Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUPOKEA GAWIO KUTOKA KAMPUNI, TAASISI NA MASHIRIKA MBALIMBALI DAR ES SALAAM, TAREHE 23 JULAI, 2018

Monday 23rd July 2018

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUPOKEA GAWIO KUTOKA KAMPUNI, TAASISI NA MASHIRIKA MBALIMBALI

DAR ES SALAAM, TAREHE 23 JULAI, 2018

 

Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango,

Waziri wa Fedha na Mipango;

 

Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wengine mliopo;

 

Mheshimiwa Mhandisi Evarist Ndikilo,

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;

 

Mheshimiwa Kate Kamba, Mwenyekiti wa CCM,

Mkoa wa Dar es Salaam;

 

Waheshimiwa Wenyeviti wa Kamati za Bunge za Uwekezaji na Mitaji ya Umma; Hesabu za Serikali; pamoja na Bajeti;

 

Waheshimiwa Wabunge wengine mliopo;

Ndugu Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu mliopo;

 

Waheshimiwa Mabalozi mliopo

 

Waheshimiwa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;

 

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa

pamoja na Dini mliopo;

 

Ndugu Athumani Mbuttuka, Msajili wa Hazina;

 

 Wenyeviti wa Bodi, Watendaji Wakuu pamoja na Watumishi wa Taasisi, Makampuni na Mashirika mbalimbali mliopo;

 

Wageni wote Waalikwa, Mabibi na Mabwana:

 

Napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa uzima na kutuwezesha tukutane hapa. Aidha, namshukuru Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Philip Mpango, kwa kunialika kwenye tukio hili la kupokea gawio la shilingi bilioni 717.56 kutoka kwenye taasisi, makampuni na mashirika yapatayo 40, ambayo Serikali ina hisa ama inayamiliki kwa asilimia mia moja. Kwa hakika, hili ni tukio muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu; hivyo basi, napenda kurudia tena kukushuru Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa kunialika.

 

Napenda pia kutumia fursa hii, hapa mwanzoni kabisa, kutoa shukrani na pongezi zangu nyingi kwa Wenyeviti wa Bodi, Watendaji Wakuu pamoja Watumishi wote wa Taasisi pamoja na Makampuni yote, ambayo leo yanakabidhi gawio kwa Serikali. Gawio hili litaiwezesha Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo na pia kuboresha huduma mbalimbali za jamii. Hivyo basi, tunawashukuru na hongereni sana.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Duniani kote, Serikali zina njia kuu mbili za kupata mapato yake. Njia ya kwanza ni kupitia makusanyo ya kodi.  Wamerekani wana usemi usemao, “Nothing is certain but death and taxes (maanake ni kwamba, kuna mambo mawili tu ambayo ni hakika au ya lazima duniani, kifo na kodi)”. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, naye aliwahi kusema, nanukuu “Serikali isiyokusanya kodi ni Serikali ya wala rushwa”, mwisho wa kunukuu.

 

Hii inaonesha kuwa, kodi ni chanzo muhimu cha kukusanya mapato ya Serikali. Na ninafurahi kuona kuwa, katika miaka ya hivi karibuni, licha ya kwamba bado hatujaweza kufikia malengo yetu kwa asilimia 100, Serikali imejitahidi sana kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya kodi. Mathalan, wakati Serikali ya Awamu ya Tano ikiingia madarakani, mwaka 2015, wastani wa makusanyo ya kodi kwa mwezi ulikuwa shilingi bilioni 850. Hivi sasa wastani kwa mwezi ni shilingi trilioni 1.3, ongezeko la takriban asilimia 65. Mapato kwa mwaka pia yamekuwa yakiongezeka. Katika mwaka wa Fedha 2016/2017 tulikusanya shilingi trilioni 14.4, lakini kwenye Mwaka wa Fedha uliopita (2017/2018), tumekusanya shilingi trilioni 15.5.

 

Kwa tathmini yangu binafsi, ongezeko hili limetokana na mambo makubwa mawili. Kwanza, hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuziba mianya ya ukwepaji kodi. Pili, wananchi wengi kuhamasika kulipa kodi na hasa baada ya kuona kodi zao zinatumika vizuri. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuipongeza Mamalaka ya Mapato (TRA) kwa kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya kodi. Waswahili husema “mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni”. Licha ya changamato ambazo bado zipo, lakini wamejitahidi. Hongereni TRA.

