Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUPOKEA GAWIO NA KUZINDUA UPATIKANAJI WA HUDUMA ZA SIMU NA VIDEO CONFERENCE YA SHIRIKA LA SIMU (TTCL), DAR ES SALAAM, TAREHE 21 JUNI, 2018

Thursday 21st June 2018

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUPOKEA GAWIO NA KUZINDUA UPATIKANAJI WA HUDUMA ZA SIMU NA VIDEO CONFERENCE YA SHIRIKA LA SIMU (TTCL), DAR ES SALAAM,

TAREHE 21 JUNI, 2018

 

Mheshimiwa Prof. Makame Mbarawa,

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano;

 

Mheshimiwa Paul Makonda,

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;

 

Mama Mary Sassabo, Katibu Mkuu anayesimamia

Sekta ya Mawasiliano kwenye Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano;

 

Mheshimiwa Mama Kate Kamba, Mweyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam;

 

Waheshimiwa Wabunge wa Kamati ya Miundombinu;

 

Mheshimiwa Mhadisi Omary Nundu, Mwenyekiti wa TTCL;

 

Ndugu Waziri Kindamba, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL;

 

Waheshimiwa Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;

 

Waheshimiwa Viongozi mbalimbali mliopo hapa;

 

Ndugu Wafanyakazi wa TTCL;

 

Wageni Waalikwa wote, Mabibi na Mabwana:

 

RUDINI NYUMBANI – KUMENOGA!

 

         Kwanza kabisa, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha tukutane hapa tukiwa wenye afya njema. Aidha, napenda nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na uongozi mzima wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (yaani TTCL) kwa kunialika kwenye tukio hili muhimu na la kihistoria hapa nchini. Ahsanteni sana.

 

Napenda nikiri kuwa leo najisikia kuwa mwenye furaha sana. Nina furaha kwanza kwa kupata fursa hii adimu ya kukutana na wafanyakazi wa Shirika letu la Mawasiliano. Pili, nina furaha kwa sababu, kama mlivyosikia, miaka miwili iliyopita, mwezi Juni mwaka 2016, tulifanya uamuzi wa kuirejesha TTCL Serikalini baada ya kununua asilimia 39 ya hisa zilizokuwa zikimilikiwa na Kampuni ya Bharti Airtel, kwa gharama ya shilingi bilioni 14.9. Wakati tukinunua hisa hizo, TTCL ilikuwa haijatoa gawio lolote kwa Serikali kwa kipindi cha miaka 15, tangu ilipoingia ubia na Kampuni ya Bharti Airtel mwaka 2001.

 

Lakini ndani ya kipindi kifupi cha miaka miwili tu, leo tupo hapa kushuhudia TTCL ikitoa gawio la shilingi bilioni 1.5 kwa Serikali. Haya ni mafanikio makubwa ambayo naamini kila mwenye kuitakia mema nchi yetu hana budi kufurahia; japokuwa mimi binafsi gawio hili limenifanya nijiulize maswali mengi sana. Nimejiuliza hivi wakati wa ubia kwa nini Shirika hili lilishindwa kutoa gawio kwa Serikali? Je, tulikuwa tukiibiwa? Je, usimamizi wa utendaji kazi haukuwa mzuri? Ama kulikuwa na hujuma? Mpaka sasa bado sijapata majibu, ingawa nimejifunza jambo moja kuwa sio kila ubia kwenye biashara ni mzuri.

 

Wageni Waalikwa wote, Mabibi na Mabwana;

Mbali na kupokea gawio, kama mlivyosikia, leo pia tunaishuhudia TTCL ikizindua huduma zake za mawasiliano kwa nchi nzima pamoja na huduma za mkutano mtandao (yaani video conference). Haya, kwa hakika, ni mafanikio makubwa sana, ambayo yanaonesha kuwa Shirika hili linazidi kukua. Na nimeambiwa kuwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, TTCL imefanikiwa pia kuongeza idadi ya wateja wake kutoka 247,000 hadi kufikia takriban laki nane hivi sasa. Hii inatupa moyo kwamba uamuzi wa kulirejesha Shirika hili Serikalini ulikuwa sahihi.

