Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE CHUO KIKUU CHA KILIMO CHA SOKOINE, MOROGORO, TAREHE 7 MEI, 2018

Monday 7th May 2018

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE CHUO KIKUU CHA KILIMO CHA SOKOINE, MOROGORO, TAREHE 7 MEI, 2018

 

Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako;

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi;

 

Mheshimiwa Steven Kebwe,

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro;

 

Prof. Raphael Chibunda, Makamu Mkuu wa Chuo

Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA);

 

Prof. Lughano Kusiluka, Makamu Mkuu wa Chuo

Kikuu cha Mzumbe;

 

Rasi na Manaibu Rasi wa Chuo Kikuu cha SUA;

 

Viongozi Wengine wa Serikali mliopo;

 

Waheshimiwa Viongozi wa Dini mliopo;

 

Ndugu Wanajumuiya wa Chuo Kikuu Kilimo

Cha Sokoine (SUA)

 

Wageni Waalikwa wote, Mabibi na Mabwana:

 

Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kufika hapa Chuo Kikuu cha Kilimo; Chuo ambacho kimepewa Jina la mmoja wa viongozi mahiri, shupavu na mtetezi wa wanyonge, aliyewahi kutokea katika nchi yetu, Hayati Edward Moringe Sokoine. Ingawa ametangulia mbele za haki, nina imani, kupitia jina la Chuo hiki, Watanzania wengi, kizazi kwa kizazi, wataendelea kumkumbuka na kumuenzi Kiongozi wetu huyo.

 

Napenda pia kutumia fursa hii kuwashukuru wana-SUA kwa mapokezi yenu mazuri. Nafahamu kuwa kama sio wote basi wengi weu hapa mlinipigia kura. Hivyo basi, kwa kuwa hii ni mara yangu kufika hapa tangu nimechaguliwa, napenda nitumie fursa hii kuwashukuru kwa dhati kabisa kwa kunichagua kuwa Rais wenu. Nasema “ahsanteni sana wana-SUA”. Niwaahidi tu kwamba sitowaangusha. Nitakuwa pamoja nanyina wakati wote.

 

Ndugu Wanajumuiya wa SUA;

Mabibi na Mabwana;

Tangu ijumaa iliyopita nimekuwa kwenye ziara ya Mkoa huu wa Morogoro. Nimepata fursa ya kukutana na kuzungumza na wananchi na halikadhalika kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo. Nimeweka Jiwe la Msingi la Barabara ya Kidatu – Ifakara yenye urefu wa kilometa 66.9 inayojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 104.5. Nimeshiriki Uzinduzi wa Daraja la Kilombero lenye urefu wa mita 384, ambalo ni la nne kwa ukubwa nchini na ambalo wameamua kulipa jina la Magufuli.

 

Jana niliingia hapa Morogoro mjini, ambapo mchana nilizindua Stendi ya Kisasa ya Mabasi pale Msamvu. Leo asubuhi nilitakiwa niondoke kurudi Dar es Salaam. Sikuwa nimepangiwa kuja hapa SUA. Lakini, nikasema hapana; siwezi kumaliza ziara yangu bila kufika hapa SUA; Chuo Kikuu cha pekee cha Kilimo hapa nchini. Hii ndio maana mnaniona nipo hapa muda huu.

 

Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;

Nimekuja hapa kwa sababu kubwa tatu. Kwanza kuwasalimu wana-Jumuiya wa Chuo Kikuu hiki. Sababu ya pili iliyonileta hapa ni kutambua mchango mkubwa unaotolewa na Chuo hiki katika maendeleo ya nchi yetu. Hakuna shaka yoyote kuwa Chuo hiki, tangu kianzishwe tarehe 1 Julai, 1984 kimetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi yetu, kupitia kozi mbalimbali kinazofundisha na tafiti kilizofanya katika fani mbalimbali (sayansi ya kilimo, misitu, tiba ya mifugo, ufugaji wa samaki, maendeleo vijijini, utalii, ualimu, n.k.).  Na mojawapo ya tafiti kubwa zilizowahi kufanywa na Chuo hiki, ambazo zinatambulika kimataifa, ni ule wa kuwafundisha panya kubaini mabomu na kuweza kugundua vimelea vya ugonjwa wa Kifua Kikuu.

