Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA CHAMA CHA WALIMU TANZANIA (CWT) DODOMA, TAREHE 14 DESEMBA, 2017

Thursday 14th December 2017

Mheshimiwa Mwalimu Leah Ulaya, Kaimu Rais

wa Chama Cha Walimu Tanzania;

 

Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu

         wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Job Ndugai, Spika wa Bunge

         la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Seleman Jafo, Waziri wa Nchi

Ofisi ya Rais – TAMISEMI;

 

Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu

na Mafunzo ya Ufundi;

 

Mheshimiwa George Mkuchika, Waziri wa Nchi,

Ofisi ya Rais – UTUMISHI;

 

Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi,

Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu;

 

Waheshimiwa Mwalimu Janet Magufuli,

Mke wa Rais, na Mwalimu Mary Majaliwa, Mke wa Waziri Mkuu;

 

Mheshimiwa Binilith Mahenge, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;

 

Waheshimiwa Wabunge mliopo;

 

Mheshimiwa Makatibu Wakuu mliopo;

 

Mheshimiwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama

vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA);

 

Ndugu Katibu Mtendaji wa Tume ya Utumishi wa Walimu;

 

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi

mliohudhuria kutoka Ndani na Nje ya Tanzania;

 

Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa

wa Chama Cha Walimu Tanzania;

 

Waheshimiwa Viongozi mbalimbali mliopo;

 

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana:

 

Awali ya yote napenda niwashukuru sana walimu kwa kunikaribisha. Kwangu mimi, leo ni siku ya pekee sana. Na nakiri kwamba nimefurahi sana. Nimefurahi, kwanza, kwa kupata fursa hii adhimu ya kuzungumza nanyi walimu wenzangu. Kama mnavyofahamu, mimi ni mwalimu. Mke wangu naye ni mwalimu. Nazijua shida na raha za ualimu. Hivyo basi, kuwepo mahali hapa, ni faraja kubwa kwangu. Lakini, jambo la pili lililonifurahisha ni kwamba, sasa nimetambua kuwa Chama Cha Walimu kimedhamiria kufanya kazi na Serikali. Ahsanteni sana walimu wenzangu. Na napenda kutumia fursa hii kuwahikikishia kuwa Serikali itashirikiana na ninyi kwa karibu.

Kabla sijaendelea zaidi, napenda nami niungane nanyi katika kutoa salamu zangu za pole kwa familia, ndugu na jamaa wa Marehemu Alhaji Yahya Msulwa, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CWT, ambaye aliaga dunia tarehe 17 Novemba, 2017, wakati akiwa kwenye maandalizi ya Mkutano huu. Sambamba na hilo, kama mnavyofahamu, leo nchi yetu imeiaga rasmi miili ya askari wetu mashujaa 14 waliouawa hivi karibuni nchini DRC wakiwa katika ulinzi wa amani. Hivyo basi, naomba tuzidi kuwaombea mashujaa wetu roho zao zipumzike mahali pema pepoi. Aidha, tuwaombee mashujaa wengie waliojeruhiwa kwenye tukio hilo ili wapone kwa haraka. Amina.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Ndugu Walimu Wenzangu;

Leo ni mara yangu ya kwanza kukutana rasmi na walimu tangu nimechaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano ya Nchi yetu. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru walimu kote nchini kwa kura nyingi mlizonipa zilizoniwezesha kuibuka mshindi kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita. Ahsanteni sana walimu wenzangu.  Nawaahidi kufanya kazi kwa bidii kwa manufaa ya Watanzania wote.

