Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA MWENYEKITI WA CHAMA CHA MAPINDUZI KWENYE UFUNGUZI WA MKUTANO MAALUM WA MAJADILIANO KATI YA CHAMA CHA KIKOMUNISTI CHA CHINA NA VYAMA VYA SIASA VYA NCHI MBALIMBALI ZA AFRIKA HOTELI YA SERENA, DAR ES SALAAM, TAREHE 17 JULAI, 2018

Tuesday 17th July 2018

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA MWENYEKITI WA CHAMA CHA MAPINDUZI KWENYE

UFUNGUZI WA MKUTANO MAALUM WA MAJADILIANO

 KATI YA CHAMA CHA KIKOMUNISTI CHA CHINA

NA VYAMA VYA SIASA VYA NCHI MBALIMBALI ZA AFRIKA

HOTELI YA SERENA, DAR ES SALAAM, TAREHE 17 JULAI, 2018

 

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa kutoka

Nchi mbalimbali za Afrika mkiongozwa na Mwenyeji

wenu Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally;

 

 Mheshimiwa Song Tao, Waziri wa Masuala ya Uhusiano wa

Kimataifa wa Chama cha Kikomunisti cha China;

 

Waheshimiwa Viongozi wa Chama na Serikali mliopo;

 

Waheshimiwa Wazee Wetu Wastaafu mliopo;

 

Mheshimiwa Wang Ke, Balozi wa China nchini;

 

Waheshimiwa Mabalozi wengine mliopo;

 

Waheshimiwa Wageni Wote Waalikwa;

 

Mabibi na Mabwana:

 

Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa. Binafsi, najisikia heshima kubwa kuwepo mahali hapa na kupata fursa hii adimu ya Kufungua Mkutano huu Maalum wa Majadiliano kati ya Chama cha Kikomunisti cha China na Vyama Siasa vya Afrika, unaofanyika kwa mara ya kwanza nje ya China hapa Dar es Salaam. Kwa niaba yangu binafsi, na kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Serikali pamoja na Watanzania wote, napenda niwakaribishe wageni wetu wote hapa nchini.

 

Nawakaribisha Viongozi wa Vyama vya Siasa kutoka nchi mbalimbali za Afrika, ambao nimearifiwa kuwa mnatoka kwenye nchi zaidi ya 40 za Afrika. Karibuni sana. Vilevile, na kwa namna ya pekee kabisa, napenda kuukaribisha nchini ujumbe kutoka Chama cha Kikomunisti cha China (the Communist Party of China – CPC), ukiongozwa na Mheshimiwa Song Tao, Waziri wa Masuala ya Mambo ya Nje wa CPC. Karibuni Tanzania. Karibuni sana Dar es Salaam.

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Napenda pia, hapa mwanzoni kabisa, kutumia fursa hii kuishukuru CPC kwa kuichagua Afrika kuwa sehemu ya kwanza nje ya China kufanya Mkutano huu. Kama mjuavyo, Mkutano wa Kwanza wa namna hii ulifanyika Beijing, China, tarehe 30 Novemba hadi 3 Desemba, 2017 na uliikutanisha CPC na Vyama Vya Siasa kutoka sehemu mbalimbali duniani. Hivyo basi, tunaishukuru CPC kwa kuichagua Afrika kuwa sehemu ya kwanza nje ya China kufanya Mkutano huu.

 

Vilevile, naishukuru CPC pamoja na Vyama vyote shiriki kwa kuichagua na kuridhia Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano huu. Tunawashukuru sana. Tunaahidi kuwa tutajitahidi kutimiza majukumu yetu ili Mkutano huu uwe wenye mafanikio makubwa. Na napenda niseme kuwa, hamjakosea kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano huu. Tanzania ni mahali sahihi kabisa pa kufanyia Mkutano huu. Zipo sababu nyingi zenye kufanya Tanzania iwe sehemu sahihi; lakini kwa sababu ya muda nitataja mbili. Kwanza kabisa, kama mjuavyo, mwenyeji wa Mkutano huu ni Chama Cha Mapinduzi (CCM); na sote hapa tunafahamu kuwa CCM ni miongoni mwa vyama vikongwe Barani Afrika, ambacho kimedumu madarakani kwa muda mrefu. Na kama mnavyofahamu, moja ya mila na desturi za Waafrika ni kuheshimu wakubwa. Hivyo basi, ni wazi kuwa uamuzi wa kufanya Mkutano huu hapa Tanzania ulikuwa sahihi kabisa.

