Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA MWENYEKITI WA CCM KWENYE UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA TISA WA TAIFA WA CHAMA CHA MAPINDUZI DODOMA, TAREHE 18 DESEMBA, 2017

Monday 18th December 2017

Ndugu Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar

na Makamu Mwenyekiti wa CCM - Zanzibar;

 

Ndugu Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti

wa CCM- Tanzania Bara;

 

Ndugu Wenyeviti na Makamu Wenyeviti

         Wa CCM wa Taifa Wastaafu mliopo;

 

Ndugu Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM;

Ndugu Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais

wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Ndugu Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu

wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili

         wa Rais wa Zanzibar;

 

Waheshimiwa Mawaziri Wakuu Wastaafu mliopo;

 

Ndugu Wake za Viongozi Wastaafu mkiongozwa

na Mama Maria Nyerere na Fatuma Karume;

 

Ndugu Wajumbe wa Kamati Kuu;

Ndugu Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa;

Ndugu Viongozi Wastaafu mliopo;

Ndugu Wawakilishi wa Vyama Rafiki

na Shindani vya CCM mliopo;

 

Ndugu Viongozi na Wazee Wastaafu wa CCM mliopo;

 

Ndugu Wageni Wetu Wote Waalikwa: Viongozi wa

         Serikali na Dini mliopo;

 

Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu;

 

Ndugu Wana-CCM Wenzangu; Mabibi na Mabwana:

 

CCM OYEE! MAPINDUZI, DAIMA!

 

Awali ya yote, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, kwa kutujulia uhai na kutuwezesha kukutana hapa Dodoma leo. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuwakaribisha ndugu wajumbe pamoja na wageni wote waalikwa katika Mkutano huu Mkuu wa Tisa wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) unaofanyika hapa Dodoma; Makao Makuu ya Chama chetu pamoja na Serikali. Karibuni sana.

 

Natambua kuwa baadhi yenu mmelazimika kusafiri umbali mrefu kuja kuhudhuria Mkutano huu. Hivyo basi, napenda nitumie fursa hii kuwapa pole ya safari. Bila shaka, mmesafiri umbali mrefu kuja kuhudhuria Mkutano kwa kuwa mnafahamu umuhimu wake, lakini pia hii ni ishara ya mapenzi ya kweli mliyonayo kwa Chama hiki. Na ningependa kutumia fursa hii kuwapongeza wajumbe wote wa Mkutano huu kwa kuchaguliwa kwenu. Hongereni sana.

 

Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu na Wana-CCM Wenzangu;

Mkutano huu unafanyika zikiwa zimepita takriban wiki 3 tangu nchi yetu ifanye Uchaguzi Mdogo wa Madiwani katika kata 43. Na kama mtakavyokumbuka, katika uchaguzi huo, Chama chetu kilishinda viti vya udiwani 42. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii, hapa mwanzoni kabisa, kutoa pongezi nyingi kwa wanachama, wapenzi na mashabiki wa CCM kwa ushindi mkubwa tuliopata.

 

Kwa tathmini yangu binafsi, ushindi huu tuliopata umetokana na mambo makubwa manne. Kwanza kabisa, ni matokeo ya uungwaji mkono mkubwa na kukubalika kwa Chama chetu miongoni mwa Watanzania. Pili, unatokana na uimara na ukomavu wa Chama chenyewe. Sio siri kuwa Chama hiki ni kikongwe. Mwaka huu kimetimiza miaka 40 tangu kianzishwe. Hakuna Chama kikongwe kama hiki hapa nchini. Kimeongoza Dola tangu kimeanzishwa mwaka 1977 na tangu kurejeshwa kwa Mfumo wa Vyama vingi nchini 1992. Kina mashina, matawi, pamoja na wanachama, wapenzi na washabiki nchi nzima. Na katika kudhihirisha kuwa Chama hiki ni kikubwa na kikongwe, ni katika kudhihirisha hili, ninyi wenyewe mnajionea hapa viongozi wakuu wastaafu wa Chama na Serikali wapo hapa. Tunaye hapa Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa, Mzee Kikwete, Mzee Karume, Mzee Malecela, Mzee Msekwa, Mzee Msuya, Mzee Dkt. Salim na Mzee Pinda. Hii inadhihirisha kuwa Chama hiki ni kikongwe na kina hazina kubwa.