 

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Nitumie fursa hii pia kuwapongeza Watanzania wote kwa kuhamasika kulipa kodi. Endeleeni na moyo huo huo. Kodi zenu ndizo zinaiwezesha Serikali kutekeleza miradi ya miundombinu (ujenzi wa reli, barabara, bandari, viwanja vya ndege, utekelezaji wa miradi ya umeme, n.k.). Mathalan, kabla ya kuja hapa, nimetoka kushuhudia uwekaji saini Mkataba wa Ujenzi wa Daraja la Salender. Daraja hili, ambalo litapita kwenye Bahari, litajengwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 250 ambazo ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Korea Kusini, na ambazo baadaye tutazilipa kupitia kodi zenu.

 

Zaidi ya hapo, kodi tunazokusanya kutoka kwa wananchi ndizo zinaiwezesha Serikali kuboresha huduma mbalimbali za jamii kama vile afya, elimu na maji. Hivyo basi, narudia tena kuwasihi Watanzania wenzangu kuendelea kulipa kodi ili kuiwezesha Serikali kutekeleza shughuli za maendeleo.

 

 

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Ukiachilia mbali mapato ya kodi, njia ya pili inayoiwezesha Serikali kupata mapato, ni kupitia vyanzo visivyo vya kodi. Kuna vyanzo vingi visivyo vya kodi, lakini kimojawapo ni kupokea gawio kutoka kwenye taasisi au mashirika ambayo Serikali imefanya uwekezaji. Mathalan, hivi punde tumesikia kuwa Serikali yetu imewekeza kiasi cha shilingi trilioni 49.05 kwenye taasisi na makampuni mbalimbali. Na kama mtakavyokumbuka, wakati nikipokea gawio la TTCL, nilisema kuwa tunayo mashirika zaidi ya 90 yenye kustahili kutoa gawio kwa Serikali.

 

Lakini, licha ya idadi hiyo kubwa ya taasisi pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanyika, niwe mkweli, nchi yetu bado haijanufaika na uwekezaji ilioufanya. Gawio tunalopata ni dogo sana na mashirika mengi bado hayatoi gawio kwa Serikali. Mathalan, mwaka 2014/2015 tulipata gawio la shilingi bilioni 130.686 kutoka mashirika 24 tu. Mwaka 2015/2016 mashirika 25 yalitoa gawio la shilingi bilioni 249.3.

 

Hali hii haikuturidhisha. Kama mjuavyo, huwezi kuendesha nchi kwa kutegemea mapato ya kodi peke yake. Na baada ya kufanya utafiti, tuligundua mambo kadhaa yanayofanya taasisi na mashirika yetu yasitoe ama yatoe gawio dogo. Baadhi ya mambo hayo ni: uongozi mbovu; kutokuwepo kwa ufuatiliaji madhubuti, hususan kwenye mashirika ambayo Serikali ina hisa; udanganyifu; ubadhirifu; rushwa; n.k. Baada ya kugundua hayo, tulianza kuchukua hatua. Na ninafurahi kuona kuwa, hatua zetu zimeanza kuzaa matunda. Kama mlivyosikia, leo tunapokea gawio la shilingi bilioni 717.56. Haya ni mafanikio makubwa sana.

 

Hivyo basi, napenda kurudia tena kuwapongeza Wenyeviti wa Bodi, Watendaji Wakuu, Watumishi, Wasimamaizi pamoja na watu wote waliofanikisha Makampuni haya yote kutoa gawio kwa Serikali kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/2018. Kwa namna ya pekee kabisa, napenda kuzitambua taasisi tatu zilizotajwa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha ambazo zimevuka malengo ya kutoa gawio kwa Mwaka wa Fedha uliopita. Hongereni sana. Binafsi nimefurahishwa zaidi na Shirika kama la TAZAMA, ambalo halikuwahi kutoa gawio, lakini leo limetoa. Hongereni sana. Ni matumaini yangu kuwa, katika Mwaka huu wa Fedha tuliouanza, makampuni na mashirika mengi yatatoa gawio kwa Serikali.

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Hatukuja hapa kusikiliza hotuba. Tumekuja hapa kupokea fedha. Na kama mjuavyo, kwenye masuala ya fedha, huwa hakuna maneno mengi. Hata hivyo, kabla sijahitimisha hotuba yangu, naomba mniruhusu niseme masuala machache ya mwisho.

 

Suala la kwanza, napenda kurudia tena agizo langu kwa Msajili wa Hazina kuhakikisha mashirika na taasisi zote zenye kustahili kutoa gawio kwa Serikali zinafanya hivyo. Ni kweli, katika miaka hii miwili, gawio kwa Serikali kutoka kwenye taasisi na mashirika limeongezeka. Hata hivyo, kiasi kinachopatikana bado ni kidogo sana ukilingaisha na uwekezaji uliofanyika. Kama nilivyosema, tumewekeza zaidi ya shilingi trilioni 49. Haiwezekani tupate gawio la shilingi bilioni 717 tu kwa mwaka. Hivyo basi, Msajili wa Hazina hakikisha mashirika yote yanatoa gawio. Yatakayoshindwa, uongozi wake ubadilishwe ama mashirika hayo yafutwe kabisa.