 

Napenda pia kutumia fursa hii, kutoa shukrani zangu nyingi kwa uongozi wa CWT kwa uamuzi wenu wa kuhamishia Mkutano huu hapa Dodoma. Kama mnavyofahamu, Mkutano huu awali ulipangwa kufanyika Arusha. Lakini baadaye, mliamua kuuhamishia hapa Dodoma. Nawashukuru sana. Hapa Dodoma ndio Makao Makuu ya nchi yetu. Hapa pia ni Makao Makuu ya Ofisi za Bunge. Aidha, hapa ni mahali ambako, chuo kikubwa zaidi katika eneo zima la Afrika Mashariki na Kati, Chuo Kikuu cha Dodoma, kipo. Hivyo basi, nina imani kuwa Wajumbe wa Mkutano wamefurahi kuja kufanya mkutano wao hapa Dodoma.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Ndugu Wajumbe wa Mkutano;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Sekta ya elimu ni nyeti na muhimu katika jamii na pia kwa maendeleo ya Taifa lolote. Sisi Waswahili tuna msemo usemao “Elimu ni Ufunguo wa Maisha”. Marafiki zetu Wachina nao wana msemo usemao, naomba niunukuu kwa Lugha yetu adhimu ya Kiswahili, “Ukitaka kuwekeza kwa mwaka mmoja, panda mpunga; Ukitaka kuwekeza kwa miaka kumi, panda miti; lakini ukitaka kuwekeza katika maisha, wekeza kwenye elimu”. Hii yote ni katika kudhihirisha kuwa elimu ni muhimu kwa mtu mmoja mmoja, katika jamii na kwa maendeleo ya nchi kwa ujumla.

 

Na bila shaka, kwa kutambua umuhimu huo, Serikali za Awamu zote za nchi yetu, ya kwanza hadi ya sasa, imeweka mkazo mkubwa katika kukuza na kuboresha sekta hii. Juzi kwenye Maadhimisho ya Sherehe za Uhuru nimeeleza kuwa wakati tunapata Uhuru, mwaka 1961, baada ya utawala wa Kikoloni uliodumu kwa takriban miaka 76, nchi yetu ilikuwa na shule za msingi 3,100. Lakini katika kipindi cha miaka 56 ya Uhuru wetu, tumeweza kujenga shule za msingi mpya 14,279 na hivyo kutufanya tuwe na jumla ya shule za msingi 17,379. Katika kipindi hicho Shule za sekondari zilikuwa 41, lakini hivi sasa zipo 4,817. Tulikuwa na Chuo Kikuu kimoja, lakini leo hii tuna vyuo vikuu 48

                         

Mtakubaliana nami kuwa haya ni mafanikio makubwa sana. Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kutoa pongezi zangu nyingi kwa viongozi wa awamu zote za nchi yetu kwa kufanikisha kupatikana kwa mafanikio haya. Pamoja na pongezi hizo nilizozielekeza kwa viongozi watangulizi wangu, upo usemi usemao “unaweza kuwa na shule, chuo au chuo kikuu bila ya kuwepo kwa majengo, vitabu, madawati, maabara, chaki na kalamu; lakini kamwe huwezi kuwa na shule au chuo bila ya walimu”. Kwa maana hiyo, pongezi nyingi zaidi inafaa ziwaendee ninyi walimu. Hivyo basi, kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya Serikali na wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania napenda kutumia fursa hii kutoa pongezi nyingi sana kwenu walimu kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya ya kuwaelimisha Watanzania. Kwa hakika, walimu mnafanya kazi kubwa sana. Hongereni na ahsanteni sana.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CWT;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Kama nilivyotangulia kusema hapo awali, Serikali za Awamu zilizotangulia zimefanya juhudi kubwa za kukuza na kuendeleza sekta ya elimu nchini. Kwa lengo la kuendeleza mafanikio hayo, na sisi Serikali ya Awamu ya Tano tunachukua hatua mbalimbali za kupanua wigo na kuboresha sekta ya elimu. Kama mnavyofahamu, hivi sasa tunatekeleza elimu bila malipo kuanzia shule ya msingi  hadi sekondari, ambapo awali tulikuwa tukitenga shilingi bilioni 18.77 kwa mwezi kugharamia, lakini kuanzia mwezi Julai 2016 tuliongeza fedha hizo hadi kufikia shilingi bilioni 23.868. Hii maana yake ni kwamba, tangu utaratibu huu uanze mwezi Desemba 2015 hadi Novemba 2017, Serikali imetumia kiasi cha takribani shilingi bilioni 535.

