Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEFU MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUFUNGA MKUTANO WA 39 WA WAKUU WA NCHI WA SADC DAR ES SALAAM, TAREHE 18 AGOSTI, 2019

Sunday 18th August 2019

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEFU MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO

WA TANZANIA WAKATI WA KUFUNGA MKUTANO

WA 39 WA WAKUU WA NCHI WA SADC

DAR ES SALAAM, TAREHE 18 AGOSTI, 2019

 

Mheshimiwa Emmerson Mnangagwa, Mwenyekiti

wa Taasisi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC;

 

Waheshimiwa Wakuu wa Nchi wa SADC mliopo;

 

Waheshimiwa Wake wa Viongozi mliopo;

 

Waheshimiwa Viongozi mnaowakilisha Nchi Wanachama;

 

Mheshimiwa Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu

wa Awamu wa Pili wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais

wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar n

a Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;

 

Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri

ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Rais wa Zanzibar;

 

Mheshimiwa Job Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri

ya Muungano wa Tanzania;

 

Waheshimiwa Mawaziri Wakuu Wastaafu wa Tanzania

 (Mzee John Malecela na Peter Pinda);

 

Mheshimiwa Tulia Ackson, Naibu Spika wa Bunge

la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Othmani Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;

 

Mheshimiwa Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri mliopo;

 

Waheshimiwa Mawaziri wengine mliopo;

 

Mheshimiwa Dkt. Stergomena Tax, Katibu Mtendaji

wa Sekretarieti ya SADC;

 

Waheshimiwa Wakuu wa Taasisi za Kikanda

na Kimataifa mliopo;

 

Waheshimiwa Mabalozi mliopo;

 

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama mliopo;

 

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;

 

Maafisa Waadamizi na Wajumbe wengine wa Mkutano;

 

Wageni Waalikwa Wote, Mabibi na Mabwana;

Naomba nianze kwa kutoa taarifa. Jana, baada ya kusoma sehemu ya Hotuba yangu ya Ukaribisho kwa Lugha ya Kiswahili; Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC walifurahi na kuvutiwa sana. Hivyo basi, tulipoenda tu kwenye Mkutano wetu wa Ndani, wote kwa pamoja na kwa kauli moja, walifanya uamuzi wa kukifanya Kiswahili kuwa Lugha Rasmi ya Nne ya SADC. Hii ndiyo sababu nimeamua kuhutubia kwa Kiswahili.

 

Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza Waheshimiwa Wakuu wa Nchi Wenzangu kwa uamuzi huu mkubwa na wa kihistoria, ambao pia unaendana na kumuenzi Baba wa Taifa letu, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kama mnavyofahamu, wakati wa uongozi wa Mwalimu Nyerere, Tanzania ilifanya kazi kubwa ya kusaidia harakati za ukombozi, hususan wa nchi za Kusini mwa Afrika.  Nchi yetu ilitenga maeneo mengi kwa ajili ya kuanzisha Kambi za Wapigania Uhuru kutoka ANC, FRELIMO, MPLA SWAPO, ZANU-PF, (Nachingwea, Mgagawa, Kongwa, Kaole, Dakawa na Mazimbu), nimefurahi hivi majuzi tu Mheshimiwa Rais Ramaphosa alienda kutembelea Mazimbu hivi karibuni. Lakini hata Mheshimiwa Rais Mnangagwa wa Zimbabwe alipokuja alikwenda Bagamoyo (Kaole) ambako alipata mafunzo ya kupigania uhuru.

 

Tanzania pia, wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, ilisaidia kuzuia jaribio la mapinduzi nchini Shelisheli lililopangwa kufanywa na Utawala wa Makaburu wa Afrika Kusini. Baada ya kuzimwa kwa jaribio hilo, Mtanzania, Marehemu Brigredia Jenerali Hassan Ngwilizi, aliongoza nchi hiyo kwa muda. Hii ni mifano michache tu ya mchango uliootolewa na Tanzania chini ya uongozi wa Baba wa Taifa. Na katika harakati zote hizo, lugha ambayo ilitumika sana ni Kiswahili. Hivyo basi, uamuzi wa kukifanya Kiswahili kuwa Lugha Rasmi ya SADC ni sahihi na muafaka katika kuenzi kazi zilizofanywa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.

