Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE UFUNGUZI WA TAWI JIPYA LA BENKI YA CRDB DODOMA, TAREHE 13 DESEMBA, 2017

Wednesday 13th December 2017

Mheshimiwa Job Ndugai, Spika wa Bunge

la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango;

 

Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;

 

Mheshimiwa Tulia Ackson, Naibu Spika wa

         Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa John Malecela, Waziri Mkuu

Mstaafu wa Tanzania;

 

Ndugu Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania;

 

Ndugu Ally Hussein Laay, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi

wa Benki ya CRDB;

 

Dkt. Charles Kimei, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB;

 

Waheshimiwa Viongozi mbalimbali mliopo hapa;

 

Waheshimiwa Wazee wa Mkoa wa Dodoma;

 

Wageni Waalikwa wote, Mabibi na Mabwana:

 

         Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wetu kwa kutupa afya njema na kutuwezesha kukutana hapa leo. Napenda pia, kwa namna ya pekee kabisa, kuushukuru uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Benki ya CRDB kwa kuniliaka kushiriki kwenye tukio hili la kuzindua Tawi la Benki yenu hapa Dodoma.

 

Napenda kukiri kuwa nimefurahi sana kushiriki kwenye hafla hii. Nimefurahi kwa sababu kwanza mimi ni mteja wa Benki ya CRDB kwa muda mrefu; tangu nikiwa Mwanafunzi wa Chuo Kikuu. Zaidi ya hapo, hapa Dodoma ndio Makao Makuu ya nchi yetu. Ni hivi karibuni tu tumefanya maamuzi makubwa ya kuhakikisha Serikali yote inahamia Dodoma ifikapo mwaka 2020. Kama mnavyofahamu, Waziri Mkuu pamoja na Viongozi na Watendaji wa Wizara tayari wamehamia. Aidha, Makamu wa Rais naye anatarajiwa kuhamia mwezi huu; na mimi nitahamia mwakani.

 

Ni dhahiri kuwa, kutokana na uamuzi huu wa kuhamia Dodoma, idadi ya watu katika Mji huu hapa itaongezeka sana. Na huduma za taasisi kama za benki zitahitajika zaidi. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuushukuru na kuupongeza uongozi wa Benki hii kwa uamuzi wenu wa kufungua Tawi hili hapa Dodoma. Kwa kufungua Tawi hili, mmeunga mkono uamuzi wa Serikali wa kuhamia Dodoma. Ahsanteni sana.

 

 

 

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Sekta ya benki ni muhimu sana katika maendeleo ya nchi. Ni muhimu kwanza kabisa katika ukuzaji uchumi. Sekta ya benki inatoa mchango mkubwa katika pato la taifa. Mathalan, mwaka 2014, sekta hii ilichangia asilimia 3.4 ya pato la taifa; mwaka 2015 na mwaka jana 2016 ilichangia asilimia  3.6. Aidha, benki zinachangia ukuaji uchumi kupitia ulipaji wa kodi kwa Serikali. Hivi punde mmetoka kumsikia Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dkt. Kimei, akisema kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita Benki yake imelipa kodi zaidi ya shilingi bilioni 800 na hivyo kuiwezesha kushinda tuzo ya kuwa mlipaji kodi bora mara kadhaa. Hongereni sana CRDB.

 

Lakini mbali na kukuza uchumi, sekta ya benki ni muhimu katika kupiga vita umaskini. Benki zinashiriki katika kupiga vita umaskini, kupitia kwanza mikopo inayoitoa kwa wananchi, hususan wafanyabiashara na wajasiliamali wadogo kama vile machinga na mama lishe. Pili, zinachangia kupiga vita umaskini kwa namna inavyoshiriki katika kukuza sekta nyingine. Kama mnavyofahamu, sekta ya benki ni muhimu sekta nyingine zote. Iwe viwanda, kilimo, uvuvi, ufugaji, ujenzi, biashara, usafirishaji; na hata sekta za huduma kama afya, elimu, maji, n.k. Kwa mfano,  benki ikitoa mkopo wa mtaji wa kujenga kiwanda; kupitia mkopo huo, wananchi watapata ajira wakati wa ujenzi na baada ya kiwanda kukamilika. Fikiria pia benki ikitoa mkopo kwa ajili ya ujenzi wa barabara; wakati wa ujenzi wa barabara hiyo wananchi wanapata ajira, lakini pia ikikamilika itapunguza gharama na usafiri kwa wananchi, na hivyo kusaidia kupunguza umaskini.

