Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE HAFLA YA UZINDUZI WA DARAJA LA JUU (FLYOVER) KATIKA MAKUTANO YA BARABARA ZA MANDELA NA NYERERE ENEO LA TAZARA, TAREHE 27 SEPTEMBA, 2018

Thursday 27th September 2018

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE HAFLA

YA UZINDUZI WA DARAJA LA JUU (FLYOVER) KATIKA MAKUTANO YA BARABARA ZA MANDELA NA NYERERE

ENEO LA TAZARA, TAREHE 27 SEPTEMBA, 2018

 

Mheshimiwa Elias Kwandikwa, Naibu Waziri

wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano;

 

Mheshimiwa Paul Makonda,

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;

 

Mheshimiwa Masaharu Yoshida,

Balozi wa Japan nchini;

 

Mheshimiwa Bashiru Ally,

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi;

 

Mheshimiwa Mama Kate Kamba,

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam;

 

Mheshimiwa Selemani Kakoso, Mwenyekiti

wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu;

 

Waheshimiwa Wabunge wengine mliopo;

Mwakilishi wa JICA nchini Tanzania;

Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama mliopo;

Ndugu Viongozi wengine na Wafanyakazi wa Wizara

ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano;

 

Viongozi wa Vyama vya Siasa na Dini mliopo;

Waheshimiwa Wageni Wote Waalikwa;

Ndugu Wana-Dar es Salaam;

Mabibi na Mabwana:

Kwanza kabisa, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa. Lakini, kama mjuavyo, wiki iliyopita, Taifa letu lilipatwa na simanzi kubwa kufuatia ajali ya kuzama kwa Kivuko cha Mv. Nyerere iliyosababisha vifo vya Watanzania wenzetu takriban 230. Kwa heshima ya marehemu hao, naomba sote tusimame ili tuweze kuwakumbuka kwa dakika moja. Roho za marehemu wetu zipumzike mahali pema peponi. Amina. Napenda, kwa mara nyingine tena, kutoa pole nyingi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao. Aidha, nawaombea majeruhi wote wapone haraka.

 

Nawashukuru pia marafiki zetu kutoka nchi mbalimbali ambao wametutumia salamu za rambirambi na pole kufuatia ajali iliyotokea. Salamu zao, kwa hakika, zimetufariji sana. Tunawashukuru. Lakini, kwa namna ya pekee kabisa, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Watanzania wote kwa mshikamano mkubwa mlioonesha tangu kutokea kwa ajali hiyo mpaka sasa. Hongereni sana. Natambua kuwa wengi wetu bado tupo kwenye huzuni na simanzi kubwa; hata hivyo, hatuna budi kuendelea na kazi ya kulijenga Taifa letu. Hivyo ndivyo, hata Vitabu vyetu Vitakatifu vinatufundisha.

 

Lakini napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa Watanzania wenzangu, tutumie ajali iliyotokea kujitafakari kwa kina kwa lengo la kujifunza. Kila mmoja wetu ajitafakari. Viongozi wenye dhamana ya kusimamia vyombo vya usafiri watafakari na kujifunza. Watendaji wanaosimamia usafiri pia watafakari. Na halikadhalika, wananchi ambao ndio watumiaji wakubwa wa vyombo vya usafiri nao wanapaswa kujitafakari. Nina imani kuwa, kama sote tutatafakari vizuri na kuweza kujifunza, ajali kama hizi zitaepukika; na endapo zitatokea, basi madhara yake hayatakuwa makubwa sana.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Tupo hapa kushuhudia Uzinduzi wa Daraja la Juu (flyover) hapa TAZARA. Napenda kumshukuru Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Kamwelwe, kwa kunialika kushuhudia tukio hili la maendeleo na historia kwa nchi yetu. Hii ni “flyover” ya kwanza kabisa kujengwa hapa nchini. Hivyo basi, nasema “ahsante sana Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi kwa kunialika”.

 

Mtakumbuka kuwa takriban miezi 29 iliyopita, tarehe 16 Aprili 2016 nilikuja hapa kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Daraja hili la Juu. Leo nimekuja tena hapa kwa ajili ya kulizindua. Kwa hakika, nimefurahi sana.  Kama mjuavyo, Daraja hili ni moja ya ahadi za CCM kwenye Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015. Hivyo, kukamilika kwake, ni uthibitisho kuwa CCM ikiahidi jambo, inalitekeleza. Nimefurahi sana kuona kwenye Hafla hii wenye Ilani yao pia wapo. Hongereni sana Wana-CCM kwa kuweza kutimiza ahadi hii.

Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;

Kama walivyosema walionitangulia kuzungumza, Daraja hili, mbali na kurahisisha usafiri na kupunguza kero ya foleni barabarani, litasaidia kuzuia upotevu mkubwa wa fedha. Utafiti uliofanyika mwaka 2013, ulibainisha kuwa nchi yetu ilikuwa ikipoteza takriban shilingi bilioni 400 kwa mwaka kwa sababu ya msongamano wa magari barabarai. Zaidi ya hapo, Daraja hili litapendezesha mandhari ya Jiji la Dar es Salaam, ambalo ni miongoni mwa Majiji yanayokua kwa kasi Barani Afrika.

 

Hivyo basi, nitumie fursa hii kumpongeza Mkandarasi, Kampuni  ya Sumitomo Mitsui Construction ya Japan iliyoshirikiana na Kampuni ya Mak Contractor ya Tanzania kwa kukamilisha mradi huu mapema. Daraja hili lilipangwa kukamilika tarehe 30 Oktoba 2018. Lakini, limekamilika mapema mwezi huu (Septemba). Hongera sana Wakandarasi pamoja na Wahandisi Washauri, Kampuni ya The Consortium of Oriental Consultants Global Ltd na Eight – Japan Engineering Consultants Inc. ya Japan.

 

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Napenda pia kutumia fursa hii kuishukuru Serikali ya Japan kwa kutuunga mkono katika kutekeleza mradi huu. Daraja hili limegharimu takriban shilingi bilioni 106.965. Sehemu kubwa ya fedha hizo zimetolewa na marafiki zetu wa Japan; na kiasi kingine kimechangiwa na Serikali yetu. Tunawashukuru sana marafiki zetu hawa wa Japan. Na niseme tu kwamba, Japan ni marafiki zetu wa kweli na tena wa muda mrefu. Tumeshirikiana nao katika kutekeleza miradi mingi ya maendeleo: kwenye sekta za miundombinu ya usafiri na nishati ya umeme; elimu; afya; kilimo; maji; ujenzi; n.k. Tunawashukuru sana. Nimefurahi kumwona Balozi wa Japan nchini, Mheshimiwa Yoshida, yupo hapa. Tunakushukuru sana Mheshimiwa Balozi kwa kuja kuungana nasi katika tukio hili. Tunakuomba utufikishie shukrani zetu nyingi kwa Waziri Mkuu, Serikali pamoja na wananchi wa Japan.

 

Natambua kuwa siku chache zijazo utarejea nyumbani baada ya kumaliza muda wako hapa nchini. Tunaomba ukaendelee kuwa Balozi wetu. Na katika hili, nikuombe sana Mheshimiwa Balozi utusaidie kuikumbusha Serikali yako kuhusu ahadi iliyotoa ya kutusaidia kujenga Barabara ya Morocco – Mwenge; Daraja la Juu pale eneo la Gerezani pamoja na Barabara za Mzunguko (Ring – Roads) kule Dodoma. Watanzania tunasubiri kwa hamu kuona utekelezaji wa miradi hiyo.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Napenda pia kutumia fursa hii kuipongeza Wizara ya Ujenzi pamoja na TANROADS kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa Mradi huu. Nampongeza Prof. Mbarawa, ambaye wakati ujenzi wa Daraja hili unaanza, alikuwa Waziri wa Ujenzi. Lakini, kwa namna ya pekee kabisa, nampongeze Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale ambaye ameshiriki kikamilifu katika kubuni, kuandaa mchoro na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Daraja hili. Hongera sana Mhandisi Mfugale na wote ulioshirikiana nao.

Mengi tayari yameelezwa kumhusu Mhandisi Mfugale. Binafsi namfahamu sana. Nimefanya naye kazi kwa karibu wakati nikiwa Waziri wa Ujenzi. Najua uchapa kazi wake, uzalendo alionao, pamoja na uaminifu na ubunifu. Mbali na Daraja hili la Juu, ameshiriki pia katika kubuni michoro ya madaraja mengine makubwa nchini, ikiwa ni pamoja na Daraja ya Mkapa, Umoja, Kikwete, Magufuli kule Kilombero, n.k. Lakini zaidi ya sifa hizo zilizotajwa, Mhandisi Mfugale pia ni mtu muadilifu sana. Na kutokana na uadilifu wake, kuna wakati alikaribia kufukuzwa kazi.

