Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE UFUNGUZI WA BARABARA YA IYOVI - IRINGA –MAFINGA PAMOJA NA KIWANDA CHA KUTENGENEZA CHAKULA CHA KUKU (SILVERLANDS TANZANIA LTD) IHEMI, IRINGA, TAREHE 3MEI, 2018

Thursday 3rd May 2018

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE UFUNGUZI WA BARABARA YA IYOVI - IRINGA –MAFINGA PAMOJA NA KIWANDA CHA KUTENGENEZA CHAKULA CHA KUKU (SILVERLANDS TANZANIA LTD)

IHEMI, IRINGA, TAREHE 3MEI, 2018

 

Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa,

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano;

 

Mheshimiwa Charles Mwijage, Waziri wa Viwanda,

         Biashara na Uwekezaji;

 

Bibi Camilla Christensen, Naibu Balozi wa Denmark;

 

Mheshimiwa Amina Masenza, Mkuu wa Mkoa

wa Iringa na Wakuu wa Mikoa wote mliopo;

 

Waheshimiwa Makatibu Wakuu mliopo;

 

Mheshimiwa Suleiman Kakoso, Mwenyekiti wa Kamati

ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu;

 

Waheshimiwa Wabunge na Madiwani wote mliopo;

 

Viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;

 

Mtendaji Mkuu na Wafanyakazi wa TANROADS;

Viongozi wengine wa Serikali, Vyama vya Siasa

na Dini mliopo;

 

Waheshimiwa Wageni Wote Waalikwa;

Ndugu Wananchi Wenzangu, Mabibi na Mabwana:

Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai na kutuwezesha kukutana mahali hapa. Nawashukuru pia Waheshimiwa Mawaziri Prof. Mbarawa na Charles Mwijage, Uongozi wa Mkoa wa Iringa pamoja na Uongozi wa Kiwanda cha Silverlands Tanzania Ltd kwa kunialika kuja kuzindua barabara ya Iyovi – Iringa – Mafinga pamoja na Kiwanda cha Kutengeneza Chakula cha Kuku cha Silverlands Tanzania Ltd. Ahsanteni sana kwa kunialika.

 

Kwa namna ya pekee, napenda niwashukuru wananchi wa hapa Ihemipamoja na wakazi wote wa Wilaya hii ya Iringa Vijijini kwa mapokezi yenu mazuri. Hii ni mara yangu ya kwanza kuja hapa Ihemi tangu niwe Rais wa nchi yetu. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru sana wana-Ihemi kwa kunipa kura nyingi za “ndiyo” zilizoniwezesha kuchaguliwa. Ahsanteni sana. Nawaahidi nitaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuwatumikia na kuiletea maendeleo nchi yetu.

 

Ndugu Wananchi Wenzangu, Mabibi na Mabwana:

Kama mtakavyokumbuka, moja ya ahadi kubwa tulizotoa wakati wa kampeni ilikuwa kujenga uchumi wa viwanda. Nakumbuka pia tulitaja na kuelezea sifa za viwanda tulivyolenga kuvijenga. Kwanza, vyenye kuajiri watu wengi ili kupunguza tatizo la ajira nchini. Pili, vyenye kutumia malighafi zinazopatikana kwa wingi hapa nchini ili mazao yetu na rasilimali nyingine tulizonazo zipate masoko. Tatu, ambayo bidhaa zake zinatumika kwa wingi hapa nchini na pia kuweza kuuzwa nje ya nchi. Lengo hapa ni kupunguza utegemezi wa kununua bidhaa kutoka nje, lakini pia kuipatia nchi yetu fedha za kigeni. Na nne, vyenye kutumia teknolojia ya kati ili iwe rahisi kwa wananchi wetu kujifunza.