Ninyi walimu ni mashahidi wazuri. Uamuzi wa Serikali wa kuanzisha elimu bila malipo, umeleta mafanikio makubwa sana, hususan katika kuongeza idadi ya wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza na kidato cha kwanza. Lakini, kutokana na ongezeko hilo la wanafunzi, zilijitokeza changamoto, ikiwemo upungufu wa madawati, vyumba vya madarasa, pamoja na vifaa na vitendea kazi vingine. Kutokana na matatizo hayo, Serikali ilianza kuchukua hatua ili kushughulikia.

Tulishirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo wananchi, na kuweza kupunguza kwa takriban asilimia 95 tatizo la madawati kwenye shule zetu za msingi na sekondari nchini kote. Aidha, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Serikali imejenga na kukarabati miundombinu katika shule za msingi na sekondari 365, zikiwemo shule za sekondari kongwe 88; kwenye halmashauri 129. Miundombinu hiyo ni nyumba za walimu 12, vyumba vya madarasa 1,435, mabweni 261, majengo ya utawala 11, mabwalo 6, matundu ya vyoo 2,832, maktaba 4, na visima vya maji safi 4.  Aidha, katika bajeti ya Mwaka huu wa Fedha 2017/2018, Serikali, kupitia bajeti ya Halmashauri, imetenga shilingi bilioni 126.65 kwa ajili ya kujenga na kukarabati miundombinu ya shule za msingi na sekondari, itakayojumuisha nyumba za walimu 2,364; madarasa 6,636; vyoo 9,355; madawati 118,921; mabweni 157; hosteli 176 na maabara zipatazo 1,817. Waheshimiwa Mawaziri wahusika hakikisheni haya yanatekelezwa.

Sambamba na hayo, tumeanza kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha elimu yenyewe. Ninyi walimu ni mashahidi, mwaka huu wa 2017 tumegawa vifaa vya maabara kwenye shule za sekondari 1,696 pamoja na vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule za msingi 213 na shule za sekondari 22.  

Ukiachilia mbali Elimu ya Msingi na Sekondari, Serikali pia inaboresha Elimu ya Juu, hususan kwa kutoa mikopo kwa wanafunzi.  Idadi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu wanaopewa mikopo imeongezeka kutoka 98,300 mwaka 2015 hadi kufikia takriban 124,000 hivi sasa.  Hii imewezekana baada ya Serikali kuongeza bajeti ya mikopo kutoka shilingi bilion 373 hadi kufikia shilingi bilion 483. Wanafunzi walimu wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu ni 22,867, ambapo mwaka huu Serikali itatumia shilingi billion 79.63 kuwagharamia. Na ninyi wenyewe ni mashahidi kuwa hivi sasa mikopo inatolewa kwa wakati; na hata rufaa za mikopo hivi sasa zinashughulikiwa mapema. Wito wangu kwa walimu wanaopata mikopo; wakimaliza, wakubali kufanya kazi kwenye vituo wanavyopangiwa.

Ndugu Wajumbe wa Mkutano;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Mbali na kupanua wigo na kuboresha sekta ya elimu, tunafanya jitihada za kuboresha maslahi na kushughulikia kero mbalimbali za walimu. Hivi punde mmemsikia Kaimu Katibu Mkuu wa CWT akiipongeza Serikali kwa jitihada inazofanya kuboresha maslahi ya walimu na kushughulikia kero mbalimbali zinazowakabili. Mathalan, ameipongeza Serikali kwa kutoa Waraka wa Muundo Mpya wa Watumishi wa Walimu; Upandishwaji madaraja ya Walimu; uanzishaji wa Tume ya Utumishi wa Walimu, n.k.