 

Ni kwa kutambua na kuthamini mchango wake, nilipendekeza na nafurahi Wizara ilinikubali, kuliita Daraja hili la Juu hapa Tazara jina  la Mhandisi Mfugale. Hivyo, kuanzia sasa hapa pataitwa Mfugale Flyover. Ni matumaini yangu kuwa hatua hii itatoa hamasa kwa Watanzania wengine kufanya kazi kwa kujituma, uadilifu na kuweka maslahi ya Taifa mbele. Na napenda kutumia fursa kuwasihi sana Watanzania, hususan wataalam wetu, kuiga mfano wa Mhandisi Mfugale. Wapo baadhi ya wataalam wetu sio wazalendo. Wanakubali kutumika katika kukwamisha maendeleo ya nchi yetu. Hii ni aibu kubwa sana.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Ujenzi wa Daraja hili la Juu ni moja ya mikakati mingi inayotekelezwa na Serikali ya kutatua tatizo la msongamano wa magari na kuliboresha Jiji letu la Dar es Salaam. Kama mnavyokumbuka, mwaka Juzi (2016) tulizindua Daraja la Nyerere (Kigamboni) na Mradi wa Magari ya Mwendokasi (BRT). Mwaka jana tuliweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Daraja la Pete/Mpishano (interchange) pale Ubungo, ambalo ujenzi wake unaendelea. Mwaka huu pia tumeanza ujenzi wa barabara ya njia sita kutoka Kimara Mwisho hadi Kiluvya na pia Ujenzi wa Daraja la Salender. Aidha, ujenzi wa Miundombinu ya Mabasi ya Mwendokasi Awamu ya Pili kutoka maeneo ya Kariakoo kwenda Mbagala unatarajiwa kuanza Mwaka huu wa Fedha; pamoja na Madaraja mengine ya Juu katika maeneo ya Chag’ombe, Uhasibu na Magomeni. Na kama mnavyofahamu, upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam pamoja na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere nao unaendelea.

 

Zaidi ya hapo, kupitia Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (Dar es salaam Metropolitan Development Project - DMDP), Serikali imeanza ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 210 katika Wilaya zote za Jiji la Dar es Salaam. Ninyi wananchi ni mashahidi, hivi sasa kuna barabara nyingi zinajengwa kwenye mitaa yetu. Na Mradi huu wa DMDP utahusisha pia ujenzi wa mifereji ya kuzuia mafuriko yenye urefu wa kilometa 40 (ikiwemo katika Bonde la Mto Msimbazi); kujenga masoko na stendi, mifumo ya maji taka, n.k. Miradi hii inatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 660. Nina imani kuwa miradi hii yote itakapokamilika, Jiji la Dar es Salaam litazidi kupendeza na kuwa la kisasa zaidi. Lakini, katika kuongeza ufanisi kwenye utadaji kazi, napenda kuiagiza TAMISEMI kuuhamishia TARURA Mradi huu wa DMDP.

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Napenda nihitimishe hotuba yangu kwa kurudia tena kuwashukuru na kuwapongeza wote walioshiriki katika ujenzi wa Daraja hili. Naishukuru Serikali ya Japan. Nawapongeza Wakandarasi na Wahandisi Washauri wa Mradi. Naipongeza Wizara ya Ujenzi. Naipongeza TANROADS, hususan Mtendaji wake Mkuu, Mhandisi Mfugale. Na mwisho lakini sio kwa umuhimu, nawapongeza Watanzania wote kwa kufanikisha ujenzi wa mradi huu.

 

Wito wangu kwa viongozi, watendaji na wananchi, tulitunze Daraja hili. Na katika hili, naiagiza Wizara kuhakikisha inafunga kamera kwenye daraja hili na kwenye miundombinu mingine ya namna hii tuliyoijenga ili kudhibiti vitendo vya uharibifu wa miundombinu yetu.

 

Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kutekeleza jukumu lililonileta la Kuzindua Daraja hili la Mfugale hapa TAZARA.

 

Mungu Libariki Daraja hili!

 

Mungu Wabariki Wana-Dar es Salaam!

 

Mungu Ibariki Tanzania!

 

“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”