 

Sababu ya tatu, iliyotufanya tushinde Uchaguzi huu ni kwamba tunatekeleza kwa vitendo mambo tuliyoahidi wakati wa Kampeni kupitia Ilani yetu ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 – 2020. Na nne, tumeshinda kwa vile hivi sasa wana-CCM tuna umoja. Na tunashirikiana. Hivyo basi, napenda kurudia tena kuwapongeza wana-CCM kote nchini kwa ushindi tuliopata.

 

Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu;

Mabibi na Mabwana;

Kama nilivyotangulia kusema kuwa huu ni Mkutano Mkuu wa Tisa wa Taifa wa Chama chetu. Mkutano Mkuu wa CCM wa Taifa ndiyo kikao kikubwa zaidi kuliko vyote vya Chama; na kina madaraka ya mwisho kwa mujibu wa Katiba. Kwa kuzingatia hilo, na kwa kuwa Chama chetu ni Chama Tawala, ni dhahiri kuwa Mkutano huu ni muhimu sana. Maamuzi yatakayofanywa na Mkutano huu yatakuwa na athari (impact) sio tu kwenye Chama chetu bali Taifa letu kwa ujumla.

 

Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu na Wana-CCM Wenzangu;

Kama mnavyofahamu, Mkutano huu una ajenda kubwa tatu. Kwanza, utapokea na kujadili Taarifa ya Kazi za Chama itakayotolewa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na kutoa maelekezo ya mipango ya utekelezaji wa Siasa ya CCM kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Aidha, Mkutano huu utapokea na kujadili Taarifa za Serikali zote mbili (yaani Muungano na Zanzibar) kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi pamoja na uongozi wa Serikali na Nchi kwa ujumla. Vilevile, Mkutano huu utafanya uchaguzi wa Mwenyekiti wa CCM Taifa; Makamu wake wawili, mmoja wa Zanzibar na mwingine Tanzania Bara; pamoja na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa.

 

Na kwa mujibu wa ratiba iliyopo, Taarifa ya Kazi za Chama itawasilishwa na Katibu Mkuu wa Chama, Ndugu Abdulrahaman Kinana. Aidha, Taarifa za Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na Uendeshaji  wa Serikali zitawasilishwa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, kwa upande wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idd kwa upande wa Serikali ya Zanzibar. Kwa sababu hiyo, hotuba yangu haitagusia sana masuala hayo. Nitajikita zaidi katika suala la uchaguzi wa Chama chetu na nitaeleza baadhi ya mambo ambayo natamani sana kuona Chama hiki kikifanya katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

 

Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu;

Mabibi na Mabwana;

Kama mnavyofahamu, tangu mwezi Aprili mwaka huu Chama chetu pamoja na Jumuiya zake zote tatu (Umoja wa Wazazi, Umoja wa Wanawake na Umoja wa Vijana) kimekuwa kwenye zoezi muhimu la uchaguzi. Tulianza uchaguzi kwenye ngazi ya mashina, kisha tukaelekea kwenye ngazi ya tawi, kata, wilaya na mkoa; na kwenye Jumuiya, uchaguzi tayari umekamilika hadi katika ngazi ya Taifa. Nimefarijika sana kuona kuwa katika zoezi hili la uchaguzi wagombea wengi walijitokeza, tena wengi sana. Hii inathibitisha  ukukomavu wa demokrasia ndani ya Chama chetu.

 

Baada ya kukamilisha uchaguzi wa Chama kuanzia ngazi ya shina hadi mkoa; na kwa upande wa Jumuiya hadi ngazi ya Taifa; sasa tunakwenda kuhitimisha zoezi la uchaguzi wa Chama katika ngazi ya Taifa. Kama nilivyotangulia kusema, Mkutano huu  utamchagua Mwenyekiti wa CCM Taifa; Makamu Wenyeviti wawili, pamoja na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa. Na nawaomba ndugu wajumbe mchague kwa umakini. Usimchague mtu kwa sababu ya urafiki, udini, ukabila, ukanda, au kwa kutegemea kupata maslahi fulani fulani binafsi. Zaidi ya hapo, kamwe! Narudia tena, kamwe, msimchague mtoa rushwa. Ahadi Namba 3 ya mwana- CCM inasema, nanukuu, “rushwa ni adui wa haki sitapokea wala kutoa rushwa”, mwisho wa kunukuu.

