Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA MWENYEKITI WA CHAMA CHA MAPINDUZI KWENYE HAFLA UWEKAJI JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA CHUO CHA UONGOZI CHA JULIUS NYERERE KIBAHA, PWANI, TAREHE 16 JULAI, 2018

Monday 16th July 2018

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA MWENYEKITI WA CHAMA CHA MAPINDUZI KWENYE

HAFLA UWEKAJI JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA CHUO

CHA UONGOZI CHA JULIUS NYERERE

KIBAHA, PWANI, TAREHE 16 JULAI, 2018

 

Waheshimiwa Makatibu Wakuu wa Vyama Vyetu Sita Rafiki

(ANC, CCM, FRELIMO, MPLA, SWAPO na ZANU-PF);

 

 Mheshimiwa Song Tao, Waziri wa Masuala ya Mambo ya Nje

wa Chama Cha Kikomunisti Cha China;

 

 Mheshimiwa Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM

Taifa (Tanzania Bara);

 

Waheshimiwa Mawaziri na Makatibu Wakuu mliopo;

 

Mheshimiwa Mhandisi Evarist Ndikilo,

Mkuu wa Mkoa wa Pwani;

 

Waheshimiwa Mabalozi mliopo;

 

Waheshimiwa Wabunge mliopo;

 

Waheshimiwa Viongozi wengine wa Chama na Serikali mliopo;

 

Waheshimiwa Wageni Waalikwa Wote;

 

Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana:

 

Leo ni siku muhimu na kihistoria kwa nchi zetu sita; yaani Afrika Kusini, Angola, Msumbiji, Namibia, Tanzania na Zimbabwe; ambazo wakati wa harakati za ukombozi tulishirikiana kwa karibu, ikiwa ni pamoja na marafiki zetu wa China. Binafsi, najisikia furaha na heshima kubwa kuwepo mahali hapa na kuweza kushiriki tukio hili muhimu la Uwekaji Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere (Mwalimu Nyerere Leadership School).

 

Lakini, kabla sijaendelea zaidi kuzungumzia tukio hili, naomba kwanza, kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya Watanzania wote, niwakaribishe wageni wetu hapa nchini. Nawakaribisha Makatibu Wakuu Vyama vya ANC, FRELIMO, MPLA, SWAPO na ZANU-PF. Aidha, kwa namna ya pekee kabisa, napenda nimkaribishe nchini Mgeni wetu Maalumu, Mheshimiwa Song Tao, Waziri wa Mambo ya Nje wa Chama cha Kikomunisti Cha China.  Karibuni Tanzania. Karibuni sana hapa Kibaha.

 

Napenda pia kutumia fursa hii kuwashukuru sana wana-Kibaha kwa kujitokeza kwenu kwa wingi kwenye tukio hili. Ndugu Wageni wetu; hapa Kibaha ni Makao Makuu ya Mkoa wa Pwani; Mkoa ambao, kama yalivyokuwa maeneo mengi ya nchi yetu, nao ulishiriki kikamilifu na kutoa mchango mkubwa katika harakati za ukombozi, sio tu wa nchi yetu bali pia wa nchi nyingi za Afrika, hususan zilizopo Kusini mwa Bara letu. Nina uhakika, marafiki zetu, na hasa kutoka FRELIMO na ZANU-PF, bado wanaikumbuka vizuri Kambi ya Wapigania Uhuru ya Kaole, Bagamoyo, kilometa chache tu kutoka hapa.

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Tupo hapa kushuhudia uwekaji Jiwe la Msingi la Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere (Mwalimu Nyerere Leadership School). Kama mlivyosikia, Chuo hiki kitakapokamilika, kitakuwa mali ya Vyama vyetu sita rafiki vya ANC, CCM, FRELIMO, MPLA, SWAPO na ZANU-PF. Vyama hivi  vilishirikiana kwa karibu sana wakati wa harakati za kupigania uhuru wa nchi za Kusini mwa Bara letu. Hivyo basi, ili kuendeleza uhusiano wetu wa kidugu na kihistoria, ambao umeendelea kudumu mpaka sasa, ndipo lilipokuja wazo la kukijenga Chuo hiki.

