Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA UFUNGUZI WA MKUTANO WA MAWAZIRI WA MAMBO YA NJE KUTOKA NCHI ZA AFRICA NA NORDIC, UKUMBI WA JULIUS NYERERE, DAR ES SALAAM- TAREHE 08 OKTOBA, 2019

Friday 8th November 2019

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA UFUNGUZI WA MKUTANO WA MAWAZIRI WA MAMBO YA NJE KUTOKA NCHI ZA AFRICA NA NORDIC, UKUMBI WA JULIUS NYERERE, DAR ES SALAAM-

TAREHE 08 OKTOBA, 2019

 

Waheshimiwa Marais Wastaafu wa Jamhuri ya

         Muungano wa Tanzania;

 

Waheshimiwa Makamu wa Rais na Mawaziri

 Wakuu Wastaafu wa Tanzania mliopo;

 

Mheshimiwa Profesa Palamagamba Kabudi,

         Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa

         Afrika Mashariki na Mwenyeji wa Mkutano

         huu;

 

Waheshimiwa Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka

 Nchi za Nordic na Afrika mliopo;

 

Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa

         Mashirika ya Kimataifa mliopo;

 

Waheshimiwa Viongozi wote wa Chama na

 Serikali;

 

Wageni wote Waalikwa, Mabibi na Mabwana:

 

Najisikia furaha kubwa kuweza kushiriki, kwa mara ya kwanza, katika Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika na Nordic. Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano huu tangu kuanzishwa kwa utaratibu wa mikutano kama hii mwaka 2001. Hivyo basi, nitumie fursa hii kuwashukuru Waandaji wa Mkutano huu kwa kunipa heshima ya kuwa Mgeni Rasmi kwenye Hafla ya Ufunguzi wa Mkutano huu.

 

Aidha, kwa namna ya pekee kabisa, niwashukuru kwa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano huu muhimu katika kukuza ushirikiano kati ya mataifa ya Nordic na Afrika. Ahsanteni sana.

 

Natambua kuwa wengi mmesafiri umbali mrefu, na baadhi yenu, hii ni mara ya kwanza kufika Tanzania. Hivyo basi, karibuni sana nchini kwetu, hususan kwenye Jiji letu la Dar es Salaam. Dar es Salaam maana yake ni mahali pa amani na usalama. Kwa sababu hiyo, nina uhakika kuwa Mkutano huu utafanyika kwa amani na salama; na kuleta mafanikio kwa pande zote mbili.

 

Waheshimiwa  Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:

 

Mkutano huu ni wa siku moja. Kwa hiyo, nitajitahidi kuzungumza kwa kifupi ili nisiwachukulie muda wenu wa majadiliano. Mabibi na Mabwana, kwa ufupi kabisa, uhusiano kati ya nchi za Afrika na Nordic ni wa muda mrefu; na ulianza kabla ya uhuru wa nchi nyingi za Afrika kupatikana. Na kusema kweli, nchi za Nordic zilisaidia sana harakati za ukombozi kwenye nchi mbalimbali, hususan Kusini mwa Afrika.

 

Kama mnavyofahamu, Tanzania ilikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya  Ukombozi ya Afrika. Hivyo, harakati nyingi ziliendeshwa nchini mwetu, ambapo kulikuwa na kambi nyingi za wapigania uhuru.  Hivyo, tunafahamu mchango mkubwa uliotolewa na nchi za Nordic, ikiwemo ujenzi wa kilichokuwa Chuo cha Wapigania Uhuru wa Afrika Kusini kilichofahamika kwa jina la Solomon Mahlangu Freedom College (SOMAFCO). Chuo hiki kilijengwa mwaka 1975 Mkoani Morogoro, takriban kilomita miambili kutoka hapa Dar es Salaam. Ikumbukwe kwamba, nyakati hizo, ilikuwa siyo rahisi kwa mataifa ya Ulaya kuja kuunga mkono jitihada za ukombozi Afrika lakini marafiki zetu

wa nchi za Nordic walikuja.  Na huu ndio upekee wa nchi za Nordic.

 

Baada ya kusaidia harakati za kupigania uhuru, nchi za Nordic zimeendelea kuwa washirika wakubwa wa maendeleo ya nchi za Afrika. Tumekuwa tukishirikiana katika nyanja nyingi, ikiwemo afya, elimu, kilimo, sayansi na teknolojia, nishati, mazingira na, bila kusahau, masuala ya amani na usalama.   Nchi za Nordic zimesaidia sana kujenga uwezo wa Bara letu kukabiliana na changamoto za migogoro.