Lakini, licha ya hatua hizo, Serikali pia imefanya mambo mengine mengi ya kuboresha maslahi na kushughulikia kero za walimu.  Mathalan, awali nilieleza kuwa Serikali iliongeza kiwango cha ruzuku inayopelekwa kwenye shule kutoka shilingi bilioni 18.77 hadi shilingi bilioni 23.868 kwa mwezi. Kiasi kilichoongezeka ni mahususi kwa ajili ya kutoa posho za madaraka kwa Wakuu wa Shule na Waratibu wa Elimu Kata. Tangu utaratibu huu uanze tayari tumetoa shilingi bilioni 86.56. Niwaombe watu wanaopewa, posho hizo ziwaongezee motisha ya kufanya kazi kwa maslahi ya Taifa. Aidha, naziagiza mamlaka za uteuzi kutoa vyeo kwa watu wenye sifa na wenye kustahili.

Sambamba na hilo la kutoa posho, tangu tumeingia madarakani, tumetoa kiasi cha shilingi bilioni 56.92 kulipia madeni ya walimu, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 14.23 tumelipa madeni ya mshahara na shilingi bilioni 42.69 ni madeni yasiyo ya mshahara. Kadri tutakavyokamilisha uhakiki wa madeni, tutalipa madeni yote halali.

Mheshimiwa Kaimu Rais wa CWT,

NduguWajumbe wa Mkutano;

Licha ya jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali katika kuimarisha sekta ya elimu na kuboresha maslahi ya walimu nchini, ni dhahiri kuwa sekta ya elimu na ninyi walimu wenyewe bado mnakabiliwa na matatizo kadhaa. Mathalan, tuna upungufu wa madarasa, vyoo, nyumba za walimu, madawati na maabara.

Sambamba na matatizo hayo, hivi punde, Kaimu Katibu Mkuu wa CWT, katika Risala yake, ameeleza matatizo na kero mbalimbali zenye kuwakabili walimu. Ametaja suala la upandishaji vyeo kwa wakati; suala la walimu waliopandishwa madaraja mwaka jana na kisha kusitishwa; malipo ya walimu wastaafu; suala la posho ya kufundishia (teaching allowance); upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi; n.k. Amezungumzia pia hofu mliyonayo walimu kuhusu uwezekano wa kupungua kwa mafao ya kustaafu kufuatia uamuzi wa kuiunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii ili ibaki miwili.

Kama nilivyotangulia kusema hapo awali, mimi ni mwalimu. Hivyo basi, hata kabla sijawa Rais, nilikuwa nikizifahamu shida na matatizo mbalimbali yanayowakabili walimu wa Tanzania. Na kama nilivyosema, Mke wangu, naye ni mwalimu; na amekuwa kila mara akinikumbusha kuhusu masuala ya walimu. Lakini, mbali na yeye, kwa bahati nzuri viongozi wengi niliowateua kushika nyadhifa mbalimbali ni walimu. Waziri Mkuu ni mwalimu. Mke wake ni mwalimu Hapa pia tunao Mawaziri  Mhagama na Prof. Ndalichako, ambao wote ni walimu. Na wote hawa wamekuwa wakiwatetea sana. Lakini zaidi ya hapo, Makamu wa Rais, Mama Samia, naye ni mtetezi mkubwa sana wa walimu. Kwa hiyo, viongozi wote wamekuwa wakiwatetea sana ninyi walimu.

 Na niseme tu kuwa, kutokana na kazi kubwa ambayo ninyi walimu mnayoifanya, ni haki yenu kutetewa na kwa kweli Serikali inao wajibu wa kuhakikisha inashughulikia shida na kero zenu. Mimi binafsi natamani sana; tena sana, kuona shida mbalimbali za walimu zinaisha kabisa. Hata haya, matatizo mliyonieleza leo ningetamani sana nitoe majibu yake yote hapa hapa ili yaweze kushughulikiwa mara moja. Lakini, hilo ni jambo lisilowezekana. Kama mnavyofahamu, uwezo wa Serikali bado mdogo na majukumu iliyonayo ni mengi. Mbali na kushughulikia sekta ya elimu, tunawajibika kushughulikia masuala ya afya, maji, umeme, barabara, ulinzi, n.k., ambayo yote haya ni muhimu kwa nchi, lakini pia ni muhimu hata kwenu ninyi walimu. Walimu mnahitaji huduma bora za afya, mnahitaji maji, umeme, barabara, ulinzi na usalama, n.k.