 

Narudia tena kuwashukuru na kuwapongeza Waheshimiwa Wakuu wa Nchi na Serikali kwa uamuzi huu mkubwa na wa kihistoria. Kwa hakika, mmeingia kwenye vitabu vya historia. Vizazi na vizazi vitawakumbuka. Kama mnavyofahamu, lugha ni chombo muhimu katika kuimarisha mahusiano baina ya watu lakini pia katika kukuza na kuimarisha ushirikiano na utengamano kati na baina ya mataifa. Mwanasosholojia na Mtaalam wa Lugha Dkt. Joshua Fishman aliwahi kusema, napenda nimnukuu “…a common indigenous language in the modern nation states is a powerful factor of unity…it promotes a feeling of single community. Additionally, it makes possible the expansion of ideas, economic targets and cultural identity”, mwisho wa kunukuu.

 

Kiswahili ni lugha ya Kiafrika; na sisi ni Waafrika. Hivyo basi, nina imani kuwa uamuzi huu wa kukifanya Kiswahili kuwa Lugha Rasmi ya SADC utasaidia kuimarisha uhusiano miongoni mwa wananchi wetu na pia kukuza na kuimarisha ushirikiano na utengamano kati ya mataifa yetu. Na napenda nitumie fursa hii, kuzisihi Nchi Wanachama ambazo Kiswahili hakitumiki, kuiga mfano wa Afrika Kusini, ambayo kuanzia mwakani, wataanza kufundisha Kiswahili kwenye shule zao. Sisi Tanzania tutakuwa tayari kuwaunga mkono, ikiwemo kwa kutoa walimu na nyenzo mbalimbali za kufundishia. 

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

         Tupo hapa kwa ajili ya kuhitimisha Mkutano wetu. Kwa takribani siku mbili, tumekutana kujadili masuala mbalimbali yenye lengo la kuiletea maendeleo Jumuiya yetu. Napenda nitumie fursa hii kutamka kuwa, Mkutano wetu umekuwa wa mafanikio makubwa sana. Nasema hivyo, kwa sababu, kwanza, umefanyika kwenye mazingira ya utulivu, upendo, na maeleweno makubwa. Ni kweli, mara chache chache, kulikuwa na kutofautiana kwenye baadhi ya hoja, lakini tulijadiliana kwa urafiki mkubwa na hatimaye kuweza kufikia makubaliano.

 

Pili, Mkutano wetu ulikuwa wa mafanikio kwa sababu ya ajenda zenyewe tulizozijadili na maazimio tuliyoyafikia. Tumejadili ajenda nyingi na kufikia maamuzi makubwa, ambayo binafsi naamini, endapo yatatekelezwa, yataleta manufaa mengi kwenye Nchi Wanachama pamoja na Jumuiya yetu kwa ujumla.

 

Naomba, kwa haraka haraka, mniruhusu nitoe muhtasari wa baadhi ya masuala tuliyoyajadili na kuyafanyia maamuzi.

 

 

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Kama mnavyofahamu, Mkutano wetu umefanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Mazingira Wezeshi ya Biashara kwa ajili ya Kuwezesha Maendeleo Jumuishi na Endelevu ya Viwanda, Kukuza Biashara na Kuongeza Fursa za Ajira (A Conducive Environment for Inclusive and Sustainable Industrial Development, Increased Intra-Regional Trade and Job Creation)”. Kaulimbiu hii ni mwendelezo wa kaulimbiu za Mikutano ya Wakuu wa Nchi iliyofanyika Zimbabwe mwaka 2014; Botswana mwaka 2015, Eswatini mwaka 2016, Afrika Kusini mwaka 2017 na Namibia mwaka 2018; ambapo zote ziliweka mkazo kwenye utekelezaji wa Mkakati na Mpango Mwongozo wa Maendeleo ya Viwanda wa SADC wa Mwaka 2015 – 2063 (the SADC Industrialization Strategy and Roadmap 2015 – 2063).

