Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE HAFLA YA KUWEKA SAINI MKATABA WA MRADI WA KUZALISHA UMEME KWENYE BONDE LA MTO RUFIJI IKULU, DAR ES SALAAM, TAREHE 12 DESEMBA, 2018

Wednesday 12th December 2018

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI,

RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

KWENYE HAFLA YA KUWEKA SAINI MKATABA WA MRADI

WA KUZALISHA UMEME KWENYE BONDE LA MTO RUFIJI

IKULU, DAR ES SALAAM, TAREHE 12 DESEMBA, 2018

 

Mheshimiwa Dkt. Mostafa Madbouly, Waziri Mkuu

wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri;

 

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais

wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu

wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Job Ndugai, Spika wa Bunge

la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Prof. Ibrahim Juma,

Jaji Mkuu wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Bashiru Ally, Katibu Mkuu

wa Chama Cha Mapinduzi;

 

Waheshimiwa Mawaziri kutoka Tanzania na Misri mliopo;

Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa;

Waheshimiwa Wabunge mliopo;

Waheshimiwa Mabalozi na Wakuu wa Taasisi za Kimataifa;

Ndugu Makatibu Wakuu mliopo;

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa na Dini mliopo;

Wageni Waalikwa Wote, Mabibi na Mabwana:

         Awali ya yote, napenda kumkaribisha Mgeni wetu, Mheshimiwa Dkt. Mostafa Madbouly, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri pamoja na ujumbe wake hapa nchini. Mheshimiwa Waziri Mkuu; karibu sana hapa Ikulu; karibu sana Dar es Salaam, na karibu sana Tanzania. Tunakushukuru sana kwa uamuzi wako wa kuja kuungana nasi katika tukio hili muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu. Hii ni ishara tosha kuwa nchi zetu mbili zina uhusiano mzuri.

 

Na niseme tu kwamba, Tanzania na Misri ni marafiki wa muda mrefu sana. Zamani kabisa, hata kabla ya kuja kwa wakoloni, wafanyabiashara kutoka Misri pamoja na Mataifa mengine ya Kiarabu na Asia walifika kwenye Ukanda wetu wa Pwani kufanya biashara; ambapo pia waliweza kueneza tamaduni zao, ikiwemo lugha ya kiarabu pamoja na dini. Inaelezwa kuwa hata muziki wa taarabu ambao ni maarufu sana hapa nchini, asili yake ni nchi ya Misri.

 

Uhusiano wetu huo ulikuzwa zaidi na waasisi wa mataifa yetu mawili, yaani Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Gamal Abdel Nasser wa Misri. Viongozi hawa wawili, ambao walishibana sana, walikuwa na maono yenye kufanana kwenye masuala mbalimbali. Kupitia viongozi hawa, mataifa yetu mawili yalitoa mchango mkubwa katika kuanzisha Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), hivi sasa unajulikana kama Umoja wa Afrika (AU); na pia katika harakati za ukombozi wa Bara letu. Kwa sasa, Mataifa yetu mawili yanashirikiana vizuri kwenye nyanja nyingi, ikiwemo biashara na uwekezaji.

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Napenda pia nitumie fursa hii kuwashukuru wageni wetu mbalimbali (Waheshimiwa Wabunge, Waheshimiwa Mabalozi, Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa, Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa, Viongozi wa Dini, Vyama vya Siasa, Wana-habari, n.k.) ambao wamekuja kujumuika nasi kwenye tukio hili. Kuwepo kwenu hapa ni uthibitisho kwamba mnatambua umuhimu wa mradi huu. Tunawashukuru sana.

 

Mheshimiwa Waziri Mkuu Dkt. Madbouly;

Waheshimiwa Viongozi mliopo;

Mabibi na Mabwana;

Tupo hapa kushuhudia Uwekaji Saini wa Mkataba wa Mradi wa Kufua Umeme wa Bonde la Mto Rufiji. Binafsi najisikia furaha kubwa sana. Kama mnavyofahamu, Mradi wa Umeme wa Bonde la Mto Rufiji ni wa muda mrefu sana. Ulianza tangu enzi za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwenye miaka ya 1970. Kati ya mwaka 1976 mpaka 1980, Serikali yetu kwa kushirikiana na Serikali ya Norway, kupitia Kampuni ya Norplan & Hafslud, zilifanya upembuzi yakinifu (feasibility study), na kubaini kuwa, Mradi huu wa Bonde la Mto Rufiji una uwezo wa kuzalisha umeme Megawati 2,100. Hata hivyo, kwa sababu mbalimbali, ikiwemo matatizo ya kifedha, nchi yetu haikuweza kuutekeleza. Ni kwa sababu hiyo, nimefurahi sana leo tupo hapa, baada ya kipindi cha zaidi ya miaka arobaini, kushuhudia uwekaji saini wa Mkataba huu.