 

Nitumie fursa hii, kukipongeza sana Chuo hiki kwa utafiti huo mkubwa ambao umeiletea sifa kubwa nchi yetu. Kwa hakika, mmetekeleza kwa vitendo dhamira ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, ya kuanzisha Chuo hiki. Nawapongezeni pia kwa ubunifu wenu wa kuongeza idadi ya kozi na fani mnazozifundisha. Nafahamu kuwa wakati Chuo hiki kinaanzishwa mwaka 1984, kilikuwa na vitivo vitatu tu; yaani kitivo cha kilimo, kitivo cha misitu na kitivo cha tiba ya mifuko. Sasa mmeongeza kozi nyingine, ikiwa ni pamoja na utalii, maendeleo vijijini, ualimu, n.k. Hongereni sana.

 

Ndugu Wanajumuiya wa SUA;

Sababu ya tatu iliyonisukuma kuja hapa leo ni kuwapa moyo na kuamsha ari na hamasa mpya kwenu ya kuendelea kujituma zaidi. Na katika hili, naomba nitaje maeneo machache, ambayo nitatamani sana Chuo hiki kiyape kipaumbele cha kutosha.

 

Eneo la kwanza ni kuendelea kufanya utafiti wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi. Ndugu zangu wana-SUA, mimi niliwahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi. Ninafahamu,  kama tukiweka mkazo na kuisimamia vizuri sekta hizi za kilimo, mifugo na uvuvi, nchi yetu itapata maendeleo ya haraka. Hii ni kwa sababu takriban asilimia 70 ya Watanzania wanaendesha maisha yao kupitia shughuli za kilimo, mifugo na uvuvi. Aidha, nchi yetu inashika nafasi ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya mifugo Barani Afrika. Zaidi ya hapo, tunayo maeneo mengi yenye kufaa kufanya shughuli za uvuvi. Hivyo basi, ni wazi kuwa endapo tutaziwekea mkazo sekta hizi; tutapiga hatua kubwa kimaendeleo.

 

Sambamba na hilo, hivi sasa nchi yetu imejipanga kujenga uchumi wa viwanda kwa lengo la kuharakisha maendeleo na kukabiliana na tatizo la ajira. Viwanda tunavyovilenga kuvijenga ni vile vyenye kutumia malighafi zinazopatikana kwa wingi hapa nchini, hususan mazao ya kilimo, mifuko na uvuvi. Hii yote inafanya sekta hii ya kilimo, mifugo na uvuvi kuwa na umuhimu wa pekee kwa nchi yetu. Hii ndio sababu nakisisitiza sana Chuo hiki cha pekee cha Kilimo nchini kuendelea kufanya tafiti zaidi ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi na hatimaye kuiwezesha nchi yetu kufanya mageuzi ya kiuchumi.

 

Nimefurahi wakati nikija hapa nimeona shamba lenu zuri la mfano. Nimeona mipapai midogo kabisa ikiwa tayari imezaa matunda. Hayo ni mafanikio makubwa. Na ni matumaini yangu kuwa utaalamu kama ule utasambazwa kwenye maeneo mengi ya nchi yetu. Tunataka wakulima wetu wajifunze mbinu za kisasa za kilimo ili waongeze uzalishaji. Na mahali pekee pa kujifunza mbinu hizo ni kwenye Chuo chenu hiki. Hakuna mahali pengine. Hii ndio sababu Serikali inakithamini sana Chuo hiki.  Na nitumie fursa hii kuwahakikishia kuwa tutaendelea kuwathamini na kushirikiana kwa karibu na ninyi. Baadhi yenu mtakuwa mkifahamu kuwa, mimi, tangu nikiwa Waziri mpaka sasa nimekuwa Rais, nimekuwa nikiwaamini sana wasomi wa Chuo hiki na nimewateua kushika nyadhifa mbalimbali. Naahidi nitaendelea kuwatumia wasomi wa Chuo hiki. Na katika kudhihirisha dhamira ya Serikali ya kutaka kuona Chuo hiki kinachangia maendeleo ya kilimo nchini, leo niwaahidi kuwapatia fedha za kununua matrekta 10 mapya kwa ajili ya kufanya mafunzo ya vitendo.

