Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA UWEKAJI JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU, DODOMA, TAREHE 20 DESEMBA, 2017

Wednesday 20th December 2017

Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu

wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Dkt. Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango;

 

Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri mliopo;

 

Mheshimiwa John Malecela, Waziri Mkuu Mstaafu;

 

Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;

 

Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma;

 

Mheshimiwa Hawa Ghasia, Mwenyekiti wa Kamati

ya Bunge ya Bajeti;

 

Mheshimiwa Ian Myles, Balozi wa Canada nchini;

 

Mheshimiwa Mama Bella Bird, Mwakilishi

wa Benki ya Dunia nchini;

 

Waheshimiwa Wabunge na Mstahiki Meya

wa Manispaa ya Dodoma;

 

Ndugu Mkurugenzi Mkuu pamoja na Watumishi

wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu;

 

Waheshimiwa Viongozi mbalimbali mliopo hapa;

 

Wageni Waalikwa wote, Mabibi na Mabwana:

 

         Napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wetu, kwa kutupa uhai na kutuwezesha kukutana hapa leo. Aidha, naushukuru uongozi wa Wizara ya Fedha pamoja na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kunialika kwenye hafla hii ya kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu hapa Dodoma, ambako ndiko Makao Makuu ya Nchi yetu.  Ahsanteni sana.

 

Aidha, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru wageni wote waalikwa pamoja na wananchi wa Dodoma kwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hili. Nina uhakika kuwa mmejitokeza kwa wingi sio tu kwa sababu mnafahamu manufaa ya Jengo hili kujengwa hapa Dodoma, Makao Makuu ya Nchi yetu; bali pia kwa kuwa mnatambua umuhimu wa takwimu kwa maendeleo ya nchi.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wananchi Wenzangu, Mabibi na Mabwana;

Nafahamu kuwa wengi wetu hapa tunajua umuhimu wa takwimu. Hata hivyo, napenda kutumia fursa hii kusisitiza kuwa takwimu ni muhimu. Na ni muhimu katika nyanja zote. Iwe kiuchumi, kisiasa, kijamii na halikadhalika kiulinzi na usalama; na hata kiutamaduni.

 

Takwimu, na hasa zikiwa sahihi, zinaiwezesha Serikali kutambua mahitaji ya nchi au wananchi; kuweka malengo na kuandaa mipango ya maendeleo; pamoja na kufuatilia utekelezaji wake. Mathalan, kupitia takwimu za idadi ya watu, Serikali inatambua kiasi gani cha fedha kinachotakiwa kutengwa kwa ajili ya kununua dawa; au kufahamu mahali gani shule au kituo cha afya kijengwe.

 

Sambamba na hayo, takwimu zinaliwezesha Taifa kujipima limefikia hatua gani kimaendeleo, hususan kwa kutumia vigezo mbalimbali, ikiwemo pato la taifa, wastani wa umri wa kuishi, kiwango cha vifo kwa makundi mbalimbali (watoto wachanga, akinamama wajawazito) n.k. Zaidi ya hapo, takwimu ni muhimu kwa nchi kama yetu kwa ajili ya kufahamu utajiri na rasilimali tulizonazo, kama vile madini, gesi, mafuta, wanyama pori, mifugo, rasilimali za kwenye maji, n.k.

 

Hivyo basi, kwa ujumla, naweza kusema kuwa, takwimu ni muhimu sio tu katika nyanja zote, bali pia katika ngazi zote. Iwe ngazi ya mtu mmoja mmoja, familia, taasisi ya Serikali au isiyo ya Serikali; na Taifa kwa ujumla.  Hii ndio sababu kuna usemi wa Kiingereza usemao “Without good statistics, the development process is blind”. Tafsiri ya Kiswahili isiyo rasmi ya usemi huu ni kwamba “bila ya takwimu sahihi, ni vigumu kupata maendeleo”.

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Ni kutokana na ukweli huo, napenda kutumia fursa hii kuipongeza Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya katika kuandaa takwimu mbalimbali nchini. Hongereni sana. Napenda pia kutumia fursa hii, kuwapongeza kwa uamuzi wenu wa kujenga Ofisi hii hapa Dodoma. Kama mnavyofahamu, Serikali imedhamiria kwa dhati kabisa kuhamia Dodoma. Hivyo basi, ujenzi wa Jengo hili, ambalo, bila shaka litaboresha mandhari ya Mji wa Dodoma, unaenda sambamba na azma ya Serikali ya kuhamia Dodoma. Nimefurahi kusikia kuwa kazi ya ujenzi wa Jengo hili umekuwa ukitoa wastani wa ajira za moja kwa moja zipatazo 120 kwa siku; na kwamba kazi ya usanifu, ushauri na usimamizi inafanywa na Wataalam wa Tanzania. Hili ni jambo zuri kwa vile linawajengea uwezo wataalam wetu wa ndani.

