Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE UZINDUZI WA MAKTABA YA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM KAMPASI YA MLIMANI TAREHE 27 NOVEMBA, 2018

Tuesday 27th November 2018

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE UZINDUZI WA MAKTABA YA CHUO KIKUU

CHA DAR ES SALAAM KAMPASI YA MLIMANI

TAREHE 27 NOVEMBA, 2018

 

Mheshimiwa Jaji Mstaafu Damian Lubuva, Mwenyekiti

wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;

 

Mheshimiwa Prof. Ibrahimu Juma,

Jaji Mkuu wa Tanzania;

 

Waheshimiwa Mawaziri Wakuu Wastaafu,

Mzee Joseph Warioba na Mzee Edward Lowasa;

 

Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu,

Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi;

 

Waheshimiwa Mawaziri wengine mliopo;

 

Mheshimiwa Wang Ke, Balozi wa China nchini;

 

Mheshimiwa Paul Makonda,

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;

 

Mheshimiwa Peter Serukamba, Mwenyekiti

wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii

pamoja na Wabunge wengine mliopo;

 

Waheshimiwa Mabalozi mliopo;

 

Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;

 

 

Prof. William Anangisye, Makamu Mkuu wa Chuo

Kikuu cha Dar es Salaam;

 

Viongozi wengine wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;

 

Waheshimiwa Viongozi wengine wa Serikali mliopo;

 

Ndugu Wana-Jumuiya wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

(Wahadhiri, Watumishi na Wanafunzi);

 

Wageni wote Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

 

Napenda, kwanza kabisa, kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha tukutane hapa. Aidha, namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Prof. Ndalichako, pamoja na uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kunialika kuzindua Maktaba hii, ambayo ni kubwa na ya kisasa kwa nchi za Afrika zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara. Nawashukuru sana kwa mwaliko wenu.

 

Leo ni mara yangu ya tano kufika kwenye Chuo Kikuu hiki tangu nimechaguliwa kuwa Rais. Nilifika mara ya kwanza kuweka Jiwe la Msingi la Maktaba hii. Kisha nilikuja kukagua ujenzi wa Hosteli zenu. Baadaye nikaja kuzizindua. Mwezi huu mwanzoni mlinialika kuhudhuria Mdahalo. Hivyo, leo ni mara ya tano. Ahsanteni sana wana-Jumuiya wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hiki ni Chuo Kikuu kikongwe nchini, hivyo, nimekuwa nikifurahi sana kufika hapa. Na nashukuru, mara zote mmekuwa mkinipokea vizuri. Hata hivyo, napenda kusema kuwa, mimi navipenda vyuo vyote nchini. Hii ni kwa sababu, vyuo vyote ni vyangu.

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Tupo hapa kuzindua Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyojengwa kwa ufadhili wa marafiki zetu wa China kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 41.28, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 90. Kama mlivyosikia, Maktaba hii ni kubwa na ya kisasa kwa nchi za Afrika zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara. Ina Jengo la Maktaba lenye uwezo wa kuhudumia wasomaji 2,100; eneo la makasha yenye uwezo wa kuweka vitabu laki nane; eneo la kusomea lenye kompyuta 160, ukumbi wa mikutano wa kukaa watu 600. Aidha, mradi huu umejumuisha Jengo la Taasisi ya Confucius inayofundisha lugha na tamaduni za Kichina kwa ajili ya wanafunzi wa Chuo hiki pamoja na Watanzania wengine.

 

Napenda kutumia fursa kumpongeza Mkandarasi aliyejenga Maktaba hii, Kampuni ya Jiangsu Jiangdu kutoka China kwa kukamilisha mradi huu kwa wakati; na kwa viwango vya hali ya juu sana. Kwa hakika, jengo linapendeza sana. Hongereni sana. Aidha, kama nilivyosema wakati wa kuweka Jiwe la Msingi, mradi huu ulipatikana wakati wa uongozi wa Awamu ya Nne. Hivyo, sisi wengine tumekuja kusimamia utekelezaji wake tu. Hivyo basi, kwa dhati kabisa, napenda kurudia tena kumshukuru na kumpongeza Rais wa Awamu ya Nne, Mzee Kikwete, pamoja na watendaji wote waliofanikisha kupatikana kwa Mradi huu. Tunawashukuru sana.