Kwa sababu hiyo, Serikali inawajibika kuhakikisha kuwa kidogo kinachopatikana, tunakigawa kwenye sekta zote muhimu. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alipata kusema, nanukuu, “Ndama hunyonya kiwango cha maziwa ambacho mama yake anacho”. Hivyo, nawasihi sana walimu wenzangu, kwa kile kidogo tunachokileta kwenu mkipokee na kuiona dhamira nzuri ya Serikali ya kushughulikia shida na kero zenu mbalimbali. Napenda tu niwahakikishie kuwa Serikali inatambua kero zenu zote na kadri uwezo wa Serikali kifedha utakavyokuwa ukiongezeka, tutaendelea sio tu kuboresha maslahi yenu bali sekta ya elimu kwa ujumla.

Mheshimiwa Kaimu Rais wa CWT,

Ndugu Wajumbe wa Mkutano huu;

Pamoja na maelezo hayo, napenda kutolea ufafanuzi baadhi ya hoja zilizotolewa na Kaimu Katibu Mkuu katika Risala yake. Moja ya hoja aliyoizungumza ni uhaba wa walimu wa sayansi nchini. Ni kweli kuwa tatizo hili lipo na limeongezeka baada ya Serikali kuanza kutoa elimu bila malipo, ambapo idadi ya wanafunzi kwenye shule zetu imeongezeka. Serikali inachukua hatua mbalimbali kushughulikia tatizo hili. Mwaka huu pekee tumeajiri walimu wa masomo ya sayansi na hisabati wapatao 3,462. Aidha, walimu wengine wapatao 15,135, wakiwemo wa sayansi, wanatarajiwa kuajiriwa wakati wowote baada ya vyeti vyao kuhakikiwa na kuthibitishwa uhalali wake.

Vilevile, tunaendelea kupanua wigo wa kuzalisha walimu. Mathalan, kati ya wanafunzi 22,867 wanaosomea ualimu niliowataja awali na ambao Serikali inawapa mikopo ya vyuo vikuu, wanafunzi 13,510 ni wa masomo ya sayansi na hesabu. Zaidi ya hapo, Serikali ipo katika ukarabati wa vyuo vyake takriban 20 na ujenzi wa vyuo 3. Ujenzi na ukarabati huu utakapokamilika, utaongeza idadi ya udahili wa wanafunzi wa ualimu kutoka 20,535 hadi kufikia wanafunzi takriban 30,000. Hatua hizi, bila shaka, zitapunguza tatizo la uhaba wa walimu. 

Hata hivyo, nafahamu kuwa wakati mwingine, tatizo la uhaba wa walimu linatokana na mgawanyo usio linganifu. Shule nyingi za mijini zina walimu wengi kuliko mahitaji yake. Hivyo niziombe Mamlaka husika kuliangalia suala hili kwa umakini. Lakini huu usiwe mwanya wa kuwahamisha walimu bila kufuata utaratibu. Agizo langu kuhusu kutomhamisha mwalimu mpaka atakapolipwa stahiki zake liko pale pale.  Lakini pia nitoe wito kwenu walimu; mkipangiwa kazi mahali, mkubali kwenda.