 

Tumearifiwa hivi punde kuwa Chuo hiki kitatoa mafunzo ya muda mfupi (miezi mitatu), muda wa kati (mwaka mmoja) na muda mrefu (miaka mitatu). Na masomo yatakayofundishwa hapa yatahusu masuala ya uongozi na itikadi. Kama mjuavyo, masuala haya mawili (uongozi na itikadi) ni miongoni mwa matatizo makubwa yenye kuzikabili nchi za Afrika, hususan katika zama hizi za demokrasia ya vyama vingi. Vyama vingi vimeanzishwa bila kuwa na itikadi ya kueleweka na pia vinakosa watu wenye uzoefu wa uongozi ambao wameandaliwa na kuiva. Na hali hii pia, kwa kiwango kikubwa, imekuwa ikiviathiri hata vyama vyetu vikongwe.

 

Hivyo basi, ili kukabiliana na hali hiyo na kwa kutambua kuwa Vyama vyetu ni Vyama Tawala, ambavyo wananchi wanavitegemea katika kuendelea kuziongoza nchi zetu kwa muda mrefu, tumeona tunao wajibu wa kuonesha njia kwa kuanzisha Chuo hiki. Tunataka Vyama vyetu viwe na viongozi walioandaliwa vizuri, viongozi madhubuti wenye kufahamu miiko yao; na ambao wataielewa, wataisimamia na kuielimisha jamii kuhusu itikadi yetu.  Tunataka Chuo hiki kitusaidie kuzalisha akina Nyerere wengi, akina Mandela wengi, akina Samora Machel, akina Mzee Augustino Neto, akina Mzee Sam Nujoma, akina Mzee Mugabe, akina Mzee Kaunda n.k. Na suala hili mimi naamini linawezekana kabisa, na hasa kwa kuzingatia kuwa Vyama vyetu hivi vina misingi ya kiitikadi inayofanana. Itikadi ya kimapinduzi yenye lengo la kuwakomboa wananchi wanyonge na kuziletea maendeleo nchi zetu. Zaidi ya hapo, Vyama vyetu hivi, hivi sasa vinalenga kuleta mageuzi ya kiuchumi kwenye nchi zetu; hivyo basi, itakuwa rahisi kwa Chuo hiki kutuunganisha na kutuwezesha kufikia dhamira hiyo.

 

Mabibi na Mabwana;

Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza wote waliobuni wazo la kuanzisha Chuo hiki.  Nafahamu wengi wameshiriki kufikia hatua hii. Lakini, kwa hapa nchini, napenda kutambua mchango wa Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Mzee Jakaya Mrisho Kikwete; Makamu Mwenyekiti wa CCM, Mzee Mangula; pamoja na Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Mzee Abdulrahaman Kinana. Wametoa mchango mkubwa katika kufikia hatua hii. Tunawashukuru sana.

 

Napenda pia, kwa namna ya pekee, kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi na Vyama vyetu vyote sita, kutoa shukrani nyingi kwa ndugu zetu na marafiki zetu wa Chama cha Kikomunisti cha Watu wa China ambao wamekubali kutujengea Chuo hiki. Ujenzi wa Chuo hiki utagharimu Dola za Marekani milioni 45, sawa na takriban Shilingi bilioni 100 za Tanzania. Fedha zote hizo ni ufadhili wa ndugu na marafiki zetu wa China. Tunawashukuru sana.