 

Kwa namna ya pekee kabisa, napenda kutoa shukrani zangu nyingi kwa marafiki zetu wa China kwa kutujengea Maktaba hii kubwa, nzuri na ya kisasa. Ahsanteni sana marafiki zetu wa China. Na niseme tu kwamba, China wamekuwa marafiki wa kweli wa nchi yetu kwa muda mrefu. Uhusiano huu uliimarika zaidi kutokana na urafiki uliokuwepo kati ya waasisi wa Mataifa yetu mawili, yaani Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na Mwenyekiti Mao Zedong. Kupitia viongozi hao wawili, nchi zetu mbili zimekuwa zikishirikiana kwenye mambo mengi katika nyanja za kitaifa na kimataifa; ambapo sisi Tanzania tumenufaika na misaada mingi kutoka China. Jambo la kufurahisha ni kwamba, misaada kutoka China haina masharti. Wenyewe wakiamua kukupa, wanakupa tu. Walitujengea TAZARA, Kiwanda cha URAFIKI; lakini pia tunashirikiana nao kwenye nyanja afya, elimu, maji, kilimo, miundombinu, n.k. Tunawashukuru sana.

 

Nimefurahi katika hafla hii, tunaye Balozi wa China nchini, Mheshimiwa Wang Ke. Tunakuomba Mheshimiwa Balozi utufikishie shukrani zetu kwa Mheshimiwa Rais Xi Jinping, Serikali pamoja na wananchi wa China. Maktaba hii itatumika kwa miaka mingi ijayo. Hivyo basi, tunawashukuru sana; na napenda niahidi kuwa tutaendelea kushirikiana nanyi kwa karibu; na msaada mtakayotupatia, tutaitumia vizuri.

Ndugu Wana-Jumuiya wa Chuo Kikuu;

Mabibi na Mabwana;

Maktaba ni nyumba ya maarifa; na ni taasisi muhimu sana kwa maendeleo ya sekta ya elimu. Maktaba inatoa mazingira mazuri na tulivu kwa watu kujisomea. Lakini, zaidi ya hapo, Maktaba inamwezesha mtu wa kipato chochote kusoma ama kuazima vitabu, ambavyo aghalabu, isingekuwa rahisi kuvipata kwa sababu ya bei. Hivyo, narudia tena kukipongeza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kupata Maktaba hii kubwa na ya kisasa. Nina imani Maktaba hii itasaidia kuboresha kiwango cha elimu inayotolewa katika Chuo hiki. Na katika hili, napenda kutoa wito kwa uongozi wa Chuo, kuendelea kusimamia ubora wa elimu. Baadhi ya changamoto ambazo zimeanza kusikika, hakikisheni mzishughulikia. Kama nilivyosema, Chuo hiki ni kikongwe na kinategemewa na Watanzania.

Ndugu Wana-Jumuiya wa Chuo Kikuu;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Moja ya vipaumbele vikubwa vya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuimarisha na kuboresha sekta ya elimu nchini, kuanzia elimumsingi hadi vyuo vikuu. Tangu tumeingia madarakani tumechukua hatua mbalimbali kufikia azma hiyo. Kwa mfano, mbali na msaada huu kutoka China, kwenye Chuo hiki tumejenga majengo 20 ya hosteli yenye uwezo wa kubeba wanachuo 3,840, na hivyo kupunguza tatizo la makazi kwa wanafunzi.