Suala jingine ambalo Kaimu Katibu Mkuu amelizungumzia ni hofu mliyonayo kuhusu uwezekano wa kupungua kwa malipo ya mkupuo baada ya kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii. Hakuna kitakachopungua. Lengo la Serikali kuiunganisha mifuko ya jamii na kubakisha miwili ni kuongeza ufanisi na tija katika mifuko hiyo.  Kama mnavyofahamu, kutokana na mifuko kuwa mingi, ililazimu kila mfuko kutumia fedha nyingi kutafuta wanachama. Jambo hili liliongeza gharama za uendeshaji kwenye mifuko hiyo na hivyo kusababisha mifuko hiyo kutoa mafao madogo ya kustaafu kwa wanachama wake. Sasa tumeamua kuwa na mifuko miwili tu; mmoja kwa ajili ya watumishi wa umma na mwingine sekta binafsi. Hii itasaidia sio tu kuondoa ushindani usio na tija, bali pia unatarajia kuiwezesha mifuko hii kutoa mafao mazuri zaidi kwa wanachama wake wanaostaafu. Hivyo basi, napenda kuwatoa hofu walimu wenzangu kwamba mafao hayatapungua. Lakini sambamba na hilo, sheria ya kuunganisha mifuko bado haijatungwa. Mswada umesomwa mara moja Bungeni. Na sasa maoni ya wadau mbalimbali yanaendelea kupokelewa. Hivyo, na ninyi CWT mnayo nafasi ya kuendelea kutoa maoni yenu ili kuboresha mswada huo.

Kuhusu suala la posho ya kufundishia (teaching allowance), mtakumbuka kuwa kwa mujibu wa Waraka wa Watumishi wa Serikali Na.1 wa mwaka 1996 kuhusu Mfumo, Miundo na Ngazi Mpya za Mishahara kwa Watumishi wa Serikali kuanzia tarehe 1 Julai, 1996 posho zote zilijumuishwa katika mishahara. Lengo lilikuwa kuboresha mishahara na mafao ya uzeeni ya Watumishi. Kufuatia utekelezaji wa Waraka huo, nyongeza halisi ya mshahara wa kima cha chini baada ya kujumuishwa posho katika mishahara ilikuwa ni asilimia 55.2; na nyongeza halisi ya kima cha juu baada ya kujumuishwa posho katika mshahara ilifikia asilimia 36.9. Hii ndio sababu posho ya kufundishia waliyokuwa wakipewa walimu, iliondolewa. Pamoja na maelezo hayo, natambua umuhimu wa posho hii. Hivyo, napenda kurudia tena kadri mama ndama atakapoongeza maziwa, tutaangalia uwezekano wa kurejesha posho hii ili kuwapa motisha walimu wetu. Hivyo, nawaomba Watanzania tuchape kazi kwa bidii ili kuongeza uwezo wetu kiuchumi.

Kuhusiana na suala la mafunzo kwa walimu, Serikali inafahamu umuhimu wa kuwapatia mafunzo endelevu ya mara kwa mara walimu wetu. Na kwa kweli tumekuwa tukifanya hivyo. Jumla ya walimu 5,920 wa masomo ya sayansi, hisabati na kiingereza wamepata mafunzo hivi karibuni. Na tutaendelea kutoa mafunzo hayo.

Mheshimiwa Kaimu Rais wa CWT,

Ndugu Wajumbe wa Mkutano huu;

Suala jingine ambalo ningependa nilizungumzie ni kuhusu madeni mbalimbali ya walimu. Serikali inatambua uwepo wa madeni hayo. Na tumekuwa tukiyalipa. Kama nilivyosema awali, tangu tumeingia madarakani tayari tumelipa madeni ya walimu yenye thamani ya shilingi bilioni 56.92. Lakini, madeni bado yapo. Hivi punde Kaimu Katibu Mkuu wenu ameeleza kuwa hivi sasa walimu wanaidai Serikali kiasi cha shilingi bilioni 25.6. Napenda, kwanza kabisa, kuwapongeza viongozi wa CWT kwa kuwa wakweli. Nakumbuka kuwa kuna wakati aliwahi kujitokeza mmoja wa viongozi wa CWT na kusema kuwa walimu wanaidai Serikali takriban shilingi trilioni 1.5.  Hivyo, nawapongeza sana viongozi wa sasa wa CWT kwa kuwa wakweli. Na kwa kuwa mmeonesha uungwana na mmekuwa wakweli, napenda kuwahakikishia kuwa mara tu tutakapomaliza kuhakiki deni hili, tutawalipa mara moja.