 

Ndugu zangu wana-CCM, Chama chetu kimedhamiria kwa dhati kabisa kupambana na rushwa. Hivi majuzi mmesikia wenyewe tulitengua matokeo ya kura za maoni ya kupata mgombea wa Ubunge kule Singida baada ya kupatikana kwa tuhuma za rushwa. Na niwahakikishie kuwa, hata kwenye uchaguzi huu, endapo itathibitika kuna wagombea wameshinda kwa kutoa rushwa, hatutasita kutengua. Rushwa ni kansa. Rushwa ni adui wa haki. Ninyi wenyewe ni mashahidi kuwa kuna wakati ilikuwa vigumu kwa mtu kwenye Chama chetu kupata uongozi bila kutumia rushwa. Lakini, nimeshukuru sana Mwenyekiti Mstaafu Mzee Kikwete, kama isingekuwa uimara wake mimi nisingepata nafasi hivyo. Ahsante sana Mzee Kikwete. Hivyo basi, nawasihi sana wana-CCM wenzangu, msimchague mtoa rushwa. Badala yake, chagueni watu waadilifu, wachapakazi, wasio endekeza makundi na wenye mapenzi ya dhati kwa Chama chetu.

 

Ndugu Wana-CCM wenzangu;

Nafahamu kuwa jukumu langu leo ni kufungua Mkutano wetu. Lakini kabla sijafanya hivyo, ninayo masuala mawili ambayo ningependa kueleza. Suala la kwanza, linahusu zoezi la uchaguzi tulilolifanya ndani ya Chama chetu mwaka huu. Kwenye uchaguzi wowote ule kuna kushinda au kushindwa. Hivyo basi, wakati tunaelekea kuhitimisha zoezi la uchaguzi kwenye Chama chetu, ninalo ombi moja kwenu. Uchaguzi huu tulioufanya kwenye Chama chetu kuanzia mwezi Aprili 2017 hadi mwezi huu wa Desemba 2017 usiwe chanzo cha mifarakano au kuvurugika kwa umoja na mshikamano ulioanza kujengeka ndani ya Chama chetu. Bali utuimarishe na kutufanya kuwa wamoja zaidi.

 

Tuwapongeze wale walioshinda; na napenda kutumia fursa hii kuwapongeza wale wote waliochaguliwa kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi kwenye Chama pamoja na Jumuiya zake. Hongereni sana. Ushindi mlio upata ni uthibitisho wa imani kubwa waliyonayo wana-CCM juu yenu.

 

Kwa wale ambao kura hazikutosha, msikate tamaa au kuwa wanyonge. Kama nilivyosema, kwenye uchaguzi wowote kuna kushinda na kushindwa. Safari hii kura hazikutosha; lakini huenda kwenye uchaguzi ujao, nanyi mkaibuka washindi. Hivyo, jambo la msingi kwenu hivi sasa ni kuchapakazi kwa bidii na kuwaunga mkono viongozi waliochaguliwa. Na niwaombe sana ndugu wajumbe na wana-CCM kwa ujumla, sasa tuyavunje makundi yote tuliyoanzisha wakati wa Uchaguzi. Uchaguzi umekwisha. Wakati wa kampeni umekwisha. Sasa, tunatakiwa tuchape kazi ili kukiimarisha zaidi Chama chetu. Napenda kutumia fursa hii kueleza kuwa, kamwe; narudia tena, kamwe, Chama hakitamvumilia mtu yeyote mwenye kuendeleza makundi. Awe ni kiongozi aliyechaguliwa, awe mgombea aliyeshindwa ama mwanachama wa kawaida.

 

Ndugu Viongozi;

Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu;

Mabibi na Mabwana;

         Suala la pili ambalo ningependa kueleza linahusu maono niliyonayo ya namna ambayo natamani Chama chetu kifanye kazi katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Na hili, nitalieleza kwa kirefu kidogo. Hivyo, nawaomba ndugu wajumbe mnivumilie kiasi.

 

Ndugu wajumbe na wana-CCM wenzangu, Mkutano wetu huu Mkuu wa Tisa wa Taifa unafanyika katika mazingira ya kipekee sana. Ni ya kipekee kwa sababu, kwanza, unafanyika katika kipindi ambacho Chama chetu kimetimiza miaka 40. Pili, unafanyika wakati nchi yetu imetimiza miaka 25 tangu kurejeshwa kwa Mfumo wa Vyama vingi. Na tatu, ambalo nadhani ni kubwa na muhimu zaidi ni kwamba, Mkutano huu unafanyika katika mwaka ambao Chama kimeanza kutekeleza Awamu ya Nne ya Mradi wa kuimarisha na kujenga uhai wa Chama.