 

Lakini, kwa namna ya pekee, napenda kutumia fursa hii kutoa shukrani zangu nyingi kwa washirika wetu mbalimbali, ambao wameufadhili mradi huu utakaogharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 11.6 hadi kukamilika. Tunaishukuru Benki ya Dunia, Shirika la Maendeleo la Uingereza (DfID) na Shirika la Maendeleo la Canada. Tunawashukuru sana; na nimefurahi kuona wawakilishi wa Taasisi hizi tuko nao hapa. Pokeeni shukrani zetu nyingi, na tunawaomba muendelee kutuunga mkono. Nawahakikishia kuwa kila senti mtakayotupatia tutaitumia vizuri. Hakuna hata senti moja itakayopotelea kwenye mifuko ya watu.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wananchi Wenzangu, Mabibi na Mabwana;

Mwanzoni mwa hotuba yangu nimeeleza kuwa takwimu ni muhimu kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo kutambua ukuaji uchumi wa Taifa. Hivyo basi, kwa kuwa leo nimekuja hapa kuweka Jiwe la Msingi la Ofisi ya Takwimu; na kwa kuwa nipo hapa Dodoma, Makao Makuu ya Nchi; napenda kutumia fursa hii, kueleza kwa kifupi tu hali ya ukuaji uchumi wa nchi yetu kwa kutumia takwimu mbalimbali.

 

Kwa ujumla, napenda kusema tu kuwa, ukuaji wa uchumi wetu unaendelea vizuri. Mathalan, katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, uchumi ulikua kwa kasi ya asilimia 6.8. Kasi hii imeiwezesha nchi yetu kuongoza katika eneo la Afrika Mashariki, lakini pia kuifanya kuwa miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi barani Afrika.  Aidha, mfumko wa bei umeendelea kuwa chini, ambapo mwezi Novemba 2017 umefikia asilimia 4.4. Na hii inamaanisha  kuwa ugumu wa maisha umepungua kinyume na baadhi ya watu wanavyosema kuwa “vyuma vimekaza”. Wengi ambao kwao vyuma vimekaza ni wale ambao walizoea fedha za bure, ikiwemo kupitia watumishi hewa, safari za nje, semina, n.k. Kwa wenye kujituma, vyuma haviwezi kukaza. Mathalan, kwa mkulima wa korosho ambaye bei imeongezeka kutoka wastani wa shilingi 2,000 kwa kilo hadi shilingi 4,000, unadhani kwake vyuma vitakaza? Lakini pia tujiulize, hivi kweli inawezekana kwa mtu wa kule kwetu Chato, ambako bei saruji imeshuka kutoka wastani wa shilingi 27,000 hadi shilingi 15,000 kwa mfuko iwe vyuma kwake vimekaza?

 

Mbali na kupungua kwa mfumko wa bei, akiba ya fedha za kigeni za nchi yetu imeongezeka. Hivi sasa imefika Dola za Marekani bilioni 5.82. Kiasi hiki cha fedha kinatuwezesha kununua nje bidhaa na huduma kwa miezi mitano. Kiwango kilichowekwa na Jumuia ya Afrika Mashariki ni angalau miezi minne. Hizi ni baadhi tu ya takwimu zinazoonesha kuwa uchumi wetu unaendelea vizuri. Nafahamu kuwa wapo watu wanaojaribu kupotosha ukweli huo; lakini nawaomba Watanzania muwapuuze watu hao na badala yake mziamini takwimu zinazotolewa na Ofisi yetu ya Takwimu, ambayo hivi punde Mwakilishi wa Benki ya Dunia, Mama Bella Bird, ameisifu kuwa ni mojawapo ya taasisi bora Barani Afrika.

 

Wananchi Wenzangu, Mabibi na Mabwana;

Ni dhahiri kuwa takwimu za ukuaji uchumi pekee kama haziendi sambamba na maendeleo na ustawi wa maisha ya watu hazina umuhimu wowote. Upo usemi wa Kiingereza usemao “You cannot feed the hungry on statistics (Huwezi kumlisha au kumshibisha mtu mwenye njaa kwa takwimu)”. Aidha, Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, aliwahi kusema kuwa “Maendeleo ya Uchumi ni lazima yafungamanishwe na Maendeleo ya Watu”. Kwa kutambua hilo, Serikali inafanya kila jitihada ili kuhakikisha kuwa maendeleo ya kiuchumi yaliyopatikana yanawiana na maendeleo na ustawi wa maisha ya watu. Hii ndio sababu, tumeweka mkazo mkubwa katika kuboresha huduma za jamii, ambazo zinawagusa wananchi wengi.

