Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,KWENYE MAADHIMISHO YA SIKUKUU YA WAFANYAKAZI DUNIANI, MBEYA, TAREHE 1 MEI, 2019

Wednesday 1st May 2019

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,KWENYE MAADHIMISHO YA SIKUKUU

YA WAFANYAKAZI DUNIANI, MBEYA, TAREHE 1 MEI, 2019

 

Ndugu Tumaini Nyamhokya, Rais wa Shirikisho

la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA);

 

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu

wa Rais wa Jamhuri ya Muungano

wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu

wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Job Ndugai, Spika wa Jamhuri

         ya Muungano wa Tanzania;

 

Mwakilishi wa Jaji Mkuu wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Tulia Ackson, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi,

Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi,

Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu;

 

Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri

wengine mliopo;

 

Mheshimiwa Albert Chalamila, Mkuu wa Mkoa

wa Mbeya pamoja na Wakuu wa Mikoa mingine mliopo;

 

Waheshimiwa Wabunge mliopo;

 

Ndugu Makatibu Mkuu na Naibu Makatibu Wakuu

 mliopo;

 

Jaji Mfawidhi wa Divisheni ya Kazi ya Mahakama Kuu pamoja na Waheshimiwa Majaji wengine mliopo;

 

Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani nchini;

 

Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri Tanzania;

 

Waheshimiwa Mabalozi mliopo;

 

Ndugu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya;

 

Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;

 

Ndugu Qambos Sulle, Makamu wa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi;

 

Dkt. Yahya Msigwa, Katibu Mkuu wa Shirikisho

la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA);

 

Viongozi Wengine mliopo wa Vyama Vishiriki vya TUCTA;

 

Viongozi Wengine wa Serikali mliopo;

 

Viongozi wa Vyama vya Siasa na Viongozi wa

Dini mliopo;

 

Ndugu Wafanyakazi Wenzangu;

Ndugu Wana-Mbeya, Mabibi na Mabwana:

Najisikia furaha kubwa sana, kwa mara nyingine tena, kuweza kushiriki Siku hii muhimu ya Wafanyakazi, ambayo huadhimishwa duniani kote kila mwaka. Napenda kwanza kabisa, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na kutuwezesha kuiona siku ya leo.

 

Aidha, kwa namna ya pekee, napenda kutoa shukrani zangu nyingi na za dhati kwa Uongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), wakiongozwa na Rais wa Shirikisho, Ndugu Tumaini Nyamhokya, kwa kunialika kuwa Mgeni Rasmi kwenye Maadhimisho haya. Leo ni mara yangu ya nne TUCTA wamenialika kuwa Mgeni Rasmi tangu nimekuwa Rais. Mialiko hiyo ni ishara kwamba, vyama vya wafanyakazi nchini, vinaiunga mkono Serikali ninayoiongoza. Ninawashukuru sana na napenda niwahakikishie kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nanyi katika kushughulikia masuala yenu pia kwa lengo la kusukuma mbele gurudumu la maendeleo katika Taifa letu.

 

Napenda pia kutumia fursa hii kuungana na wote walionitangulia kuzungumza kuwashukuru na kuwapongeza Waratibu wa shughuli hii, Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Huduma za Mtandao wa Mawasiliano Tanzania (TEWUTA) kwa maandalizi mazuri ya Sherehe hizi. Hongereni sana. Sherehe zimefana.

 

Vilevile, nawashukuru wenyeji wetu, wananchi wa Mbeya mkiongozwa na Mkuu wenu wa Mkoa, kwa makaribisho yenu mazuri na kwa kujitokeza kwenu kwa wingi kwenye Maadhimisho haya. Ahsanteni sana wana-Mbeya. Waswahili husema “shughuli ni watu”.

 

Nawashukuru pia Viongozi wengine wa Serikali ambao wamehudhuria Maadhimisho haya, wakiongozwa Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu; Mheshimiwa Spika na Naibu Spika, Waheshimiwa Mawaziri, Waheshimiwa Wabunge, Viongozi wa Ulinzi na Usalama, n.k. Uwepo wenu hapo unadhihirisha kuwa mnawapenda sana wafanyakazi.