 

Kama mnavyofahamu, ukiachilia mbali suala la ukongwe na kukomaa kidemokrasia, kama ambavyo nimeeleza awali; sifa nyingine muhimu na kubwa zaidi ya CCM, ni utaratibu wake wa kujitathmini na kujikosoa mara kwa mara, na kisha kufanya mageuzi yanayokwenda sambamba na wakati na hali halisi. Ni kutokana na ukweli huo, tangu imeanzishwa mwaka 1977, CCM imetekeleza awamu tatu za miradi ya kujenga na kuimarisha Chama. Mradi wa kwanza ulitekelezwa kati ya mwaka 1985 hadi 1987, ambapo Mwenyekiti wa wakati huo, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alizunguka nchi nzima kwa lengo la kukiimarisha Chama, hususan katika ngazi za chini.

 

Na wakati akihitimisha Awamu hiyo ya Kwanza, Baba wa Taifa alitangaza kuzindua Awamu ya Pili ya Mradi wa kuimarisha Chama, ambao pamoja na masuala mengine, ulihimiza Chama katika ngazi zote na kujenga itikadi; kuwa na mpango kazi unaotekelezwa; na kuimarisha mfumo wa nidhamu na demokrasia ndani ya Chama. Awamu ya Tatu ya Mradi wa kujenga na kuimarisha Chama ilianza kufuatia hotuba aliyotoa mtangulizi wangu, Mwenyekiti Mstaafu, Mzee Kikwete, wakati wa kupokea Uenyekiti wa Chama hapa hapa Dodoma tarehe 25 Juni, 2006. Msisitizo katika Awamu hii ilikuwa kujenga uongozi imara kwa kuhakikisha kuwa nafasi zote za uongozi ndani ya Chama zinakamilika; na viongozi wanakuwa mfano wa kuigwa kwa kuonesha njia.

 

Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu;

Mabibi na Mabwana;

Wakati Chama kikiendelea kutekeleza Awamu ya Tatu ya uimarishaji Chama, kutokana na mabadiliko na changamoto mbalimbali, haja ya kukifanyia Chama chetu mageuzi makubwa ya kimfumo, muundo na utendaji ilijitokeza. Hivyo basi, kufuatia majadiliano ya kina na ya muda mrefu yaliyofanyika; na hususan baada ya Chama kutazama itikadi yake, mwenendo wake, matendo yake, dhamira yake, malengo yake pamoja na kuangalia nidhamu ya viongozi wake. Na baada ya Chama kusikiliza sauti ya wanachama na wananchi kwa ujumla. Kama mnavyofahamu, Chama hiki ni cha wananchi wote. Hatimaye, mwezi Machi mwaka huu (2017), Chama chetu kilikubali kufanya mageuzi kupitia Mkutano Mkuu.

 

Mageuzi yaliyofanyika yamejikita katika mawanda makubwa matatu: mfumo, muundo na utendaji. Msingi mkuu wa mageuzi haya ni kukirejesha Chama kwa wanachama ili kukifanya kuwa kimbilio la wananchi. Na malengo mahususi ya mageuzi tuliyofanya ni kuongeza tija na ufanisi katika utendaji wa Chama, uwajibikaji miongoni mwa viongozi; pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa Chama.

 

Mambo muhimu yaliyozingatiwa katika mageuzi haya ni kupunguza idadi ya vikao na wajumbe wa vikao ili kuondoa urasimu, kuongeza tija ya vikao husika na halikadhalika kupunguza gharama. Kwa kuwakumbusha tu, tumepunguza idadi ya wajumbe wa Mkutano huu Mkuu kutoka 2,422 hadi 1,706. Tumepunguza wajumbe wa Halmashauri Kuu kutoka 388 hadi 163; na Kamati Kuu kutoka 34 hadi 26. Tumefanya hivyo, ili viongozi watumie muda mwingi kushughulikia matatizo ya wanachama na wananchi kwa ujumla, badala ya kutumia muda mwingi kukaa ofisini na kushiriki kwenye vikao.