 

Kaulimbiu ya mwaka huu imeweka msisitizo katika kuboresha mazingira ya biashara, ikiwemo kuondoa vikwazo vya mipakani, ukiritimba kwenye maamuzi, rushwa, n.k.; ili kukuza sekta ya viwanda na kustawisha biashara kwenye Ukanda wetu.  Ninayo furaha kuarifu kuwa Wakuu wa Nchi wamepitisha kaulimbi hiyo na kuilekeza Sekretarieti kusimamia utekelezaji wake na kisha kuwasilisha Ripoti kwenye Mkutano ujao wa SADC. Sambamba na hilo, kwa lengo la kukuza sekta ya viwanda kwenye Jumuiya yetu, Mkutano umezihimiza Nchi Wanachama kuendelea kutekeleza Mkakati na Mwongozo wa Maendeleo ya Viwanda wa SADC 2015 – 2063. Na kama mlivyoshuhudia, hivi punde, nchi zetu zimesaini Itifaki kuhusu Viwanda.

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Wakati wa Mkutano wetu pia tumepokea Ripoti za Mwaka za Mwenyekiti wa SADC anayemaliza muda wake na Ripoti ya Mwaka ya Mwenyekiti anayemaliza muda wake wa Taasisi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ). Wakuu wa Nchi wamewapongeza Wenyeviti hao, Mheshimiwa Rais Geingob na Mheshimiwa Rais Lungu, kwa kazi nzuri walizofanya katika wenye mwaka uliopita.

 

Wakuu wa Nchi pia wamekubaliana kuendelea kufuatilia suala la usalama nchini DRC; lakini pia wameitaka Falme ya Lesotho kuharakisha utungwaji wa sheria itakayoanzisha Mamlaka ya Kitaifa ya kusimamia Mabadiliko (National Reform Authority). Zaidi ya hapo, Wakuu wa Nchi wameiagiza Sekretarieti kuharakisha Uanzishaji wa Chombo cha SADC cha Kukabiliana na Majanga (SADC Disaster Preparedness and Response Mechanism) kitakachozisaidia Nchi Wanachama kukabiliana na majanga, kama vile mafuriko, ukame, njaa, vimbunga, magonjwa ya mlipuko, n.k.

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Sambamba na hayo, Wakuu wa Nchi walipitia hali ya uchumi kwenye Ukanda wetu. Na kama ambavyo nilieleza jana, kwa sababu ya majanga mbalimbali yaliyozikumba baadhi ya Nchi Wanachama pamoja na matatizo mbalimbali ya kiuchumi duniani, Uchumi wa Ukanda wetu ulishindwa kukua kama ilivyotarajia, kwa asilimia 7.0; badala yake ulikua kwa asilimia 3.1.  

 

Hivyo basi, Nchi Wanachama zimetakiwa kuendelea kuwekeza kwenye miundombinu na kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara; kwa kuwa ni mojawapo ya vikwazo kikubwa vya ukuaji uchumi kwenye Barani Afrika, ikiwemo kwenye Ukanda wa SADC. Zaidi ya hapo, tumekubaliana kuendelea kuboresha sera zetu za uchumi na fedha ili kuboresha mazingira ya ukuaji uchumi kwenye Ukanda wetu.

 

 Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Masuala mengine tuliyojadili ni pamoja na suala la upatikaaji mapato (resources mobilization), ombi la Burundi kujiunga na SADC pamoja na suala la vikwazo kwa Zimbabwe. Kuhusiana na suala la mapato, Mkutano umezipongeza nchi zilizokamilisha kutoa michango au ada zao za mwaka, na kuzihimiza zile ambazo bado, kufanya hivyo. Aidha, Mkutano umepitisha Mpango wa Kuongeza Mapato wa SADC (SADC Regional Resource Mobilization Framework), ambapo Nchi Wanachama zitakuwa na hiari ya kuchagua yenyewe njia bora ya kuchangia.

 

Nitumie fursa hii, kwa niaba ya Jumuiya, kuwashukuru washirika na wadau wetu wa maendeleo kwa kutuunga mkono kifedha na katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Kwenye Bajeti ya Mwaka 2019/2020 ambayo inafikia takriban Dola za Marekani milioni 74, washirika wetu wameahidi kuchangia takriban Dola za Marekani milioni 31, na kiasi kingine cha Dola za Marekani milioni 43 kitachangiwa na Nchi Wanachama.

