Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE HAFLA YA KUPOKEA NDEGE MPYA BOEING 787- 800 DREAMLINER DAR ES SALAAM, TAREHE 8 JULAI, 2018

Sunday 8th July 2018

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI,

RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

KWENYE HAFLA YA KUPOKEA NDEGE MPYA

BOEING 787- 800 DREAMLINER

DAR ES SALAAM, TAREHE 8 JULAI, 2018

 

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais

wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu

wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Mhandisi Isack Kamwelwe;

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano;

 

Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri mliopo;

 

Mheshimiwa Balozi John Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi;

 

Mheshimiwa Kaimu Balozi wa Marekani nchini;

 

Mheshimiwa Paul Makonda,

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;

 

Mheshimiwa Seleman Kakoso, Mwenyekiti

wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu;

 

Waheshimiwa Wabunge Wote mliopo;

 

Mheshimiwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam;

 

Ndugu Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu mliopo;

 

Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;

 

Wajumbe wa Bodi, Menejimenti na Watumishi wa ATCL,

TCAA na TAA mliopo;

 

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa na Dini mliopo;

 

Wageni Waalikwa Wenzangu wote;

 

Ndugu wana-Habari, Mabibi na Mabwana:

 

Nafahamu kuwa wengi hapa tuna hamu kubwa ya kuiona ndege yetu mpya. Hivyo basi, nitasema kwa kifupi na kwa haraka. Kwanza kabisa, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kushuhudia tukio hili la kihistoria. Aidha, namshukuru Mungu kwa kuifikisha ndege yetu salama hapa nchini. Ni imani yangu kuwa Watanzania wote tumefurahia ujio wa ndege yetu mpya.

 

Napenda pia nitumie fursa hii kuushukuru Uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa kunialika ili nami niwe mmoja wa mashuhuda wa tukio hili. Halikadhalika, nawashukuru wageni wote waalikwa pamoja na wananchi kwa ujumla kwa kujitokeza kwenu kwa wingi kwenye hafla hii. Ni wazi kuwa mmejitokeza kwa wingi kwa vile mnatambua umuhimu wa tukio hili kwa ustawi na maendeleo ya Taifa letu. Ahsanteni sana.

 

Vilevile, napenda nitumie fursa hii kuishuruku Kampuni ya Boeing ya Marekani pamoja na washirika wake (Kampuni ya Rolls-Royce na Panasonic) ambao wametutengenezea ndege yetu. Tunawashukuru sana. Nimefurahi kuona kuwa Balozi wa Marekani yupo hapa. Tafadhali tufikishie shukrani zetu kwenye kampuni hizo; na tunakuomba uwasisitize wajitahidi kuikamilisha mapema ile ndege nyingine. Watanzania tunaihitaji sana ndege hiyo; na fedha za malipo tayari zipo.

 

Ndugu Wananchi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Mtakumbuka kuwa mojawapo ya ahadi za CCM kwenye Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 ilikuwa kufufua Shirika letu la Ndege la Tanzania (ATCL). Wakati tunatoa ahadi hiyo, ATCL ilikuwa hoi bin taabani. Ilikuwa na ndege moja iliyokuwa ikifanya safari zake kwenye miji mitatu tu (Dar es Salaam, Arusha na Mwanza). Na ndege yenyewe ilikuwa kila mara inashinda kwenye karakana kwa ajili ya matengenezo. Hii ilifanya soko la safari za ndani la ATCL (domestic market share) kuwa dogo sana. Lilikuwa asilimia 2.5 tu.

 

Tukasema hapana. Hii haiwezekani. Ni lazima tufufue Shirika letu. Na kama tulivyoahidi, ndani ya kipindi kifupi tu cha miaka miwili na nusu, tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutekeleza ahadi yetu hiyo ya kuifufua ATCL. Tumenunua ndege mpya saba. Tena tumezinunua kwa fedha taslimu, sio kwa mkopo. Ndege tatu, aina ya Bombardier Dash 8 Q400, zenye uwezo wa kubeba abiria 76, tayari zimewasili na zinaendelea kutoa huduma. Ndege ya nne ndio hii itakayowasili leo. Aidha, ndege nyingine mbili, aina ya Bombardier CS300 zinatarajiwa kuwasili mwezi Novemba mwaka huu. Na, ndege kubwa nyingine kama hii itakayowasili leo, inatarajiwa kuja nchini mwanzoni mwa mwaka 2020.