 

Ndugu Wafanyakazi Wenzangu,

Mabibi na Mabwana;

Siku ya Wafanyakazi au maarufu Mei Mosi, ni siku ambayo dunia huitumia kuenzi na kutambua mchango unaotolewa na wafanyakazi katika kuleta maendeleo. Na hii ni kwa sababu, kama mjuavyo, maendeleo; katika ngazi yoyote ile, iwe mtu mmoja mmoja, familia, taasisi, au nchi; huwa ni matokeo ya kufanya kazi. Waingereza wana usemi usemao “all wealth is the product of labour” na mwingine unasema “Without labour, nothing prospers”. Hii yote ni katika kudhihirisha kuwa kazi na wafanyakazi ni muhimu sana katika kuleta maendeleo.

 

Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii, kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya Serikali na Watanzania wote; kuwapongeza wafanyakazi wote hapa nchini kwa kuungana na wafanyakazi wengine duniani katika kuadhimisha Siku hii muhimu. Aidha, nawapongeza kwa mchango wenu mkubwa mnaoutoa katika kuiletea maendeleo nchi yetu. Napenda niwahakikishie kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nanyi, ikiwa ni pamoja na kushughulikia changamoto zenu mbalimbali. Ni imani yangu kuwa mtaendelea kufanya kazi kwa bidii, kama Serikali ya Awamu wa Tano inavyosisitiza kuwa “Hapa Kazi tu”. Tukifanya kazi kwa bidii, tutafanikiwa katika lengo letu la kuiletea maendeleo nchi yetu.

 

Ndugu Wafanyakazi, Mabibi na Mabwana;

Hivi punde tumetoka kusikia Risala nzuri ya TUCTA iliyosomwa na Katibu wake Mkuu, Bwana Msigwa. Kupitia Risala hiyo, Katibu TUCTA ameipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali inazochukua katika kujenga miundombinu na kuboresha huduma za jamii. Aidha, Risala imetaja baadhi ya kero za wafanyakazi pamoja na kutoa mapendekezo yenye nia ya kuchochea ukuaji uchumi nchini.

 

Namshukuru Katibu Mkuu wa TUCTA kwa Risala hiyo nzuri; na leo napenda nimpongeze kwa kujitahidi kuisoma kwa muda mfupi. He was brief and very clear. Hongera sana. Napenda nikuhakikishie Ndugu Katibu Mkuu wa TUCTA pamoja na wafanyakazi wote nchini kuwa, Serikali imepokea Risala yenu na tunaahidi kuwa yote yaliyomo kwenye Risala, tutayafanyia kazi. Hata hivyo, naomba mniruhusu nizungumzie baadhi ya masuala machache yaliyomo kwenye Risala hiyo.

 

Ndugu Wafanyakazi, Mabibi na Mabwana;

Baadhi ya hoja zilizotolewa kwenye Risala ni pamoja na maombi ya kutaka Bodi za Mishahara kukutana; kupunguza viwango vya kodi kwa watumishi wote; suala la watumishi wa darasa la saba na uboreshaji wa mazingira na usalama sehemu za kazi.

 

Napenda niseme kuwa, binafsi, sina tatizo na Bodi za Mishahara kukutana; na kusema kweli, sielewi ni kwa nini hazikutani. Kwangu mimi hata wakitaka kukutana leo, sina shida. Hivyo basi, namwagiza Waziri mwenye Dhamana kuhakikisha Bodi hizo zinakutana. Hata hivyo, napenda kutoa angalizo kuwa vikao vyao visiwe kichochoro cha kutumia fedha za Serikali vibaya.

 

Kuhusu suala la kupunguza viwango vya kodi na lenyewe sina matatizo nalo. Kama tuliweza kushusha kodi kutoka asilimia 11 had asilimia 9 kwa watumishi wa kima cha chini; bado tunaweza kuendelea kujadiliana kwa ngazi nyingine. Jambo la msingi na muhimu kwa Viongozi wa TUCTA na wafanyakazi ni kutambua kuwa Serikali ina sababu za msingi za kutofautisha viwango vya kodi kulingana na madaraja ya mishahara.

 

Kuhusiana na suala la watumishi wa darasa la saba, napenda niwahakikishie kuwa, Serikali hii haina ubaguzi kwenye suala la ajira. Katika kuthibitisha hilo, kati ya Watumishi 525,506 ambao Serikali imeajiri nchi nzima, wenye elimu ya darasa la saba wapo 98,615.