 

Tanzania ni miongoni mwa wanufaika wakubwa wa ushirikiano uliopo na nchi za Nordic. Kabla na baada ya Uhuru, nchi yetu imenufaika na miradi mingi ya maendeleo, ikiwemo Kituo cha Elimu Kibaha (Kibaha Education Centre) na Kituo cha Utafiti wa Kilimo Uyole (Uyole Agricultural Research Centre).

 

Vilevile, nchi za Nordic zilitusaidia kujenga vyuo vya ufundi na pia kwenye Kampeni ya Kufuta Ujinga, yaani Literacy Campaign Programme, iliyotekelezwa kwenye miaka ya 1970 na kuiwezesha Tanzania kufuta ujinga kwa asilimia 98, na hivyo kuwa miongoni mwa nchi za kwanza kabisa Afrika kufikia kiwango hicho. 

 

Zaidi ya hayo, sisi Watanzania tunakumbuka misaada tuliyopewa na nchi za Nordic kwenye miaka ya 1980, wakati baadhi ya mataifa makubwa na taasisi za kifedha za kimataifa zilipositisha misaada kwa nchi yetu.

 

Kwa kuzingatia hayo yote, napenda nitumie fursa hii kutoa shukrani zangu  za dhati kwa ndugu na marafiki zetu wa nchi za Nordic kwa kuendelea kushirikiana na nchi yetu na nchi nyingine za Afrika kwa ujumla. Na tunawaomba Waheshimiwa Mawaziri kutoka nchi za Nordic mfikishe salamu na shukrani zetu kwa Wakuu wenu wa Nchi na Serikali.

 

Waheshimiwa Mawaziri;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:

 

Pamoja na uhusiano mzuri na mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye ushirikiano kati ya nchi za Afrika na Nordic, bado tuna fursa ya kuukuza uhusiano wetu na kuupa msukumo mpya ili kuleta manufaa makubwa zaidi kwa pande zetu mbili. Na suala hili ni muhimu kwa sababu, kwa muda mrefu, ushirikiano wetu umejikita zaidi kwenye kutoa na kupokea misaada, yaani donor-recipent relationship. Ushirikiano wa aina hii siyo endelevu na wala hauhitajiki katika mazingira ya sasa. Viongozi wengi wa Afrika tumetambua kuwa mustakabali wa Bara letu uko mikononi mwetu na kwamba uhuru wa kisiasa hauwezi kuwa na maana sana, endapo mataifa yetu yataendelea kuwa tegemezi kiuchumi. Hatuwezi kuwa na uhuru wa kujiamlia mambo yetu wenyewe endapo mataifa yetu yataendelea kuwa ombaomba.

 

 Kutafuta ukombozi wa kiuchumi ndilo jukumu tuliloachiwa sisi viongozi wa sasa wa Africa. Hata Hayati Mwalimu Julius Nyerere alisema, katika moja ya hotuba zake kwamba “The first generation of leaders led Africa to political freedom. But we, the current generation of leaders, must pick up the flickering torch and lead Africa towards economic liberation”.  

 

Hivyo basi, ni lazima tubadilishe mwelekeo na kuingia kwenye uhusiano wa kisasa baina ya mataifa ambao unajikita kwenye ushirikiano wa kiuchumi (economic partnership) kupitia biashara na uwekezaji. Diplomasia ya uchumi ndiyo iwe msingi wa uhusiano na ushirikiano baina ya mataifa yetu.

 

Kwa bahati nzuri, uwezo, fursa na mazingira ya kuingia kwenye ushirikiano madhubuti wa kiuchumi yapo. Kwa mfano, nchi za Nordic, ambazo zipo tano: Denmark, Finland, Iceland, Norway na Sweeden; licha ya kuwa na eneo dogo (kilomita za mraba milioni 3.5) na idadi ya watu wapatao milioni 27 tu; zina uchumi mkubwa. Pato lao kwa mwaka jana (2018) lilikuwa na thamani ya Dola za Marekani trilioni 1.7.

 

Kwa upande wetu Afrika, kama inavyofahamika, Bara letu ni kubwa (lina kilomita za mraba milioni 30.37) na idadi ya watu wapatao bilioni 1.2. Hata hivyo, kwa mwaka jana 2018, Pato la nchi zote za Afrika lilikuwa na thamani ya Dola za Marekani trilioni 2.334 tu.