 

Najua kwenye hadhira kama hii sio vizuri sana kutaja majina katika kutoa shukrani; maana upo uwezekano wa kuwasahau wengine. Hata hivyo, naomba mniruhusu nitaje baadhi ya washirika wetu ambao wamekuwa wakituunga mkono: Umoja wa Ulaya; Benki ya Dunia, Ujerumani, China, Sweden. Lakini, kwa namna ya pekee, napenda kuishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika pamoja na Global Fund  kwa kwa michango wanayotoa kwa nchi zetu na Jumuiya yetu; hususan katika kujenga miundombinu, kwa upande wa Benki ya Maendeleo ya Afrika; na kukabiliana na magonjwa ya UKIMWI, Malaria na Kifua Kikuu kwa upande wa Global Fund.

 

Nitoe wito kwa Sekretarieti kuendelea kujitahidi kutumia vizuri fedha zinazotolewa na Nchi Wanachama pamoja na Washirika wetu wa Maendeleo. Fedha hizo zitumike kwa malengo yalikusudiwa, na hasa katika kutekeleza miradi ya maendeleo; badala ya kutumika kwenye semina, warsha au mikutano. Kama mnavyofahamu, michango inayotolewa na Nchi Wanachama inatoka kwa wananchi masikini. Hivyo basi, ni lazima matumizi ya fedha yalete manufaa kwa wananchi hao masikini. Mathalan, binafsi, nitafurahi sana kama nitaona fedha nyingi tunazochangia zinaelekezwa katika kutekeleza miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa shule, vituo vya afya, au kufanya usanifu wa miradi ya miundombinu, ambayo italeta matokeo chanya hapo baadaye.

 

Nimeleza hivi punde kuwa kwenye Bajeti ya 2019/2020, Nchi Wanachama zitachangia Dola za Marekani milioni 43. Kama tutaamua angalau Dola za Marekani milioni 3 zitumike kwenye kutekeleza miradi ya maendeleo kama kujenga vituo vya afya, itakuwa na tija kubwa kwa wananchi. Hapa Tanzania, kwa mfano, gharama za kujenga kituo kimoja cha afya ni takriban Dola za Marekani laki mbili; hivyo katika Dola za Marekani milioni 3, unaweza kujenga vituo visivyopungua 15; na hivyo kuleta manufaa makubwa kwa wananchi wetu.

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Kuhusiana na ombi la Burundi, Mkutano umepokea taarifa kuhusu hatua iliyofikiwa ya nchi hiyo kuweza kujiunga. Hata hivyo, ilibainika kuwa, bado kuna maeneo ambayo hajakamilika vizuri. Hivyo basi, Mkutano umeiilekeza Sekretarieti kuiarifu Burundi kuhusu maeneo ambayo bado hajakamilika ili yafanyiwe kazi na hatimaye kuwezesha kutumwa tena kwa Timu ya Uchunguzi (verification mission). Kuhusu Zimbabwe, tumekubaliana kuwa tuendelee kujadiliana na kufanya mawasiliano na jumuiya ya kimataifa ili kuwezesha kuondolewa kwa vikwazo kwenye nchi hiyo, ikiwemo kupitia Mabalozi wetu waliopo sehemu mbalimbali duniani. Kwa ujumla, niseme tu kwamba, Viongozi wote wa SADC tumekubaliana na kutamka kwa kauli moja kwamba, tupo pamoja na Zimbabwe na kamwe hatutaiacha nchi hiyo.

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Mwanzoni mwa hotuba yangu nilieleza kuwa Mkutano wetu umekuwa wa mafanikio makubwa. Lakini nikiri kuwa, mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mkubwa kutoka kwa Nchi Wanachama wenyewe, Sekretarieti pamoja na wadau wengine mbalimbali. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kurudia tena kuwashukuru Waheshimiwa Wakuu wa Nchi kwanza kwa kuhudhuria Mkutano huu kwa wingi sana; lakini pili kwa michango yenu mizuri wakati wa majadiliano.

 

Napenda pia niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri pamoja na Maafisa wetu Waandamizi kwa kazi kubwa mliyoifanya ya kuandaa Mkutano wa Wakuu wa Nchi. Mmeturahisishia sana kazi yetu.  Kwa namna ya pekee, nawashukuru Watendaji wa Sekretarieti, wakiongozwa na Katibu wake Mtendaji mahiri, Dkt. Tax, kwa kufanya kazi kwa bidii, na bila kuchoka, wakati wa maandalizi, wakati wa Mkutano na mpaka muda huu tunapohitimisha. Hongereni na ahasanteni sana.

