Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE SHEREHE ZA KUKABIDHI KOMBE LA MASHINDANO YA AFRIKA MASHARIKI KWA TIMU YA TAIFA YA VIJANA WENYE UMRI CHINI YA MIAKA 17 NA MSHINDI WA LIGI KUU YA TANZANIA BARA UWANJA TAIFA, DAR ES SALAAM, TAREHE 19 MEI 2018

Saturday 19th May 2018

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI,

RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE SHEREHE ZA KUKABIDHI KOMBE LA MASHINDANO YA AFRIKA MASHARIKI KWA TIMU YA TAIFA YA VIJANA WENYE UMRI CHINI YA MIAKA 17 NA MSHINDI WA LIGI KUU YA TANZANIA BARA UWANJA TAIFA, DAR ES SALAAM, TAREHE 19 MEI 2018

 

Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Habari,

Utamaduni, Sanaa na Michezo;

 

Mheshimiwa Juliana Shonza, Naibu Waziri wa Habari,

Utamaduni, Sanaa na Michezo;

 

Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;

 

Bwana Leodger Chillah Tenga, Mwenyekiti wa Baraza

la Michezo Tanzania (BMT);

 

Bwana Wallace Karia, Rais wa Shirikisho la Mpira

wa Miguu Tanzania (TFF);

 

Waheshimiwa Viongozi na Wachezaji wa Mpira

wa Miguu na Michezo mingine mliopo;

 

Ndugu Wadhamini, Washabiki na Wapenzi wa Michezo mliopo;

 

Ndugu Wananchi Wenzangu, Mabibi na Mabwana:

 

Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufika hapa. Aidha, namshukuru Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwakyembe pamoja na Uongozi wa TFF kwa kunialika ili niweze kushiriki kwenye tukio hili la leo. Napenda kutumia fursa hii, hapa mwanzoni kabisa, kusema kuwa, mimi ni shabiki wa Timu ya Taifa, yaani Taifa Stars.

 

Nitumie fursa hii pia kuwapongeza wachezaji wa Timu za Simba na Kagera Sugar kwa burudani nzuri ambayo tumetoka kushuhudia muda mfupi uliopita. Kwa kweli mchezo ulikuwa mzuri. Timu zote zimejitahidi kuonesha uwezo wao wa kusakata kabumbu. Hongereni sana wachezaji wa Simba na Kagera Sugar. Lakini zaidi, naipongeza Timu ya Kagera Sugar kwa ushindi mlioupata.

 

Ndugu Washabiki na Wapenzi wa Michezo;

Kama mnavyofahamu, hivi karibuni Vijana wetu wa Serengeti Boys walifanikiwa kuchukua Kombe la Mashindano ya Afrika Mashariki kwa Vijana chini ya Umri wa Miaka 17 (CECAFA U17), ambayo yaliyofanyika nchini Burundi. Binafsi, nilikuwa nikifuatilia kwa karibu mashindano yale. Nilishuhudia mwenyewe jinsi vijana wetu walivyojituma na kucheza mchezo mzuri hadi kufanikiwa kuchukua Kombe.

 

Kutokana na ushindi huo mkubwa walioupata, nikaona ni vyema nikutane nao ili niwapongeze. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza kwa dhati kabisa wachezaji pamoja na walimu wa Serengeti Boys kwa kututoa kimasomaso na kuchukua kombe hilo. Hongereni sana. Na bila shaka, huu ni mwanzo tu. Nina matumaini makubwa kuwa hata mwakani Kombe la Afrika litabaki hapa nchini.

Nitumie fursa hii pia kuipongeza Timu yetu ya Wasichana wanaoishi Mazingira Magumu ambayo ilishiriki Mashindano ya Kombe la Dunia nchini Urusi na kushika nafasi ya pili. Nao wameipeperusha vyema bendera ya nchi yetu na kututangaza kimataifa. Hongera sana kwa wachezaji, walimu na viongozi wa Timu hiyo. Wito wangu kwa TFF, Vyama vingine vya Michezo, Vilabu pamoja na Wadhamini mbalimbali, endeleeni kushirikiana katika kuibua vipaji na pia kuviendeleza. Wakati mwingine tumekuwa tunaibua vipaji lakini tunashindwa kuviendeleza. Binafsi, nitafurahi sana kama baadaye nitasikia vijana hawa wa Serengati Boys na Timu ya Taifa ya Watoto wanaoishi Mazingira Magumu wakichezea Timu zetu za Taifa ya Wakubwa au hata vilabu vikubwa vya hapa nchini ama nje ya nchi.