 

Hivyo basi, napenda nitumie fursa hii, kuipongeza Wizara, Bodi, Menejimenti pamoja na Watumishi wote wa TTCL kwa kuwezesha kupatikana kwa mafanikio haya. Bila ninyi mafanikio haya yasingepatikana. Hivyo, tembeeni kifua mbele. Nakumbuka wakati nawateua Mwenyekiti wa Bodi na Mkurugenzi Mkuu niliwapa maagizo ya kufanya mabadiliko kwenye Shirika hili. Mafanikio yaliyopatikana yanaonesha kuwa mlizingatia maelekezo yangu. Hongereni sana. Na hii inadhihirisha kuwa sisi Watanzania tukiamua, tunaweza.

 

Lakini zaidi ya hapo, kupitia kwa Bwana Kindamba, mafanikio haya ni uthibitisho kuwa, vijana wakipewa majukumu wanaweza sana. Na hii ndio sababu mara nyingi nimekuwa nikiteua vijana kushika nyadhifa mbalimbali Serikalini. Na kwa bahati nzuri, mpaka sasa, wengi niliowateua hawajaniangusha. Hivyo, naahidi nitaendelea kuwateua vijana kushika nafasi mbalimbali.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa wote, Mabibi na Mabwana;

Sekta ya mawasiliano na hasa mawasiliano ya simu, ni sekta nyeti ambayo imeleta mageuzi makubwa duniani katika kipindi cha hivi karibuni. Takwimu zinaonesha kuwa takriban watu bilioni 5 wanatumia simu za mikononi duniani hivi sasa. Hapa nchini kwetu, kwa takwimu za hivi karibuni, watu takriban milioni 40 wanatumia simu za mikononi. Sekta hii pia ni chanzo kikubwa cha mapato. Nakumbuka mwaka jana, tulipotembelewa na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn, alipata kunieleza kuwa mwaka 2016 Shirika la Simu la Ethiopia lilikusanya mapato yanayofikia Dola za Marekani bilioni 1.3, ambazo ziliwasaidia kujenga reli kutoka Addis Ababa hadi Bandari ya Djibouti.

 

Sambamba na hayo, sekta hii ya mawasiliano inatoa fursa nyingi za ajira. Mathalan, nimearifiwa kuwa TTCL imetoa ajira zipatazo 1,500 kwa Watanzania. Nchi yetu ina kampuni za simu takriban 8; hivyo ukijumlisha wauza vocha, watoa huduma za fedha kwa njia za mtandao, mafundi wa simu, n.k; unaweza kukadiria mwenyewe ni watu wangapi wamepata ajira kupitia sekta hii hapa nchini. Zaidi ya hapo, sekta hii ya mawasiliano ya simu imesaidia sana kuboresha maisha ya wananchi.

 

Hivi karibuni mlisikia kuwa nchi yetu iliibuka kidedea katika masuala ya uchumi jumuishi kwa Nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Moja ya mambo yaliyochangia kupatikana kwa mafanikio hayo ni kuongezeka kwa huduma za fedha kwa njia ya simu (T-Pesa, Tigo Pesa, M-Pesa, Airtel Money, n.k.). Na nimeambiwa kuwa hivi sasa wastani wa miamala ya fedha inayofanyika kwa njia ya simu nchini inafikia thamani ya shilingi trilioni 10 kwa mwezi. Hii imesaidia sana kuimarisha huduma za kifedha katika nchi yetu. Lakini, sekta hii pia imesaidia kuboresha huduma nyingine za kijamii, ikiwemo elimu na afya, kupitia huduma kama e-education, e-medicine, n.k.

 

 

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Ni kutokana na faida hizo za mawasiliano ya simu nilizozitaja, Serikali iliamua kufufua Shirika hili la Mawasiliano Tanzania. Mbali na kununua hisa kutoka Kampuni ya Bharti Airtel, tuliamua kulifutia Shirika hili madeni yenye thamani ya shilingi bilioni 100 ili yatumike kuwa sehemu ya mtaji. Na kupitia rasilimali zake, TTCL ilifanikiwa kukopa kiasi cha shilingi bilioni 96 kwa ajili ya kuongeza uwekezaji.

