Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE SHEREHE ZA MIAKA 56 YA UHURU WA TANZANIA BARA, DODOMA, TAREHE 9 DESEMBA, 2017

Saturday 9th December 2017

Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;

 

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu

wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili

wa Rais wa Zanzibar;

 

Mheshimiwa Job Ndugai, Spika wa Bunge

la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid, Spika wa Baraza la Wawakilishi;

 

Mheshimiwa Prof. Ibrahim Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Omar Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;

 

Waheshimiwa Marais Wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa na Mzee Kikwete;

 

Waheshimiwa Viongozi Wakuu Wastaafu wa        Serikali zetu mbili mliopo, Mzee Bilal, Mzee Malecela, Mzee Kificho;

 

Waheshimiwa Wake wa Viongozi Wakuu mliopo, mkiongozwa na Mama Maria Nyerere na Mama Fatuma Karume;

 

Waheshimiwa Mawaziri mliopo;

 

Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;

 

Mheshimiwa Balozi John Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi;

 

Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;

 

Waheshimiwa Wabunge;

 

Waheshimiwa Mabalozi na Viongozi wa Taasisi za Kimataifa;

 

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa na Dini mliopo;

 

Wageni waalikwa wote;

 

Wananchi Wenzangu, Mabibi na Mabwana:

 

Kabla ya kuanza hotuba yangu, naomba sote tusimame kwa dakika moja kuwaombea mashujaa wetu, askari 14, waliouawa wakiwa katika jukumu la kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) juzi. Tunamwomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mashujaa wetu mahali pema peponi na kuwaponya askari waliojeruhiwa. Amina.

 

Baada ya utangulizi huo, napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wetu, kwa kutujalia uzima na kutuwezesha kuiona siku hii adhimu kwenye historia ya nchi yetu. Siku kama ya leo ya Jumamosi, tarehe 9 Desemba mwaka 1961, Jamhuri ya Tanganyika, hivi sasa Tanzania Bara, ilipata Uhuru wake. Uhuru huu ulihitimisha utawala wa kikoloni uliodumu nchini kwa takriban miaka 76; ikijumuisha miaka 33 ya Utawala wa Ujerumani na miaka mingine 43 ya Utawala wa Uingereza.

 

Kama mnavyofahamu, harakati za kutafuta Uhuru wa nchi yetu ziliongozwa na Chama cha Tanganyika African National Union (TANU), ambacho mwaka 1977 kiliungana na Chama cha Afro Shiraz (ASP), ambacho kiliongoza mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964, na kuunda Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama Tawala. Hii ndiyo historia yenyewe. Haiwezi kubadilika. Uhuru wa nchi yetu uliletwa na Vyama Mama vya CCM, yaani TANU na ASP. Hivyo basi, leo tunaposheherekea Miaka 56 ya Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara), hatuna budi kuwashukuru na kuwapongeza Wazee wetu 17, ambao mwezi Julai 1954, wakiongozwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, walianzisha Chama cha TANU. Tunawakumbuka pia wananchi wote, ambao kabla na wakati wa Chama cha TANU, walishiriki katika harakati za kutafuta uhuru wa nchi yetu. Nafahamu wengi wao tayari wametangulia mbele za haki; hivyo, kwa niaba ya Watanzania wote, namwomba Mwenyezi Mungu azipumzishe roho zao mahali pema peponi. Amina!

 

Ndugu wananchi,

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:

Ni ukweli usiopingika kuwa, katika kipindi cha Miaka 56 ya Uhuru wa nchi yetu, tumepata mafanikio makubwa. Ndio! tumepata mafanikio makubwa, tena sana tu. Nafahamu wapo watu ambao wakisikia kauli hiyo huwa wanaumia; lakini huo ndio ukweli. Nchi yetu imepiga hatua kubwa za maendeleo tangu kupata Uhuru. Naomba nitoe mifano michache. Wakati tunapata Uhuru, baada ya utawala wa takriban miaka 76 ya Kikoloni, nchi yetu ilikuwa na mtandao wa barabara wenye urefu kilometa 33,600.  Kati ya barabara hizo ni kilometa 1,360 tu ndio zilikuwa na lami. Kwa sasa tuna mtandao barabara wenye kilomita 122,500, ambapo kilometa 80,000  zipo chini ya TAMISEMI na zinahudumiwa na  TARURA; kilometa 36,000 zipo chini ya TANROADS, na kilometa 6,500 zipo chini ya Hifadhi za Wanyama za Taifa (TANAPA). Aidha kati ya Mtandao huo wa barabara, kilometa 12,679.55, ni za lami.  Sambamba na hayo, kuna jumla ya kilometa 2,480 zinazoendelea kujengwa kwa kiwango cha lami na barabara nyingine zenye urefu wa kilometa 7,087 zipo kwenye hatua mbalimbali za maandalizi kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha lami. Vilevile, tumejenga madaraja makubwa 17, na mengine 14 yapo kwenye hatua mbalimbali.

 

Ukiachilia mbali ujenzi wa barabara, wakati tunapata Uhuru, nchi yetu ilikuwa na vituo vya kutolea huduma za afya 1,095 (hospitali 98, vituo vya afya 22 na zahanati 975), leo hii tuna vituo 7,293 (hospitali 178, vituo vya afya 795 na zahanati 6,285). Wakati tunapata Uhuru tulikuwa na Shule za Msingi 3,100 hivi sasa zipo 17,379; shule za sekondari zilikuwa 41 hivi sasa zipo 4,817; na tulikuwa na Chuo Kikuu kimoja tu, lakini leo vipo 48. Madaktari waliosajiliwa walikuwa 403, ambapo kati yao Watanganyika walikuwa 12 tu, leo tuna madaktari 9,343. Mwaka 1961, Wahandisi wazalendo walikuwa wawili (2) tu; lakini hadi kufikia mwezi Juni 2017 nchi yetu imefikisha wahandisi 19,164. Makandarasi nao walikuwa wawili tu (2), lakini hivi sasa wakandarasi waliosajaliwa wamefikia 9,350. Halikadhalika, wakati tunapata Uhuru, wastani wa umri wa mtu kuishi ulikuwa miaka 37, leo hii wastani ni miaka 61. Mifano ipo mingi. Siwezi kuitaja yote leo.

 

Itoshe tu kusema kuwa katika kipindi cha miaka 56 ya uhuru wetu, tumepiga hatua kubwa za kimaendeleo kwenye nyanja mbalimbali, ikiwemo huduma za jamii, ulinzi, umeme, kilimo, utalii, biashara, mifugo, uvuvi, demokrasia, diplomasia, utamaduni, n.k. Zaidi ya hapo, na pegine kubwa zaidi ni kwamba, katika kipindi cha miaka 56 ya Uhuru, tumeweza kulinda na kudumisha amani, umoja na Muungano wetu.

 

Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii, kuwashukuru na kuwapongeza kwa dhati kabisa Viongozi wa Awamu zote za Serikali zetu mbili, ya Muungano na ya Zanzibar, kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 56 ya Uhuru wa nchi yetu. Na nimefarijika sana kuona kuwa viongozi wastaafu wa nchi yetu, Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa, Mzee Kikwete, Mzee Bilal, Mzee Malecela tunao hapa. Na niwaambie ndugu zangu Watanzania kuwa mambo kama haya ya kuwaona viongozi wastaafu wakishiriki kwenye tukio kama hili kwa pamoja ni nadra sana Duniani. Sio kwenye nchi zote jambo kama hili linawezekana. Kwenye nchi nyingine haiwezekani. Hivyo basi, nawasihi Watanzania wenzangu tuzidi kudumisha amani na umoja wetu. Na mimi namuomba Mwenyezi Mungu siku moja niweze kuhudhuria tukio kama hili nikiwa nimeungana na viongozi wengine wastaafu.