 

  Kuhusu suala la uboreshaji wa Mazingira na Usalama sehemu za Kazi, natoa wito kwa waajiri wote kuhakikisha wanazingatia Sheria za Kazi, ikiwemo Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi. Aidha, Waajiri hawana budi kutekeleza matakwa mengine ya kisheria, ikiwemo kutoa mikataba ya ajira na pia kuruhusu uwepo wa vyama vya wafanyakazi sehemu zao za kazi. Kama mtakavyokumbuka, suala hili nimelieleza mara nyingi. Hivyo, kwa mara nyingine tena, naziagiza mamlaka husika kuhakikisha masharti hayo ya sheria yanatekelezwa.

Ndugu Rais wa TUCTA;

Ndugu Katibu Mkuu wa TUCTA;

Ndugu Wafanyakazi Wenzangu;

Sambamba na hayo, kama nilivyoeleza awali, kwenye Risala yenu mmetoa mapendekezo yenye nia ya kukuza uchumi na kuongeza fursa za ajira. Mmeshauri tuongeze bidii kwenye ujenzi wa viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini; kuongeza bidii katika kutangaza vivutio vyetu vya utalii; kusimamia vizuri masuala ya uchumi wa bahari, ikiwemo kununua meli ya mizigo itakayotoa huduma baharini, n.k.

 

Mapendekezo yenu yote ni mazuri; na tunakubaliana nayo kwa asilimia 100, japokuwa mengine, utekelezaji wake utategemea upatikanaji wa fedha. Hata hivyo, napenda niwaarifu kuwa, baadhi ya mapendekezo tumeanza kuyafanyia kazi. Mathalan, kuhusu uchumi wa bahari; tumeanza kuchukua hatua za kulifufua Shirika letu la Uvuvi (TAFIRI), ambapo marafiki zetu wa Japan na Korea, wameonesha nia ya kutuunga mkono. Na kuhusu ununuzi wa Meli ya Mizigo, hilo na lenyewe halina shida. Tumeshaanza kujenga meli mpya za mizigo Ziwa Nyasa; na tunaendelea na ujenzi wa meli nyingine Ziwa Victoria na Tanganyika. Tukishishamaliza huko, tutaelekeza nguvu zetu katika Bahari ya Hindi.

 

Kwa upande wa utalii, ninyi wenyewe ni mashahidi. Tunajitahidi sana kutangaza vivutio vyetu vya utalii, vikiwemo vilivyo kwenye Ukanda huu wa Nyanda za Juu Kusini; ambavyo kwa bahati mbaya, kwa muda mrefu vilikuwa havitangazwi. Na kutokana na jitihada tulizoanza kuzifanya, idadi ya watalii imeendelea kuongezeka. Mwaka juzi tulipokea watalii milioni 1.2; lakini mwaka jana tumepokea watalii milioni 1.5.

 

Hivi majuzi mmeshuhudia wenyewe tumepokea takriban watalii 1,000 kutoka Israel. Aidha, Bodi yetu ya Utalii imeingia makubaliano na Kampuni moja ya China kuleta watalii 10,000 kwa mwaka, ambapo kundi la kwanza la watalii 342 linatarajiwa kuwasili nchini tarehe 12 mwezi huu.

 

Lakini katika juhudi hizo hizo za kuvutia watalii wengi zaidi; na kwa kutambua kuwa watalii wengi husafiri kwa ndege; tunafanya upanuzi wa viwanja vya ndege 11 na tayari tumenunua ndege mpya 8 kwa mpigo. Juzi mmeona, kwa mara ya kwanza, ndege ya abiria imetua kwenye Uwanja wa Ndege wa Nduli, Iringa, baada ya Uwanja kufanyiwa matengenezo.

 

Ndugu Wafanyakazi, Mabibi na Mabwana;

Ni kweli pia kuwa, kutokana na jitihada mbalimbali tulizozifanya kwa kushirikiana na ninyi wafanyakazi, Serikali imeweza kuongeza ukusanyaji wa mapato. Kwa mfano, mapato ya kodi yameongezeka kutoka wastani wa shilingi bilioni 850 kwa mwezi mwaka 2015 hadi kufikia shilingi trilioni 1.3 hivi sasa. Mapato yasiyo ya kodi pia yameongezeka, na hasa baada ya kudhibiti wizi wa rasilimali zetu na pia kuyabana mashirika na kampuni kulipa gawio. Mathalan, mwaka jana, Wizara ya Madini ilipanga kukusanya maduhuli ya shilingi bilioni 190; lakini wakakusanya shilingi bilioni 301. Aidha, mashirika na kampuni zilitoa gawio la shilingi bilioni 717.56 kwa Serikali; kutoka shilingi bilioni 130.686 Mwaka 2014/2015.