 

Na niseme tu kwamba, Chama cha Kikomunisti Cha China na nchi ya China kwa ujumla ni marafiki zetu wa muda mrefu sana. Tumekuwa tukishirikiana na ndugu zetu hawa kwenye mambo mengi sana, tangu enzi za harakati za ukombozi. Walitupatia silaha na vifaa vya kijeshi kwa ajili ya kuendesha mapambano ya ukombozi. Walitoa mafunzo kwa wapigania uhuru na kuwafundisha masuala ya itikadi na propaganda ambazo ziliwapa hamasa wapigania uhuru kuendeleza mapambano. Baada ya uhuru, China imeendelea kushirikiana na nchi zetu na kutupatia misaada mbalimbali. Sisi Tanzania ni miongoni mwa wanufaika wakubwa wa misaada kutoka China. Reli ya TAZARA inayounganisha nchi yetu na marafiki zetu wa Zambia ni miongoni mwa misaada mikubwa ambayo China imeitoa kwa nchi yetu. Tunawashukuru sana. Reli hii ilisaidia sana harakati za ukombozi kwa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika.

 

Nimefurahi, kwenye tukio hili, tunaye Mheshimiwa Tao, Mkuu wa Kitengo cha Mambo ya Nje wa Chama Cha Kikomunisti Cha China. Tunakushukuru kwa kuungana nasi; na kwa niaba ya Vyama vyetu sita, tunaomba utufikishie shukrani zetu kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha China, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa Xi Jinping, Serikali pamoja na wananchi wote wa China kwa ujumla kwa kutujengea Chuo hiki; na halikadhalika kwa misaada mbalimbali mnayotoa kwa nchi zetu. Tunaithamini sana misaada mnayotupatia na tunaahidi kuendelea kuuenzi urafiki wetu.

 

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

 Napenda pia kutumia fursa hii kuvishukuru vyama rafiki vya CCM, yaani ANC, FRELIMO, MPLA, SWAPO na ZANU-PF, kwa kukubali Chuo hiki kujengwa hapa nchini kwetu. Chuo hiki kingeweza kujengwa mahali popote ndani ya nchi zetu sita; lakini mmetupa heshima ya kujengwa hapa nchini. Tunawashukuru sana na tutaenzi heshima mliyotupatia. Na bila shaka, mmetupatia heshima hii kwa kutambua mchango wa nchi yetu katika harakati za ukombozi wa Bara letu.

 

Vilevile, napenda nivipongeze vyama vyetu sita kwa kuamua kukipa Chuo hiki jina la Mwalimu Julius Nyerere, Baba wa Taifa letu. Huu ni uamuzi wa busara na unaakisi madhumuni ya kujenga Chuo hiki. Mwalimu Nyerere ni mmoja wa viongozi bora, imara, madhubuti, mtetezi wa wanyonge, mwanamapinduzi na muumini mzuri wa itikadi na falsafa ya Uafrika (Pan-Africanism) aliyewahi kutokea katika Bara letu. Sisi Tanzania tunajivunia sana Mwalimu Nyerere kuwa Baba yetu wa Taifa. Kama sote tujuavyo, Mwalimu Nyerere alitoa mchango mkubwa katika harakati za ukombozi wa Bara letu. Hivyo basi, ni wazi kuwa, kukipa Chuo hiki jina lake ni jambo sahihi kabisa. Anastahili kupewa heshima hii. Nimefurahi kuona kuwa katika shughuli hii tunaye Mwakilishi kutoka familia ya Mwalimu Nyerere. Tunaishukuru familia kwa kuwepo mahali hapa lakini pia kwa kuridhia Chuo hiki kupewa jina la Baba wa Taifa. Na nina imani kubwa kuwa watumishi na wanafunzi wa Chuo hiki wataenzi mambo yote mazuri ya Baba wa Taifa.

 

Mwisho, kuhusu shukran, napenda kutumia fursa hii kukishukuru Chama changu Cha Mapinduzi (CCM) kwa kukubali kutoa eneo la ujenzi wa Chuo hiki bure. Kama mjuavyo, eneo hili lilikuwa mali ya CCM. Hivyo, nakipongeza Chama changu kwa kulitoa bure. Bila shaka, nasi tumemuenzi Mwenyekiti wetu wa Kwanza vizuri.

