Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE KIKAO KAZI NA VIONGOZI WA MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA PAMOJA NA TAASISI NYINGINE ZA USIMAMIZI UKUMBI WA MWALIMU JULIUS NYERERE, TAREHE 10 DESEMBA, 2018

Monday 10th December 2018

 

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE KIKAO KAZI NA VIONGOZI WA MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA PAMOJA NA TAASISI NYINGINE ZA USIMAMIZI

UKUMBI WA MWALIMU JULIUS NYERERE,

 TAREHE 10 DESEMBA, 2018

 

Mheshimiwa Philip Mpango,

         Waziri wa Fedha na Mipango;

 

Waheshimiwa Mawaziri wengine mliopo;

Mheshimiwa Balozi Mhandisi John Kijazi,

Katibu Mkuu Kiongozi;

 

Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa mliopo;

Ndugu Makatibu Wakuu mliopo;

Prof. Frolens Luoga, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania;

Ndugu Charles Kichere, Kamishna Mkuu

wa Mamlaka ya Mapato Tanzania pamoja

na Watendaji wengine wa TRA;

 

Wakuu wa Taasisi nyingine za Serikali mliopo;

Ndugu Makatibu Tawala wa Mikoa;

Mabibi na Mabwana:

Kwanza kabisa, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha tukutane hapa. Aidha, napenda nitumie fursa hii kuwapongeza waandaji, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa maandalizi mazuri ya kikao hiki. Nafahamu kuwa muda wa kuandaa kikao hiki ulikuwa mdogo; lakini mmejitahidi hadi kukifanikisha. Hongereni sana.

Kikao hiki, kimsingi, kina madhumuni makubwa mawili. Kwanza, kujadili suala la ukusanyaji mapato nchini, hususan mapato ya kodi. Na pili, kubadilishana mawazo ya namna ya kuboresha mazingira ya biashara nchini; ili hatimaye tuweze kuongeza uzalishaji pamoja na kukuza shughuli za kiuchumi (viwanda, kilimo, biashara, uwekezaji, n.k.). Hii ndio sababu kwenye kikao hiki, tumewaalika pia Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa. Hawa ni wadau muhimu katika masuala ya ukusanyaji kodi na pia kwenye uboreshaji wa mazingira ya biashara nchini.

 

Waheshimiwa Mawaziri;

Ndugu Watendaji wa Taasisi mbalimbali mliopo;

Suala ukusanyaji mapato, hususan mapato ya kodi, ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi. Wamerekani wana usemi “Hapa duniani kuna mambo mawili tu ya uhakika: kifo na kulipa kodi”. Aidha, Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusema “Serikali isiyokusanya kodi ni Serikali mufilisi/iliyofilisika. Ni Serikali ya wala rushwa”. Hii inadhihirisha kuwa suala la ukusanyaji kodi ni muhimu sana katika nchi.

 

Ni kwa sababu hiyo, napenda niwapongeze watendaji wote wa TRA kwa kazi kubwa mnayofanya ya kukusanya kodi. Kwa hakika, kazi yenu ni ngumu sana. Tangu enzi na enzi, watoza kodi ni watu wasiopendwa. Kwa Wakristu, watakuwa wakifahamu habari za Zakayo. Alichukiwa na watu kwa sababu ya kazi yake ya kutoza kodi.

Nitumie fursa hii pia kuwapongeza wafanyakazi wa TRA kwa jitihada mbalimbali mnazofanya za kuongeza mapato. Wakati Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani, wastani wa makusanyo ya kodi kwa mwezi yalikuwa shilingi bilioni 850, lakini sasa ni shilingi trilioni 1.3. Hongereni sana.

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Licha ya mafanikio hayo yaliyopatikana katika ukusanyaji kodi, ni wazi kuwa mfumo na taratibu zetu za kodi bado zina mapungufu. Baadhi ya mapungufu tuliyonayo ni wigo mdogo wa walipa kodi. Nchi yetu ina wigo mdogo sana wa kodi (tax base) kwa uwiano wa Makusanyo ya Kodi na Pato la Taifa (GDP) ukilinganisha na nchi nyingi za Afrika. Naomba nitoe takwimu chache zifuatazo:

 

Nchi

Idadi ya watu

Idadi yaw a walipa kodi

Uwiano wa kodi kwa GDP  (%)