 

Pili, kama ambavyo sote tunakumbuka, wakati wa harakati za kupigania uhuru wa Bara la Afrika, Tanzania ilikuwa Makao Makuu ya Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (Organization of the African Unity – OAU). Kupitia Kamati hiyo, ambayo ilikuwa chini ya Uenyekiti wa Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Tanzania ilikuwa kitovu cha harakati za Ukombozi wa Bara letu. Wapigania Uhuru kutoka nchi mbalimbali waliishi na kupata misaada mbalimbali, ikiwemo mafunzo na mbinu za mapambano, na hatimaye kufanikiwa kuzipatia nchi zao uhuru. Hivi sasa nchi za Afrika zipo kwenye harakati za kujikomboa kiuchumi na sisi Tanzania tumedhamiria kuongoza mapambano haya ya kiuchumi. Hivyo basi, ni sahihi kabisa Mkutano huu kufanyika hapa Tanzania. Napenda kurudia tena kuwashukuru kwa kuridhia Mkutano huu kufanyika hapa Tanzania. Na kama nilivyoahidi, tutajitahidi kuufanya Mkutano huu uwe wa mafanikio makubwa kwa ustawi na maendeleo ya pande zetu mbili.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Uhusiano na ushirikiano kati ya Afrika na China ni wa kihistoria na ni wa muda mrefu sana. Kwa mujibu wa Mwana Historia wa Uchina, Li Anshan, uhusiano kati ya Afrika na China ulianza takriban miaka 138 kabla ya Ujio wa Kristo, ambapo kulikuwa na uhusiano wa kibiashara kati ya tawala mbalimbali za China na Watawala wa Misri na maeneo mengine ya Afrika.  Kadri miaka ilivyozidi kupita, uhusiano huo ulizidi kukua na kupanuka na hasa kuanzia karne ya 14. Upo ushahidi mwingi wa kihistoria na vitu vya kale unaoonesha kuwepo kwa uhusiano wa karibu kati ya China na Afrika. Ushahidi huu unapatikana kwenye maeneo mengi kule China; na pia kwenye maeneo mbalimbali ya Afrika, ikiwemo Cairo, Bandari ya Aizhabu kule Sudan, maeneo ya Kenya, Somalia na halikadhalika Zanzibar hapa nchini Tanzania.

 

Pamoja na uhusiano huo wa kihistoria, ni ukweli usiopingika kuwa ushirikiano wetu ulikua na kuimarika zaidi kufuatia Mapinduzi ya Mwaka 1949 nchini China; na baada ya nchi za Afrika kuanza kupata uhuru kwenye miaka ya 1950 na mwanzoni mwa miaka ya 1960. Nchi nyingi za Afrika zilizopata uhuru zilianzisha uhusiano na China. Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo, mara tu baada ya kupata uhuru, ilianzisha uhusiano na China.

 

Na napenda niseme kuwa, China ilitoa mchango mkubwa sana katika harakati za ukombozi Barani Afrika. Kama nilivyosema awali, Tanzania chini ya Mwalimu Julius Nyerere ilikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ukombozi wa OAU. Hivyo, tunafahamu mchango wa China katika harakati za ukombozi wa Bara letu. Ndugu zetu hawa walitoa silaha na vifaa mbalimbali kwa wapigania uhuru. Halikadhalika, waliwapatia wapigania uhuru mafunzo ya kijeshi na pia kiitikadi. Na kwa wasiofahamu, ni hawa hawa marafiki zetu Wachina ndio waliojenga Reli kati ya Tanzania na Zambia yenye urefu wa zaidi ya kilometa 1,800, maarufu kama reli ya TAZARA, ambayo ilitoa mchango mkubwa sana katika harakati za ukombozi, hususan Kusini mwa Bara la Afrika. Na bila shaka, kwa kutambua mchango wa China kwenye harakati hizo za ukombozi, nchi nyingi za Afrika zilisimama pamoja na China katika kuhakikisha inapewa hadhi yake kwenye Umoja wa Mataifa.

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Baada ya nchi nyingi za Afrika kupata uhuru, uhusiano na China ulizidi kupanuka; kwenye masuala ya ulinzi na usalama, biashara, uwekezaji, ujenzi wa miundombinu, kilimo, afya, elimu, sayansi na teknolojia, mazingira, utalii, habari, utamaduni, n.k. Na mwaka 2000, Afrika na China zilianzisha rasmi jukwaa la ushirikiano (China – Africa Forum). Jukwaa hili, ambalo mikutano yake hufanyika kila baada ya miaka mitatu kwa kubadilishana kati ya Afrika na China, limeweka misingi imara ya ushirikiano kati ya pande hizi mbili. Mkutano wa Saba wa Jukwaa unatarajiwa kufanyika Beijing, China, mwezi Septemba 2018.

