EAC waliamua kutuongezea mwaka mwingine mmoja hadi mwezi Machi 2017. Mwezi Agosti 2019, nchi yetu pia iliaminiwa na kukabidhiwa jukumu la kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya SADC, ambalo tunaendelea nalo hadi mwezi Agosti 2020. Sambamba na hayo, nchi yetu imeendelea kushiriki katika shughuli na mipango mbalimbali ya kimataifa, ikiwemo ulinzi wa amani, ambapo kwa sasa tuna askari wapatao 2,297 katika nchi za DRC, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Lebanon, Sudan na Sudan Kusini. Aidha, mwezi Julai 2019, Tanzania iliwasilisha Ripoti yake kwenye Umoja wa Mataifa kuhusu utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), na hivyo kuifanya iwe miongoni mwa nchi za mwanzo kabisa duniani kufanya hivyo.

Haya ni baadhi tu ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne iliyopita. Na kama nyote mjuavyo, sehemu yoyote, mafanikio hupatikana kutokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali. Hivyo basi, kwa moyo wa dhati kabisa, napenda kutumia fursa hii kuyashukuru mataifa na taasisi mbalimbali za kimataifa kwa ushirikiano mkubwa mliotupatia hadi kuweza kupatikana kwa mafanikio hayo. Tunawasihi muendelee kutuunga mkono.

Waheshimiwa Mabalozi;

Waheshimiwa Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;

Katika kipindi cha Mwaka 2020, Serikali imejipanga kuendelea kutekeleza Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano, ambapo kipaumbele chetu kitakuwa kuendelea kudumisha amani na kuimarisha Muungano wetu. Vipaumbele vingine ni kukuza uchumi, ambapo tunalenga uchumi ukue kwa asilimia 7.1;  kudhibiti mfumko wa bei ili usizidi asilimia 5; kuimarisha akiba ya fedha za kigeni; kuongeza ukusanyaji wa mapato; na kukuza sekta zetu kuu za uchumi na uzalishaji, yaani kilimo, viwanda, ujenzi, madini pamoja na utalii. Halikadhalika, tutaendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji nchini. Kama mnavyofahamu, mwezi Julai 2019, nchi yetu imeanza kutekeleza rasmi Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (yaani Blueprint for Regulatory Reforms to Improve the Business Environment). Napenda kutumia fursa hii kuwaomba Waheshimiwa Mabalozi kuwashawishi wafanyabiashara kutoka kwenye nchi zenu kuja kuwekeza hapa nchini.

 

Sambamba na hayo, kama nilivyoeleza awali, mwaka huu mwezi Oktoba, nchi yetu itafanya Uchaguzi Mkuu. Zoezi la Uchaguzi ni muhimu kwa nchi yoyote inayofuata misingi ya kidemokrasia kama yetu. Hivyo basi, Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 unafanyika katika mazingira ya amani, uhuru na haki. Na kama ilivyo kawaida yetu, wakati ukifika, tutazikaribisha nchi na taasisi mbalimbali kuja kuangalia uchaguzi wetu ili kujionea jinsi nchi yetu ilivyokomaa katika nyanja za demokrasia.

Katika nyanja za kimataifa, tumejipanga mwaka 2020 kuendelea kukuza diplomasia yetu, kwa kuimarisha ujirani mwema na uhusiano na mataifa mengine. Tutaendelea pia kutekeleza majukumu yetu kimataifa kwa mujibu wa mikataba mbalimbali tuliyosaini na kuridhia, ikiwemo jukumu letu la kuwahudumia wakimbizi. Na katika hilo, napenda kutumia fursa hii kuishukuru Jumuiya ya Kimataifa kwa kuunga mkono utekelezaji wa zoezi la kuwarejesha kwa hiyari nchini mwao wakimbizi wa Burundi. Zoezi hili linafuata sheria, kanuni na taratibu zote za kitaifa, kikanda na kimataifa na linafanyika kwa ushirikiano wa karibu wa wadau wote wanaohusika ikiwemo Serikali ya Burundi na mashirika ya kimataifa ya UNHCR na IOM. Hata hivyo, tunasikitishwa na hujuma na propaganda zinazofanywa kwa lengo la kukwamisha zoezi hilo.

 

Mwaka huu, kama mjuavyo, Umoja wa Mataifa utatimiza miaka 75. Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1945, Umoja huo umepata mafanikio mengi, lakini pia umeendelea kukabiliwa na chagamoto mbalimbali. Hivyo basi, tunaahidi kuendelea kushirikiana na mataifa yote duniani katika kushughulikia changomoto hizo ili kuufanya Umoja huo kuwa imara zaidi, ikiwemo kwa kuhimiza kuendelea kwa majadiliano ya kuufanyia mageuzi ili kujenga usawa na kuimarisha demokrasia ndani ya Umoja huo. Na katika hilo, tunaahidi kuendelea kutetea msimamo wa Umoja wa Afrika kama ilivyobainishwa kwenye Makubaliano ya Ezulwini (yaani Ezulwini Consensus) pamoja na Azimio la Sirte (yaani Sirte Declaration).