 

Tunaamini kuwa, endapo Chama kitaweza kushughulikia vizuri matatizo ya wananchi, kitaweza kuwavuta watu wengi zaidi kujiunga nacho. Katika mageuzi tuliyofanya pia, tumefuta utaratibu wa mtu mmoja kuwa na vyeo zaidi ya kimoja. Tumefuta vyeo ambavyo havikuwepo Kikatiba (kamanda, mlezi, n.k).  Mageuzi tuliyoyafanya pia yamehimiza uadilifu na uwajibikaji miongoni mwa viongozi na wanachama, pamoja na kusisitiza Chama chetu kujitegemea kiuchumi. Ili kuhakikisha kuwa mageuzi tuliyofanya yanapata msingi wa kisheria, tumelazimika kuifanyia marekebisho Katiba ya Chama pamoja na Jumuiya zake.

 

Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu;

Mabibi na Mabwana;

Sio siri kuwa mageuzi tuliyoyafanya mwaka huu ni makubwa sana. Na ni lazima tuyasimamie. Na watu wa kwanza ambao watawajibika kuyasimamia ni viongozi ambao wamechaguliwa kushika nafasi mbalimbali hivi karibuni. Napenda kutumia fursa hii kuwasisitiza viongozi wote wa Chama waliochaguliwa kwenda kusimamia mageuzi tuliyoyafanya. Na niseme tu kuwa binafsi nitafurahi sana endapo viongozi waliochaguliwa wataweza kusimamia masuala makubwa manne, ambayo Mkutano huu ukiridhia unaweza kuyafanya kuwa ndiyo malengo makuu ya Mradi wa Awamu ya Nne ya kujenga na kuimarisha Chama.

 

Suala la kwanza kabisa, ni kukiimarisha Chama chetu kwa kuongeza idadi ya wanachama. Kama mnavyofahamu, lengo kuu la Chama chochote cha siasa ni kushinda uchaguzi na kushika Dola. Na katika nchi ya kidemokrasia kama yetu, mtaji pekee wa kufanikisha hili ni kwa Chama kuhakikisha kinakuwa na idadi kubwa ya wanachama, wapenzi na washabiki. Hivyo basi, viongozi mliochaguliwa, jukumu lenu la kwanza, ni kuhakikisha kuwa mnaongeza idadi ya wanachama, wapenzi na washabiki wa Chama chetu katika maeneo yenu. Tunataka ikifika wakati wa uchaguzi, washindani wetu, wasiambulie chochote.

 

Jambo la pili, ambalo naomba viongozi waliochaguliwa kulisimamia ipasavyo, ni katika kuhakikisha kuwa Chama chetu kinajitegemea kiuchumi. Chama chetu ni kikubwa na kikongwe. Hivyo, ni aibu kwa Chama hiki kuwa tegemezi. Kwa sababu hiyo, natoa wito kwa viongozi wote waliochaguliwa kuhakikisha Chama chetu kinajitegemea kiuchumi. Hivyo, tuwahimize wanachama waliopo kwenye maeneo yenu kulipa ada zao za mwaka. Na njia nzuri ya kuwashawishi wanachama kulipa ada ni kuhakikisha kunakuwa na uwazi katika ukusanyaji na matumizi wa mapato. Watu wanataka waone fedha zao wanazotoa zimeenda na kufanya nini. Sambamba na kuweka uwazi kwenye mapato na matumizi, jengeni utamaduni wa kuwatembelea wanachama. Msikae ofisini kuwasubiri wanachama walete michango. Na niwaombe wana-CCM wenzangu tujitahidi kulipa ada zetu za mwaka. Zama za kusubiria matajiri watulipie ada zetu wakati wa kampeni, zimepitwa na wakati. Ni lazima sisi wenyewe tujitoe. Chama kitajengwa na wenye chama, siyo matajiri wachache.

 

Njia nyingine ya kuhakikisha Chama kinajitegemea kiuchumi ni kusimamia vizuri rasilimali za Chama. Kama ambavyo nimesema mara kadhaa, Chama hiki kina rasilimali nyingi: viwanja vya michezo, majengo, mashamba, n.k.; lakini kwa bahati mbaya, kwa muda mrefu, rasilimali hizi hazijakinufaisha Chama chetu. Hii imetufanya, tutegemee zaidi ruzuku na michango ya wahisani. Mathalan, mapato ya Chama kwa mwaka wa fedha 2014/2015 ilikuwa takriban shilingi bilioni 29.35. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 21.95 ni ruzuku na michango ya hiari. Mwaka 2015/2016, mwaka wa uchaguzi, mapato yalikuwa shilingi bilioni 73.19, ambapo ruzuku na michango ya hiari ni shilingi bilioni 56.82; na katika mwaka 2016/2017, mapato yalikuwa shilingi bilioni 40.01, ambapo ruzuku na michango ya hiari ni shilingi bilioni 27.56. Hii inadhihirisha kuwa uwezo wetu wa kujitegemea ni mdogo. Ni lazima turekebisha hali hii, na kwa bahati nzuri tumeanza kuchukua hatua, ikiwemo kufanya uhakiki wa mali zetu zote,  halikadhalika tupo mbioni kuanzisha mfumo wa kielektroniki utakaokiwezesha Chama kutambua na kusimamia rasilimali na mali zake zote, mapato na kusimamia uendeshaji kwa ujumla. Hivyo basi, niwaombe viongozi wapya mkaendeleze jitihada zilizoanzishwa.