 

Tangu Jukwaa hili limeanzishwa, mafanikio mengi makubwa yamepatikana katika nyanja mbalimbali. Mathalan, biashara kati ya Afrika na China imeongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 10 na hivi sasa inakadiriwa kufikia zaidi ya Dola za Marekani bilioni 250. Aidha, uwekezaji wa China Barani Afrika umeongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 200 mwaka 2000 na kufikia zaidi ya Dola za Marekani bilioni 35 hivi sasa. Hii imeifanya China kuwa mshirika mkubwa wa kiuchumi wa Afrika. Vilevile, nchi za Afrika inashirikiana na China katika kutekeleza miradi ya miundombinu, hususan ya usafiri, umeme na maji. Halikadhalika, China wamekuwa wakitoa misaada mbalimbali kwa Afrika katika nyanja za afya, elimu, kilimo, sayansi na teknolojia, n.k. Maelfu ya Waafrika wamepata fursa za udhamini wa masomo nchini China. Na kama ambayo mmesikia hivi punde kutoka kwa Mheshimiwa Tao, China itatoa nafasi 4,000 za mafunzo kwa viongozi wa vyama vya siasa vya Afrika.

Zaidi ya hapo, China inashirikiana na Umoja wa Afrika katika kuimarisha amani na usalama Barani Afrika kwa kutoa fedha, mafunzo kwa walinda amani kutoka nchi za Kiafrika, wanatoa vifaa vya kijeshi na pia China inaongoza kwa kuwa na walinda amani wengi kwenye Bara letu. Kwa ujumla, naweza kusema kuwa ushirikiano kati ya China na Afrika kwa sasa umefikia kiwango cha juu sana. Na jambo la kufurahisha ni kwamba ushirikiano wetu umejengwa kwenye misingi ya kuelewana na kuheshimiana. Na hii ndio sababu misaada ya China kwetu imekuwa haiambatani na masharti yoyote. Na hili ndilo haswaa nchi za Afrika tunataka; ushirikiano ambao sote tunajiona tupo sawa na sote tunanufaika. Tunawashukuru sana marafiki zetu hawa wa China kwa kuheshimu msingi huu mkubwa wa ushirikiano.

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Licha ya mafanikio haya makubwa yaliyopatikana kwenye ushirikiano wetu, ni wazi kuwa bado tunayo fursa ya kuukuza na kuuimarisha. Tuna maeneo mengi ambayo tunaweza kuanzisha au kuimarisha ushirikiano.Tuna fursa kubwa ya kukuza biashara kati yetu. Mathalan, nchi zetu za Afrika tunahitaji soko la China kupanuliwa zaidi ili kuuza bidhaa zetu. Hivi sasa China ina watu watu wapatao bilioni 1.4. Hili ni soko kubwa ambalo nchi za Afrika inaweza kulitumia kwa ajili ya kuuza bidhaa zake mbalimbali (kahawa, chai, n.k.). Zaidi ya hapo, tunaihitaji China kuongeza uwekezaji Barani Afrika, hususan kwenye sekta za kilimo, viwanda, madini, utalii, n.k. Aidha, nchi za Afrika zingependa kukuza ushirikiano na China katika ujenzi wa miundombinu, hususan ya usafiri na nishati ya umeme. Tunahitaji pia kuendeleza ushirikiano na China kwenye masuala ya sayansi na teknolojia, utamaduni, kupata fursa za masomo kwa ajili ya kujenga uwezo wa wananchi wetu. Na vilevile, nchi za Afrika zinahitaji kushirikiana na China katika masuala ya kimataifa, ikiwemo masuala ya ulinzi na usalama, kushughulikia mabadiliko ya tabianchi pamoja na mageuzi kwenye umoja wa mataifa.