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Ukiachilia mbali ubingwa wa Serengeti Boys, nimekuja hapa kukabidhi Kombe la Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa Timu ya Simba. Mimi huwa nafuatilia fuatilia ligi mbalimbali, za hapa nyumbani lakini pia nje ya nchi. Katika ufuatiliaji wangu wa ligi mbalimbali duniani, jumamosi iliyopita, niligundua kuwa ni timu mbili tu ndizo zilikuwa zimechukua ubingwa bila kufungwa. Simba na Barcelona ya Hispania. Barcelona baadaye ikafungwa; lakini na leo Simba nayo wamefungwa. Hata hivyo, kwa namna walivyokuwa wamechukua ubingwa, na kwa kuwa kilikuwa kimepita kipindi kirefu bila ya wao kuchukua ubingwa, niliona nije kuwapongeza. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza wachezaji, walimu na viongozi wa Simba, akiwemo Msemaji wao, Bwana Haji Manara, kwa kufanikiwa kuchukua ubingwa kwa stahili hii ya pekee. Nafahamu hii sio mara ya kwanza kwa Simba kuchukua ubingwa kwa staili hiyo. Walishawahi kufanya hivyo siku za nyuma.

 

Nazipongeza timu nyingine zilizoshiriki Ligi kwa kuonesha ushindani, lakini pia kwa kukubali matokeo. Nimefurahi kuwa Msimu huu hakuna Timu iliyokwenda FIFA kudai pointi. Napenda niseme pia kuwa ushindi ambao Timu ya Kagera Sugar leo umeipata umethibitisha kuwa Ligi ilikuwa ya ushindani; lakini pia unatoa changamoto kwa Timu ya Simba kujipanga vizuri zaidi kuweza kuiwakilisha vyema nchi yetu kwenye mashindano ya kimataifa. Na kwa kusema kweli, kwa kiwango hiki kilichooneshwa na Simba leo, endapo wataendelea hivi, hawawezi kufika mbali kimataifa. Ni lazima wajipange vizuri.

 

Ndugu Wapenzi wa Michezo;

Sababu ya tatu iliyoisukuma kukubali mwaliko wa kuja hapa ni kuunga mkono jitihada za viongozi wapya wa TFF. Kama mnavyofahamu, vyama vingi vya michezo, vikiwemo vilabu, vimekuwa na matatizo mengi ya uongozi. Vimekuwa vikikabiliwa na tuhuma za rushwa, ufisadi, wizi, matumizi mabaya ya madaraka, n.k. Pamoja na ukweli huo, bila shaka, wengi wenu, mtakubaliana nami kuwa, tangu uongozi mpya wa TFF umeingia madarakani umeonesha mabadiliko makubwa. Wanaonesha uadilifu na kujitahidi kufuata sheria na kanuni. Ni kweli, mapungufu bado yapo, lakini wanajitahidi.

 

Kutokana na jitihada walizoanza kuzifanya, nimeona nikubali mwaliko wao kwanza ili kuwaunga mkono, lakini pili, kuwapa moyo kuendelea na jitihada hizo. Na niwape moyo TFF, “endeleeni na jitihada hizo”. Serikali inawaunga mkono. Na napenda kutumia fursa hii, pia kuviomba vyama vingine vya michezo kuiga mfano huu ulioanza kuoneshwa na Viongozi wapya wa TFF. Tusiruhusu Vyama vyetu vya Michezo kuwa vichaka vya kujificha wahalifu.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Ndugu Wanamichezo;

 Mabibi na Mabwana;

Michezo ni burudani. Michezo ni afya. Michezo ni ajira. Lakini pia, katika dunia ya sasa, michezo ni biashara kubwa. Kwa kutambua hilo, Serikali ya Awamu ya Tano ninayoiongoza itaendeleza jitihada zilizoazishwa na Serikali zilizotangulia katika kukuza sekta ya michezo nchini. Na napenda kutumia fursa hii kuipongeza sana Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, chini ya Dkt. Mwakyembe, kwa jitihada mbalimbali inazofanya kuimarisha sekta ya michezo nchini.