 

Sambamba na hilo, viongozi wapya hamna budi kubuni miradi mipya. Na katika hili, niseme tu kwamba, itakuwa aibu kwa Chama chetu, ambacho Serikali yake inahubiri ujenzi wa uchumi wa viwanda, tutashindwa hadi ikifika mwaka 2020 kuanzisha angalau kiwanda kimoja.

 

Tatu, nawasihi sana viongozi wapya, kila mtu mahali pake alipo, ahakikishe kuwa Chama chetu kinakuwa kiungo kati ya Serikali na wananchi. Chama, hususan Chama tawala kama chetu, kinao wajibu wa msingi wa kuwaeleza na kuwafafanulia wananchi umuhimu wa utekelezaji mipango na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali. Zaidi ya hapo, kinao wajibu wa kuchukua maoni, mapendekezo na kero mbalimbali za wananchi na kuziwasilisha Serikalini. Niwe mkweli, hivi sasa, Chama chetu hakitekelezi vizuri jukumu hili. Tumekuwa hodari sana wa kufanya kampeni na kuhakikisha Chama kinashinda uchaguzi. Lakini, baada ya hapo, huwa tunajiweka pembeni, ama kwa kuvaa sura ya Userikali au kwa kuwaogopa watendaji wa Serikali. Nilisema kwenye Mkutano Mkuu uliopita, viongozi wa Chama hawapaswi kuwaogopa watendaji wa Serikali, hususan katika kutetea maslahi ya wananchi wanyonge.

 

Katika kusisitiza umuhimu wa Chama chetu kuwa kiungo kati ya Serikali na wananchi, napenda ninukuu maneno yafuatayo, ambayo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyatamka tarehe 7 Juni, 1968 alipohutubia Mkutano Mkuu wa Chama cha Uganda People’s Congress, na nitanukuu kwa lugha yetu adhimu ya Kiswahili:“Kazi ya Chama kilicho imara ni kuwa daraja linalowaunganisha wananchi na Serikali yao. Ni wajibu wa Chama kuwasaidia wananchi kuelewa Serikali yao inafanya nini na kwanini; na kuwashawishi wananchi kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali yao, ikiwemo kuondoa umaskini wao....Zaidi ya hapo, Chama kina jukumu au wajibu wa kuwasemea wananchi (The Party must speak for the people)”, mwisho wa kunukuu.

 

Hivyo basi, nawasihi sana viongozi wapya, nendeni makatekeleze jukumu hili ipasavyo. Pongezeni pale inapobidi kupongeza, na kosoeni inapobidi. Na ili muweze kutekeleza jukumu hili vizuri, hakikisheni kuwa mnakuwa karibu na wananchi, lakini pia mnaifahamu vizuri mipango ya Serikali na mikakati ya kutekeleza mipango hiyo, ikiwemo bajeti zinazotengwa. Nitashangaa na kwa kweli nitasikitika, kama nitaona wananchi wanadai kufahamishwa mapato na matumizi ya Serikali ya Kijiji, huku Mwenyekiti wa CCM wa Shina au Tawi yupo; nitashangaa wananchi walalamike kuhusu ubadhirifu katika ujenzi wa kituo cha afya au shule wakati Mwenyekiti wa CCM na Kamati ya Siasa ya Kata wapo; na vilevile nitashangaa wananchi kushindwa kuelewa umuhimu wa kununua ndege, kujenga reli ya standard gauge na mradi wa umeme wa Stiglier’s Gorge wakati kuna Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Mkoa na Wajumbe wa Halmashauri Kuu na Mbunge wa CCM. Nitashangaa sana. Na niwaombe viongozi wa Serikali kutoa ushirikiano na ufafanuzi kwa viongozi wa Chama. Lakini ningependa pia kusema kuwa wana-CCM mkitaka kukosoa jambo linalofanywa na Serikali, mkumbuke kuwa ninyi ni Chama Tawala. Mnazo njia nyingi za kufikisha mapungufu mnayoyaona kwenye Serikali. Kuna usemi ambao Umoja wa Wazazi hupenda kuutumia, usemao “Uchungu wa Mwana, Aujuaye Mzazi”.  CCM Oyeee! Mapinduzi, Daima mbele!