 

Hayo ni baadhi tu ya maeneo ambayo Afrika na China zinaweza kuimarisha ushirikiano. Na kama ukiniuliza mimi, hivi sasa ndio wakati muafaka wa kukuza ushirikiano kati ya Afrika na China. Nasema hivyo, kwa sababu, kama mjuavyo, mwaka 2013, Mheshimiwa Rais Xi Jinping wa China alianzisha mpango au mkakati ujulikanao kwa jina la “Belt and Road Initiative” wenye lengo la kukuza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria kati China, nchi nyingine za Asia pamoja na Mabara mengine, ikiwa ni pamoja na Bara letu la Afrika. Aidha, mwaka huu China imetimiza miaka 40 tangu ilipoanza kufanya mageuzi ya kiuchumi ambayo yameiletea mafanikio makubwa nchi hiyo; na mwaka jana China ilipitisha Mwogozo wa Maendeleo wa China hadi mwaka 2050 (a blueprint for China’s development) wenye lengo la kuifanya China kuwa ya kisasa na imara zaidi.

 

 Kwa upande wetu Afrika, sote hapa tunafahamu kuwa mwaka 2015, kupitia Umoja wa Afrika, tulipitisha Agenda ya Maendeleo ya Afrika hadi kufikia mwaka 2063 (The AU Agenda 2063), ambayo lengo lake ni kujenga Afrika moja yenye ustawi na amani (an integrated, prosperous and peaceful Africa). Aidha, kama mjuavyo, nchi nyingi za Afrika hivi sasa zinaongoza kwa ukuaji uchumi duniani; na nyingine nyingi zinatekeleza Dira pamoja na Mipango ya Maendeleo yenye lengo za kuzifanya ziwe za uchumi wa kati katika kipindi cha muongo mmoja ujao. Haya yote yanafanya huu uwe ni wakati muafaka zaidi kwa Afrika na China kuimarisha uhusiano na ushirikiano; na hasa kwa sababu mipango na malengo yetu yanafanana.

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Ni kwa kuzingatia hayo yote, napenda nitumie fursa hii kutoa pongezi na shukrani zangu nyingi kwa vyama vyetu viwili, yaani Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Chama Cha Mapinduzi (CCM) cha Tanzania ambavyo vimeshirikiana kuandaa Mkutano huu wa Majadiliano kati ya CPC na Vyama vya Siasa vya Afrika.  Kama sote tujuavyo, vyama vya siasa ni taasisi muhimu ambazo zinatoa mchango mkubwa wa maendeleo duniani. Vyama Vya Siasa ni sauti ya watu lakini pia ndivyo vyenye kuunda na kuzisimia serikali. Hivyo basi, nina matumaini makubwa kuwa yote yatakayojadiliwa hapa yatakuwa yanawakilisha sauti za wananchi wetu; na kwa kuwa Mkutano huu unahusisha Watendaji Wakuu wa Vyama, basi maamuzi au mapendekezo yatakayofikiwa, ni lazima yatatekelezwa na Serikali zetu. Na kwa bahati nzuri, kama nilivyosema, Mkutano huu unafanyika miezi michache tu kabla ya kufanyika kwa Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya Afrika na China mwezi Septemba 2018. Hivyo, nina imani baadhi ya mapedekezo ya mkutano huu yatajumuishwa kwenye Maazimio ya Mkutano huo wa Septemba kwa ajili ya kutekelezwa na Serikali zetu katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

 

Nimefurahishwa sana na kaulimbiu ya Mkutano huu, ambayo inasema “Nadharia na Mikakati Halisi ya Vyama vya Siasa vya Afrika na China katika kutafuta Njia za Maendeleo kwenye nchi zetu (Theories and Practices of Chinese and African Political Parties in Exploring Development Paths Suitable to National Situation)”.  Binafsi naiona kaulimbiu hii kuwa nzuri sana. Inatoa nafasi kwa vyama vyetu kujadili namna ya kukuza ushirikiano kati ya Afrika na China. Aidha, inatoa fursa ya kubadilishana mawazo na kupeana uzoefu wa namna Vyama vyetu vitaweza kushiriki kwenye masuala ya maendeleo; fursa zilizopo na changamoto ambazo vyama vyetu vinakumbana navyo katika kusimamia shughuli za maendeleo katika nchi zetu, n.k. Masuala haya yote ni muhimu katika kukuza ushirikiano wetu lakini pia katika kuleta maendeleo kwenye nchi zetu. Hivyo basi, niwaombe sana wajumbe wa mkutano huu mjadili kwa uwazi na kina masuala haya. Msiogope kujadili suala lolote. Kama nilivyosema, Vyama ni sauti ya watu lakini pia ndio vyenye kuunda Serikali. Hivyo mjadili kwa uwazi bila kuogopa. Naamini yapo mambo mazuri mengi ambayo Vyama vya Siasa kutoka nchi za Afrika zitajifunza kutoka Chama cha Kikomunisti cha China na pia yapo mambo mazuri ambayo CPC itajifunza kutoka kwetu Afrika.