 

Lakini pia ningependa kutumia fursa hii kueleza kuwa, Serikali imekuwa ikichelewa kulipa madeni yenu pamoja na ya watumishi wengine wa umma, kutokana na kuwepo kwa matatizo kadhaa, ikiwemo tatizo la watumishi hewa na wenye vyeti feki. Hii ndio sababu mwaka jana tuliamua kusitisha zoezi la upandishaji vyeo na madaraja kwa watumishi; na tukaanzisha zoezi la uhakiki kwa watumishi wote wa Serikali. Zoezi la uhakiki mpaka sasa limetuwezesha kubaini watumishi hewa wapatao 19,706, ambao walikuwa wakiigharimu Serikali kiasi cha shilingi bilioni 19.848 kwa mwezi, sawa na shilingi bilioni 238.17 kwa mwaka. Aidha, tumeweza kubaini watumishi wenye vyeti feki wapatao 12,000, wakiwemo walimu 3,655. Baada ya kukamilisha zoezi hili, Serikali mwezi Novemba 2017, imewapandishaji vyeo watumishi 59,967, wakiwemo walimu na ambao marekebisho ya mishahara yao itaanza kutolewa kuanzia mwezi huu. Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 159.33 kwenye bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya marekebisho hayo ya mishahara.

 

Na kuhusu zoezi la uhakiki wa madeni, lenyewe bado linaendelea. Na kimsingi, zoezi hili ni endelevu. Hata hivyo, nawahakikishia kuwa kadri tutakavyokuwa tunakamilisha uhakiki wa madeni tunayodaiwa, tutayalipa. Wito wangu kwenu walimu wenzangu, endapo unafahamu kuwa katika madeni uliyowasilisha Serikalini kuna udanganyifu, ni vyema ujaze upya. Na niwaombe viongozi wa CWT kupitia tena madeni yote ya walimu ili kujiridhisha; na mkijiridhisha pelekeni madeni hayo kwa viongozi wa Wilaya na Mikoa, nao wakijiridhisha na kuweka saini zao; baada ya hapo madeni hayo yawasilishwe kwa Waziri Mkuu. Nawaahidi kuwa, Serikali ikijiridhisha kuwa madeni hayo ni sahihi, tutayalipa mara moja. Lakini nitoe onyo kwamba, endapo itatokea mtu ameidhinisha madeni yenye udanganyifu, naye tutawachukulia hatua.

Kuhusiana na hoja zenu nyingine mlizoziwasilisha, ikiwemo upandishaji wa vyeo kwa wakati; Serikali kutoa mikopo ya ujenzi wa nyumba isiyo na riba; uhaba wa vifaa vya kufundishia; kushirikishwa katika mabadiliko yoyote ya mitaala; masomo ya TEHAMA; Serikali imepokea hoja zenu zote na tutashirikiana nanyi katika kuzitafutia ufumbuzi. Nafahamu baadhi ni masuala ya kiutendaji tu na hayahitaji gharama yoyote; hivyo, naziagiza mamlaka husika kushughulikia kwa haraka. Na kwa yale yenye kuhitaji fedha, tutaendelea kuyashughulikia taratibu, kadri uwezo wa Serikali kifedha utakavyokuwa ukiimarika.

 

 

Waheshimiwa Viongozi;

Mheshimiwa Kaimu Rais wa CWT,

Ndugu Wajumbe wa Mkutano;

Jukumu langu leo ni kufungua tu Mkutano wenu. Lakini kabla sijatekeleza suala hili, ninalo suala moja la mwisho ambalo ningependa kulizungumza. Nafahamu kuwa, kwenye Mkutano huu, pamoja na mambo mengine, mtafanya uchaguzi wa Rais wa CWT kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Rais wenu Mstaafu, Mwalimu Gratian Mukoba. Napenda kutumia fursa hii kuwasihi sana walimu wenzangu, kuchagua kwa umakini mkubwa. Chagueni mtu atakayeshughulikia masuala yenu. Na kamwe msichague mtu mwenye nia ya kuitumia CWT kutekeleza maslahi yake binafsi.