 

Ndugu Makatibu Wakuu wa Vyama vyetu Sita;

Waheshimiwa Viongozi Wengine mliopo;

Wageni Waalikwa Wote, Mabibi na Mabwana;

Leo sio siku ya hotuba. Tupo hapa ili kuweka Jiwe la Msingi la Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere. Hata hivyo, kabla sijahitimisha hotuba yangu, naomba mniruhusu niseme masuala machache yafuatayo:

 

Kwanza, tumesikia kuwa ujenzi wa Chuo hiki unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miaka miwili. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuwaomba Makatibu Wakuu wa Vyama vyetu sita kukamilisha masuala mengine yote ili ujenzi utakapokamilika tu, Chuo kianze kufanya kazi. Kamilisheni masuala ya mitaala ya Chuo; ajira za watumishi, hususan wakufunzi; pamoja na masuala mengine muhimu, ikiwemo upatikanaji wa fedha za kuendesha Chuo hiki. Tusisubiri mpaka ujenzi ukamilike ndipo tuanze kukimbizana. Na nitumie fursa hii pia kumwomba Mkandarasi atekeleze mradi huu kwa haraka, ikiwezekana, ukamilike kabla ya muda uliopangwa.  Hakuna sababu za kuchelewa wakati fedha zipo. Fanyeni kazi usiku na mchana kukamilisha ujenzi wa Chuo hiki.

 

Pili, ni kuhusiana na masomo yatakayofundishwa. Tumeelezwa nami pia nimeeleza kuwa, Chuo hiki kitajikita kufundisha masuala ya uongozi na Itikadi. Lakini mbali na masomo hayo, ningependa kushauri kuwa tufikirie pia kupanua wigo, ikiwezekana tujumuishe masomo kuhusu masuala ya maendeleo na masuala mengine ya kimkakati (development studies and other strategic issues). Hii itakifanya Chuo hiki kiwavutie watu wengi kuja kusoma na pia itakiwezesha kutoa mchango mkubwa wa maendeleo kwenye nchi zetu. Na katika hili, nishauri pia, badala ya Chuo hiki kufundisha watu kutoka kwenye Vyama vyetu sita pekee, ni vyema tukaangalia uwezekao wa kukaribisha watu kutoka vyama vingine, na hasa vyenye mrengo na itikadi inayofanana na Vyama vyetu.

 

Tatu, ni kwenu ndugu zangu wananchi wa hapa Kibaha. Fursa imekuja kwenu. Chuo hiki kitatoa fursa za ajira kwenu wakati wa ujenzi na baada ya ujenzi. Hivyo basi, nawasihi mjipange kutumia fursa hiyo. Na ni matumaini yangu kuwa Mkandarasi ataajiri wafanyakazi wengi kutoka hapa Kibaha. Napenda pia kuziagiza mamlaka za Mkoa huu wa Pwani kuhakikisha barabara kutoka kwenye barabara kuu hadi hapa Chuoni inajengwa kwa kiwango cha lami.

 

Mabibi na Mabwana;

Nihitimishe kwa kurudia tena kukishukuru Chama cha Kikomunisti cha China kwa kufadhili ujenzi wa Chuo hiki. Kwa mara nyingine tena mmedhihirisha kuwa ninyi ni marafiki wa kweli wa Afrika. Aidha, nawashukuru viongozi wa vyama rafiki vya CCM kwa kushiriki kwenye tukio hili. Ushirikiano huu hatuna budi kuuendeleza, na hasa katika kipindi hiki ambacho nchi zetu zimeamua kujikomboa kiuchumi. Mwisho lakini sio kwa umuhimu, nawashukuru viongozi na wanachama wa CCM, pamoja na wana-Pwani kwa ujumla, kwa kujitokeza kwa wingi kwenye tukio hili.

 

Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kutekeleza jukumu lililonileta la Kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Chuo Cha Uongozi Cha Mwalimu Nyerere kwa ufadhili ya Chama Cha Kikomunisti cha Watu wa China kwa gharama ya takriban shilingi bilioni 100 za Tanzania.

 

“Ahsanteni sana kwa Kunisikiliza”