Tanzania

52,554,628

2,273,153

12.8

Kenya

46,600,000

3,940,00

18.5

Rwanda

11,671,371

172,422

15.8

Uganda

37,746,217

1,320,691

14.2

Burundi

10,400,938

22,591

13.0

Afrika Kusini

56,522,000

19,980,110

26.0

Botswana

2,254,021

734,470

14

Zambia

16,405,229

872,748

15.8

Msumbiji

27,128,530

5,321,669

18.0

Namibia

2,368,747

666,763

12

 

Wigo huu mdogo, kimsingi, unatokana na nchi yetu kushindwa kutumia vizuri vyanzo vya mapato vilivyopo katika kukusanya kodi. Kwanza, tumeshindwa kurasamisha sekta isiyo rasmi (informal sector), ambayo inakadiriwa kufikia asilimia 60 – 70. Hivi sasa tunakusanya kwenye sekta rasmi tu, ambayo ni asilimia 30 hadi 40. Hii maana yake ni kwamba tunakosa fedha nyingi kutoka sekta isiyo rasmi (kwenye kilimo, ufugaji, nyumba, huduma (hoteli), n.k.).

Aidha, nchi yetu bado haijafanikiwa kutumia vizuri rasilimali zake katika kukusanya mapato, na hasa ya kodi. Kwa mfano, Ripoti ya Kamati Maalum ya Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu Uvuvi wa Bahari Kuu ilibainisha, na napenda ninukuu “kiwango cha mapato ambayo Taifa linapoteza kwa kipindi cha miaka 9 iliyopita (2009 – 2017) inakadiriwa kufikia shilingi trilioni 5.985, mwisho wa kunukuu. Hiki ni kiwango kikubwa sana; na hii ni kwenye sekta ya uvuvi peke yake.  Upotevu mkubwa wa mapato kama huo pia  upo kwenye sekta za madini na uchimbaji wa gesi asilia. Hivyo basi, Wizara ya Fedha na TRA hamna budi kulifanyia kazi.

Ukiachilia mbali tatizo la kuwa na wigo mdogo wa walipa kodi, ufanisi katika kusanya kodi pia ni mdogo. Ni kweli kuwa, kama nilivyotangulia kusema, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita ukusanyaji kodi umeongeza. Hata hivyo, kiwango tunachokusanya bado ni kidogo; na nitatoa mfano. Kwenye Mwaka wa Fedha 2013/2014, wenzetu wa Kenya walipanga kukusanya Dola za Marekani bilioni 9.74, na walifanikiwa kukusanya Dola za Marekani bilioni 9.64. Sisi tulipanga kukusanya Dola za Marekani bilioni 4.8, tukakusanya Dola za Marekani bilioni 4.4. Katika Mwaka wa Fedha uliopita (2017/2018), Kenya ilipanga kukusanya Dola za Marekani bilioni 15.4, wakakusanya Dola za Marekani bilioni 14.3. Sisi tulipanga kukusanya Dola za Marekani bilioni 7.67, tukakusanya Dola za Marekani bilioni 6.8. Huu uthibitisho kuwa ufanisi wa ukusanyaji kodi nchini bado ni mdogo.

Tatu, viwango vya kodi nchini vipo juu. Yapo malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu viwango vya kodi wanavyotozwa. Na mfano mzuri ni kwenye kodi ya majengo. Kodi za majengo ni kubwa sana. Hii ndio sababu mapato na idadi ya majengo yaliyosajiliwa mpaka sasa ni ndogo sana. Mathalani, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, tumekusanya shilingi bilioni 74.5 tu; na majengo yaliyosajiliwa mpaka sasa ni milioni 1.6. Hiki ni kichekesho. Kwa ukubwa wa nchi yetu na idadi ya watu iliyopo, takriban milioni 55, haiwezekani tuwe na idadi hiyo ya majengo. Kilichofanya msajili idadi ndogo ni viwango vyenu kuwa juu.

Hivyo basi, napenda nitumie fursa hii kurudia tena maelekezo yangu niliyowahi kutoa siku za nyuma kwa TRA, kwamba, kodi ya nyumba iwe shilingi elfu kumi kwa nyumba za kawaida na shilingi elfu ishirini kwa nyumba za ghorofa zilizopo maeneo ya Wilayani na Vijijini; na shilingi 50,000 kwa nyumba za kawaida na kwa kila sakafu (floor) moja ya nyumba ya ghorofa kwa maeneo ya mijini. Na kodi hizo zitozwe kwa kuzingatia hati ya viwanja na sio idadi ya nyumba zilizopo kwenye kiwanja husika.