Sio siri kuwa kuna wakati mliwachagua watu ili wawaongoze na kuwatumikia, lakini hawakufaya hivyo. Badala yake, walitumia Chama hiki kutekeleza maslahi yao binafsi. Na walitumia Chama chenu kujinufaisha. Niwaulize walimu wenzangu, hivi mnafahamu fedha za michango mnazokatwa kila mwezi zinatumikaje? Au mmeshawahi kujiuliza kuhusu utendaji kazi wa Benki yenu na ni namna gani inawanufaisha? Sina hakika kama mnafahamu. Lakini niwaambie, kwa taarifa nilizonazo, Benki yenu haifanyi vizuri, na ni miongoni mwa Benki ambazo wakati wowote inaweza kufungwa. Nakumbuka wakati fulani nilialikwa kwenda kuizindua lakini sikwenda, baada ya kujiridhisha kuwa Benki hiyo haifanyi vizuri na haipo kwa maslahi ya walimu. Ni watu wachache tu ndio wananufaika nayo. Hivyo basi, nawasihi tena walimu wenzangu, katika uchaguzi huu, msichague watu wenye nia ya kujinufaisha kupitia CWT.

Lakini zaidi ya hapo, msiwachague watoa rushwa. Rushwa ni ugonjwa. Ni kansa. Ukimchagua mtoa rushwa hutoweza kamwe kumuuliza michango yenu ya kila mwezi inatumikaje; na utashindwa kumuuliza manufaa yaliyopatikana kwenye Benki yenu. Hivyo basi, narudia tena kuwasihi walimu wenzangu katika uchaguzi huu chagueni vizuri. Chagueni watu watakaowatetea na kuwasemea matatizo yenu. Na kamwe msimchague mtu ambaye lengo lake ni kuigombanisha CWT na Serikali. Mapambano mara nyingi hayajengi. Na niwashauri walimu wenzangu, wakati mwingine, mkitaka kufanikisha jambo, tumieni ule usemi usemao, “If you want to win an enemy, join him and work with him…” Siwapigii kampeni; lakini kwa dhati kabisa nawapongeza viongozi wa sasa wa CWT kwa kuonesha nia ya kweli ya kuwatetea na kushughulia shida za walimu. Wameonesha kuwa wapo tofauti na wapo tayari kufanya kazi na Serikali. Huo ndio unapaswa kuwa muelekeo wa CWT hivi sasa. Mimi naamini kuwa kama Serikali na CWT tukiwa kitu kimoja tutaweza kushughulikia matatizo mengi yanayowakabili walimu tena kwa haraka.

 

 

 

 

Mheshimiwa Kaimu Rais wa CWT,

Waheshimiwa Viongozi mliopo;

Ndugu Wajumbe wa Mkutano;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kuushukuru tena uongozi wa CWT kwa kunikaribisha kufungua Mkutano huu. Aidha, kwa namna ya pekee, naushukuru uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kukubali kuwa wenyeji wa Mkutano huu. Tunawashukuru sana na tunawashukuru pia walimu wanafunzi wa Chuo hiki kwa kujitokeza kwenu kwa wingi kwenye ufunguzi wa Mkutano wa CWT.

Halikadhalika, nawashukuru viongozi wa vyama vya wafanyakazi kwa kuhudhuria kwenye Mkutano huu. Na vilevile, nawashukuru wageni wote waalikwa kutoka ndani na nje kwa kuamua kutenga muda wenu kuja kushiriki kwenye Mkutano huu. Mwisho lakini sio kwa umuhimu, wajumbe wa Mkutano huu, na nawaomba mfikishe salamu kwa walimu wote nchini kuwa Serikali ipo pamoja nao.

Baada ya kusema hayo, sasa natamka rasmi kuwa nimeufungua Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa CWT. Nawatakia Mkutano mwema.

Mungu Ibariki CWT!

Mungu Wabariki Walimu Wote!

Mungu Ibariki Tanzania!

“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”