 

Bila shaka, mtakubaliana nami kuwa, haya ni mafanikio makubwa. Lakini mafanikio haya hayajajileta yenyewe. Ni matokeo ya jitihada za Watanzania wote; lakini zaidi ni jitihada za wale wenye kufanya kazi kwa bidii na kulipa kodi. Kwa sababu hiyo, napenda nitumie fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza Watanzania wote wanaofanya kazi kwa kujituma. Aidha, nawashukuru kwa kuendelea kulipa kodi. Kwa hakika, kodi zenu ndizo zimeiwezesha Serikali kununua ndege hizi saba mpya kwa mpigo. Hongereni sana Watanzania. Na huu ni uthibitisho kuwa sisi Watanzania tukiamua tunaweza. Nitumie fursa hii pia kuishukuru Kamati ya Bunge ya Miundombinu pamoja na Bunge zima la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia ununuzi wa ndege hizi; na kwa namna mnavyounga mkono jitihada mbalimbali za Serikali za kuiletea maendeleo nchi yetu. Tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge.

 

Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;

Nafahamu nimekuwa nikieleza suala hili mara kadhaa. Lakini napenda na leo nilirudie. Serikali ya CCM iliamua kulifufua Shirika letu la Ndege kwa sababu kubwa tatu. Kwanza, ili kujenga heshima na kulinda hadhi ya Taifa letu. Kama mjuavyo, Tanzania ni kubwa na imejijengea sifa kemukemu duniani. Hivyo, ilikuwa aibu sana kwa Taifa kubwa kama letu kutokuwa na ndege.

 

Pili, tumeifufua ATCL ili kuimarisha na kuboresha huduma za usafiri wa anga nchini. Nafahamu kwenye hili, wapo watu wanadai Watanzania hawahitaji usafiri wa ndege. Ndugu zangu, hiyo sio kweli. Watanzania wanahitaji usafiri wa ndege. Na kwa kusema kweli, katika ulimwengu wa sasa, hakuna nchi isiyohitaji usafiri wa ndege.  Bila ya usafiri wa ndege wa uhakika, wakulima wetu wa maua waliopo Mbeya, Njombe na Arusha hawataweza kuyafikia masoko ya kimataifa. Bila usafiri wa ndege, itakuwa vigumu kwa wavuvi wetu kwenye Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa kusafirisha samaki kwenda kwenye masoko ya kimataifa. Hivyo basi, napenda nirudie tena kusema kuwa Watanzania wanahitaji usafiri wa ndege.

 

Natambua kuwa, hivi sasa Watanzania wengi hawatumii usafiri wa ndege. Lakini hii haimaanishi kuwa hatuhitaji usafiri huo. Tumekuwa hatutumii usafiri huu kwanza kutokana na kukosekana kwa safari za ndege za uhakika kwenye maeneo mengi ya nchi yetu. Nimeeleza hivi punde kuwa, zamani ATCL ilikuwa ikifanya safari zake kwenye miji mitatu tu ya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza. Hivyo, ni wazi kuwa, katika hali kama hiyo, ilikuwa vigumu kwa watu wa maeneo mengine kusafiri kwa ndege. Sababu ya pili iliyofanya Watanzania wasitumie usafiri wa ndege ni gharama kuwa juu. Sio siri kuwa kwa muda mrefu gharama za usafiri wa ndege nchini zilikuwa juu sana. Mathalan, kabla ya ndege zetu za Bombardier kuanza kutoa huduma, gharama za kusafiri kwenda na kurudi Bukoba ilikuwa zaidi ya shilingi milioni moja. Hiki ni kiasi kikubwa sana ambacho sio Watanzania wanaweza kumudu. Lakini, tangu Bombardier zimeanza kufanya kazi, gharama zimepungua sana. Hivi sasa gharama za kwenda na kurudi Bukoba ni wastani wa shilingi laki nne tu.

 

Hii imefanya idadi ya wasafiri nchini kuongezeka. Kwa mfano, nimeambiwa kuwa, zamani ATCL ilikuwa inasafirisha wastani wa abiria 4,700 kwa mwezi lakini sasa inasafirisha wastani wa abiria 21,000. Na hii imewezekana kutokana na kupungua kwa gharama lakini pia kuongezeka kwa maeneo inakotoa huduma; kutoka maeneo matatu ya awali hadi kufikia maeneo 12 hivi sasa. Ni matumaini kuwa, kadri bei zitakapozidi kupungua; na kutokana na jitihada kubwa tunazozifanya za kujenga na kuboresha viwanja vyetu vya ndege sehemu mbalimbali nchini; idadi ya wasafiri itazidi kuongezeka.