Nne, ni kuendelea kuwepo kwa mianya ya ukwepaji kodi. Pamoja na jitihada zilizofanyika, bado kuna ukwepaji mkubwa wa kodi kwenye Bonded Warehouses; EPZA, ICDs, maduka ya kubadilisha fedha za kigeni, bandari bubu pamoja na njia za magendo mipakani; na halikadhalika kupitia wafanyabiashara wanaosafirisha na kuingiza bidhaa nchini.  Vilevile, baadhi ya wafanyabiashara, kwa kutumia udhaifu uliopo kwenye sheria zetu, wameendelea kukwepa kodi kwa ujanja wa kuongeza gharama za uzalishaji au kuongeza gharama za uendeshaji wa kampuni/masharika yao (transfer pricing and management fee). Zipo kampuni ambazo kila mwaka zinatangaza kupata hasara ili kukwepa kulipa kodi.

Tano, ni matatizo ndani ya TRA yenyewe. Mgawanyo wa watumishi usioendana na potentiality na majukumu katika mikoa na wilaya. Baadhi ya maeneo kuna watumishi wengi, lakini tija haionekani. Aidha, matumizi ya TEHAMA na mifumo ya kieletroniki, yakiwemo matumizi ya EFD, bado hayajaimarika na hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa mapato. Vilevile, kuna suala la kukosekana kwa ushirikiano ndani ya TRA. Mathalan, Meneja wa Mikoa na Wilaya hawawajibiki kwenye masuala ya Forodha na Huduma Saidizi kwa sababu tu wao wanatoka Idara moja ya Mapato ya Ndani. Na kwa upande mwingine, wanaohusika na Forodha nao hawawajibiki kwa Mameneja wa Mikoa na Wilaya isipokuwa kwa Kamishna wa Idara Kuu ya Forodha. Hili ni tatizo ambalo TRA ni lazima mlirekebishe.

Matatizo mengine yaliyopo kwenye TRA ni kupanga malengo bila kufanya utafiti; kuruhusu kuwepo wa watu wanaowakilisha walipa kodi kinyume cha sheria. Vilevile, baadhi ya watumishi wa TRA sio waaminifu. Mathalan, zipo tuhuma kuwa ni wafanyabiashara wachache tu wenye uhusiano na watumishi wa TRA ndio wameruhusiwa kuingiza mashine za EFD na risiti zake. Aidha, zipo tuhuma kuwa, kwa kutumia Mfumo wa Ukadiriaji wa Kodi kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati (Presumptive tax assessment); baadhi ya watumishi wamekuwa wakiomba rushwa ama kuwababimbikiza kodi kubwa wafanyabiashara wadogo na hivyo kulazimika kufunga biashara zao; hali inayofanya waichukie Serikali yao.

Hizo nilizotaja ni baadhi tu ya changamoto zinahusu mifumo na taratibu za kodi nchini. Lakini, ukiachilia mbali mapungufu hayo ya ukusanyaji kodi, nchi yetu pia haifanyi vizuri sana katika kukusanya mapato yasiyo ya kodi. Ni kweli kuwa tumefanikiwa kuongeza ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi kutoka shilingi bilioni 284 Mwaka wa Fedha 2010/2011 hadi kufikia shilingi trilioni 2.2 katika Mwaka wa Fedha 2017/18. Hata hivyo, kiwango hiki bado ni kidogo.

Hivyo basi, natoa wito kwa mamlaka zote zinazohusika na ukusanyaji wa mapato nchini, ya kodi na yale yasiyo ya kodi, zikiwemo Halmashauri, kuongeza bidii katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameeleza hivi punde kuwa, fedha za mikopo na misaada kutoka kwa wahisani na wafadhili zinakuja taratibu sana; na hata zikija, wakati mwingine zinaambatana na masharti magumu. Hivyo basi, ni lazima sisi wenyewe tutafute mbinu za kujitegemea kifedha. Faida za kujitegemea kifedha zipo nyingi baadhi zimeanza kuziona; tumenunua ndege mpya saba kwa fedha zetu wenyewe, tunajenga reli, meli; tunaboresha huduma za jamii, ikiwemo elimu, maji na afya. Kesho kutwa tunaweka saini Mkataba wa kutekeleza mradi wa umeme wa Bonde la Mto Rufiji. Hivyo, narudia kuzihimiza mamlaka husika kuongeza bidii ya ukusanyaji mapato ya Serikali. Na katika kutekeleza jukumu, msimwogope au kumwonea mtu yeyote.