 

Ndugu Wana-SUA;

Ukiachilia mbali utafiti wa mazao, eneo jingine ambalo nitafurahi kama mtalipa kipaumbele ni sekta ya utalii. Kama mnavyofahamu, nchi yetu ina vivutio vingi vya utalii. Na hivi sasa tumeanza kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuikuza sekta hii ili iweze kutunufaisha zaidi kuliko ilivyo sasa. Tumejipanga kuanza kutangaza vivutio vyetu vyote, vikiwemo vya Ukanda wa Kusini, ambavyo ni karibu kabisa na hapa Morogoro. Sambamba na hayo, tunaimarisha miundombinu na huduma za usafiri, hususan usafiri wa ndege. Tunajenga viwanja vya ndege lakini pia tumenunua ndege mpya saba, tatu tayari zimeshawasili. Tumefanya hivyo kwa vile tunatambua kuwa ustawi wa sekta ya utalii kwa kiwango kikubwa inategemea usafiri wa anga. Takriban asilimia 70 ya watalii husafiri kwa kutumia ndege.

 

Kutokana na hatua tunazozichukua, ni wazi kuwa idadi ya watalii itaongezeka. Hii maana yake ni kwamba, nchi yetu itahitaji wataalam na watoa huduma wenye katika sekta ya utalii. Ni kwa sababu hiyo, narudia tena kukipongeza Chuo hiki kwa kuanzisha kozi ya utalii. Ombi langu kwenu endeleeni kuboresha elimu mnayoitoa na pia shirikianeni na mamlaka husika za utalii nchini katika kuibua na kutangaza vivutio vipya vya utalii. Vipo vivutio vingi ambavyo bado hatujavitangaza.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Ndugu Wanajumuiya wa SUA;

 Mabibi na Mabwana;

Moja ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuimarisha na kuboresha elimu nchini. Tangu tumeingia madarani tumechukua hatua mbalimbali kuendeleza jitihada zilizoanzishwa na Awamu zilizotangulia katika kuimarisha na kuiboresha sekta ya elimu nchini. Kama mjuavyo, elimu yetu imetoka mbali na kupitia kwenye changamoto nyingi. Hivyo basi, kwa upande wetu, tuliamua tuanze kwa kutoa elimu bila malipo kuanzia shule ya msingi hadi sekondari, ambapo kila mwezi tunatenga shilingi bilioni 23.868 kuigharamia. Tangu utaratibu huu uanze mwezi Desemba 2015 hadi mwezi Machi 2018, Serikali imetumia takriban shilingi bilioni 650.

 

Uamuzi huu wa kutoa elimu bila malipo umeongeza idadi ya wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza na kidato cha kwanza maradufu. Mathalan, kwa upande wa shule ya msingi, idadi ya wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza imeongezeka kutoka wastani wa watoto milioni 1 hadi kufikia milioni 2. Kwa upande wa sekondari idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kidato cha kwanza imeongezeka kwa wastani wa takriban asilimia 30. Hii maana yake ni kwamba watoto wengi, hususan kutoka familia masikini, walikuwa wakishindwa kupata elimu kwa kukosa ada au karo.

 

Kwa upande wa Elimu ya Juu, ninyi hapa mnafahamu vizuri, kuwa tumeongeza idadi ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo kutoka 98,300 mwaka 2015 hadi kufikia takriban 124,000 hivi sasa.  Hii imewezekana baada ya Serikali kuongeza bajeti ya mikopo kutoka shilingi bilioni 365. Mwaka wa Fedha 2015/2016 hadi kufikia shilingi bilioni 427 Mwaka 2017/2018. Na siku hizi fedha za mikopo zinatoka kwa wakati. Hata hivyo, ni ukweli kuwa, kutokana na rasilimali fedha kuwa ndogo na mahitaji kuwa makubwa, imefanya isiwe rahisi kutoa mikopo kwa wanafunzi wote. Hii ndio sababu tumeamua kuweka baadhi ya vigezo, ikiwemo uwezo wa familia ya mwanafunzi, masomo anayosomea, n.k. Kwa bahati nzuri, kama mlivyosikia, wanafunzi wa Chuo hiki cha Sokoine ni wanufaika wakubwa wa mikopo inayotolewa. Kati ya wanafunzi wapatao 8,000 wa Chuo hiki, zaidi ya wanafunzi wanafunzi 6,000 wamepata mikopo. Tumeamua kuwapatia mikopo wanafunzi wengi wa Chuo hiki kwa sababu hivi sasa nchi yetu inahitaji wataalamu wengi wa kilimo. Kupanga ni kuchagua.