 

Nimefurahi pia kwa sababu, Mradi huu tunautekeleza kwa fedha zetu wenyewe, Dola za Marekani bilioni 2.9, sawa na takriban shilingi trilioni 6.558. Na jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba, Kampuni itakayotekeleza Mradi huu, M/S Arab Contractors inatoka kwa marafiki zetu wa Misri, ambao ni Waafrika wenzetu. Huu ni uthibitisho kuwa sisi Watanzania tukiamua, tunaweza. Na pia Waafrika tukiamua, tunaweza.

 

Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza Watanzania wote kwa kuweza kufikia hatua hii muhimu ya kuanza kutekeleza Mradi huu, ambao tumeusubiri kwa zaidi ya miaka 40. Naipongeza pia Kampuni ya M/S Arab Contractors kutoka Misri kwa kushinda zabuni ya mradi huu. Kampuni nyingi za nchi mbalimbali zilijitokeza kuomba zabuni hii; lakini iliyofanikiwa ni Kampuni ya M/S Arab Contractors.  Hongereni sana.

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Tanzania imebarikiwa kuwa na vyanzo vingi sana vya kuzalisha umeme. Na kimsingi, tunavyo karibu vyanzo vyote vya kuzalisha umeme: maji, gesi asilia, makaa ya mawe, jua, upepo, joto ardhi, pamoja na madini ya urania. Hata hivyo, kabla ya kuamua kutekeleza Mradi huu, ilibidi tukae chini na kutafakari kwa kina; ni chanzo kipi hasa kitatufaa katika mazingira yetu ya sasa. Na baada ya tafakuri hiyo, ambapo tulitumia vigezo vikubwa vinne: yaani uhakika wa chanzo chenyewe; gharama za utekelezaji (investment cost); gharama za uzalishaji (cost of generation); pamoja na tija au manufaa yanayotarajiwa kupatikana; tulibaini kuwa Mradi huu ndio unaifaa zaidi nchi yetu kwa sasa.

 

Kwanza, kwa sababu chanzo chake ni cha uhakika. Kama mnavyofahamu, Mradi huu utatekelezwa kwa kutumia maji yanayotoka kwenye mtandao wa mito iliyopo kwenye maeneo yenye wastani mkubwa wa mvua. Kwa tathmini ya awali, Mradi huu utazalisha umeme kwa zaidi ya miaka 60.  Pili, gharama za utekelezaji sio kubwa sana ukilinganisha na vyanzo vingine. Kama nilivyosema, Mradi huu utagharimu shilingi trilioni 6.5. Kama tungeamua kuzalisha Megawati 2,115 kwa kutumia vyanzo vingine, tungelazimika kutumia fedha nyingi zaidi. 

 

Zaidi ya hapo, gharama za kuzalisha umeme wa maji ni ndogo kuliko vyanzo vingine. Uniti moja ya umeme wa maji inazalishwa kwa shilingi 36; wakati uniti moja ya umeme wa nyuklia inazalishwa kwa shilingi 65; jua shilingi 103.05; upepo shilingi 103.05, joto ardhi shilingi 114.5; makaa mawe shilingi 118; gesi asilia shilingi 147; na mafuta shilingi 546. Hii inafanya umeme wa maji uwe nafuu sana kuuzalisha.

 

Muhimu zaidi ni kwamba, Mradi huu unatarajiwa kutaleta manufaa mengi makubwa kwa nchi yetu. Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Kalemani, ametaja baadhi ya faida hizo.  Lakini faida nyingine kubwa ni kwamba, Mradi huu utatuzalishia umeme mwingi zaidi (Megawati 2,115) ambazo ni nyingi kuliko umeme wote ambao unazalishwa kwa sasa hapa nchini, takriban Megawati 1,560. Na kwa vile umeme huo utazalishwa kwa gharama nafuu, bei yake ya kuuza pia itakuwa nafuu. Tunatarajia, Mradi huu utakapokamilika, bei ya umeme nchini itashuka na kuwa nafuu kuliko ilivyo sasa. Zaidi ya hapo, Mradi huu utachochea shughuli nyingine za kiuchumi, ikiwemo viwanda, kilimo, utalii, uvuvi, michezo, n.k. Kwa sababu hiyo, narudia tena kuwapongeza Watanzania wote kwa kuanza kutekeleza mradi huu.