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Sambamba na matatizo hayo ya ukusanyaji mapato niliyotaja, mazingira ya kufanya biashara nchini pia sio mazuri sana. Tuna shida katika kutoa vibali vya uwekezaji, huduma za usafirishaji, umeme, utitiri wa taasisi za usimamizi unaombatana na kodi, ada, ushuru na tozo mbalimbali. Ni kweli kuwa, katika miaka ya hivi karibuni, tumejitahidi sana kuimarisha miundombinu ya usafiri pamoja na upatikanaji wa huduma za umeme; ambapo, kwa mfano kesho kutwa tunaweka saini ya ujenzi wa mradi mkubwa wa kufua umeme wa Bonde la Mto Rufiji.

Hata hivyo, bado tuna matatizo ya ucheleweshaji kwenye Bandari, vizuizi barabarani (rasmi na visivyo rasmi), n.k. Wafanyabiashara wanahangaika sana kutoa mizigo yao bandarini; na wawekezaji inawachukua muda mrefu kupata vibali vya uwekezaji. Hii ndio sababu kwenye kikao hiki, tumewaalika pia Mamlaka ya Bandari, Shirika la Reli, Benki Kuu ya Tanzania, TIC, BRELA, TBS, TFDA, Mkemia Mkuu wa Serikali; lengo ni kutaka kutafuta ufumbuzi wa matatizo hayo yote. Nina imani, watu wa Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Idara ya Kazi, NEMC, OSHA, pia wapo. Kama hawapo, mambo yatakayoamuliwa hapa, yafikishwe kwao.

Waheshimiwa Mawaziri;

Ndugu Watendaji wa Taasisi mbalimbali;

Nimeeleza mengi. Hata hivyo, kabla sijahitimisha hotuba yangu, naomba niseme suala moja la mwisho.  Ndugu zangu, upo uhusiano wa karibu sana kati ya mifumo au taratibu za kodi kwa upande mmoja; na kuimarika kwa mazingira ya biashara, kuongezeka kwa uzalishaji na mapato kwa upande mwingine. Taratibu za kodi zikiwa rahisi na viwango vyake vikiwa chini; watu uhamasika kufanya biashara na kuwekeza; na kama watu wengi watafanya biashara na kuwekeza, maana mapato nayo yataongezeka. Lakini kinyume chake; viwango vikiwa juu na taratibu zikiwa ngumu, mazingira ya biashara yanakuwa magumu, watu wanashindwa kufanya biashara na kuwekeza; na hatimaye mapato yanapungua. Kwa kuzingatia hayo, napenda kutoa wito ufuatao:

 

Kwanza, ni kwa TRA na mamlaka nyingine zinazohusika na ukusanyaji wa mapato nchini. Hakikisheni mnatengeneza mazingira rahisi ya watu kulipa kodi. Imarisheni mifumo ya kielektroniki ili watu wasilazimike kutembea umbali mrefu ama kutumia muda mwingi kulipa kodi. Muda ni mali. Aidha, kama nilivyosema hivi majuzi pale Arusha, pitieni upya viwango vya kodi mnazotoza. Watu wengi wanawalalamikia kuhusu viwango vyenu. Viwango vya kodi vikiwa chini, sio tu itawapunguzia gharama za kuwafuatilia walipa kodi bali pia itapunguza vitendo vya rushwa. Sambamba na hilo, nawasihi mpanue wigo wa walipa kodi.

Pili, ni kwa taasisi zinazohusika na masuala ya biashara na uwekezaji nchini. Nia na makusudi ya Serikali kuanzisha taasisi hizi ilikuwa kuongeza ufanisi. Lakini, kwa bahati mbaya, nyingi zimegeuka kuwa kikwazo. Wamekuwa kikwazo Bandarini; lakini pia pale TIC. Hivyo, natoa wito kwa taasisi hizo kujirekebisha, ikiwa ni pamoja na Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, NEMC, Idara ya Kazi. Nahimiza pia TPA pamoja na Shirika la Reli kuzidi kuboresha huduma zenu.

