Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE UWEKAJI JIWE LA MSINGI LA MRADI WA MAJI SAFI NA MAZINGIRA WA ARUSHA, KIMYAKI, ARUMERU, TAREHE 2 DESEMBA, 2018

Sunday 2nd December 2018

 

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE UWEKAJI JIWE LA MSINGI LA MRADI WA MAJI SAFI NA MAZINGIRA WA ARUSHA, KIMYAKI, ARUMERU, TAREHE 2 DESEMBA, 2018

 

Mheshimiwa Prof. Makame Mbarawa,

Waziri wa Maji;

 

Mheshimiwa Mhandisi Isack Kamwelwe, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano;

 

Mheshimiwa Alex Mubiru, Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo Afrika nchini Tanzania;

 

Mheshimiwa Mrisho Gambo,

Mkuu wa Mkoa wa Arusha;

 

Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM – Mkoa wa Arusha;

 

Waheshimiwa Wabunge mliopo;

 

Ndugu Makatibu Wakuu wa Wizara ya Maji pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa;

 

Mstahiki Meya pamoja na Madiwani wa Jiji la Arusha;

 

Viongozi wengine wa Serikali mliopo;

 

Ndugu Wana-Arusha, Mabibi na Mabwana;

Napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa siku ya leo. Aidha, namshukuru Mheshimiwa Waziri Prof. Mbarawa kwa kunialika ili nami nishiriki katika tukio hili muhimu kwa wakazi wa Jiji la Arusha. Ahsante sana.

 

Napenda pia nitumie fursa hii kuwashukuru wana-Arumeru na wana-Arusha kwa ujumla kwa kujitokeza kwenu kwa wingi katika hafla hii. Lakini, kwa vile hii ni mara yangu ya kwanza kufika kwenye eneo hili tangu nimekuwa Rais, napenda niwashukuru wana-Arumeru kwa kunichagua. Nawaahidi kuendelea kuwatumikia kwa moyo wangu wote.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Maji ni rasilimali muhimu sana. Ni muhimu, kwanza, katika maisha ya binadamu. Ninyi nyote hapa mnafahamu kuhusu usemi usemao “maji ni uhai”. Usemi huu unamaanisha kuwa maisha ya binadamu yanategemea maji. Bila ya maji hakuna uhai. Lakini, zaidi ya hapo, maji ni muhimu kwa shughuli za kiuchumi na uzalishaji, ikiwemo kilimo, uvuvi, ufugaji, viwanda, utalii, ujenzi, n.k. Kwa ujumla, shughuli zote za maendeleo duniani zinahitaji maji.

Pamoja na ukweli huo, ni ukweli pia usiopingika kuwa upatikanaji wa maji nchini bado sio wa kuridhisha sana. Hadi kufikia mwaka 2015, takwimu zilionesha kuwa upatikanaji wa maji nchini ulikuwa wa kiwango cha asilimia 50.2. Hapa Arusha penyewe, kwa mfano, mpaka sasa uzalishaji wa maji ni mita za ujazo 40,000, sawa na asilimia 42.9 tu ya mahitaji ambayo ni mita za ujazo 93,270.

 

Ni kwakuzingatia hilo, Serikali ya Awamu ya Tano, kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 - 2020; na nimefurahi kuona Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha yupo hapa; tuliahidi kuwa tutaboresha upatikanaji wa maji nchini, hususan kwa kuhakikisha tunakamilisha miradi ya zamani ambayo ilikuwa imekwama na pia kutekeleza miradi mipya. Waswahili husema “ahadi ni deni”. Hivyo basi, leo nafurahi nipo hapa Arusha kuweka Jiwe la Msingi la Mradi huu. Hii maana yake ni kwamba, CCM ikiahidi jambo, inatekeleza.

 

Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;

Mradi wenu wa maji ni mkubwa sana. Kama mlivyosikia, utakapokamilika, utakuwa na uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 208,000, zaidi ya mara nne ya kiwango kinachozalishwa sasa; na mara mbili zaidi ya mahitaji yenu ya sasa. Kwa maana hiyo, maji yatakuwa mengi zaidi kuliko mahitaji yenu. Hongereni sana wana-Arusha.

 

Utekelezaji wa mradi huu utagharimu Dola za Marekani milioni 233.9, zaidi ya shilingi bilioni 520. Fedha hizi ni za mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (The African Development Bank – AfDB). Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuishukuru AfDB kwa kutupatia mkopo huu. Benki hii imekuwa ni mdau mkubwa wa maendeleo wa nchi yetu.  Wameshirikiana nasi katika kutekeleza miradi mingi ya maendeleo. Kwa mfano, kwa upande wa sekta ya maji, hawa ndio walitupa mkopo wa kutekeleza Miradi wa Maji ya Sengerema na Nansio, ambayo tayari nimeizindua. Wametufadhili pia kwenye miradi ya miundombinu, hususan usafiri na umeme. Tunawashukuru sana.