 

Mathalan, kama mnavyofahamu, hivi sasa tunatoa elimu bila malipo kuanzia shule ya msingi hadi sekondari. Mpaka kufikia mwezi Novemba 2017, Serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni 535 tangu utaratibu huu uanze mwezi Desemba 2015. Mkoa wa Dodoma pekee umepokea kiasi cha shilingi bilioni 16.6. Bila shaka, mtakubaliana nami kuwa, utaratibu huu umewezesha watoto wengi kutoka familia maskini kupata fursa ya elimu. Na hii inathibitishwa na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza na kidato cha kwanza. Na kama mnavyofahamu, njia rahisi ya kumsaidia mtu maskini, ni kumpa elimu.

 

Sambamba na elimu, tumeboresha huduma za afya nchini, ambapo tumeongeza bajeti ya dawa pamoja na kununua vifaa vya uchunguzi, vitanda, magodoro na mashuka; na halikadhalika tumeajiri watumishi wapya wa afya. Mathalan, nimeambiwa kuwa upatikanaji wa dawa muhimu kwenye Mkoa huu, umefikia asilimia 90 hivi sasa. Aidha, hapa Dodoma tumekamilisha jengo la wodi ya akina mama katika Hospitali ya Mkoa kwa gharama ya shilingi milioni 600, na tunatarajia kuanza ukarabati na ujenzi wa miundombinu mingine ya hospitali hiyo kwa gharama ya takriban shilingi bilioni 2.5. Vilevile, jumla ya vituo 5 vya afya, kikiwemo cha Makole na Bahi, tumevikarabati kuviwezesha kutoa huduma za dharura, ikiwemo upasuaji kwa akina mama wajawazito. Uboreshaji wa vituo hivyo umegharimu shilingi bilioni 2.5.

 

Sambamba na hayo, Hospitali ya Benjamin Mkapa nayo imeanza kutoa huduma; ambapo Serikali imeipatia vifaa vya kisasa kama MRI, CT-Scan pamoja na vifaa vya kupandikiza figo na kufanya upasuaji bila kuchana mwili. Vilevile, hivi sasa tupo kwenye mazungumzo na marafiki zetu wa Israel ili kuanzisha kitengo cha Huduma za Wagonjwa Mahututi cha Kisasa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa. Hatua hizi, bila shaka, zimeimarisha upatikanaji wa huduma ya afya hapa Dodoma.

 

Tunachukua pia hatua za kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji. Kwenye kila Mkoa hivi sasa kuna miradi ya maji inayotekelezwa. Hapa Dodoma, tumetekeleza miradi kadhaa ya maji, ukiwemo Mradi wa kupeleka maji Chuo Kikuu cha Dodoma. Lakini sambamba na miradi hiyo, tupo mbioni kuanza ujenzi wa mradi wa mkubwa wa maji wa Bwawa la Farkwa kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 420, zaidi ya shilingi bilioni 920, ambapo mpaka sasa usanifu na mchoro wake umekamilika. Bwawa hili litakapokamilika, linatarajiwa kuondoa kabisa tatizo la maji katika Wilaya za Bahi, Chemba, Chamwino na hapa Manispaa.

 

Hizi ni baadhi tu ya hatua tunazochukua kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi tuliyoyapata tunayatafsiri kwenye maisha ya watu. Lakini mbali na hatua hizi za kuboresha huduma za jamii, tumeelekeza nguvu katika kuimarisha miundombinu ya usafiri na umeme, ambayo nayo ni muhimu sana sio tu katika kukuza uchumi bali pia kuleta ustawi katika maisha ya wananchi. Tunajenga reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza; tunatekeleza miradi mikubwa ya umeme.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wananchi Wenzangu, Mabibi na Mabwana;

Jukumu langu leo ni kuweka Jiwe la Msingi la Jengo hili. Hivyo, nisingependa kuwachosha kwa hotuba ndefu. Hata hivyo, kabla sijahitimisha, ninayo masuala kama manne ambayo ningependa niyaseme.