 

Ndugu Wana-SUA, Mabibi na Mabwana;

Mbali na kuongeza wigo wa elimu kwa kuongeza idadi ya wanafunzi wa elimu msingi na vyuo vikuu, tunaboresha miundombinu mbalimbali ya taasisi zetu za kutolea elimu. Hivi sasa tupo kwenye utekelezaji wa mradi kabambe wa kukarabati shule za sekondari kongwe 88, zikiwemo Kilakala na Mzumbe zilizopo katika Manispaa hii ya Morogoro. Serikali pia imejenga na kukarabati miundombinu ya shule za msingi na sekondari za wananchi zipatazo 542, ambapo mpaka sasa tumetumia kiasi cha shilingi bilioni 88.402. Aidha, tumefanikiwa kumaliza kwa kiasi kikubwa tatizo la uhaba wa madawati kwenye shule nyingi za msingi na sekondari.

 

Kwa upande wa elimu ya juu, miradi mbalimbali ya miundombinu inaendelea. Mathalan, hapa SUA, kwenye bajeti ya mwaka huu, tumetoa shilingi bilioni 2 kwa ajili ya kujenga maabara kubwa (Multi-purpose Laboratory), ambayo ujenzi wake unatarajiwa kuanza mwezi Juni 2018. Tumetoa pia shilingi milioni 700 kwa ajili ya kujenga Mgahawa (Cafeteria) itakayochukua wanafunzi 400 kwa mpigo, ambayo nimeambiwa kuwa ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2018.  Vilevile, hapa SUA, kwenye bajeti ya Mwaka ujao wa Fedha (2018/2019) tumetenga shilingi bilioni 8 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Na napenda nitumie fursa hii kumwagiza Waziri wa Elimu fedha zilizotengwa kwa ajili ya kujengea Hosteli katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, shilingi bilioni 2, nazo zihamishiwe hapa SUA ili zisaidie kupunguza kwenye Chuo hiki. Nitoe wito kwa uongozi wa Chuo, kuhakikisha wanatumia vizuri fedha zinazoletwa na Serikali kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Chuo chenu.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Ndugu Wanajumuiya wa SUA;

 Mabibi na Mabwana;

Hivi punde nimetoka kusikiliza hoja mbalimbali kutoka kwa wana-Jumuiya wa Chuo hiki. Niseme tu kwa ujumla kuwa hoja zenu nimezipokea. Na kama mtakavyoona, baadhi tayari nimezijibu katika maelezo yangu, hususan kuhusu masuala mikopo na makazi ya wanafunzi. Hoja nyingine nadhani zipo ndani ya uwezo wenu wenyewe kuzitatua. Mathalan, masuala kama michango kuwa mingi kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza, suala la kubebana, n.k. Haya mnaweza kuyatatua ninyi wenyewe. Hivyo basi, nitatumia fursa hii kujibu au kutolea ufafanuzi baadhi ya hoja chache mlizowasilisha.

 

Kwanza, ni kuhusu suala la kuimarisha uhusiano na nchi ya Israeli, hususan katika masuala ya kilimo. Hili nakubaliana nalo na binafsi sina pingamizi kwa wataalam wetu kutembelea Israeli kwenda kujifunza. Na sio Israeli pekee, pamoja na nchi nyingine. Hatuwezi kuendelea endapo tutabaki tukijifungia tu sisi wenyewe hapa nchini. Hatuna budi tutoke nje ili kupata uzoefu kutoka kwa wenzetu. Na kwa bahati nzuri, nchi yetu ina marafiki wengi ambao wamekuwa wakitupatia fursa nyingi za masomo: Austaralia, China, Cuba, India, Urusi, Marekani, n.k. Lakini kwa bahati mbaya, fursa hizo hatujazitumia vizuri.Hivyo basi, nitoe wito kwa mamlaka husika kuhakikisha nchi yetu inanufaika na fursa hizo za elimu.

 

Suala la pili ambalo napenda kulizungumzia ni kuhusu madeni ya watumishi. Suala hili nimelieleza kwenye Sherehe za Mei Mosi hivi karibuni.  Serikali ina dhamira ya dhati kabisa ya kulipa madeni yote inayodaiwa na watumishi wake. Tangu tumeingia madarakani, tayari tumelipa madai ya watumishi yenye thamani ya takriban shilingi bilioni 220.4.  Tuendelea kulipa madeni yaliyosalia kwa kadri tutakavyokamilisha uhakiki. Kama mjuavyo, baadhi ya watumishi hawakuwa wakweli. Walitengeneza madeni mengi ya uongo. Hii ndio sababu inatulazimu tujiridhishe vizuri kabla ya kulipa madeni tunayodaiwa. Hivyo basi, nitoe wito kwa Mheshimiwa Waziri wa Elimu kuwasiliana na vyuo vyako vyote ili kupata madeni halali ya watumishi ili tuweze kuyalipa kwa haraka.