 

Sambamba na hayo, sekta ya benki ni umuhimu kwa vile inatoa ajira za moja kwa moja. Mathalan, nimeambiwa kuwa Benki hii imetoa ajira kwa Watanzania wapatao 3,200. Lakini pia sekta ya benki ni muhimu kwa vile inawasaidia wananchi kutunza amana (fedha) kwa usalama, na wakati wowote wakihitaji, wanapewa. Tena kwa siku hizi, kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, hata ukihitaji fedha zako usiku wa manane unazipata kwa njia ya ATMs au Simu kiganjani.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Kwa kuzingatia hayo yote, ni dhahiri kuwa sekta ya benki ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa lolote. Na kwa sababu hiyo, inatia moyo kuona kuwa kwa takriban miongo mitatu iliyopita, sekta ya benki imezidi kuimarika hapa nchini. Mathalan, mwaka 1990, nchi yetu ilikuwa na benki 3 tu, lakini kwa sasa nchi yetu ina zaidi ya benki 58. Na jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba miongoni mwa benki zinazofanya vizuri ni Benki hii ya CRDB, ambayo kwa takriban asilimia 86 zinamilikiwa na Watanzania (asilimia 40 watu binafsi, asilimia 21 Serikali na mifuko ya pensheni ina asilimia 15).

 

Hivi punde, Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Kimei, ameeleza mafanikio ambayo Benki hii imepata tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996. Baadhi ya mafanikio aliyoyataja ni kuongezeka kwa rasilimali zake kutoka thamani ya shilingi bilioni 54 hadi kufikia shilingi trilioni 5.5; kupanua wigo wa benki kutoka matawi 19 hadi 260, ukiachilia mbali ATMs 600 ilizonazo, Mawakala 3,000, SACCOS shirikishi 455 na matawi ya kutembea 21. Benki pia imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 3.5; ambapo shilingi trilioni 1 zimekwenda kwenye sekta mbili za kilimo na viwanda. Aidha, kama nilivyosema awali, benki imelipa kodi ya shilingi bilioni 800 na kutoa ajira 3,200 kwa Watanzania. Vilevile, mwaka huu, baada ya kuwabana sana hatimaye wametoa gawio la shilingi bilioni 19 kwa Serikali. Na natumaini wataendelea kutupa gawio letu kila mwaka. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii, kwa dhati kabisa, kutoa pongezi nyingi sana kwa Benki hii chini ya Dkt. Kimei kwa kazi kubwa inazofanya kwa ajili ya kukuza uchumi lakini pia kupiga vita umaskini katika nchi yetu.

 

Mtakumbuka kuwa Benki hii kihistoria ilikuwa ikimilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali, wakati huo ikijulikana kama Tanzania Rural Development Bank (TRDB). Mwaka 1996 ilibinafsishwa ili kuongeza ufanisi wake. Kwa mfano mzuri uliooneshwa na Benki hii, ni dhahiri kuwa kama mashirika na taasisi zote zilizobinafsishwa zingefanya kazi kama Benki hii, nchi yetu ingekuwa imepiga hatua kubwa za kimaendeleo. Lakini mashirika na viwanda vingi vilivyobinafsishwa, hivi sasa havifanyi kazi.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Jukumu langu leo ni kufungua benki hii. Hata hivyo, kabla sijatekeleza jukumu hilo, ninayo masuala machache ya kueleza. Suala la kwanza kabisa, ni malalamiko kuhusu kupungua kwa kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi. Serikali inalitambua suala hili, na kupitia Benki Kuu,  imechukua hatua mbalimbali kulishughulikia. Mathalan, Mwezi Aprili, mwaka huu tuliamua kupunguza kiwango cha kisheria cha sehemu ya amana inayotakiwa kuwekwa benki kuu na benki za Biashara kutoka asilimia 10 hadi asilimia 8. Sambamba na hilo, tumeshusha riba ya Benki Kuu (discount rate) mara mbili kutoka asilimia 16 hadi 12 mwezi Machi 2017, na mwezi Agosti tukaishusha tena hadi asilimia 9. Pamoja na hayo, tumetoa mikopo maalum kwa benki za biashara na halikadhalika Benki Kuu inanunua fedha za kigeni kwenye soko la jumla la benki ili kuongeza ukwasi wa shilingi kwenye uchumi. Hatua nyingine tulizochukua ni kuendelea mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuongeza chachu katika shughuli za uchumi.