 

Haya ni mafanikio makubwa, ingawa changamoto bado zipo. Na changamoto kubwa iliyopo ni kwamba, gharama za uendeshaji wa Serikali bado zipo juu. Kwa mfano, kila mwezi inatulazimu kutumia takriban shilingi bilioni 580 kulipa mishahara; na wakati huo huo tunatakiwa kulipa madeni ya mikopo ya nyuma, kutekeleza miradi ya maendeleo pamoja na kulipia OC. Hivyo, mnaweza kujionea wenyewe, ni kiasi gani kinabaki baada ya matumizi hayo.

 

Na hapo ndiyo tumekuwa tukijiuliza maswali mengi kuhusu namna ya kutumia kiasi hicho kinachobaki.  Tumekuwa tukijiuliza sana, kama ambavyo mkulima mwenye mbegu hujiuliza wakati wa njaa. Je, azitumie mbegu zake kwa chakula na baada ya muda mfupi arudi tena kwenye njaa; ama azitunze kusubiri msimu wa mvua ili azipande na kumletea mavuno mengi. Tumekuwa pia tukijiuliza kama ambavyo mfanyabiashara hujiuliza wakati wa mtikisiko wa kiuchumi au biashara; je, autumie mtaji wake wote kutatua shida alizonazo kwa wakati huo, ama atafute biashara au shughuli nyingine itakayomwongezea mapato. Tumekuwa tumejiuliza sana maswali hayo.

 

Na kama nilivyoeleza kwenye Sherehe za Mei Mosi mwaka jana, baada ya kutafakari kwa kina, sisi mliotupa dhamana ya kuwaongoza, tuliona ni busara tutumie kiasi kidogo tunachobakiwa nacho kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo itakayosisimua na kuchochea uchumi shughuli za kiuchumi. Shughuli ambazo zitasaidia kuongeza fursa za ajira na kukuza uchumi kwa kasi.

 

Ni kwa kuzingatia hayo yote, tuliamua kutumia fedha inayobaki kuanza kujenga reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kwa gharama ya shilingi trilioni 7.026. Tunajenga pia barabara; na napenda nitumie fursa hii kuwaarifu kuwa, jana Benki ya Maendeleo ya Afrika imeidhinishia nchi yetu mkopo wa shilingi bilioni 415.3 kwa ajili ya kujenga barabara ya mzunguko ya njia nne katika Jiji la Dodoma yenye urefu wa kilometa 110.

 

 Zaidi ya hapo, tumeamua kukarabati na kujenga meli mpya kwenye Maziwa yetu Makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa kwa takriban shilingi bilioni 287.9 na pia tunapanua Bandari zetu kuu tatu za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga kwa zaidi ya shilingi trilioni 1.2. Tunafanya upanuzi wa viwanja vya ndege 11 na tumenunua ndege mpya 8. Aidha, tunatekeleza mradi mkubwa wa umeme katika Bonde la Mto Rufiji ambao utagharimu zaidi ya shilingi trilioni 6.5.

 

Ni imani yetu kuwa, miradi hii yote itakapokamilika, itarahisisha na kupunguza gharama za usafiri na upatikanaji wa nishati ya umeme; na hivyo, kuchochea shughuli za kiuchumi, ikiwemo viwanda, kilimo, biashara, uvuvi, ufugaji, utalii, uchimbaji madini. Na hayo yakitokea, uchumi wetu utaimarika na mapato ya Serikali yataongezeka.

 

Ndugu zangu Wafanyakazi, sambamba na kutekeleza miradi hiyo ya miundombinu, tunaendelea kuimarisha na kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu za jamii, hususan elimu, afya na maji. Kwa mfano, kwa upande wa afya, tunajenga Hospitali za Wilaya 67 kwa gharama ya shilingi bilioni 105, tumekarabati vituo vya afya 352 kwa shilingi bilioni 184.67 na kuzipatia vifaa vyenye thamani ya shilingi bilioni 41.6. Tumeongeza pia bajeti ya afya kutoka shilingi bilioni 31 hadi shilingi bilioni 270. Kwenye elimu nyote mnafahamu kwamba tunatoa elimu bila malipo, tunajenga miundombinu na tumeongeza mikopo ya vyuo vikuu.