 

Serikali inaahidi kuendelea kutenga bajeti kwa ajili ya michezo. Tutaendelea kutoa mafunzo na kuajiri wataalam wa michezo. Zaidi ya hapo, tutaendelea kujenga miundombinu ya michezo mbalimbali. Hivi karibuni, tunatarajia kuanza ujenzi wa Uwanja Mkubwa wa Kisasa kwenye Jiji la Dodoma kwa kushirikiana na marafiki zetu wa Morocco. Nitumie fursa hii kuzihimiza Halmashauri zote nchini kuendelea kutenga maeneo ya michezo na kuhakikisha hayavamiwi. Aidha, nakihimiza Chama changu (CCM) ambacho kinamiliki viwanja vingi nchini, nacho kuboresha viwanja vyake. Kwa Watanzania, hususan washabiki na wapenzi wa michezo nchini, nawasihi kuilinda  miundombinu inayojengwa. Tukio kama lile la kung’oa viti uwanjani halipaswi kujirudia tena.

 

Sambamba na hayo, Serikali itaendelea kushirikiana, kwa hali na mali,  na Vyama vyote vya Michezo katika kuziandaa Timu zetu za Taifa ili zituwakilishe vyema kwenye mashindano ya kimataifa. Mathalan, kama nilivyogusia awali, mwezi Aprili mwakani, nchi yetu itakuwa mwenyeji wa Mashindano ya Afrika ya Vijana chini ya umri wa Miaka 17. Napenda niahidi kuwa Serikali itashirikiana na TFF katika kufanikisha maandalizi ya mashindano hayo; lakini pia katika kuiandaa Serengeti Boys ili kombe hilo libaki hapa nchini, na kuweza kuhitimisha dhana kuwa sisi ni “kichwa cha mwendawazi”.

 

Niwaombe wadau na wadhamini mbalimbali kuendelea kushirikiana na Serikali pamoja na Vyama vya Michezo na Vilabu katika kuinua sekta ya michezo nchini. Mimi naamini, kama sote tukishirikiana, sekta ya michezo itazidi kukua na kuchangia maendeleo ya nchi yetu.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wanamichezo;

Sikuja hapa kuhutubia. Nimekuja hapa kuungana na Timu zetu ambazo zimeshinda mashindano mbalimbali. Timu ya Serengeti Boys, Timu ya Wasichana wanaoishi Mazingira Magumu pamoja na Timu ya Simba. Nazipongeza sana timu hizo zote kwa ushindi walioupata. Lakini, nitumie fursa hii pia kutoa wito kwa wanamichezo na Watanzania kwa ujumla kujipanga vizuri katika michezo. Kwa muda mrefu, tumekuwa wasindikizaji. Sasa tubadilike ili angalau timu zetu ziweze kushinda mashindano ya Afrika na kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia.  Watanzania wengi wanatamani kuona timu zao zikishinda na sio kila siku kuwa wasindikizaji. Hii ndio sababu nimekuja hapa kutoa hamasa kwa timu zetu zote. Na niseme tu kwamba, timu yoyote itakayoshinda, mimi nitaipongeza. Iwe Simba, Yanga, Kagera au timu nyingine yoyote ile, nitaipongeza. Ninachotaka mimi ni kuona timu zetu za michezo yote, zinashinda. Na kwa kweli, timu zetu zinao uwezo wa kushinda. Kinachohitajika ni kujiandaa na kujipanga vizuri.

 

Nihitimishe kwa kuishukuru tena Wizara na TFF kwa kunialika. Aidha, narudia tena kuzipongeza Timu za Serengati Boys, Timu ya Simba na Timu ya Wasichana wanaoishi Mazingira Magumu kwa ushindi walioupata. Nimefurahi kuwa leo Uwanja umejaa. Hongereni sana wapenzi na washabiki kwa kujitokeza kwa wingi.

Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kutekeleza jukumu lililonileta la kukabidhi Kombe kwa timu zetu za Serengeti Boys, Timu ya Wasichana wanaoishi Mazingira Magumu pamoja na Simba Sports Club.

 

Mungu Ibariki Sekta ya Michezo nchini!

 

Mungu Ibariki Tanzania!

 

“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”