 

Kutokana na hatua hizi, hali ya ukwasi imeanza kuimarika na kusaidia  kupunguza riba katika soko la fedha baina ya benki (IBCM rate) kutoka asilimia 13.69 mwezi Desemba 2016 hadi asilimia 3.29 mwezi Novemba 2017. Aidha, riba katika soko la dhamana za Serikali zimepungua kutoka wastani wa asilimia 15.12 mwezi Desemba 2016 hadi asilimia 8.76 mwezi Novemba 2017. Kwa matokeo haya, tuna matumaini makubwa kuwa kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi utazidi kuimarika katika siku za hivi karibuni.

 

Suala jingine ambalo ningependa kuzungumzia ni kuhusu benki kushiriki kwenye shughuli za maendeleo. Kama nilivyosema hapo awali, sekta ya benki ni muhimu kwenye sekta zote, ikiwemo viwanda na kilimo. Hivyo basi, napenda kutoa wito kwa benki zote nchini kuangalia wa kutenga fedha nyingi za mikopo kwenye sekta hizi mbili. Kama mnavyofahamu, nchi yetu kwa sasa imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda; na miongoni mwa viwanda tunavyolenga kuvijenga ni vile vinavyotumia zaidi malighafi za hapa nchini, hususan mazao ya kilimo. Hivyo basi, naziomba benki kuunga mkono dhamira hiyo ya Serikali. Nimefurahi kusikia kuwa ninyi CRDB mmekuwa mkitenga asilimia 15 kwa ajili ya sekta ya viwanda, na mwakani mmepanga kuongeza hadi kufikia asilimia 20, sawa na shilingi bilioni 700. Hongereni sana. Na naziomba benki nyingine ziige mfano wenu.

 

Napenda pia kuzungumzia kidogo suala la benki kupanua wigo wa mtandao wenu. Ni kweli kuwa idadi ya benki imeongezeka hapa nchini. Lakini kwa bahati mbaya, benki nyingi zipo Dar es Salaam na kwenye baadhi ya miji mikuu ya mikoa na wilaya.  Mathalan kwa taarifa za mwaka 2015 asilimia 36.3 ya matawi yote ya Benki yalikuwa Dar es Salaam asalimia 7.1 Arusha, asilimia 6.5  Mwanza, asilimia 5.4 Mbeya na asilimia 4.6 Moshi.  Ni benki chache tu ndizo zina matawi kwenye vijijini. Hivyo, natoa wito kwenu kusambaza huduma zenu hadi vijijini, ambako Watanzania wengi wanaishi. Na ninaposema kusambaza huduma hadi vijijini simaanishi kwamba lazima mjenge majengo, ninachomaanisha ni kwenu ninyi kubuni njia mbalimbali za kufikisha huduma za kibenki kwa wananchi waliopo vijijini, ikiwemo kuanzisha matawi mengi zaidi ya kutembea, kuingia ubia na mawakala  (Bank Agents), kuanzisha huduma za kifedha za kwa njia za mtandao (Sim Banking, Internet Baking n.k.) kama ambavyo ninyi CRDB na baadhi ya Benki nyingi mmeanza kufanya.

 

Nina imani mkiweza kufikisha huduma zenu hadi vijijini, sio tu mtawasaidia wananchi kupata huduma za kibenki bali pia itawaongezea benki nchini ukwasi wa kutosha. Kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2015, ukwasi wa benki zote nchini mwaka 2014 ulikuwa una thamani ya shilingi trilioni 22.5. Kiasi hiki bado ni kidogo sana ukilinganisha na mahitaji makubwa ya fedha (mikopo) yaliyopo hapa nchini. Mathalan, Mpango wetu wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano, ambao tumeanza kuutekeleza katika mwaka wa fedha 2016/2017 unahitaji kiasi cha shilingi trilioni 107. Hivyo, nawahimiza benki kusambaza huduma zenu kwenye maeneo ya vijijini ili muweze kuongeza ukwasi katika benki zenu.  Aidha, nawakaribisha wawekezaji wengine kuja kuwekeza kwenye sekta hii ya benki hapa nchini.

 