 

Suala la kwanza, kama mtakavyokumbuka, mwanzoni mwa hotuba yangu nimeeleza kuhusu umuhimu wa takwimu. Lakini ili takwimu ziwe muhimu ni lazima ziwe sahihi. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuhimiza Ofisi ya Takwimu kuendelea kuandaa taarifa zenu kwa weledi mkubwa. Aidha, natoa wito kwa wananchi na Taasisi zote za Serikali kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu pindi wakihitaji taarifa mbalimbali. Sambamba na hayo, natoa onyo kwa wale watu wote wenye kutoa takwimu za uongo au upotoshaji. Naziagiza mamlaka husika kuchukua hatua dhidi ya watu wa namna hiyo. Sheria ya Takwimu kifungu Namba 37 kifungu kidogo cha 3 hadi cha 5 kinatamka wazi kwamba mtu au Taasisi akitoa takwimu za uongo au kusababisha wananchi kushindwa kutoa ushirikiano kwa ofisi ya Taifa ya Takwimu, adhabu yake ni kifungo cha miezi sita hadi miaka mitatu, ama kulipa faini kati ya shilingi milioni moja hadi shilingi milioni kumi; au adhabu zote kwa pamoja. Nimefurahi kusikia kuwa mchakato wa kuifanyia marekebisho sheria hiyo ili kuiongezea makali umeanza.  Haiwezekani taasisi za kitaifa na kimataifa zenye wajibu wa kutoa takwimu zitoa takwimu fulani, halafu ajitokeze mtu mwingine aseme kuwa ana takwimu nyingine zinazotofautiana  na hizo. Jambo hili halikubaliki.

 

Suala la pili, napenda pia kutumia fursa hii kurudia wito wangu nilioutoa hivi majuzi wakati nafungua tawi la CRDB  kwa Wizara ya Fedha pamoja na Benki Kuu kuhusu kuimarisha usimamizi wa Benki, matumizi ya Dola, pamoja na usajili wa makampuni ya Simu na Benki kwenye mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia ya Kielectroniki. Mheshimiwa Waziri wa Fedha, hakikisha  suala hili linatekelezwa kabla ya mwisho wa mwaka huu. Na pia Mheshimiwa Waziri fuatilia suala la umiliki wa Kampuni ya Simu ya Airtel, ambalo kwa taarifa zilizopo, ni mali ya Serikali.

 

Suala la tatu, mwezi Juni mwaka huu, wakati nikiwa pale Kijitonyama kuzindua Kituo cha Data na Mfumo wa Ukusanyaji Mapato kwa njia ya Kielektroniki niliagiza kuwa Taasisi zote za Serikali kutumia Kituo cha Data cha Taifa na kuachana na utaratibu wa kila taasisi kutengeneza Kituo chake. Mheshimiwa Waziri katika taarifa yake ameeleza kuwa Ujenzi wa Jengo hili utahusisha pia ujenzi wa kanzidata. Hivyo basi, natoa wito kwenu kutafakari suala hili vizuri. Kama hakuna sababu za msingi za kujenga kanzidata yenu wenyewe, ni vyema mtumie Kituo cha Data cha Taifa, ambacho kina viwango vya kimataifa na Serikali ilitumia fedha nyingi kuwekeza.

 

Suala la nne, ni kwa wana-Dodoma wote. Dodoma sasa inafunguka. Fursa nyingi za kiuchumi zinakuja, hususan kutokana na uamuzi wa Serikali kuhamishia Makao Makuu hapa Dodoma. Aidha, kuna miradi mingi na mikubwa imepangwa kutekelezwa hapa Dodoma, ikiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa, kutoka Dar es Salaam kupita hapa Dodoma kuelekea mikoa ya Mwanza na Kigoma.  Ujenzi wa kipanda cha Reli hii kutoka Dar Es Salaam mpaka hapa Dodoma (Makutupora) chenye urefu wa takriban kilometa 712 kimeanza kujengwa kwa gharama ya shilingi trilioni 7.062 ambazo zote zitatolewa na Serikali.  Sambamba na hayo nafahamu kuwa Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii imepanga kutekeleza miradi kadhaa ya viwanda hapa Dodoma, ikiwa ni pamoja na kufufua Kiwanda cha kusindika nafaka na kukamua mafuta cha National Milling Corporation (NMC), Kiwanda cha kutengeneza matofali na vigae, na Kiwanda cha Kusindika Juisi na Mvinyo wa Zabibu ambacho kitajengwa Chinangali, Chamwino. Hivyo basi, nawasihi sana wana-Dodoma kujipanga vizuri kutumia fursa hizo.

 

Mwisho kabisa, nawashukuru tena kwa kunikaribisha. Aidha, nawapongeza tena Ofisi ya Takwimu kwa kazi nzuri mnayoifanya. Nawashukuru pia tena washirika kwa misaada yenu mbalimbali mnayotupatia. Naomba muendelee na moyo huo.

 

Mabibi na Mabwana; baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kutekeleza jukumu lililonileta la kuweka Jiwe la Msingi la Jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu hapa Dodoma.

 

Mungu Ibariki Ofisi ya Taifa ya Takwimu!

Mungu Ibariki Dodoma!

Mungu Ibariki Tanzania!

“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”