 

Kusema kweli, sisi Waafrika tuna jambo kubwa la kujifunza. Kwa sababu, wakati nchi za Nordic zenye jumla ya watu milioni 27 tu, Pato lao kwa mwaka ni Dola za Marekani trilioni 1.7; sisi Tanzania ambao tuko milioni 55, mara mbili zaidi ya nchi za Nordic, Pato letu la Taifa kwa mwaka jana lilikuwa na thamani ya Dola za Marekani bilioni 56.99 tu.

 

Lakini hata ukilinganisha Pato la mtu mmoja mmoja katika nchi za Nordic na Afrika, tofauti ipo kubwa sana. Kwa mfano, ukigawa Pato la nchi za Nordic la Dola za Marekani trilioni 1.7 kwa watu milioni 27, maana yake pato la mtu mmoja ni wastani wa Dola za Marekani 62,963. Lakini kwenye nchi za Afrika ni wastani wa Dola za Marekani 1,945 tu. Tofauti hii ni kubwa sana; hivyo basi, sisi Waafrika ni lazima tujitafakari ili tujue tunapokosea na tujifunze kutoka kwa marafiki zetu wa nchi za Nordic.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Mabibi na Mabwana

Bara letu la Afrika limebarikiwa kuwa na utajiri mwingi wa rasilimali na maliasili. Mathalan, Bara letu lina eneo kubwa lenye kufaa kwa kilimo. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, asilimia 30 ya ardhi yenye kufaa kwa kilimo duniani ipo Barani Afrika. Aidha, Afrika ina utajiri wa rasilimali za bahari kwenye ukanda wa pwani wenye urefu wa kilomita 30,500. Rasilimali zingine ni pamoja na mifugo, wanyamapori, misitu, madini, mafuta, gesi, vivutio vya utalii, nk.

 

Muhimu zaidi, ni kwamba, katika miaka ya karibuni, Afrika imefanya mageuzi makubwa kwenye nyanja za ulinzi na usalama. Licha ya kuendelea kwa baadhi ya migogoro, hali ya amani na usalama imeimarika. Uchumi pia unakua vizuri, ambapo Afrika inashika nafasi ya pili kwa kasi ya ukuaji wa uchumi duniani. Mathalan, mwaka 2018, uchumi wa Afrika ulikua kwa wastani wa asilimia 4.1. Na kati ya nchi 10 zenye uchumi unaokuwa kwa kasi zaidi duniani, tano zinatoka Afrika. Haya yote yanatoa fursa kwa pande zetu mbili kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Mabibi na Mabwana:

Nimetaja baadhi ya fursa za ushirikiano wa kiuchumi katika Afrika. Lakini hata hapa nchini, tumejaliwa rasilimali na maliasili lukuki na fursa za uwekezaji zipo kwenye sekta zote. Mathalan, tunayo madini karibu yote yanayopatikana duniani: dhahabu, almasi, rubi, sapphire, chuma, soda ash, shaba, nikeli, cobalt, tin, urania, helium, nk. Siwezi kuyataja yote hapa na mengine, kama vile tanzanite, yanapatikana hapa Tanzania pekee. Kwenye uvuvi, Tanzania ina ukanda wa pwani wenye urefu wa kilomita 1,424. Vilevile, tunayo mito na maziwa makubwa ambayo yanafaa kwa uvuvi. Utalii ni sekta nyingine yenye fursa nyingi za uwekezaji, kwani nchi yetu inashika nafasi ya pili duniani kwa uwingi wa vivutio vya utalii. Tuna mbuga ya wanyama, Mlima Kilimanjaro, fukwe nzuri, nk. Halikadhalika, zipo fursa nyingi sana kwenye sekta ya kilimo, mifugo, viwanda, nk.

 

Ni wazi kwamba pamoja na utajiri mkubwa wa rasilimali na maliasili, changamoto kubwa inayolikabili Bara la Afrika ni ukosefu wa viwanda. Afrika haitaweza kupiga hatua endapo itaendelea kuwa muuzaji wa bidhaa ghafi na muagizaji wa bidhaa za viwandani. Kwa sasa, asilimia 60 ya mauzo ya nje kutoka nchi za Afrika ni mazao ghafi. Ni lazima Waafrika tufike hatua ambapo tutaweza kusindika na kuongeza thamani ya mazao yetu, ikiwemo mazao ya kilimo, madini, uvuvi, nk.