 

Aidha, katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine kilichopo Morogoro, tumetoa shilingi bilioni 2 kwa ajili ya kujenga maabara kubwa (Multi-purpose Laboratory). Tuliwapatia pia shilingi milioni 700 za kujenga Mgahawa (Cafeteria) itakayochukua wanafunzi 400 kwa mpigo, na shilingi bilioni 2 nyingine za ujenzi wa hosteli zitakazochukua wanachuo 700.

 

Kwenye Chuo Kikuu cha Mzumbe, tunajenga hosteli itakayochukua wanachuo 1,000 kwa gharama ya shilingi bilioni 6.5 na pia tumetoa kiasi cha shilingi bilioni 2.84 kwa ajili ya kujenga Maktaba na Hosteli kwenye Kampasi yake ya Mbeya. Ujenzi na ukarabati wa miundombinu mingine (nyumba, maabara, kumbi za mihadhara, n.k.) inaendelea kwenye vyuo vikuu vya umma kwa gharama ya shilingi bilioni 18. Kwa upande wa elimumsingi, tumejenga na kukarabati miundombinu ya shule za msingi na sekondari 551 kwa gharama ya shilingi bilioni 84.7.

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Mbali na kujenga miundombinu, tumepanua wigo na kuchukua hatua za kuboresha na kuimarisha elimu yetu. Nyote mnafahamu, hivi sasa tunatoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari, ambapo kila mwezi tunatenga kiasi cha shilingi 23.8 kugharamia. Tumeongeza idadi ya wanafunzi wanaopata mikopo ya elimu ya juu kutoka 98,000 hadi kufikia 124,000 hivi sasa. Hii imewezekana baada ya Serikali kuongeza bajeti ya mikopo kutoka shilingi bilioni 348 mwaka 2014/2015 hadi kufikia shilingi bilioni 427 mwaka huu.

 

Nitumie fursa hii pia kuipongeza Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kwa kutoa mikopo kwa wakati; japo mwaka huu nimesikia kuna ucheleweshaji kidogo. Baadhi ya wanafunzi hawajapata mikopo yao mpaka sasa. Wizara ya Fedha na Bodi ya Mikopo hakikisheni mnashughulikia suala hilo haraka. Lakini napenda kuipongeza pia Bodi kwa kuanza kusimamia vizuri suala la urejeshaji wa mikopo iliyotolewa. Mwaka 2015/2016 walikusanya shilingi bilioni 21.74 lakini mwaka jana (2017/2018) walikusanya shilingi bilioni 181.49. Hongereni sana.

 

Sambamba na hayo, Serikali imesambaza vifaa vya maabara vyenye thamani ya shiligi bilioni 16.9 kwenye shule za sekondari 1,696 pamoja na vifaa vya kufundishia kwenye shule za mahitaji maalum. Vilevile, tumenunua pikipiki 2,894 na magari 45 kwa ajili ya kuwezesha ukaguzi wa mara kwa mara. Tunafanya haya yote kwa ajili ya kuhakikisha elimu yetu inaendelea kuwa bora.

Waheshimiwa Viongozi mliopo;

Ndugu Wana-Jumuiya wa Chuo Kikuu;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Tupo hapa kuzidua Maktaba. Hata hivyo, kabla sijahitimisha hotuba yangu, napenda nitoe wito kwa wana-Jumuiya wa Chuo Kikuu kuhakikisha kwanza mnaitunza Maktaba hii ili iweze kutumika kwa muda mrefu. Kitunze kidumu. Aidha, hakikisheni Maktaba hii inakuwa na vitabu vya kutosha. Maktaba ni vitabu; sio jengo peke yake. Na katika hili, nawakumbusha waandishi na wachipishaji vitabu kote nchini kuhakikisha wanatekeleza Sheria inayowataka kupeleka nakala mbili za kila Chapisho wanaloandaa kwenye Maktaba Kuu pamoja na Maktaba ya Chuo Kikuu.