 

Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;

Sababu ya tatu iliyotusukuma tuifufue ATCL, ambayo pengine ndio kubwa zaidi, ni kukuza sekta yetu ya utalii. Kama mjuavyo, nchi yetu ina vivutio vingi vya utalii. Tunashika nafasi ya pili duniani. Lakini, licha ya kwamba, sekta ya utalii inaongoza kwa kutupatia fedha nyingi za kigeni, bado mchango wake sio mkubwa sana ukilingaisha na vivutio tulivyonavyo. Hii imetokana na nchi yetu kupokea idadi ndogo ya watalii. Mathalan, mwaka jana tulipokea watalii milioni 1.3 tu.

 

Katika tathmini tuliyoifanya tumegundua kuwa watalii wengi duniani hutumia usafiri wa ndege. Mathalan, asilimia 70 ya watalii bilioni 1.3 waliosafiri mwaka 2017 walitumia usafiri wa ndege. Na kwa ujumla, idadi ya watu waliosafiri kwa ndege mwaka jana ilifikia bilioni 4. Vilevile, tathmini yetu ilituonesha kuwa nchi zenye mashirika imara ya ndege ndizo pia zimekuwa zikipokea idadi kubwa ya watalii. Mathalan, Barani Afrika, nchi zenye kuongoza kwa kupokea idadi kubwa ya Watalii ni Moroco, Afrika Kusini na Misri; ambazo zote zina mashirika makubwa ya ndege. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2017, Morocco ilipokea takriban watalii milioni 12, Afrika Kusini watalii milioni 10.2 na Misri watalii milioni 10.1. Hata majirani zetu wa Kenya ni vivyo hivyo. Mashirika ya Ndege kwenye nchi hizo yamekuwa chachu ya kuongezeka kwa idadi ya watalii.

 

Hii ndio sababu na sisi tukaamua tulifufue Shirika letu la Ndege. Na kimsingi, hii ndio sababu pia iliyotufanya tununue ndege hii kubwa. Tunataka ndege hii iwe inafanya safari za kimataifa na kutusaidia kutuletea watalii wengi nchini. Na binafsi nina amini kuwa, ndege hii ikianza kufanya kazi, na baada ya kuwasili kwa ndege ile nyingine kubwa mwaka 2020, idadi ya watalii wanaokuja nchini itaongezeka maradufu.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Ndugu Wananchi Wenzangu;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Azma na dhamira ya Serikali ya CCM ya Awamu ya Tano ni kuleta maendeleo kwa nchi yetu. Hii ndio sababu, mbali na kuimarisha huduma na miundombinu ya usafiri wa anga, tunaimarisha pia usafiri wa kwenye maji. Kama mjuavyo, hivi sasa tunazipanua Bandari zetu za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga pamoja na kuboresha utendaji kazi na utoaji huduma. Nakumbuka, tulipoanza kuchukua hatua kwenye Bandari yetu ya Dar es Salaam walijitokeza “watabiri” waliosema tunawafukuza wateja. Lakini, sasa “watabiri” wameanza kuaibika. Utendaji kazi wa Bandari yetu unazidi kuimarika. Ni hivi majuzi tu mmemsikia Rais Mnangagwa wa Zimbabwe akisema kuwa sasa Wazimbabwe wanaitumia Bandari ya Dar es Salaam.

 

Vilevile, tuboresha na kuimarisha usafiri wa ardhini, hususan reli na barabara. Kuhusu reli, kama mjuavyo, kwa sasa tupo kwenye ujenzi wa reli yetu ya standard gauge kutoka hapa Dar es Salaam hadi Dodoma. Lakini pia, tunakarabati reli yetu ya zamani. Ukarabati wa kipande cha kutoka Tanga hadi Arusha kinatarajiwa kukamilika mwaka huu. Aidha, hivi majuzi mmeshuhudia shehena ya kwanza ya mizigo inayosafirishwa kwa reli kutoka Dar es Salaam hadi Kampala nchini Uganda.  Hiyo imewezekana baada ya kuikarabati meli yetu ya Mv. Umoja ambayo ni maalum kwa kusafirisha mabehewa ya treni kwenye Ziwa Victoria.

 

Kwa upande wa barabara, nyingi hivi sasa zinajengwa katika maeneo mbalimbali nchini. Ninyi wana-Dar es Salaam ni mashahidi. Hapa Dar es Salaam tunajenga barabara kwenye maeneo mengi na pia madaraja. Pale TAZARA, Daraja la Kwanza la Juu (Flyover) nchini lipo katika hatua za mwisho kukamilika. Lakini wakazi wa Kijitonyama, Makumbusho, Sinza, Tandale kwa Mtogole wanafahamu hatua tunazozichukua za kuboresha miundombinu ya barabara kwenye maeneo hayo.