 

 Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Nimesema mengi sana. Nimeeleza kuhusu historia ya uhusiano kati ya Afrika na China; mafanikio yaliyopatikana; maeneo ya kuimarisha uhusiano; na kadhalika namna ambavyo vyama vyetu vinaweza kutoa mchango katika kukuza ushirikiano kati ya pande zetu mbili na pia kuleta maendeleo kwenye nchi zetu, hususan maendeleo ya kiuchumi. Hata hivyo, kabla ya kuhitimisha, napenda kurudia tena kuishukuru na kuipongeza CPC kwa kubuni wazo la kuanzisha majadiliano ya namna hii. Aidha, nawashukuru wajumbe kutoka nchi mbalimbali kwa kuhudhuria kwa wingi katika Mkutano huu.

 

Kwa niaba ya wana-CCM na Watanzania wote, tunawashukuru kwa kuichagua nchi yetu kuwa mwenyeji wa Mkutano huu. Narudia tena kusema hamjakosea kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huu. Mbali na sababu mbili nilizozitaja awali, Tanzania ina vivutio vingi vya utalii ambavyo huwafurahisha wageni wetu wengi. Fukwe za Zanzibar, Mbuga za Wanyama za Serengeti na Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro, n.k. Ni imani yangu kuwa, hata ninyi wajumbe wa Mkutano huu, kama sio wakati huu basi mtatafuta wakati mwingine kuvitembelea vivutio hivyo ili kujionea uzuri wa Tanzania.

 

Napenda kuhitimisha kwa kuahidi kwamba CCM pamoja na Serikali yake itaendelea kushirikiana na CPC, Serikali ya China pamoja na Vyama vingine Barani Afrika. Na katika hili, napenda niseme kuwa CCM na Serikali ya Tanzania kwa pamoja vinaishukuru CPC na Serikali ya China kwa misaada mbalimbali inayotupatia kwenye Chama na pia kwenye Serikali, hususan katika nyanja za afya, elimu, maji, kilimo, miundombinu, n.k. Nia yetu ni kuona ushirikiano wetu ukizidi kukua.

 

Hivi sasa, nchi yetu inatekeleza Dira yake ya Maendeleo ya Mwaka 2025 ambayo inalenga kuifanya nchi yetu kuwa nchi ya uchumi wa kati wenye kuongozwa na viwanda. Ili kufikia azma hiyo, tumebuni mipango na miradi mbalimbali ya kimkatati. Baadhi tumeshaiwasilisha kwa marafiki zetu mbalimbali, wakiwemo wa China, ili watuunge mkono. Miradi hiyo ni pamoja ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa kutoka hapa Dar es Salaam kwenda Mikoa ya Mwanza na Kigoma, na kisha kwenda nchi za Burundi na Rwanda; ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo; miradi ya kufua na kusafirisha umeme; mradi wa kuchimba chuma pamoja na kufua umeme wa makaa ya mawe wa Mchuchuma na Liganga, na mradi mkubwa wa Kiwanda cha Kuchakata Gesi Asilia, n.k.

 

Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuwaomba marafiki zetu wa China kutuuga mkono katika kutekeleza miradi hiyo mikubwa ya maendeleo kwa nchi yetu. Tunawakaribisha pia rafiki zetu wa China pamoja na nchi nyingine, zikiwemo za Afrika, kuja kuwekeza hapa nchini, hususan kwenye viwanda vya kusindika na kuongezea thamani mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi; kilimo chenyewe, uchakataji madini, sekta ya utalii, n.k. Aidha, tunawaomba marafiki zetu wa China waendelee kutupatia fursa za masomo hususan kwenye fani za afya, kilimo, mafuta na gesi, sayansi na teknolojia, n.k. Kwa namna hii ushirikiano wetu utazidi kuimarika na wananchi wetu watanufaika.

 

Baada ya kusema hayo, natamka rasmi kuufungua Mkutano huu. Nawatakia Wajumbe majadiliano mema na nina matumaini makubwa kuwa Mkutano huu utakuwa wa mafanikio.

 

Mungu Ubariki Ushirikiano kati ya Afrika na China!

Mungu Ibariki Afrika!

Mungu Ibariki Tanzania!

 

“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”