 

Nimefurahi kuona Mwakilishi wa Benki hiyo nchini, Bwana Alex Mubiru pamoja wapo hapa. Tunawaomba utufikishie shukrani zetu nyingi kwa uongozi wa juu wa Benki.  Tunaomba muendelee kutuunga mkono.

 

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Mbali na mradi huu, Serikali inatekeleza miradi mingine mikubwa ya maji. Mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka miji ya Nzega, Igunga na Tabora wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 268, takriban shilingi bilioni 600. Aidha, tumepata mkopo kutoka India wenye thamani ya shilingi trilioni 1.2 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kupeleka maji kwenye miji 25.

 

Hivi majuzi tu, tumepata fedha nyingine kutoka Benki ya Dunia, Dola za Marekani milioni 350, takriban shilingi bilioni 800, kwa ajili ya kufanya ukarabati wa miradi iliyokuwa imesimama au haifanyi kazi. Katika Mkoa wenu wa Arusha, mbali na mradi huu nitakaoweka Jiwe la Msingi leo, tunatekeleza miradi mikubwa ya maji Simanjiro, Longido, Loliondo pamoja na Karatu.

 

Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;

Ukiachilia mbali miradi ya maji, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Serikali imechukua hatua nyingine muhimu za kuiletea maendeleo nchi yetu.  Tumeongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu shilingi bilioni 365 hadi kufikia shilingi bilioni 427. Tunatoa elimu bure, ambapo kila mwezi tunatenga shilingi bilioni 23.863. Tumeongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 31 hadi shilingi bilioni 270 hivi sasa. Tumekarabati vituo vya afya zaidi ya 300. Tunajenga hospitali mpya za wilaya 67.

 

Tunajenga miundombinu ya barabara na tunasambaza umeme. Hapa Arusha, tumekamilisha ujenzi wa barabara ya kisasa ya njia nne ya Sakina - Tengeru yenye urefu wa kilometa 14.1. Aidha, hivi sasa tunajenga barabara za mzunguko zenye urefu wa kilometa 42.3. Hizi zote ni jitihada za kueletea maendeleo nchi yetu.

 

Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;

Wabunge wenu wameeleza kuhusu kusuasua kwa utekelezaji wa mradi wa kupeleka umeme vijijini na pia wameombea barabara ya kutoka Mianzini hadi Ngaramtoni yenye urefu wa takriban kilometa 18 ijengwe kwa lami. Napenda, kwanza kabisa, kutumia fursa hii kumwagiza Waziri wa Nishati kuhakikisha anamfuatilia kwa karibu Mkandarasi huyo aliyepewa zabuni ya kusambaza umeme hapa Arusha. Na endapo itathibitika kuwa, Mkandarasi hana uwezo, basi asisite kumchukulia hatua. Na kuhusu ujenzi wa Barabara, naagiza, kwanza, ipandishwe hadhi kuwa ya Mkoa, na taratibu za ujenzi zianze mara moja. Kwa bahati nzuri, Waziri wa Ujenzi upo hapa. Mnaweza kuanza na kipande cha kilometa 8 kutoka Mianzini hadi hapa; na kisha mmalizie sehemu iliyobaki ya kilometa 10 hadi Ngaramtoni. Kama zipo fedha zilizotengwa na TARURA kwa ajili ya kujenga barabara hii sasa zihamishiwe TANROADS. Lakini niwaombe wananchi nanyi muwe wavumilivu. Ujenzi wa barabara una taratibu zake.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Tupo hapa kuweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Maji wa Arusha. Kabla ya kuhitimisha hotuba yangu, napenda nitumie fursa hii kutoa wito kwa Wakandarasi wote kumi wanaotekeleza Mradi huu kuhakikisha wanaukamilisha kwa wakati. Sitaki kabisa kusikia habari za ucheleweshaji. Nayasema hayo kwa sababu nafahamu, moja ya changamoto zenye kuikabili sekta ya maji nchini ni kuchelewa kutekelezwa kwa miradi. Narudia tena hilo sitaki litokee kwenye Mradi huu. Nakupongeza Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa kuanza kuchukua hatua dhidi ya wakandarasi wazembe wanaochelewesha miradi. Endelea hivyo hivyo. Lakini, nakuagiza pia Mheshimiwa Waziri kuhakikisha maeneo/vijiji ambavyo mradi huu utapita, wananchi wapate maji; na pia angalia uwezekano wa Mradi huu kufikisha maji kwenye kijiji cha Oldonyosambu, ambacho jana wananchi waliniomba maji.