 

Suala la pili, ambalo nitalieleza kwa kirefu kidogo, ni kuhusu ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali, na hasa kwenye masuala ya uwazi katika biashara. Napenda nisisitize kuwa Serikali inatambua mchango wa sekta binafsi katika kuchangia maendeleo ya taifa letu. Na naahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa sekta binafsi ya hapa nchini. Lakini, pamoja na ahadi hiyo, napenda niwe mkweli. Baadhi ya washirika wetu kutoka sekta binafsi sio waaminifu na wana tabia ya kufanya udanganyifu. Napenda nitoe mifano michache.

 

Mabibi na Mabwana;

Kama mjuavyo, baadhi ya kampuni au mashirika yanayofanya kazi hapa nchini yana kampuni zake tanzu au mama nje ya nchi. Hili kimsingi halina ubaya. Ubaya unakuja pale ambapo kampuni hizo tanzu au kampuni mama; zinapotumika kufanya udanganyifu wa kukwepa kodi, tozo, malipo ya mrahaba pamoja na gawio. Na udanganyifu huo mara nyingi hufanyika kwa kuongeza gharama za uendeshaji ili kupunguza kiwango cha faida ambacho kampuni zilizopo hapa nchini zinapata; ama zinaonekane zinapata hasara. Ujanja huu kwa kitaalamu unaitwa transfer pricing.

 

Mbinu mojawapo inayotumika ni katika ununuzi wa mitambo na vipuri. Ili kupandisha gharama za uendeshaji, kampuni za hapa nchini huagiza vifaa hivyo kupitia kampuni tanzu au mama zilizopo nje ili Serikali isifahamu gharama halisi. Kampuni hizo tanzu zikishanunua vifaa hivyo huviuza kwa kampuni za hapa nchini kwa bei ya juu; wakati mwingine mara tano zaidi ya bei halisi. Na kwa vile sheria zetu za kodi na uwekezaji zinatoa misamaha ya kodi, gharama hizi za kununua vifaa zinaendelea kukatwa katika mapato ya kampuni hizo miaka nenda miaka rudi; na hivyo kuzifanya kampuni hizo zisilipe kabisa ama zilipe kiwango kidogo sana cha kodi na tozo mbalimbali.

 

Njia nyingine inayotumika ni kupitia mikopo. Kampuni za hapa nchini huchukua mikopo kwa riba kubwa kutoka kwenye kampuni zao tanzu au mama zilizopo nje ya nchi. Hii inaongeza gharama za uendeshaji na kuzifanya kampuni za hapa nchini kila wakati zionekane zinajiendesha kwa hasara na hivyo kuzifanya zisilipe kodi. Lakini, cha kushangaza ni kwamba, licha ya kupata hasara, makampuni hayo yanaendelea kufanya kazi.

 

Mbinu nyingine inayotumika na makampuni kukwepa kutoa gawio au kulipa kodi na tozo mbalimbali, ni kupitia gharama za usimamizi (yaani management fee). Kampuni hizi hulipa menejimenti zao gharama kubwa; na wakati mwingine huajiri kampuni nyingine kuzisimamia kampuni zao. Hii inapandisha gharama za uendeshaji na kuzifanya kampuni husika zionekane zinapata hasara kila kukicha na hivyo zishindwe kulipa kodi na tozo nyingine.

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Mambo haya yote kwa ujumla wake sio tu yanapunguza mapato kwa Serikali, bali pia yanasababisha kuwepo kwa hali ya kutoaminiana kati ya Serikali na Sekta Binafsi. Hivyo basi, nitumie fursa hii kuisihi sana sekta binafsi ya hapa nchini kushirikiana kwa karibu na Serikali. Fanyeni biashara zenu kwa uwazi. Acheni usiri. Kama unaendesha shughuli zako kihalali, kwanini ufichefiche?

 

Mathalan, nimearifiwa kuwa ipo kampuni moja ya madini ilikataa ombi la Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali la kwenda kuangalia mahesabu ili kujiridhisha kama kodi iliyolipwa TRA ni sahihi. Nimeambiwa kuwa Kampuni hiyo imekataa kwa kisingizio kuwa yenyewe ni kampuni binafsi. Wasichofahamu ni kwamba, Sheria ya Ukaguzi wa Umma inaipa Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali mamlaka ya kupata taarifa kutoka mtu au taasisi yoyote katika kutimiza majukumu yake ya ukaguzi katika Serikali.