 

Nawashukuru pia wote waliofanya kazi nyuma ya pazia na kuwezesha kufanikisha Mkutano wetu. Navishukuru vyombo vya ulinzi na usalama, hususan kwa kuhakikisha usalama wa nchi na wageni wetu; nawashukuru wakalimani, vyombo vya habari, madereva, wahudumu, vikundi vya burudani na kadhalika.

 

Nawashukuru pia wageni wetu kutoka nchi mbalimbali. Tunawasihi sana, kama mnayo nafasi, msiondoke bila ya kutembelea vivutio tulivyo navyo. Kama mjuavyo, Tanzania ina vivutio vingi, ikiwemo visiwa vizuri vya marashi ya karafuu vya Zanzibar, Mlima Kilimanjaro, Mbuga za Serengeti na Ngorongoro. Hapa Tanzania pia ndio mahali penye mti mrefu zaidi Barani Afrika na pia Ziwa kubwa zaidi Barani Afrika, Ziwa Victoria.

 

Lakini pia, kwa wawekezaji, msiondoke bila kupata fursa ya kuwekeza. Tanzania ni mahali penye fursa nyingi za uwekezaji. Kwenye sekta za viwanda, kilimo, uvuvi, ufugaji, madini, gesi, nishati, utalii, n.k. Hivyo basi, nawasihi mchangamkie  fursa hizo.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Kabla ya kuhitimisha hotuba yangu, napenda kurudia tena kuwashukuru Waheshimiwa Wakuu wa Nchi kwa kuniamini na kunikabidhi jukumu la kuwa Mwenyekiti wenu. Nimelipokea jukumu hilo kwa uenyenyekevu mkubwa. Narudia tena kumpongeza Mwenyekiti anayemaliza muda wake, Mheshimiwa Rais Dkt. Geingob wa Namibia kwa kazi nzuri aliyoifanya katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Naahidi kuendeleza mambo yote mazuri aliyoyaanzisha.

 Napenda pia kumpongeza kaka yangu, Mheshimiwa Emmerson Mnangagwa, Rais wa Zimbabwe, kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Taasisi yetu muhimu ya kusimamia masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama (SADC Organ). Naahidi kushirikiana naye kwa karibu ili kuhakikisha amani, utulivu na usalama unatawala kwenye Jumuiya yetu.

 

Natambua kuwa katika kipindi chetu cha Uenyekiti, takriban nchi nne zinatarajiwa kufanya uchaguzi (Botswana, Msumbiji, Namibia na Mauritius). Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuzitakia nchi hizo uchaguzi mwema. Nina matumaini makubwa kuwa chaguzi hizo zitafanyika kwenye mazingira ya amani na utulivu mkubwa na kwa kuzingatia vigezo vya Jumuiya yetu.

 

Waheshimiwa Wakuu wa Nchi;

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Jana wakati wa kuwakaribisha nilieleza kuwa mwaka huu nchi yetu inaadhimisha miaka 20 tangu kufariki kwa Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kwa kuzingatia hilo, nawajibika kuhitimisha hotuba yangu, kwa kunukuu baadhi ya maneno yake ambayo aliyatoa mwaka 1997 wakati akihutubia Bunge la Afrika Kusini, alisema “Kila nchi inapaswa kutegemea raia wake na rasilimali ilizonazo katika kujiletea maendeleo. Hata hivyo, hiyo peke yake haitoshi. Ni lazima pia kushirikiana na nchi nyingine. Nchi zinaposhirikiana zinaongeza uwezo wa kujiletea maendeleo”, mwisho wa kunukuu. Kwa kutumia maneno hayo ya Baba wa Taifa letu, napenda kurudia tena kuwaomba Waheshimiwa Viongozi tushirikiane ili kuleta maendeleo kwenye nchi zetu na Jumuiya yetu kwa ujumla. Umoja wetu ndiyo nguvu yetu. Na katika hilo, nawaahidi kuwa, Tanzania ikiwa Mwenyekiti wa Jumuiya itashirikiana na Nchi zote Wanachama ili kufanikisha utekelezaji wa malengo na kuiletea maendeleo Jumuiya yetu.

 

Baada ya kusema, natamka kuwa Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi za SADC umefungwa rasmi. Nawatakieni wageni wetu wote safari njema wakati wa kurejea nyumbani.

 

Mungu Ibariki SADC!

 

Mungu Ibariki Afrika!

 

“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”.