Jambo jingine ambalo ningependa kuzungumzia ni kuhusu tatizo la riba za mikopo kuendelea kuwa juu. Riba za mikopo hapa nchini bado zipo juu. Natambua kuwa tatizo hili linasababishwa na mambo mengi, ikiwemo kutokuwepo kwa taarifa za kutosha za wakopaji, wasiwasi wa benki kutolipwa na wakopaji na hivyo kuongeza gharama za ufuatiliaji, n.k. Pamoja na matatizo hayo, Serikali imechukua hatua mbalimbali, ambazo binafsi nilidhani zingeweza kushusha kiwango cha riba nchini ili kuwawezesha wananchi, hususan wa kipato cha chini kuchukua mikopo. Mojawapo ya hatua hizo ni kuanzisha Mfumo wa Kuhifadhi Taarifa za Wakopaji ( yaani Credit Reference Bureau) ambao unaziwezesha benki zote kuwatambua wakopaji na kuweza kuchukua tahadhari stahiki. Aidha, tunaendelea kutoa vitambulisho vya taifa ambavyo kwa sasa vina taarifa nyingi. Hivyo, basi naziomba benki kuanza kupunguza viwango vya riba. Aidha, naihimiza Benki Kuu kukamilisha zoezi la kutangaza Sera ya Riba (Policy Rate), ambayo itazifanya taasisi za kifedha kuwa na riba zinazowiana na sera hiyo. Vilevile, napenda kutumia fursa hii kuwahimiza wananchi kuwa na utamaduni wa kurejesha mikopo. Dawa ya deni ni kulipa. Na niiombe Mahakama ya Biashara kuharakisha kesi zinazohusiana na madeni ya mikopo.

 

Mbali na hayo, napenda kutoa wito kwa Wizara ya Fedha na Benki ya Kuu kudhibiti matumizi ya ya fedha za kigeni (Dola) nchini. Na jambo hili, liende sawia na kuongeza usimamizi kwa Maduka ya Kubadilisha Fedha (Bureau De Change). Ni lazima tuondokane na utaratibu wa matumizi holela ya fedha za kigeni nchini; lakini pia Maduka ya Kubadilisha Fedha yasitumike kuwa sehemu za kutakatisha fedha zisizo halali kutoka nje. Aidha, natoa wito kwa Benki Kuu kuongeza usimamizi katika uanzishaji na uendeshaji wa shughuli za Kibenki hapa nchini. Kabla Benki haijaanzishwa wamiliki wake wafuatiliwe kwa makini; na halikadhalika, benki inayoshindwa kujiendesha ifutwe hata kama ni ya Serikali.

 

Sambamba na hayo, mtakumbuka kuwa mwezi Juni mwaka huu, nikiwa pale Kijitonyama kuzindua Kituo cha Data na Mfumo wa Ukusanyaji Mapato kwa njia ya Kielektroniki, niliagiza kuwa benki zijiunge na Mfumo huo wa kukusanya mapato kwa njia ya kielektroniki. Na nakumbuka Kamishna wa TRA aliahidi kuwa hadi mwezi Desemba makampuni yote ya benki na simu yatakuwa yamejiunga.  Hivi sasa tupo katikati ya mwezi Desemba, lakini kwa taarifa nilizonazo ni benki chache tu ndizo tayari zimejiunga na mfumo huo. Benki nyingi pamoja na baadhi ya Makampuni ya Simu bado hazijajiunga na mfumo huo.  Napenda kurudia tena agizo langu kwa benki na kampuni zote za simu kuhakikisha zinajiunga na mfumo huo kabla ya mwaka huu kwisha. Kwa kampuni ya simu au benki itakayoshindwa kutekeleza agizo hili, taratibu husika zifanyike, ikiwezekana makampuni au benki hizo zifungiwe kufanya kazi nchini.

 

Jambo la mwisho ambalo ningependa kulisema ni kutoa wito kwa Watanzania wote kutumia huduma za kibenki hususan kwa kufungua akaunti za benki. Mbali na usalama, benki inasaidia mtu kupanga matumizi yake vizuri. Unakuwa huwezi kutumia fedha ovyo. Lakini, nawasihi na nanyi wamiliki wa Benki kuimarisha mifumo yenu ya usalama ili kukabiliana na vitendo vya wizi kwa njia za mtandao. Aidha, wachukulieni hatua  watumishi wenu ambao sio waaminifu.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kuushukuru tena uongozi wa CRDB kwa kunikaribisha na kwa zawadi ya hundi ya kiasi cha shilingi milioni 100 mliyonikabidhi. Hundi hii mmenikabidhi hadharani. Hivyo basi, na mimi naikabidhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ili fedha hizo zikatumike kwa ya kujenga Wodi katika Hospitali ya Mkoa.  Siku moja nitakuja kuikagua hiyo wodi.

 

Mwisho kabisa lakini sio kwa umuhimu napenda kuwapongeza LAPF kwa kujenga jengo hili hapa Dodoma. Jengo ni zuri sana.

 

Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kutekeleza jukumu lililonileta la kufungua Tawi la Sita la Benki ya CRDB hapa Dodoma.

 

Mungu Ibariki CRDB!

Mungu zibariki Benki zote nchini!

Mungu wabariki wana-Dodoma!

Mungu Ibariki Tanzania!

 

“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”