 

Kwa upande wa maji, tunayo miradi mingi mikubwa tunaitekeleza, ikiwemo Mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenye miji ya Nzega, Igunga, Tabora na Sikonge pamoja na mradi mwingine katika Jiji la Arusha, ambayo kwa pamoja tunatumia zaidi ya shilingi trilioni 1.  Zaidi ya hapo, tumepata mkopo kutoka India wenye thamani ya shilingi trilioni 1.2 kwa ajili ya miradi ya maji kwenye miji 28, ambapo Mkoa wa Mbeya umepata miradi miwili yenye thamani ya shilingi bilioni 22.5. Tunatekeleza pia miradi ya kusambaza umeme vijijini.

 

Ni wazi kuwa uboreshaji huu wa huduma hizi muhimu za jamii utasaidia kupunguza gharama za maisha kwa Wafanyakazi na Watanzania kwa ujumla. Hii ni kwa sababu huduma za maji, afya na elimu sasa zinapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu.

 

Ndugu Viongozi wa TUCTA;

Wafanyakazi Wenzangu;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Kwa kutekeleza miradi hiyo ya maendeleo na kuboresha huduma za jamii, haina maana kuwa tumeacha kushughulikia masuala ya maslahi ya wafanyakazi. La hasha! Tumeendelea kuyashughulikia. Mathalan, baada ya kukamilisha zoezi la uhakiki wa wafanyakazi hewa na wenye vyeti feki, tangu Mwaka wa Fedha uliopita, tumeanza kutoa nyongeza ya mwaka ya mshahara (annual increment) kwa watumishi 505,985 kwa gharama ya shilingi bilioni 72.8 ambapo shilingi bilioni 37.2 zimelipwa kwa walimu 270,878 na kiasi kingine cha shilingi bilioni 35.7 kwa watumishi wengine wapatao 235,107.

 

Mbali na nyongeza ya mwaka ya mshahara, kuanzia mwezi Novemba 2015, tumelipa malimbikizo ya mishahara yenye thamani ya shilingi bilioni 75.5 kwa watumishi 50,386. Kati yao, walimu ni 28,115 na wamelipwa shilingi bilioni 27.9. Vilevile, tumelipa shilingi bilioni 9.5 kwa watumishi wastaafu 1,829, ambao nao walikuwa wakiidai Serikali.

 

Ndugu Wafanyakazi wenzangu, miongoni mwa mabango ya Mei Mosi mwaka huu, mojawapo limeandikwa “tupandishe madaraja ili na sisi tupande bombardier”. Napenda niwaarifu kuwa, tangu mwezi Novemba 2015, tumewapandisha madaraja/vyeo watumishi 118,989 kwa gharama ya shilingi bilioni 29.5, ambapo walimu ni 75,502 na wamelipwa shilingi bilioni 16.3 na watumishi wasio walimu ni 43,487 na wamelipwa shilingi bilioni 13.2. Kwenye Mwaka ujao wa Fedha, tumepanga kuwapandisha vyeo watumishi 193,116. Sambamba na hayo, tumelipa madai mbalimbali yasiyo ya mishahara yenye thamani ya shilingi bilioni 291.3. Na mengi ya madai hayo, yalikuwepo kwa zaidi ya miaka 10.

 

Kama mlivyoona, kwenye maeneo mengi nimeamua kutofautisha kati ya watumishi walimu na wasio walimu, kwa kuwa walimu ni zaidi ya asilimia 50 ya watumishi wote Serikali.

 

Ndugu zangu Wafanyakazi;

Ukiachilia mbali hayo niliyoyaeleza, Serikali imelipa kiasi cha shilingi trilioni 1.5 kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Kabla ya kulipa fedha hizo, Mifuko hiyo ilikuwa ikidai Serikali kiasi cha shilingi trilioni 1.6 kwa kushindwa kupeleka michango ya watumishi wake tangu mwaka 2013. Hii iliifanya Mifuko ishindwe kulipa mafao ya wastaafu. Lakini baada ya kulipa deni hilo sasa wanawalipa wastaafu.