 

Jambo la nne, na la mwisho lakini sio kwa umuhimu, ambalo ningependa viongozi wapya mlipe mkazo unaostahili, ni uadilifu. Na uadilifu unapaswa kuanza na ninyi. Kiongozi anapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa wanachama na wananchi kwa ujumla. Haifai, na kwa kweli, kamwe Chama hakitamvumilia kiongozi au mwanachama wa CCM mwenye kutuhumiwa au kujihusisha na vitendo vya rushwa, utapeli, wizi, ubadhirifu, ujambazi, ulevi uliopindukia, kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, n.k. Upo usemi wa enzi usemao “Mke wa Mfalme hapaswi hata kuhisiwa kuwa anachepuka”. Hivyo basi, kama kuna viongozi wa namna hiyo wamechaguliwa, ni vyema wakajirekebisha.

 

Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu;

Mabibi na Mabwana;

 

         Kama nilivyotangulia kusema, taarifa ya Utekelezaji wa Ilani na uendeshaji wa Serikali zitawasilishwa na Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.  Hata hivyo, napenda nitumie fursa hii kueleza mambo machache kuhusiana na masuala hayo. Kwanza kabisa, kama mnavyofahamu, jukumu kubwa la Serikali zetu mbili ni kuhakikisha amani, umoja na Muungano wa nchi yetu unadumishwa.  Hii pia ni moja ya ahadi zilizopo kwenye Ilani yetu ya Uchaguzi.  Bila shaka,  mtakubaliana nami kuwa Serikali zetu mbili zimeweza kutekeleza jukumu na ahadi hii kikamilifu. Nchi yetu ipo salama na ina utulivu.  Muungano wetu upo imara.  Na watanzania tumeendelea kuwa wamoja.  Watu wachache waliojaribu kutishia amani, Muungano na umoja wetu tumewadhibiti kikamilifu. 

 

         Suala la pili ambalo ningependa kuzungumzia ni kuhusu utekelezaji wa ahadi kubwa ya uchaguzi ya kujenga nchi ya uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025.  Ahadi hii nayo tunaitekeleza vizuri. Uchumi wetu unaendelea kuimarika, ambapo nchi yetu ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika ambao uchumi wake unakua kwa kasi.  Aidha, mfumuko wa bei unaendelea kushuka, ambapo mwaka huu mwezi Novemba ulishuka  kumefikia asilimia 4.4.   Vilevile, akiba ya fedha za kigeni imefikia Dola za Marekani milioni 5,820.4 mwezi Septemba 2017.  Kiasi hiki kinaiwezesha nchi yetu kulipia gharama ya kununua bidhaa kwa miezi mitano.  Hii ina maana kwamba leo hii Watanzania tunaweza kukaa bila kufanya kazi yoyote kwa miezi mitano na tukaendelea kupata huduma kama kawaida.  Lakini hii haimanisha kwamba watu waache kufanya kazi.  Ni lazima tuendelee kufanya kazi.  Kama maandiko matakatifu yanavyosema, asiye fanyakazi na asile.  Nanyi mnafahamu kuwa mtu asiye kula maana yake atakufa.

 