 

Kiwanda cha Silverlands Tanzania Ltd kinazo sifa zote hizo nne nilizozitaja. Kinaajiri watu wengi. Tumesikia hivi punde kuwa Kiwanda kimetoa ajira zipatazo 938.  Hii ni idadi kubwa. Kiwanda pia kinatumia malighafi nyingi za hapa nchini. Wamesema wenyewe hapa, asilimia 80 ya malighafi za Kiwanda chao zinapatikana hapa hapa nchini. Mahindi na Soya. Hii inamaanisha kuwa wakulima wa mazao hayo, hususan wa Wilaya hii ya Iringa Vijijini, hivi sasa wana uhakika wa soko la mazao yao. Aidha, bidhaa zinazozalishwa na Kiwanda (yaani chakula cha kuku) zinatumika kwa wingi hapa nchini. Kama mnavyofahamu, siku hizi Watanzania wengi wanafuga kuku. Lakini kama mlivyosikia, chakula cha kuku wanachozalisha, wanakiuza pia nje ya nchi. Wanauza Ethiopia, Kenya, Nigeria na Uganda. Hii maana yake ni kwamba Kiwanda cha Silverlands kinaingiza nchi yetu fedha za kigeni.

 

Napenda nitumie fursa kuwapongeza wamilikiwa Kiwanda cha Silverlandskwa kuamua kuwekeza kiasi cha Dola za Marekani milioni 71 hapanchini. Mmetoa ajira kwa Watanzania, mmewapa wakulima soko la mazao yao, mnaipatia Serikali yetu mapato kupitia kodi, na pia kuingiza fedha za kigeni nchini. Ninawashukuru na kuwapongeza sana. Aidha, nawapongeza kwa kuanzisha Kituo cha Mafunzo, ambapo mpaka sasa mmesema mmetoa mafunzo ya watu wapatao 895. Tunawashukuru na kuwapongeza sana. Na ninawahakikishia kuwa Serikali ipo pamoja nanyi. Ninafahamu kuwa yapo matatizo madogo kati ya Kiwanda na wananchi wa hapa, lakini nimefurahi Uongozi wa Kiwanda umeahidi kuyashughulikia. Hilo ni jambo zuri; na ni imani yangu kuwa Kiwanda hiki pia sasa kitaanza kulipa kodi kwa Serikali.

 

Napenda pia kuipongeza Wizara ya Viwanda kwa kuendelea kuwahamasisha wawekezaji wa hapa nchini na nje ya nchi kuwekeza kwenye sekta ya viwanda nchini. Vilevile, naupongeza uongozi wa Mkoa wa Iringa kwa kuweka mazingira mazuri yaliyowezesha Kiwanda cha Silverlands Tanzania Ltd kujengwa. Nimeambiwa Mkoa wa Iringa hivi sasa una jumla ya viwanda 2,663. Hongereni sana wana-Iringa. Endeleeni kuwavutia wawekezaji kwenye Mkoa wenu ili kusaidia kuondoa tatizo la ukosefu wa ajira, hususan kwa vijana.

 

Ndugu Wananchi Wenzangu, Mabibi na Mabwana:

         Ili sekta yetu ya viwanda izidi kukua, kustawi na kushamiri, tunahitaji kufanya mambo mawili muhimu. Kwanza, kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme. Umeme ni injini ya viwanda. Mitambo mingi ya viwandani inahitaji umeme ili iweze kufanya kazi. Pili, miundombinu ya usafiri. Ili malighafi ziweze kufika viwandani zinahitaji kusafirishwa. Na vilevile, ili bidhaa za viwandani ziweze kufika kwenye masoko, zinahitaji huduma ya usafiri. Mathalan, ili mahindi na soya yaweze kufika kwenye Kiwanda cha Silverlands inabidi yasafirishwe. Na vivyo hivyo, ili chakula cha kuku cha Kiwanda cha Silverlands kiweze kufika kwenye masoko, huduma ya usafiri inahitajika. Hii inadhihirisha kuwa miundombinu ya usafiri ni muhimu katika kujenga viwanda.