Tatu, ni kwenu Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa. Kama nilivyosema awali, ninyi ni wadau muhimu sana katika masuala ya kodi na uboreshaji wa mazingira ya biashara nchini. Sheria ya Kodi ya Mapato ya Tanzania ya Mwaka 2004 pamoja na Kanuni zake, Kanuni ya 41 (1), imeanzisha Kamati ya Wilaya ya ushauri kuhusu masuala ya kodi katika Wilaya. Aidha, Kanuni ya 41 (2) inamtaja Mkuu wa Wilaya kuwa Mwenyekiti na Afisa Mapato wa Wilaya wa TRA kuwa Katibu. Miongoni mwa watu wanaoweza kuteuliwa kuwa Wajumbe wa Kamati hii wanachaguliwa na Mkuu wa Mkoa, ambaye naye ana wajibu wa kudai kumbukumbu za vikao vya Kamati ili kufahamu masuala mbalimbali ya kodi katika Mkoa wake. Sina hakika, kama Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa mnafahamu hili. Na hii ndio sababu hasa ya kuwajumuisha kwenye kikao chetu hiki, ili mkasimamie haya yote mkishirikiana na viongozi walio chini yenu. Wakuu wa Mikoa pia mna wajibu wa kutengeneza mazingira mazuri ya biashara katika maeneo yenu, ikiwemo kutenga maeneo maalum ya kufanya biashara, hususan kwa wafanyabiashara wadogo, na pia maeneo ya uwekezaji.

Nne, ni kwa Watanzania wenzangu kwa ujumla. Napenda niwahimize kuendelea kulipa kodi. Kodi ndiyo inawezesha Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo na pia kuboresha huduma za jamii. Najua bado wapo Watanzania wachache wenye kuona fahari kukwepa kodi.  Nitoe wito kwa TRA kuendelea kuwaelimisha watu wa namna hiyo. Zaidi ya hapo, hakikisheni mnatoa adhabu kali kwa wakwepa kodi.

Waheshimiwa Mawaziri;

Ndugu Watendaji wa Taasisi mbalimbali;

Napenda kuhitimisha kwa kurudia tena kuwapongeza TRA kwa kuandaa Mkutano huu. Aidha, nawapongeza wote mliohudhuria Kikao hii. Nawatakia majadiliano mema, na yote mtakayoyaamua hakikisheni kuwa mnayatekeleza. Binafsi, nina matumaini makubwa kuwa, baada ya kikao hiki, tutaanza kuona mageuzi makubwa ya kiutendaji katika TRA pamoja na taasisi nyingine zinazohusika na masuala ya ukusanyaji mapato na uboreshaji wa mazingira ya biashara nchini.

 

Mwisho kabisa, kutokana na kasi ndogo ya zoezi la usajili wa wafanyabiashara wadogo, Ofisi yangu (TAMISEMI) imeamua kuandaa Vitambulisho vya Wafanyabiashara Wadogo, ambavyo vitawawesha kufanya shughuli zao kwa uhuru. Baada ya kumaliza hotuba yangu, nitamkabidhi kila Mkuu wa Mkoa vitambulisho 25,000 kwa ajili ya kwenda kuvigawa kwa wafanyabiashara wadogo kwenye mikoa yao. Kitambulisho hiki, ambacho kimewekewa alama za usalama zisizogushika kwa urahisi, kimsingi kitatolewa bure. Hata hivyo, wafanyabiashara wadogo itabidi wachangie gharama ndogo utenganezaji, kiasi cha shilingi 20,000 tu. Mfanyabiashara anayestahili kupata kitambulisho hiki ni mwenye kufanya mauzo (turnover) yasiyozidi shilingi milioni 4 kwa mwaka. Lakini, napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa wafanyabiashara wadogo watakaopata vitambulisho hivyo, kutokubali kutumiwa na wafanyabiashara wakubwa kukwepa kodi. Aidha, hakikisheni kuwa shughuli zenu  mnazifanya kwenye maeneo yaliyoruhusiwa.

Mungu zibariki Mamlaka za Ukusanyaji Mapato nchini!

Mungu Zibariki Mamlaka zote zenye Kuhusika na  Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara nchini!

 

Mungu Ibariki Tanzania!

 

“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”