 

Vilevile, tuliiwezesha TTCL kupata masafa ya Megahezi 1,800 na 2,100 ili iweze kufunga mitambo ya mawasiliano ya teknolojia ya 2G (GSM), 3G (UMTS) na 4G (LTE) na hivyo kuondokana na teknolojia ya kizamani waliyokuwa wakitumia ya CDMA. Aidha, tuliikabidhi TTCL dhamana ya kusimamia na kuendesha Mkonga wa Taifa wa Mawasiliano na Kituo cha Kitaifa cha Kuhifadhi Kumbukumbu za Kimtandao (National Internet Data Centre). Hii imetuhakikishia usalama wa nchi yetu.

 

Nirudie tena kuwapongeza viongozi na watendaji wote wa TTCL kwa kazi kubwa na nzuri mnazofanya. Na binafsi nina imani, kutokana na kasi hii kubwa mnayokwenda nayo, baada ya kipindi kifupi kijacho, TTCL itakuwa imerejea kwenye hadhi yake na kuweza kutimiza malengo yaliyowekwa wakati wa kuanzishwa kwake mwaka 1993 kufuatia uamuzi wa kuligawa Shirika la Posta na Simu. Na ninafurahi Shirika la Posta nalo sasa limeanza kufanya kazi vizuri.

 

Nitumie fursa hii pia kuipongeza Kamati ya Bunge ya Miundombinu kwa kuishawishi Wabunge wengine kuridhia Sheria Mpya iliyoanzisha Shirika jipya la Mawasiliano la Tanzania. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Spika, Naibu Spika pamoja na Wabunge wote wa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali katika jitihada mbalimbali za kuleta maendeleo kwa nchi yetu. Hivi sasa tumeleta mapendekezo Bungeni kuhusu kuanzisha Akanti Jumuishi ya Serikali (Single Akaunti) ili kupunguza gharama za uendeshaji. Hivi sasa tuna akaunti takriban 1,013. Zaidi ya hapo, Akaunti hii Jumuishi itasaidia kudhibiti matumizi ya fedha za Serikali. Nina imani kuwa Waheshimiwa Wabunge wataliunga mkono pendekezo hilo.  

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa wote, Mabibi na Mabwana;

Tumekuja hapa kupokea fedha. Na kama nilivyosema awali, leo mimi ni mtu mwenye furaha sana. Kwa hiyo sitapenda kuwachosha kwa hotuba ndefu. Hata hivyo, kabla ya kuhitimisha naomba mniruhusu niseme mambo machache ya mwisho.

 

Kwanza, ni kwenu wafanyakazi wa TTCL. Napenda kuwahimiza kuchapakazi kwa uzalendo na bidii. Nimewasifia kwa mafanikio makubwa mliyoyapata ndani ya kipindi kifupi. Lakini msibweteke. Bado mna safari ndefu ya kufikia malengo tuliojiwekea. Hivyo basi, nawasihi sana ongezeni bidii. Boresheni huduma zenu na kuhakikisha zinapatikana kwa gharama nafuu. Itunzeni miundombinu mliyonayo. Lakini zaidi ya hapo, jitahidini kuwa wabunifu katika kubuni bidhaa mpya kwa ajili ya soko.

 

Shirika la Simu la Ethiopia limeweza kubuni Huduma ya Taarifa za Masoko ya Bidhaa. Wakulima wengi nchini Ethiopia wanaipenda sana huduma hii kwa vile inawapa taarifa za bei za mazao yao kwa wakati (yaani real time). Nchini Ghana, walibuni huduma ya kugundua uhalali au ubora wa bidhaa. Mtu akinunua bidhaa tu, anaingiza code ya bidhaa hiyo kwenye simu yake na muda huo huo anagundua kama bidhaa hiyo ni halisi au feki? Na ninyi mnaweza kuanzisha huduma kama hizo na kubuni bidhaa nyingine za namna hiyo ili kupata wateja wengi zaidi.

 

Pili, napenda kuhimiza menejimeti ya TTCL kutokuwa na kigugumizi katika kukusanya madeni kwa wateja. Kumbukeni kuwa mko kwenye ushindani wa kibiashara. Msipokusanya madeni kutoka kwa wateja wenu, hamtaweza kushindana. Hivyo, hakikisheni mnakusanya madeni yenu kwa wakati. Msibembeleze mtu. Biashara haina kubembelezana.