 

Ni kwa kutambua hilo, Serikali imeweka mkazo mkubwa katika kujenga miundombinu ya usafiri. Tunajenga reli. Tunapanua Bandari. Tunajenga viwanja vya ndege. Na halikadhalika, tunajenga barabara. Wiki iliyopita nilizindua Barabara ya Dodoma – Babati yenye urefu wa kilometa 251. Juzi tena (Jumapili) nimezindua Barabara ya Fufu – Migori – Iringa yenye urefu wa kilometa 189. Na leo nimefurahi kuja hapa Ihemikuzindua barabara hii ya Iyovi – Iringa – Mafinga yenye urefu wa kilometa 218.6. Nimefurahi sana.

 

Barabara hii ya Iyovi – Iringa – Mafinga ni muhimu sana, sio tu katika kujenga viwanda, bali pia katika kukuza uchumi wa nchi yetu. Kama mlivyosikia, Barabara hii ni sehemu ya Barabara Kuu ya TANZAM (Tanzania na Zambia) inayoanzia Dar es Salaam na kupita Mikoa ya Pwani, Morogoro, Iringa, Njombe, Mbeya na kuishia Tunduma, Mkoani Songwe, kwenye mpaka wa nchi yetu na Zambia, yenye urefu wa kilometa 918. Barabara hii pia inaungana na Barabara Kuu ya Kaskazini (The Great North) inayoanzia Cairo hadi Cape Town, ambayo inapita kwenye nchi 8. Kwa kuzingatia hilo, ni wazi kuwa, kukamilika kwa barabara hii kutafungua fursa nyingi za kiuchumi kwenye maeneo inakopita. Kuanzia biashara, kilimo, ufugaji, shughuli za misitu, n.k. Na kwa kuwa Barabara hii inapita kwenye maeneo ya vivutio vingi vya utalii, ikiwemo Hifadhi za Taifa za Ruaha, Mikumi, Selous, Milima ya Udzungwa, n.k., ni imani yangu kuwa watalii wengi watakuja. Kwa sababu hiyo, nawasihi sana wananchi wanaoishi kandokando ya barabara hii, kuchangamkia fursa. Itumieni barabara hii kuinua vipato vyenu na kuboresha hali yenu ya maisha. Hayo ndio malengo makuu ya Serikali kukopa fedha ili kujenga barabara hii.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa;

Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana:

Kama mlivyosikia, ujenzi wa Barabara hii ya Iyovi – Iringa – Mafinga umegharimu shilingi bilioni 283.715. Fedha hizo ni mkopo kutoka kwa marafiki zetu wa Denmark. Mbali na kutufadhili mradi huu, Denmark tulishirikiana nao katika ukarabati wa barabara ya Ubungo – Mlandizi yenye urefu wa kilometa 65.7; Chalinze – Melela yenye urefu wa kilometa 129 pamoja na Chalinze – Segera – Tanga yenye urefu wa kilometa 245. Vilevile, Denmark wamefadhili ukarabati wa barabara za kiwango cha changarawe zenye urefu wa kilometa 900 hapa nchini.

 

Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii, kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Tanzania, kutoa shukran zangu nyingi kwa Serikali na Wananchi wa Denmark kwa kutufadhili kutekeleza mradi huu pamoja na miradi mingine ya maendeleo. Tunawashukuru sana, tena sana. Nimefurahi kuona Naibu Balozi wa Denmark, Bibi Camilla yupo hapa. Tunaomba utufikishie shukrani zetu kwenye Serikali na Wananchi wa Denmark. Endeleeni kutuunga mkono. Misaada mtakayotupatia, tutaitumia vizuri. Hakuna senti itakayopotea.

 

Lakini kupitia kwako, Naibu Balozi, Bi. Camilla, naomba nichomekee jambo moja. Barabara hii mliyotufadhili imejengwa vizuri sana. Na napenda nitumie fursa hii kumpongeza sana Mkandarasi aliyeijenga. Hata hivyo, Barabara hii tatizo lake inapita katikati ya Mji wa Iringa na hivyo imeanza kusababisha msongamano wa magari. Zaidi ya hapo, kama unavyofahamu, kupitisha barabara kubwa kama hii katikati ya mji ni hatari. Hivyo basi, nitumie fursa hii, kuiomba Serikali ya Denmark kuona uwezekano wa kufadhili ujenzi wa Barabara ya Mzunguko ya takriban kilometa 12 ili magari makubwa yasilazimike kupita mjini. Ni imani yangu kuwa  Serikali ya Denmark itakubali ombi letu, hata kama itakuwa mkopo.