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Nafahamu kuwa yapo madai kwamba Mradi huu utaharibu mazingira. Niseme tu kwamba, hiyo siyo kweli. Mradi huu, katika hali halisi kabisa, utasaidia kutunza mazingira yetu. Kwanza, kwa sababu, umeme wa maji ni rafiki wa mazingira. Pili, eneo litakalotumika kuutekeleza ni dogo; litakuwa kati ya asilimia 1.8 hadi asilimia 2 ya eneo zima la Hifadhi ya Selous, ambalo ni kubwa kuliko baadhi ya nchi. Sababu ya tatu ni kwamba, Mradi huu utapunguza ukataji miti nchini. Kwa mujibu wa Taarifa ya Tathmini ya Hali ya Misitu Nchini (National Forest Resources Monitorig and Assessment - NAFORMA) ya Mwaka 2013, mgawanyo wa matumizi ya nishati kwa sasa hapa nchini ni asilimia 92 kwa kuni na mkaa; petroli ni asilimia 7, na umeme ni asilimia 1. Matumizi ya mkaa kwa mwaka yanakadiriwa kuwa zaidi ya tani milioni 2.3, ambapo takriban asilimia 90 ya mkaa wote unaozalishwa, unatumika Dar es Salaam. Matumizi ya mkaa nchini yanatarajiwa kuongezeka maradufu ifikapo mwaka 2030.

 

Utafiti unaonesha kuwa, ili kuzalisha tani moja ya mkaa kwa kutumia matanuri ya kienyeji, zinahitajika tani 10 hadi tani 12 za miti. Hii maana yake ni kwamba, kwa tani milioni 2.3 za mkaa tunazotumia kwa mwaka, zinahitajika tani milioni 23 hadi milioni 27.6 za miti yenye kipenyo cha zaidi ya sentimita 32 kwa mwaka. Utafiti pia unaonesha kuwa kwa kila miti 18 yenye kipenyo cha sentimita 32, inatoa magunia 26 ya mkaa yenye kilo 53 kila moja. Kwa hiyo, tani milioni 2.3 za mkaa zinazozalishwa kwa mwaka, zinatumia miti milioni 30 yenye kipenyo kisichopungua sentimita 32. Hii ni idadi kubwa sana ya miti.

 

Hivyo, ni wazi kuwa upatikanaji wa umeme wa uhakika utaokoa idadi hii kubwa ya miti inayokatwa kwa mwaka; na hivyo kusaidia kutunza mazingira yetu. Hivi sasa, kwa sababu ya mahitaji ya mkaa, kila siku, zinavunwa hekta 583 za miti. Hii ni sawa na hekta 212,795 za miti kwa mwaka. Eneo la Selous lina ukubwa wa hekta milioni 5. Hivyo, kwa kasi ya ukataji miti ya sasa, inahitajika miaka 23 tu ili miti yote ya Selous iwe imemalizika; na hiyo ni kwa kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2013. Kwa vile idadi ya Watanzania inaendelea kuongezeka, ambapo kwa sasa tunakadiriwa kufikia milioni 55, inahitajika miaka isiyozidi 15 kumaliza miti yote ya Hifadhi ya Selous.

 

Ni kwa sababu hiyo, narudia tena kusisitiza kuwa Mradi huu ni muhimu sana kwa utunzaji wa mazingira ya nchi yetu. Tuna matumaini makubwa kuwa, utakapokamilika, wananchi wengi wataachana na matumizi ya kuni na mkaa na kuhamia kwenye umeme, ambao utapatikana kwa bei nafuu.  Nawaombe basi wapenda-mazingira wote kuunga mkono mradi huu ambao utaisaidia nchi yetu kutunza mazingira. Kama mnavyofahamu, sisi Watanzania ni watunzaji wazuri sana wa mazingira. Tumetenga zaidi ya asilimia 32 ya nchi yetu kwa ajili ya hifadhi. Sina hakika kama ipo nchi nyingine duniani iliyotenga eneo kubwa kiasi hicho.