 

Lakini mbali na kuwapongeza viongozi wastaafu kwa mafanikio yaliyopatikana, napenda kuwapongeza Watanzania wote: wakulima, wafanyakazi, wavuvi, wafugaji, wafanyabiashara, wasanii, n.k.; kwa michango yenu ya hali na mali iliyowezesha kupatikana mafanikio niliyoyataja na mengine ambayo sikuyataja. Bila ya ninyi kujitoa, mafanikio haya kamwe yasingepatikana. Navipongeza pia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama (JWTZ, Polisi, Usalama wa Taifa, Magereza, Uhamiaji, Zimamoto, n.k.), kwa kushiriki kikamilifu na kufanikisha kupatikana kwa mafanikio haya. Napenda kuwahakikishia vyombo vyote vya ulinzi kuwa Serikali yenu ipo pamoja nanyi na tutaendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zinawakabili.

 

 

 

Ndugu wananchi,

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:

Sherehe za Uhuru wa Tanzania Bara mwaka huu zinafanyika hapa Dodoma. Hapa Dodoma ndio Makao Makuu ya Nchi yetu. Na zitaendelea kufanyika hapa. Napenda niwahakikishie ndugu Watanzania kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza mambo yote mazuri yaliyopatikana, na kutekeleza mambo mengine mapya kwa lengo la kuhakikisha kuwa Watanzania wote wanafaidi matunda ya uhuru.

 

Ombi langu kwa Watanzania endeleeni kuziamini Serikali zetu mbili, za Muungano na ya Zanzibar. Mimi na mwenzangu Dkt. Shein, tunaahidi kuwa tutasimamia na kutekeleza mambo yote tuliyowaahidi, ikiwemo ahadi zilizomo kwenye Ilani yetu ya Uchaguzi. Na kutekeleza hayo, hatutambagua mtu kwa misingi ya dini, kabila, itikadi ya kisiasa, jinsia au rangi. Daima tutakuwa watumishi wenu.

 

Ndugu wananchi,

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:

 Leo wakati tunaadhimisha Sherehe za Miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania Bara, napenda kuwakumbusha Watanzania wenzangu kuwa Ibara ya 45 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa mamlaka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa msamaha kwa wafungwa wa makosa mbalimbali. Kwa faida ya hadhira hii, napenda kuinukuu Ibara hiyo, kama ifutavyo:

45 (1)         bila kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Ibara hii, Rais anaweza kutenda lolote kati ya mambo yafuatayo:-

(a)     kutoa msamaha kwa mtu yeyote aliyepatikana na hatia mbele ya mahakama kwa kosa lolote, na aweza kutoa msamaha huo ama bila ya masharti au kwa masharti, kwa mujibu wa sheria;

(b)     kumwachilia kabisa au kwa muda maalum mtu yeyote aliyehukumiwa kuadhibiwa kwa ajili ya kosa lolote ili mtu huyo asitimize kabisa adhabu hiyo au asitimize adhabu hiyo wakati wa muda huo maalum;

(c)     kuibadilisha adhabu yoyote aliyopewa mtu yeyote kwa kosa lolote iwe adhabu tahafifu;

(d)     kufuta adhabu yote au sehemu ya adhabu yoyote aliyopewa mtu yeyote kwa ajili ya kosa lolote au kufuta adhabu yote au sehemu ya adhabu ya kutoza, au kuhozi (au kuchukua) kitu cha mtu mwenye hatia ambacho vinginevyo kingechukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

(2)     Bunge laweza kutunga Sheria kwa ajili ya kuweka utaratibu utakaofuatwa na Rais katika utekelezaji wa madaraka yake kwa mujibu wa Ibara hii.

(3)     Masharti ya Ibara hii yatatumika kwa watu waliohukumiwa na kuadhibiwa Tanzania Zanzibar na kwa adahabu zilizotolewa Tanzania Zanzibar kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge inayotumika Zanzibar, halikadhalika, masharti hayo yatatumika kwa watu waliohukumiwa na kuadhibiwa Tanzania Bara kwa mujibu wa sheria.

 

Sambamba na Ibara hii inayompa Rais mamlaka ya kutoa msamaha, nimesoma pia Presidential Affair Act ya mwaka 1962 cap 9 of Tanzania.

 

Ndugu Watanzania wenzangu;

Hivi sasa nchi yetu ina wafungwa wapatao 39,000, ambapo wanaume ni takriban 37,000 na wanawake ni 2,000. Kati ya wafungwa waliopo magerezani, wafungwa 522 wamehukumiwa adhabu ya kifo, ambapo wanaume ni 503 na wanawake ni 19.  Idadi ya wafungwa waliofungwa kifungo cha maisha ni 666, ambapo wanaume ni 655 na wanawake 11.