 

Tanzania pia itaendelea kushirikiana na mataifa mbalimbali katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia, ikiwemo masuala ya amani na usalama, hususan katika Bara letu la Afrika. Na katika hilo, tukiwa Wenyekiti wa SADC tutaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya usalama nchini DRC na Lesotho. Naisihi jumuiya ya kimataifa kuendelea kuunga mkono jitahada za kutafuta amani katika nchi hizo na maeneo mengine duniani.  Aidha, tutaendelea kushirikiana na mataifa mengine kushughulikia changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi. Kama mjuavyo, hii ni moja ya changamoto kubwa yenye kuikabili dunia kwa sasa. Nchi mbalimbali zimeendelea kukumbwa na majanga mbalimbali yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi. Mathalan, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, nchi kadhaa za SADC, ikiwemo Afrika Kusini, Angola, Madagasacar, Malawi, Msumbiji na Zimbabwe zilikumbwa na majanga ya vimbunga, mvua kubwa na mafuriko yaliyosababisha vifo na uharibifu mkubwa wa miundombinu.

 

Nitumie fursa hii kurudia tena kutoa pole nyingi kwa nchi zote zilizokumbwa na majanga hayo. Majanga hayo yanatukumbusha umuhimu wa jumuiya ya kimataifa kushirikiana katika kuzuia athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi. Hivyo basi, natoa wito kwa mataifa yote duniani kushirikiana katika kuzuia na kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabiachi ikiwa ni pamoja na kutekeleza Mikataba mbalimbali ya kimataifa, ukiwemo Mkataba wa Paris wa Mwaka 2015. Kwa upande wetu, Tanzania, tunaendelea kuchukua hatua zenye lengo la kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi, hususan kwa kuhakikisha tunayatuza mazingira yetu. Mathalan, mwaka jana tulisisitisha matumizi ya mifuko ya plastiki.

 

Utekelezaji wa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme katika Bonde la Mto Rufiji nao ni sehemu za jitihada zetu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kama mnavyofahamu, kwa sababu ya kukosekana kwa umeme wa uhakika, wananchi wetu wengi wamekuwa wakitumia kuni na mkaa; na hivyo, kwa wastani kwa mwaka nchi yetu inapoteza takriban ekari 400,000.  Hivyo basi, tuna imani kuwa utekelezaji wa Mradi wa Umeme wa Bonde la Mto Rufiji utapunguza matumizi ya kuni na mkaa na hivyo kusaidia kulinda misitu yetu. Zaidi ya hapo, kutokana na kuongeza kwa majanga yatokanayo na athari za tabianchi katika Ukanda wetu, mwezi Februari 2020, Tanzania, ikiwa Mwenyekiti wa SADC, itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kwanza wa Mawaziri wenye dhamana ya kushughulikia masuala ya Majanga mbalimbali.

Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje;

Waheshimiwa Mabalozi;

Waheshimiwa Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;

Nimesema mambo mengi. Lakini kabla sijahitimisha naomba nizungumzie suala moja la mwisho, nalo ni kuhusu changamoto ya tax refund; ambayo ninyi Waheshimiwa Mabalozi mmekuwa mkiilalamikia sana. Napenda niseme kuwa Serikali inaifahamu changamoto hii. Lakini niseme tu kuwa, kimsigi, changamoto hii inatokana na baadhi ya wadau kukosa uaminifu na uadilifu. Hii imefanya Serikali kuongeza umakini zaidi ili kukabiliana na udanganyifu uliokuwa ukijitokeza katika eneo hilo. Hivyo basi, ili kuondoa changamoto hii, niwahimize wadau wote kushirikiana na kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu. Lakini nitumie fursa hii pia kutoa wito kwa Mamlaka ya Mapato kuhakikisha kuwa taratibu za uhakiki zinapokamilika kujitahidi kurejesha kwa wakati fedha zilizokusanywa kwa utaratibu wa tax refund kwa wahusika.

 

Mabibi na Mabwana; napenda kuhitimisha kwa kurudia tena kuwashukuru Waheshimiwa Mabalozi kwa kuhudhuria Hafla hii. Aidha, nawashukuru kwa ushirikiano mkubwa ambao nchi na taasisi mnazoziwakilisha zinatoa kwa nchi yetu. Napenda niwaahidi kuwa Serikali ninayoingoza itaendelea kushirikiana na na nchi pamoja tasisisi zote mnazoziwakilisha sio tu katika kukuza uhusiano na ushirikiano uliopo na bali pia kwa lengo la kuifanya dunia kuwa mahali pazuri pa kuishi.

 

Mungu Ubariki Uhusiano uliopo kati ya Tanzania na nchi pamoja na Taasisi mbalimbali!

Mungu Ibariki Tanzania!

 “Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”