 

Hivyo basi, nirudie tena wito wangu kwa sekta binafsi kutoa ushirikiano kwa Serikali. Sambamba na hilo, natoa wito kwa taasisi zote za Serikali zenye dhamana ya kusimamia uwajibikaji na kufuatilia shughuli za uwekezaji katika maeneo mbalimbali (madini, gesi, uvuvi wa bahari kuu, uzalishaji, kampuni za simu pamoja na taasisi za fedha) kuhakikisha zinatekeleza majukumu yake ipasavyo. Wakati mwingine “tunaliwa” kwa sababu ya uzembe wa watendaji wa Serikali. Hivyo basi, niziagiza mamlaka zote (TR, TIC, EPZA, CAG, TRA, BOT, n.k.) kutekeleza majukumu yenu.

 

Mathalan, natarajia kuwa, kuanzia sasa, Benki Kuu itahakikisha mikopo yote inayochukuliwa na kampuni za hapa nchini kutoka nje inasajiliwa kwa mujibu wa sheria. Aidha, natarajia, TRA itakuwa ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa biashara na mialama inayofanyika baina ya kampuni zenye mahusiano, hususan kampuni zilizopo hapa nchini na kampuni mama au tazu zilizopo nje, ili kudhibiti uhamishaji wa mali au utoroshaji wa faida. 

 

Suala la mwisho, ni kwa TRA tena. Awali, nimewapongeza kwa kuongeza ukusanyaji wa mapato. Lakini napenda niwapongeze pia kwa hatua zenu za hivi karibuni za kuanza kuwarasimisha watu kutoka sekta isiyo rasmi (machinga, mamalishe, n.k.) pamoja na kutoa msamaha wa riba na faini kwa wafanyabishara mliokuwa mkiwadai. Hizi ni hatua nzuri ambazo naamini zitapanua wigo wa walipa kodi na kuongeza mapato kwa Serikali. Hongereni sana.

 

Hata hivyo, hampaswi kubweteka. Ni lazima muendelee kuboresha mifumo yenu ya ukusanyaji kodi, kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulipa kodi na pia kuhakikisha viwango vya kodi mnavyoweka vinalipika. Zaidi ya hapa, napenda niseme, na hapa napenda niwe muwazi,  baadhi ya watumishi wa TRA sio waadilifu. Wanapokea rushwa na kunyanyasa walipa kodi. Na tabia hizi ndizo zimekuwa zikichafua taswira ya TRA pamoja na Serikali. Hivyo basi, natoa wito kwa Kamishna Mkuu wa TRA kuchukua hatua kali dhidi ya watumishi wa namna hiyo. Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliwahi kusema, nanukuu, “uvundo wa yai moja bovu ni mkali zaidi kuliko harufu ya mayai mengi mazima”, mwisho wa kuukuu. Msiwaache watu wachache wawachafue.

 

Lakini, nimpongeze Kamishna Mkuu kwa hatua mbalimbali anazochukua. Mara nyingi namuona akitembelea Mikoa mbalimbali kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kulipa kodi. Ni matumaini yangu kuwa endapo maafisa wengine wataiga mfano wake, basi makusanyo ya kodi yatazidi kuimarika.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Napenda kuhitimisha kwa kurudia tena kumshukuru Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa kunialika kwenye shughuli hii. Aidha, nayapongeza tena makampuni yote 43 yaliyotoa gawio kwa Serikali katika Mwaka wa Fedha ulioisha wa 2017/2018. Napenda pia kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuishauri Serikali katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo.

 

Nawashukuru pia Waheshimiwa Mabalozi kwa kushiriki nasi kwenye tukio hili. Tunawasihi muendelee kuwahimiza na kuwahamasisha wawekezaji waaminifu kwenye nchi zenu kuja kuwekeza hapa nchini. Mwisho kabisa lakini sio kwa umuhimu, navishukuru na kuvipongeza Vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama kwa kusimamia amani na utulivu wa nchi yetu. Bila amani, hakuna kodi. Bila amani, hakuna gawio; na bila ya amani hakuna maendeleo. Hivyo basi, navipongeza vyombo vya ulinzi pamoja na Watanzania wote kwa ujumla kwa kuendelea kuitunza amani yetu.

 

Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kutekeleza jukumu lililonileta la kupokea gawio kutoka taasisi mbalimbali.

 

Mungu Zibariki Taasisi Zilizotoa Gawio!

Mungu Ibariki Tanzaia!

 

“Ahsanteni sana kwa Kunisikiliza”