 

Pili, ni kwenu wananchi. Kama mlivyosikia, Mradi huu ni wa mkopo. Baadaye Serikali itaulipa. Na Serikali haina njia nyingine ya kupata fedha zaidi ya kodi zenu. Hivyo, nawasihi sana, tulipe kodi. Nimesikitika sana kusikia tabia ya kukwepa kodi inashamiri. Baadhi ya watu wanatumia mbinu mbalimbali kukwepa kodi, ikiwemo kuwatumia wafanyabiashara wadogo kuwauzia bidhaa zao, kuacha kutumia mashine za kielektroniki, kutengeneza risiti feki ama kuandika risiti chini ya thamani halisi ya bidhaa husika.

 

Tabia za namna hiyo zinaikosesha sana Serikali mapato mengi, ambayo yangetumika kutekeleza miradi ya maendeleo. Hivyo basi, nawasihi sana wananchi tutambue umuhimu wa kulipa kodi. Na niwaombe sana marafiki zangu wamachinga, msikubali kutumika kukwepa kodi. Serikali ilimewaruhusu kufanya shughuli zenu kwa uhuru ili muweze kuinua vipato vyenu na kuondokana na umaskini. Nawasihi sana, msiitumie vibaya nia hiyo njema ya Serikali. Najua wenye tabia hiyo ni wachache. Wafichueni.

 

Napenda pia kutumia fursa hii kutoa wito kwa TRA kuwachukulia hatua kali wakwepa kodi. Lakini zaidi ya hapo, na ninyi inapaswa mjitathimini kwanini watu wanatafuta mbinu mbalimbali za kukwepa kodi. Wakati mwingine, chanzo ni ninyi wenyewe. Mnaweka viwango vikubwa sana vya kodi, ambavyo havilipiki. Ni bora muweke viwango vidogo vyenye kulipika kuliko kuweka viwango vikubwa visivyolipika.

 

Jambo la tatu, nawasihi wananchi kutunza vyanzo vya maji. Kama nilivyosema awali, maji ni rasilimali muhimu sana. Lakini, kwa bahati mbaya, rasilimali hii inaendelea kupungua kila kukicha kwa sababu ya ongezeko la idadi ya watu pamoja na uharibifu wa vyanzo vyake. Hivyo, nawasihi Watanzania tutunze vyanzo vyetu vya maji.

 

Mwisho lakini sio kwa umuhimu, napenda kuwapongeza wana-Arusha na Watanzania kwa ujumla, kwa kuendelea kuitunza amani yetu. Amani ndiyo msingi wa maendeleo. Kwa sababu hiyo, nawasihi sana tuendelee kudumisha amani. Tusikubali kufarakanishwa kwa sababu ya dini zetu, makabila yetu au vyama vyetu. Maendeleo hayana chama. Mradi huu wa maji utamnufaisha kila mwananchi. Hivyo basi, hatuna budi kushikamana na kuwa kitu kimoja. Aidha, nawasihi muendelee kuchapa kazi kwa bidii. Wakati nakuja hapa, nimeshuhudia kila mahali pamelimwa. Hongereni sana wana-Arumeru. Hiyo ndio dhana halisi ya “hapa kazi tu”.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Napenda kuhitimisha kwa kusema kuwa nchi yetu inaendelea vizuri. Tunajenga miundombinu mbalimbali na kuboresha huduma za jamii. Tunajenga reli mpya ya kisasa. Tunafufua reli yetu kutoka Tanga kuja Arusha. Tumenunua ndege. Tunajenga barabara. Na tupo mbioni kuanza kutekeleza mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa Bonde la Mto Rufiji.

 

Tunaendelea kusimamia vizuri rasilimali zetu. Tangu tumepitisha sheria ya kulinda rasilimali zetu, mapato yameongezeka. Mwaka uliopita, tulipanga kukusanya shilingi bilioni 194, lakini tumekusanya shilingi bilioni 301. Lakini ninyi wana-Arusha mnafahamu vizuri. Zamani tulikuwa tukiibiwa sana tanzanite yetu. Sasa tumefanikiwa kudhibiti wizi huo baada ya kujenga ukuta kuzunguka mgodi pale Mererani.

 

Sambamba na hayo, tunaendelea kushughulikia kero mbalimbali (rushwa; utitiri wa tozo kwenye kilimo, mifugo na uvuvi; migogoro ya ardhi; n.k.). Yote haya lengo lake ni kuiletea nchi yetu maendeleo. Na kuhusu suala la mifugo, nakuagiza Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kushirikiana na Wizara ya Mifugo kuanzisha Mnada ili wananchi wauze mifugo yao kwa uhuru na kupata faida. Hiyo ndiyo namna ya kujenga uchumi wa kisasa. Badala ya kuwazuia wananchi kupeleka mifugo nje; wekeni mazingira mazuri yatakayowawezesha wananchi kufanya biashara hapa nchini.

 

Mungu Ubariki Mradi huu!

 

Mungu Ibariki Arusha!

 

Mungu Ubariki Uhusiano kati ya Tanzania na AfDB!

 

Mungu Ibariki Tanzania!

 

“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”