 

Lakini, kama mtakavyokumbuka, kufuatia uamuzi wa Serikali kuunganisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, liliibuka sekeseke kubwa kuhusu kikokotoo kipya kilichopendekezwa. Wafanyakazi wengi hawakuunga mkono kikokotoo hicho. Hivyo, baada ya kutafakari kwa kina, ilibidi tuchukue uamuzi mgumu wa kuendelea na kikokotoo cha zamani. Nasema ulikuwa uamuzi mgumu kwa vile, kikokotoo hicho kinachotumika nchini hakitumiki mahali kokote duniani. Ni sisi tu ndiyo wenye kukitumia. Hata kwenye nchi zilizoendelea hawakitumii. Na hii ndiyo sababu, Mifuko yote mitano ya Hifadha ya Jamii ilikuwa kwenye hali ngumu kiuchumi. Na hali hiyo ilichangiwa zaidi na Mifuko hiyo kujiingiza kwenye miradi isiyo na tija. Hata hivyo, kutokana na kilio cha wafanyakazi, tuliamua kuubeba mzigo huo mzito ili kuwalinda wafanyakazi wetu.

 

Masuala mengine ambayo Serikali imefanya kwa wafanyakazi ni pamoja na kujenga nyumba za walimu 11,078 na za watumishi wa afya 301. Zaidi ya hapo, baada ya kukamilisha zoezi la uhakiki, tumeajiri watumishi wapya 42,735 ambao kwa mwezi wanalipwa shilingi bilioni 25.8. Aidha, kwenye Mwaka wa Fedha 2019/2020 tumepanga kuajiri watumishi wengine wapya wapatao 45,000. Zaidi hayo, miradi ya miundombinu tunayoitekeleza (reli, umeme, viwanja vya ndege, barabara, n.k.) imetengeneza ajira nyingine nyingi.

 

Haya yote yanadhihirisha kuwa Serikali inawapenda sana Wafanyakazi. Hivyo basi, nawasihi wafanyakazi kuendelea kuchapa kazi kwa bidii ili kuiletea maendeleo nchi yetu. Wazee wetu wa zamani walijitoa mhanga kuikomboa nchi yetu kisiasa, ni jukumu letu kizazi cha sasa, kujitoa mhanga kuikomboa nchi yetu kiuchumi.

 

 

 

 

 

 

Ndugu Viongozi wa TUCTA;

Wafanyakazi Wenzangu;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Mei Mosi mwaka huu inasema: “Tanzania ya Uchumi wa Kati inawezekana, Wakati wa Mishahara na Maslahi Bora kwa Wafanyakazi ni Sasa”. Na kutokana na kaulimbiu hiyo, Katibu Mkuu wa TUCTA amenikumbusha kuhusu ahadi yangu niliyoitoa mwaka jana, wakati wa Sherehe kama hizi zilizofanyika Iringa; kwamba, kabla sijaondoka madarakani, nitaongeza mshahara.

 

Napenda, kwanza, nimkumbushe Katibu Mkuu wa TUCTA kuwa bado sijaondoka madarakani. Aidha, kama nilivyoeleza, kutokana na hatua tulizochukua na tunazoendelea kuzichukua, uchumi wa nchi yetu umeanza kuimarika. Halikadhalika, miradi mingi tunayoitekeleza imeanza kuwanufaisha Watanzania, wakiwemo Wafanyakazi. Hivyo basi, nitumie fursa kuwasihi Wafanyakazi nchini kuendelea kuwa na moyo wa subira, maana subira yavuta heri. Waingereza husema “Before the reward there must be labour. You plant before you harvest”.

 

 

Ndugu Viongozi wa TUCTA;

Wafanyakazi Wenzangu;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Napenda kuhitimisha kwa kurudia tena kuwashukuru Viongozi wa TUCTA kwa kunialika. Aidha, nawashukuru kwa ushirikiano mkubwa mnaoutoa kwa Serikali. Hatuna budi kuendeleza ushirikiano huu.

 

  Nawashukuru pia wageni wetu walioungana nasi kwenye Maadhimisho haya, wakiwemo Waheshimiwa Mabalozi. Lakini, kwa namna ya pekee, namshukuru Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani kwa kushiriki kwenye Maadhimisho haya. Napenda nimhakikishie kuwa Tanzania itaendelea kuheshimu Mikataba yote ya Kimataifa inayohusu masuala ya kazi, ambayo tumeisaini na kuiridhia.

 

Mwisho lakini sio kwa umuhimu, narudia tena kuwashukuru wana-Mbeya kwa kujitokeza kwa wingi kwenye Maadhimisho haya. Nawasihi mwendelee kuchapa kazi kwa bidii tukikumbuka kuwa “Hapa Kazi tu” ndiyo kaulimbiu yetu kuu katika Awamu hii ya Tano.

 

Mungu Wabariki Wafanyakazi wa Tanzania!

Mungu Ibariki Tanzania!

“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”