 

Pili, natoa wito kwa Bodi ya Huduma za Maktaba, taasisi za umma na binafsi, pamoja na Watanzania kwa ujumla kuhakikisha tunakuwa na maktaba nyingi kwenye maeneo yetu, ikiwemo majumbani, ili kuwajengea watoto wetu utamaduni wa kujisomea. Tafiti nyingi zinaonesha kuwa Watanzania wengi hawapendi kusoma vitabu.

 

Tatu, kama mlivyosikia, katika Mradi huu, mbali na Jengo la Maktaba, lipo jengo la kufundisha lugha ya Kichina. Nawasihi Watanzania wenzangu kuchangamkia fursa ya kujifunza lugha ya Kichina. Yapo manufaa mengi sana ya kujifunza lugha ya kichina kwa sasa. China ni Taifa kubwa lenye idadi ya watu takriban bilioni 1.3. Ni la pili kiuchumi duniani na pia limepiga hatua kubwa kwenye masuala ya sayansi na teknolojia. Hivyo, kujifunza Kichina kuna manufaa mengi. Mathalan, kwa taarifa nilizonazo, kila mwaka, watalii milioni 130 kutoka China hutembelea sehemu mbalimbali duniani. Nchi yetu hivi sasa imejipanga kuongeza idadi ya watalii kutoka China, hususan kwa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka China kuja hapa nchini. Hivyo basi, ni wazi kuwa watu wanaofahamu lugha ya kichina watahitajika zaidi ili kuwahudumia watalii kutoka China; na hasa kwa kuwa, Wachina wengi wanajua kichina pekee.

Mheshimiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Kikuu;

Mheshimiwa Balozi wa China;

Waheshimiwa Viongozi wengine mliopo;

Ndugu Wana-Jumuiya wa Chuo Kikuu;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Napenda kuhitimisha kwa kurudia tena kuushukuru uongozi wa Wizara ya Elimu pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kunikaribisha. Naahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Chuo hiki pamoja na vyuo vingine nchini. Natambua kuwa Chuo hiki kinakabiliwa na baadhi ya changamoto. Tutaendelea kuzishughulikia.  Kama mlivyosikia kutoka kwa wanafunzi wa zamani, Chuo hiki kimetoka mbali hadi kufikia hapa. Hivyo basi, hata changamoto zenu za sasa nazo zitashughulikiwa. Na katika hilo, naahidi kuanza kushughulikia barabara zenu za hapa. Naiagiza TARURA kuziingiza kwenye Mpango wa Kuboresha Barabara za Jiji la Dar es Salaam.

 

Napenda kurudia tena kuwashukuru marafiki zetu wa China kwa kuendelea kutuunga mkono kwenye masuala mbalimbali. Tunawashukuru pia kwa kukubali kutujengea Chuo cha VETA kule Kagera, kutoa mafunzo ya watumishi wa Maktaba hii, pamoja na misaada mingine mingi mnayotupatia. Tunashukuru pia Waheshimiwa Mabalozi mliopo. Tunaahidi kuendelea kushirikiana na Mataifa pamoja na taasisi zenu kwa manufaa yetu wote.

 

Mwisho lakini sio kwa umuhimu, napenda nimshukuru na  kumpongeza Waziri Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Lowasa, ambaye alikuwa mpinzani wangu kwenye kinyang’anyiro cha Urais mwaka 2015, kwa kujumuika nasi katika tukio hili. Ameonesha ukomavu mkubwa, ambao wanasiasa wengine wa nchi hii hawana budi kujifunza. Siasa sio uadui au uhasama.

Mungu Ibariki Maktaba hii!

 

Mungu Kibariki Chuo Kikuu cha Dar es Salaam!

 

Mungu Ubariki Uhusiano wa Tanzania na China!

 

Mungu Ibariki Tanzania!

 

 

“Ahsanteni kwa kunisikiliza”