 

Hivyo basi, kwa kuwa marafiki zetu wa nchi za Nordic wamepiga hatua kiteknolojia, hususan teknolojia ya viwanda, tushirikiane kujenga viwanda vya kusindika na kuongeza thamani ya mazao yetu kwa manufaa ya pande zetu mbili. Tunataka tusindike pamba na kutengeneza nguo hapa Afrika; tunataka tuchimbe madini na kuyachenjua hapa hapa Afrika; tunataka tuvue samaki na kuwasindika hapa hapa Afrika. Africa must produce, process, consume and export finished products. Viwanda ni moja ya vipaumbele vyetu vikubwa, na washirika wetu wa maendeleo pamoja na wawekezaji wengine makini watuunge mkono kwenye mwelekeo huo.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa:

Ili kuvutia biashara na uwekezaji katika sekta mbalimbali, ni muhimu kwa nchi za Afrika kuweka mazingira muafaka, ikiwemo miundombinu wezeshi pamoja na kuondoa urasimu kwenye sheria na taratibu zetu za biashara na uwekezaji. Na hapa, naomba mnimruhusu nitaje baadhi ya jitihada ambazo tumefanya na tunaendelea kufanya hapa nchini ili kuvutia wawekezaji katika maeneo mbalimbali niliyoyataja hapo awali.

 

Moja ya jitihada tulizofanya ni kupitia na kurekebisha sheria na taratibu mbalimbali za uwekezaji nchini, ikiwa ni pamoja na kutengeneza sheria za kuwalinda wawekezaji. Vilevile, tumeanzisha Wizara mahsusi yenye dhamana ya Uwekezaji chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ili ijihusishe moja kwa moja na kurahisisha mazingira na uratibu wa uwekezaji nchini. Lakini muhimu zaidi, tunatekeleza Mkakati wa Kurekebisha na Kuboresha Mazingira ya Biashara nchini, yaani The Blueprint for Regulatory Reforms to Improve Business Environment. Jitihada zingine ni kutenga kanda maalum kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na kanda maalumu za uwekezaji, yaani Export Processing Zones and Special Economic Zones.

 

Sambamba na hayo, kwa kutambua umuhimu wa miundombinu wezeshi kama kichocheo cha biashara na uwekezaji, hivi sasa, tunajenga na kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, ikiwemo barabara, reli, usafiri wa majini na anga. Mathalan, hivi sasa tunajenga Reli ya Kisasa, yaani Standard Gauge Railway kwenye Ushoroba wa Kati yenye urefu wa kilomita 1,800 kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, ambayo baadaye itatuunganisha na nchi jirani za Rwanda na Burundi. Vile vile, tumelifufua Shirika letu la Ndege la ATCL na kuboresha viwanja vyetu vya ndege na kusimika rada za kuongozea ndege. Tunapanua na kuboresha bandari zetu za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga pamoja zilizopo kwenye Maziwa yetu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.

Na upanuzi huu unaenda sambamba na ujenzi wa meli na vivuko. Zaidi ya  hapo, tutakeleza Mradi mkubwa wa uzalishaji wa umeme wa maji kwenye Bonde la Rufiji utakaozalisha Megawati 2,115, na kuchangia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za uzalishaji wa bidhaa viwandani na kwenye sekta nyingine.

 

Kwa kuzingatia hayo yote, nitumie fursa hii adhimu kuwakaribisha ndugu na marafiki zetu wa nchi za Nordic, pamoja na mataifa mengine, yakiwemo ya Afrika, kuja kuwekeza nchini mwetu. Mazingira ya uwekezaji ni muafaka na yanatabirika, kutokana na amani na utulivu wetu kisiasa, lakini pia mwenendo wa ukuaji wa uchumi ni mzuri ambapo, kwa sasa, ni wastani wa asilimia 7. Zaidi ya hapo, sisi ni wanachama wa SADC na EAC, ambazo kwa pamoja zina idadi ya watu wapatao milioni 450.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:

 

Kwa kuhitimisha, nisisitize kwamba nchi za Afrika na Nordic zinahitajiana, kutokana na ukweli kwamba zipo fursa ambazo Afrika tunazo lakini wenzetu wa Nordic hawana na vivyo hivyo kwa Afrika. Hivyo basi, Mkutano wenu hauna budi kuja na mikakati mahsusi ya ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote. Our cooperation must be founded on a win-win principle. Nawatakia maazimio mema.

 

Asanteni kwa kunisikiliza!