 

Mheshimiwa Waziri Mkuu;

Waheshimiwa Viongozi mliopo;

Mabibi na Mabwana;

Kama nilivyosema awali, tupo hapa kushuhudia uwekaji saini ya Mkataba wa Mradi wa Umeme wa Mto Rufiji. Kwa sababu hiyo, sitapenda kuwachosha kwa hotuba ndefu. Hata hivyo, kabla sijahitimisha, naomba mniruhusu nisisitize mambo machache yafuatayo. Kwanza, narudia tena kusema kuwa Mradi huu utakapokamilika, utaipatia nchi yetu umeme wa uhakika na wa bei nafuu; na hivyo kuongeza kasi ya ujenzi wa viwanda na upatikanaji wa fursa za ajira kwa Watanzania. Bei ya umeme kwa sasa nchini ni Dola za Marekani senti 10.7. Kiwango hiki ni kikubwa ukilinganisha na nchi nyingine; ambapo kwa mfano kwa marafiki zetu wa Misri, ambao weyewe wana Megawati 30,000; bei yake ni  senti 4.6; Korea Kusini senti 8; China senti 8; Afrika Kusini senti 7.4; India senti 6.8; Algeria senti 3, Ethiopia senti 2.4; Uingereza senti 0.15; na Marekani senti 0.12. Huu ni uthibitisho kuwa gharama za umeme hapa nchini zipo juu sana. Na gharama za umeme zikiwa juu, maana yake ni kwamba gharama za uzalishaji nazo zinakuwa juu. Hii ndiyo sababu bidhaa zetu za viwandani zinashindwa kushindana kimataifa.

 

Jambo la Pili; hivi punde tumesikia kuwa, baada ya leo kusainiwa kwa Mkataba huu, Mkandarasi atapewa muda wa miezi sita ya kumwezesha kukusanya vifaa; na utekelezaji wa mradi wenyewe utachukua miezi 36. Hii maana yake ni kwamba, mradi huu unatarajiwa kukamilika baada ya kipindi cha miaka mitatu na nusu kuanzia sasa. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii, kutoa wito kwa Mkandarasi kuhakikisha anakamilisha mradi huu kwa wakati; na ikiwezekana umalizike kabla ya muda, ili kudhihirisha kuwa, Waafrika tukiamua, tunaweza. Na binafsi, naamini kuwa Mkandarasi huyu atakamilisha Mradi huu mapema; na hasa kwa kuzingatia kuwa Wamisri ni wachapakazi sana. Waliweza kujenga Ma-piramidi, ambayo mpaka sasa yamebaki kuwa maajabu ya dunia. Hivyo, hata Mradi huu wataumaliza mapema sana. Na bahati nzuri, hata Rais wa Misri, ndugu yangu, Mheshimiwa Al-Sisi, amenihakikishia kuwa mradi huu utakamilika kwa wakati. Yeye mwenyewe alitamani sana kuwepo hapa leo, lakini baadaye tulikubaliana kuwa atakuja wakati wa Kuweka Jiwe la Msingi au Uzinduzi. Hata hivyo, ameniahidi atakuwa akifuatilia kwa karibu utekelezaji wa Mradi huu.

 

Tatu, napenda nitumie fursa hii kutoa wito kwa wananchi wanaoishi maeneo ambayo Mto Rufiji unaanza, unakopita na sehemu ambako Bwawa litajengwa; kuunga mkono mradi huu, hususan kwa kutunza vyanzo vya maji. Msikate au kuchoma moto miti kiholela, au kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji karibu na vyanzo vya maji. Na hapa ninazungumza na wananchi wa Mikoa ya Pwani, Morogoro, Dodoma, Iringa, Njombe, Ruvuma, Mbeya, Lindi na Singida. Natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa hiyo kusimamia suala hili; na kwa bahati nzuri, wote mpo hapa.

 

Mabibi na Mabwana; siwezi kuhitimisha hotuba yangu bila kutoa pongezi zangu nyingi kwa Timu ya Wataalam waliosimama kidete kwenye majadiliano na mipango yote ya maandalizi ya Mradi huu, hadi leo tumeweza kufikia hatua hii. Kwa kutambua mchango wao mkubwa, naomba niwataje majina. Kwanza kabisa, ni Mwenyekiti wa Timu hiyo, Dkt. Leonard Chamuriho, Katibu Mkuu – Uchukuzi, ambaye pia aliongoza Timu yetu ya Majadiliano kuhusu ujenzi wa reli na ununuzi wa ndege. Wajumbe wengine wa Kamati hiyo ni:

 1. Mhandisi Patrick Mfugale – TANROADS (Mjumbe);
 2. Dkt. Tito Mwinuka – TANESCO (Mjumbe);
 3. Ndg. Elias Kissamo – NCC (Mjumbe);
 4. Ndg. Saidi Kalunde –Nishati (Mjumbe)
 5. Ndg. Hassan Lugwa – Ofisi ya Rais (Mjumbe);
 6. Ndg. Glory Kombe – NEMC (Mjumbe);
 7. Ndg. Beatrice Steven – TRA (Mjumbe);
 8. Ndg. Edson Mweyuge – AG Chambers (Mjumbe);
 9. Ndg. Yosepha Tamamu – Hazina (Mjumbe);
 10. Ndg. Jackson William – Nishati (Mjumbe);
 11. Ndg. Harold Katainda – TANROADS (Mjumbe);
 12. Ndg. Leonard Masanja – Nishati (Mjumbe);
 13. Ndg. James Luchagula – TANESCO (Mjumbe);
 14. Ndg. Lutengano Mwandambo – TANROADS (Mjumbe);
 15. Ndg. Stanslaus Kizzy – TANESCO (Mjumbe);
 16. Ndg. John Mageni – TANESCO (Mjumbe);
 17. Ndg. Justus Mtolela – TANESCO (Mjumbe);
 18. Ndg. Mhina Kiondo – Nishati (Mjumbe); na
 19. Ndg. Pakaya Mtamakaya – TANESCO (Mjumbe).

 

Hongereni sana wataalam wetu kwa kazi kubwa ya kizalendo mliyoifanya. Nimearifiwa kuwa Ndugu Stanslaus Kizzy anatakiwa kustaafu leo; lakini nimeamua kumwongezea muda mpaka mradi huu utakapokamilika; na kama watakuwepo wajumbe wengine watakaofikia umri wa kustaafu kabla ya mradi huu kukamilika, nao nawaongezea muda; kwa kuwa Timu hii ya Wataalam ndiyo itakayosimamia utekelezaji wa mradi huu. Nitumie fursa hii pia kuipongeza Wizara ya Nishati kwa mchango wake mkubwa kwenye Mradi huu. Aidha, naipongeza Timu ya Wataalam ya Misri, ambao nao wapo hapa.

 

Mheshimiwa Waziri Mkuu Dkt. Madbouly;

Waheshimiwa Viongozi mliopo;

Mabibi na Mabwana;

Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kurudia tena kuwapongeza Watanzania wote kwa kuanza kutekeleza Mradi huu. Tuendelee kushikamana. Kama mjuavyo, Mradi huu umekuwa ukipigwa vita sana. Na hii ni kwa sababu, umeme ni bidhaa muhimu na nyeti kwa Taifa lolote lile duniani. Baadhi ya wanaoupiga, wanafahamu kuwa, endapo tutafanikiwa kuutekeleza, tutakuwa tumepiga hatua kubwa za kimaendeleo. Hivyo basi, narudia tena kuwasihi Watanzania wenzangu tushikamane katika kutekeleza mradi huu. Na niseme tu kwamba, sisi Serikalini tumedhamiria kuutekeleza.  Nalishukuru Bunge letu kwa kupitisha Bajeti ya mradi huu; na napenda kumhakikishia Mkandarasi kuwa fedha ya kutekeleza mradi huu tayari tunazo. Lakini nitoe wito kwa Watanzania wenzangu kuendelea kulipa kodi.

 

Mwisho kabisa, naipongeza tena Kampuni ya M/S Arab Contractors kwa kushinda kandarasi ya kutekeleza mradi huu. Aidha, namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu Dkt. Madbouly kwa kuungana nasi katika tukio hili. Naahidi kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Misri katika ngazi ya kitaifa na kimataifa. Nirudie tena kuwashukuru wageni wetu mbalimbali mliohudhuria, wakiwemo Waheshimiwa Mabalozi na Viongozi wa Vyama vya Siasa. Lakini, kwa namna ya pekee kabisa, nawashukuru viongozi wa dini kwa kujitokeza kwenu kwa wingi. Hii ni ishara kuwa Mradi huu una baraka za Mwenyezi Mungu na utafanikiwa.

 

Baada ya kusema hayo:

 

Mungu Ubariki Mradi Huu!

 

Mungu Ibariki Kampuni ya Arab Contractors!

 

Mungu Ubariki Uhusiano wa Tanzania na Misri!

 

Mungu Ibariki Tanzania.

 

Mungu Ibariki Afrika!

 

“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”