 

 

Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi;

Wageni Waalikwa;

Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;

Nimekuja hapa kwa ajili ya kuzindua Kiwanda cha Silverlands Tanzania Ltd na Barabara ya Iyovi - Iringa –Mafinga yenye urefu wa kilometa 218.6. Nimetumia fursa hii pia kuwasalimu na kuwashukuru kwa kunipigia kura. Hata hivyo, kabla sijahitimisha hotuba yangu, naomba niseme maneno machache ya mwisho.

 

 Kwanza, napenda kutumia fursa hii kuendelea kuwahamasisha Watanzania na pia watu kutoka nje kuja kuwekeza nchini. Nchi yetu ina fursa nyingi za kuwekeza kwenye sekta ya viwanda. Tuna sheria nzuri za kuwalinda wawekezaji. Na halikadhalika, tunalo soko kubwa la kuuzia bidhaa. Kama mjuavyo, sisi ni wanachama wa EAC na SADC, ambapo kwa pamoja, Jumuiya hizi zina idadi ya watu wapatao milioni 500. Hili ni soko kubwa la bidhaa.

 

Pili, wahimiza wananchi na watumiaji wa barabara nitakayoizindua hivi punde, kuhakikisha mnaitunza. Ujenzi wa miundombinu ya barabara kama hii unagharimu fedha nyingi. Hivyo, ni lazima tuzitunze. Aidha, barabara hii haipaswi kuwa chanzo cha ajali. Hivyo, nawasihi madereva kuwa waangalifu pindi wanapoendesha vyombo vya moto barabarani.

 

Tatu na mwisho, lakini sio mwisho kwa umuhimu, ni kwenu wana-Ihemi na wana-Iringa kwa ujumla. Fursa nyingi sasa zinakuja kwenye Mkoa wenu. Tumeanza kutekeleza mpango kabambe wa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika Ukanda huu wa Kusini. Tunajenga Kiwanja cha Ndege cha Nduli. Barabara ndio kama hivi zinajengwa. Sambamba na hilo, hapa Iringa ni karibu kabisa na Dodoma, ambako Serikali imeamua kuhamishia Makao yake Makuu. Waswahili wanasema, “ukikaa karibu na uaridi lazima utanukia”. Hivyo, nawasihi mjiandae kutumia fursa ambazo Serikali inawaletea.

 

Lakini nina maombi mawili kwenu. Nawasihi muendelee kuiunga mkono Serikali, hususan kwa kudumisha amani na umoja wetu, kuchapa kazi kwa bidii na bila kusahau kulipa kodi. Ulipaji wa kodi ni muhimu sana. Aidha, nawasihi mjitahidi kujikinga na ugonjwa wa ukimwi. Hali ya ugonjwa huu katika Mkoa wenu sio ya kuridhisha sana.

 

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana, napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri kwa kunialika kwenye shughuli hii. Nawapongeza Wamiliki wa Kiwanda cha Silverlands kwa kuamua kuwekeza hapa nchini. Aidha, naipongeza Wizara ya Ujenzi, TANROADS, wakiongozwa na Mhandisi Mfugalea, pamoja na Mkandarasi kwa kujenga Kiwanda hiki. Mwisho lakini sio kwa umuhimu, naushukuru uongozi wa Mkoa wa Iringa pamoja na wana-Iringa kwa ujumla kwa mapokezi yenu mazuri mliyonipa tangu nimewasili kwenye Mkoa wenu.

 

Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kutekeleza jukumu lililonileta la kuzindua barabara ya Iyovi - Iringa – Mafinga yenye urefu wa kilometa 218.6 iliyojengwa kwa gharama za shilingi bilioni 283.715 kwa ufadhili wa Serikali ya Denmark.

 

Mungu Ibariki Iringa!

Mungu Ubariki Uhusiano kati ya Tanzania na Denmark!

Mungu Ibariki Tanzania!

 

“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”