 

Tatu, nafahamu kuwa hivi sasa Serikali ipo kwenye majadiliano kuhusu mgogoro wa kibiashara na Kampuni ya Bharti Airtel. Nina imani majadiliano hayo, kama yatakamilika kama tunavyotarajia, yatatoa fursa kubwa zaidi ya kuliimarisha zaidi Shirika letu la Mawasiliano. Hivyo basi, nazihimiza pande zote mbili kuongeza kasi ya majadiliano hayo ili muafaka upatikane mapema.

 

Nne, napenda nitumie fursa hii kutoa wito kwa Watanzania kuiunga mkono TTCL. Kama mlivyosikia, sasa TTCL inatoa huduma nchi nzima na huduma zake ni za kiwango cha juu kabisa. Hivyo basi, kama kaulimbiu ya TTCL inavyosema, nawasihi Watanzania “Rudini nyumbani – kumenoga”. Na katika hili, niseme tu kwamba nitashangaa sana, endapo Watumishi wenzangu tunaolipiwa huduma za simu na Serikali tutashindwa kujiunga na mtandao huu wa TTCL. Nitashangaa sana.

 

Lakini pia, nitashangaa endapo taasisi za Serikali na hata sekta binafsi zitashindwa kutumia huduma mpya ambayo tumeizindua muda mfupi ujao ya mkutano mtandao (video conference). Nitashangaa sana. Huduma hii itasaidia kupunguza gharama za kusafiri ama kukodisha kumbi za mikutano. Hivyo basi, nawasihi sana mjiunge na huduma hii inayotolewa na shirika letu la mawasiliano tena kwa gharama nafuu sana.

 

Tano, napenda kutumia fursa hii kuagiza taasisi na mashirika mengine yenye kustahili kutoa gawio kwa Serikali kufanya hivyo. Nafahamu kuwa kuna takriban mashirika na taasisi zipatazo mashirika 91 zenye kustahili kutoa gawio kwa Serikali. Lakini si zaidi ya mashirika au taasisi 50 ndio yamekuwa yakitoa gawio kwa Serikali. Mathalan, mwaka 2014/2015 ni mashirika 24 tu ndio yalitoa gawio lenye thamani yake ilikuwa shilingi bilioni 130.686. Mwaka 2015/2016 mashirika 25 yalitoa gawio la shilingi bilioni 249.3. Na baada ya kuanza kuwabana, mwaka jana (2016/2017) mashirika 38 yalitoa gawio Serikalini lenye thamani ya shilingi bilioni 677. Hii inadhirisha kuwa yapo mashirika mengi hayatoi gawio.

 

Hivyo basi, namuagiza Msajili wa Hazina kuhakikisha mashirika na taasisi zote zenye kustahili kutoa gawio kwa Serikali zinafanya hivyo. Yatakayoshindwa kufanya hivyo, viongozi wake wabadilishwe ama yafutwe. Naamini tukiyabana mashirika hayo, tutaweza kukusanya mapato mengi zaidi ambayo yatatuwezesha kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuboresha huduma za jamii kwa wananchi wetu.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa wote, Mabibi na Mabwana;

Napenda kuhitimisha kwa kurudia tena kumshukuru Mheshimiwa Waziri Prof. Mbarawa pamoja na uongozi wa TTCL kwa kunialika kwenye tukio hili. Aidha, nawapongeza tena wafanyakazi wa TTCL kwa kazi nzuri na kubwa mnayoifanya. Napenda niwaahidi kuwa Serikali ipo pamoja nanyi, na tutaendelea kuwaunga mkono ili muweze kuongeza ushindani kwenye sekta hii ya mawasiliano nchini ili hatimaye wananchi wetu wanufaike kwa huduma bora zinazopatikana kwa gharama nafuu.

 

Mwisho lakini sio mwisho kwa umuhimu, nitumie fursa hii kuwapongeza TTCL kwa kutoa ajira ya ulinzi kwa Shirika la Suma-JKT.

 

Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kupokea Hundi ya Gawio la Serikali la Shilingi Bilioni 1.5 kutoka TTCL.

 

Mungu Ibariki TTCL!

 

Mungu Wabariki Wafanyakazi wa TTCL!

 

Mungu Ibariki Tanzania!

 

“Ahsanteni sana kwa Kunisikiliza”