 

Hivyo basi, kwa mujibu wa mamlaka niliyopewa na Katiba kupitia Ibara ya 45, nimeamua kutoa msamaha kwa wafungwa 8,157. Kati ya wafungwa hao niliowapa msamaha, wafungwa 1,828 watatoka leo na waliosalia 6,329 watapunguziwa vifungo vyao vya kukaa gerezani na kutoka kulingana na vifungo vyao. Vilevile, kwa kutumia Ibara hiyo ya 45, nimetoa msamaha kwa wafungwa 61 waliokuwa wamehukumiwa kunyongwa. Halikadhalika, nimeamua kutoa msamaha kwa wafungwa kutoka Familia ya Nguza (Nguza Vicking na Johnson Nguza). Wengi niliowapa msamaha, hususan waliohukumiwa kunyongwa na kufungwa vifungo virefu, wametumikia vifungo vyao kwa muda mrefu na wameonesha tabia njema na kujutia makosa yao.  

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:

Nimeeleza mambo mengi; mengi sana. Hivyo, napenda niishie hapa. Lakini kabla sijahitimisha, napenda nitoe shukrani zangu nyingi kwa Kamati ya Maandalizi kwa kufanikisha Sherehe hii. Sherehe zimefana sana. Hongereni sana wana-Kamati. Tunavishukuru pia vyombo vya ulinzi na usalama, vikundi vya burudani, chipukizi na waandishi wa habari kwa kufanikisha sherehe hii.

 

Kwa namna ya pekee, napenda kuwashukuru wageni wetu waalikwa waliokuja hapa kushiriki nasi katika shughuli hii muhimu na ya kihistoria kwa taifa letu.Tunawashukuru Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi mbalimbali za Kimataifa. Napenda niwahakikishie kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Mataifa yenu pamoja na Taasisi mnazoziwakilisha.

 

Napenda pia kuwashukuru wana-Dodoma wote, mkiingozwa na Mkuu wenu wa Mkoa, Mheshimiwa Mahenge, kwa ukarimu mkubwa mliotuonesha na kwa kujitokeza kwa wingi kwenye Sherehe hizi. Nimejionea mwenyewe kuwa watu wengi wapo nje. Hii ina maana kuwa mnahitaji uwanja mpya. Na kwa bahati nzuri, rafiki zetu wa Morocco wamekubali kutujengea Uwanja Mpya hapa Dodoma, ambapo Jiwe la Msingi tunatarajia kuliweka mwezi Machi au Aprili 2018. Sambamba na hilo, napenda kuwahakikishia wana-Dodoma kuwa dhamira ya Serikali kuhamia Dodoma ipo pale pale. Hakuna kurudi nyuma. Makamu wa Rais atahamia kabla ya mwisho wa Mwaka huu, na mimi nitahamia mwakani. Tutaendelea kuboresha miundombinu pamoja na upatikanaji wa huduma za jamii hapa Dodoma, hususan kwa kuwa hivi sasa mji huu ndio kioo cha nchi yetu. Ahadi yetu ya kujenga barabara ya mzunguko, uwanja wa michezo, njia ya reli kutoka kitongoji cha Chalinze hadi hapa mjini pamoja na kuboresha huduma za maji na afya zipo pale pale. Nawaomba muendelee kutuamini. Na kamwe hatutawaangusha.

 

Mwisho lakini sio kwa umuhimu, napenda kurudia tena kuwashukuru viongozi wastaafu kwa kuja kujumuika nasi kwenye sherehe hizi. Aidha, navishukuru vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa na nzuri wanazofanya kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa kisiwa cha amani. Wito wangu kwa Watanzania tuendelee kuenzi na kudumisha tunu za Amani, Muungano pamoja na Umoja na Mshikamano, ambazo tumeachiwa na waasisi wetu, Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na Mzee Abeid Karume.

 

Mungu Ibariki Tanzania!

Mungu Wabariki Watanzania!

“Ahsanteni Sana kwa kunisikiliza”