 

Tunatekeleza pia miradi mbalimbali ya umeme (Kinyerezi I na II, REA Awamu ya Tatu, na tupo mbioni kuanza Mradi mkubwa wa Umeme wa Bonde la Mto Rufiji au Stiglier’s Gorge). Aidha, tunatekeleza miradi mikubwa ya maji. Rafiki zetu wa India wametupatia mkopo wa takriban shilingi trilioni 1.2 na Benki ya Dunia takriban shilingi bilioni 700 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji sehemu mbalimbali za nchi yetu. Kwenye maji pia tupo mbioni kuanza utekelezaji wa mradi mkubwa ambao uliasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, wa Bwawa la Kidunda. Mradi huu ni muhimu kwa ajili ya kuhakikisha upatikanaji wa maji katika Jiji hili la Dar es Salaam.

 

Halikadhalika, katika Mwaka huu wa Fedha tumepanga kuanza ujenzi wa hospitali za Wilaya takriban 67 kwa gharama ya shilingi bilioni 104. Aidha, tunaendelea na ujenzi wa miundombinu ya elimu, ikiwemo vyumba vya madarasa, vyoo, hosteli, maabara, maktaba, n.k. Kwa ujumla, mambo tunayotekeleza ni mengi. Na nina imani kuwa, kutokana na hatua tunazozichukua, azma na ndoto yetu ya kuwa nchi ya uchumi wa kati wenye kuongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025 itatimia.

 

Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi;

Waheshimiwa Viongozi mliopo;

Wageni Waalikwa wote;

Mabibi na Mabwana;

Tumekuja hapa kushuhudia kuwasili kwa ndege yetu mpya kubwa aina ya Boeing 787 – 800 Dreamliner, yenye uwezo wa kubeba watu 262. Naushukuru tena uongozi wa Wizara ya Ujenzi kwa kunialika kwenye hafla hii. Aidha, nawashukuru wageni wote waalikwa na wananchi kwa ujumla kwa kujitokeza kwa wingi kwenye tukio hili. Kama nilivyosema awali, kujitokeza kwenu kwa wingi namna hii ni uthibitisho tosha kuwa mnatambua umuhimu wa ndege hii kwa maendeleo ya nchi yetu.

 

Nihitimishe hotuba yangu kwa kutoa wito kwa Bodi, Menejimenti na Watumishi wote wa ATCL kuendelea kufanya kazi kwa bidii. Kama mjuavyo, Serikali imetumia fedha nyingi kulifufua Shirika lenu. Hivyo basi, nawasihi sana msiwaangushe Watanzania. Nimefurahi kusikia kutoka kwenye taarifa ya Mtendaji Mkuu wa ATCL kuwa kwa mfupi tu tangu tuanze kuchukua hatua za kufufua shirika, utendaji kazi wa Shirika umeimarika na tija imeanza kuonekana. Mmeiongeza idadi ya safari kutoka miji mitatu hadi 12, ikiwemo safari ya kwenda nchini Comoro. Mmeweza kupanua soko lenu la ndani (domestic market share) kutoka asilimia 2.5 hadi kufikia asilimia 24.  Na pia mmekifufua chuo chenu cha mafunzo (Aviation Training School) kwa ajili ya watoa huduma wenu.  

 

Haya, kwa hakika, ni mafanikio makubwa. Hongereni sana. Lakini msibweteke. Ongezeni bidii ili kulifanya Shirika lenu kuwa kubwa sio tu hapa nchini bali pia liwe miongoni mwa Mashirika makubwa Barani Afrika na duniani kwa ujumla. Na katika kufanikisha hilo, narudia tena kuwasihi kuacha uzembe, kupiga vita rushwa na ufisadi, kujituma, kuimarisha nidhamu ya kazi, na kuwa wabunifu katika kutoa huduma. Aidha, msisahau kuyapa kipaumbele masuala ya utaalam, hususan masuala ya ufundi wa ndege na marubani.

 

Baada ya maneno hayo:

 

 

Mungu Ibariki Ndege yetu Boeing 787 – 800 Dreamlier!

 

 Mungu Zibariki Ndege Zote za ATCL!

 

Mungu Ibariki Tanzania!

 

 

“Ahsanteni kwa kunisikiliza”