         Kuhusu ujenzi wa Viwanda, kwa kipindi cha miaka 2 iliyopita takriban Viwanda vipya 3,306 vimejengwa, na hizi ni takwimu za mwezi Juni 2017.  Lakini jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba viwanda vingine vinajengwa na hata  vile vya zamani vimeanza kufufuliwa.  Mathalan, Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii (NSSF, ZSSF, PSPF, GEPF, Bima ya Taifa ya Afya, LAPF na WCF) hivi sasa inatekeleza miradi takriban 15 ya viwanda, ambavyo nimeambiwa kuwa vitazalisha takriban ajira 350,000. Baadhi ya miradi ni ulimaji wa mashamba ya Miwa na ujenzi wa Viwanda vya Sukari vya Mkulazi na Mbigiri mkoani Morogoro, ambako pia kutakuwa na uzalishaji wa umeme utakaoingizwa kwenye Gridi ya Taifa; Ufufuaji wa Vinu vya Kusindika Nafaka na Ukamuaji Mafuta vya Shirika la Usagishaji la Taifa (National Milling Corporation – NMC) vilivyopo hapa Dodoma, Iringa na Mwanza; Ufufuaji wa Kiwanda cha Bidhaa za Ngozi pale Karanga, Moshi Mjini; Kiwanda cha Katani na Agave Syrup itokanayo na mabaki ya mkonge Mkoani Tanga; Kiwanda cha Madawa TPI Arusha; Kiwanda cha Kutengeneza Matofali ya Kuchoma na Vigae hapa Dodoma; Kiwanda cha Kusindika Tangawizi Kilimanjaro; Kiwanda cha Nyama cha Nguru Ranch Morogoro; Kiwanda cha Mvinyo wa Zabibu hapa Dodoma; Kiwanda cha bidhaa za hospitali (pamba na maji tiba) Simiyu, n.k.  Naipongeza Mifuko hii kwa kuitikia wito wa Serikali wa kujenga viwanda.  Na hii ndio sababu nahimiza Chama chetu nacho kushiriki katika utekelezaji wa ahadi hii.

 

Ndugu Viongozi;                          

Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu;

Wageni wetu Waalikwa;

Mabibi na Mabwana;

Nimezungumza mengi. Hivyo basi, napenda nihitimishe hotuba yangu kwa kuwashukuru wajumbe wa Mkutano huu kwa kuhudhuria kwa wingi. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru, Makamu wangu wawili, Mheshimiwa Dkt. Shein na Mzee Mangula kwa ushirikiano mkubwa walionipa tangu nilipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama chetu mwezi Julai mwaka jana. Nimejifunza na naendelea kujifunza mambo mengi kupitia kwao. Lakini, kwa namna ya pekee, namshukuru Mzee Kinana pamoja na Sekretarieti ya Chama kwa ujumla kwa kunisadia katika kutenda kazi za Chama na kufanya mageuzi mbalimbali. Nakushukuru sana Mzee Kinana. Na ni matarajio yangu kuwa Mzee huyu ataendelea kunisaidia katika kazi.

 

Napenda pia kutumia fursa hii, kuwashukuru wageni wetu waalikwa, Wawakilishi pamoja na Mabalozi mnaowakilisha Vyama Rafiki vya CCM kutoka nchi mbalimbali. Tunawashukuru sana kwa kushiriki nasi katika Mkutano huu. Napenda pia kuwashukuru wawakilishi wa vyama shindani mliohudhuria Mkutano huu. Mmeonesha ukomavu mkubwa wa kisiasa. Licha ya tofauti zetu za kiitikadi, lengo letu sisi sote ni kuijenga nchi yetu. Hii ndio sababu nimefarijika sana kwa kuja kuhudhuria Mkutano huu. Ahsanteni sana. Maendeleo hayana Chama japo naamini kuwa maendeleo ya kweli yataletwa na CCM.

 

Nitumie fursa hii pia kuwashukuru viongozi wetu wastaafu, wakiwemo Wenyeviti na Makamu Wenyeviti  Wastaafu, Makatibu Wakuu Wastaafu, pamoja na na wazee wetu wengine, wakiwemo mama zetu wapendwa, Mama Maria Nyerere na Mama Fatuma Karume kwa kuja kushiriki nasi kwenye Mkutano huu. Tunawashukuruni sana.

 

Mwisho lakini sio kwa umuhimu, napenda kuwashukuru viongozi na wanachama wapya  ambao wamejiunga na Chama chetu hivi karibuni. Na napenda kuwaarifu kuwa wapo wengi wanaotamani sana kujiunga na Chama chetu.

 

Baada ya kusema hayo, sasa natamka rasmi kuwa Mkutano Mkuu wa Tisa wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi umefunguliwa rasmi hapa Dodoma. Nawatakia wajumbe wenzangu Mkutano mwema na maamuzi ya busara.

 

Kidumu Chama Cha Mapinduzi!

Mapinduzi, Daima!

Mungu Wabariki Wajumbe wa Mkutano huu!

Mungu Ibariki CCM!

Mungu Ibariki Tanzania!

 

“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”