 

Tatu, ni kuhusu makazi na ofisi za watumishi. Suala hili nalo Serikali inalitambua. Hata hivyo, kutokana na uwezo mdogo wa kifedha na majukumu mengi tuliyonayo hivi sasa, imekuwa sio rahisi kuwapatia watumishi wetu wote makazi. Kama mnavyofahamu, Serikali ina watumishi wapatao laki 5. Hata hivyo, kupitia taasisi na mashirika yetu mbalimbali, tumekuwa tukiendelea kujenga nyumba za gharama nafuu maeneo mbalimbali nchini ili kuwawezesha watumishi kupanga au kununua. Hivyo basi, niwaombe watumishi kuchangamkia fursa hiyo. Aidha, nitumie fursa hii kuziomba taasisi za fedha, hususan benki, kujitahidi kutoa mikopo ya riba nafuu kwa watumishi ili kuwawezesha kununua na kujenga nyumba. Kuhusu tatizo la ofisi, niviombe vyuo vyote nchini kutumia vizuri fedha za malipo ya ada zinazobaki kwenye vyuo kutekeleza miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa ofisi.

 

Hoja ya mwisho ambayo napenda kuijibu ni kuhusu suala la watumishi wa darasa la saba. Suala hili ni la kisheria na ni hivi majuzi tu Serikali imelitolewa ufafanuzi Bungeni. Lakini, kwa kifupi tu napenda kusema kuwa, Mwaka 2004, Serikali ilitoa Waraka ambao uliweka katazo la kuajiri watu wenye elimu chini ya kidato cha nne kwenye taasisi zake. Uamuzi huu ulifikiwa baada ya kujiridhisha kuwa nchi yetu ilikuwa na wahitimu wengi wa kidato cha nne na kuendelea. Hata hivyo, Waraka huo haukuwahusu watumishi wenye elimu ya darasa la saba ambao tayari walikuwa wameajiriwa. Wao waliendelea na kazi zao kama kawaida kwa vile Sheria hiyo mpya iliwakuta wakiwa tayari kazini. Pamoja na kutolewa kwa Waraka huo, wapo watu, ambao kwa njia za ujanja ujanja, ikiwemo kwa kutumia vyeti vya kughushi, waliajiriwa. Kufuatia zoezi tulilolifanya la uhakiki, tuliwabaini watumishi wa namna hiyo wapatao 14,000 na hivyo ikabidi tuwaondoe kazini. Huu ndio ufafanuzi ambao naweza kuutoa kuhusu suala hili; na kama nilivyosema, hili ni suala la Sheria hivyo sina mamlaka ya kuliingilia.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Ndugu Wanajumuiya wa SUA;

 Mabibi na Mabwana;

Kama nilivyosema, nimekuja hapa kuwasalimu lakini pia kuwapa moyo ili muendelee kujituma zaidi. Napenda kurudia tena kuwapongeza kwa kazi nzuri na kubwa mnayoifanya lakini pia nawashukuru kwa mapokezi yenu mazuri. Wito wangu kwenu wana-SUA, hususan wanafunzi, someni kwa bidii. Hili ndilo jukumu lililowaleta hapa. Serikali inawapa mikopo kutoka kwenye kodi tunazokusanya kwa wananchi maskini ili muweze kusoma vizuri na hatimaye muweze kulikombea Taifa letu kiuchumi.

 

Hivyo basi, narudia sana kuwasihi wanafunzi wa Chuo hiki kuitumia vizuri fursa hii adimu mliyopata. Nitawashangaa sana na kwa kweli sitasita kuchukua hatua kali endapo, badala ya kusoma, ninyi mtatumia muda wenu hapa kufanya mambo mengine ambayo hayaendani kabisa na masuala ya elimu: kushiriki kwenye migomo au kuendesha shughuli za kisiasa. Mkifanya hivyo, nitachukua hatua kali. Na hili siwatishi bali nawaeleza ukweli.

 

Baada ya kusema hayo, narudia tena kusema kuwa, nakipenda sana Chuo hiki, na Serikali itaendelea kukiimarisha ili kiweze kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake.

 

Mungu Kibariki Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine!

Mungu Ibariki Tanzania!

 

“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”