Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE UFUNGUZI WA HOSPITALI YA TAALUMA NA TIBA YA CHUO KIKUU CHA AFYA NA SAYANSI SHIRIKISHI MUHIMBILI KATIKA KAMPASI YA MLOGANZILA, TAREHE 25 NOVEMBA, 2017

Saturday 25th November 2017

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais

wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais

Mstaafu pamoja na Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda,

Waziri Mkuu Mstaafu;

 

Mheshimiwa Anna Makinda, Spika Mstaafu wa Bunge

         la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu,

Sayansi na Teknolojia;

 

Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya,

Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto;

 

Mheshimiwa Seleman Said Jafo, Waziri wa Nchi,

Ofisi ya Rais - TAMISEMI

 

Mheshimiwa Song Geum Yong, Balozi wa Jamhuri

ya Korea ya Kusini;

 

Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani; 

Waheshimiwa Wabunge mliopo;

Waheshimiwa Makatibu Wakuu mliopo;

 

Prof. Apolinary Kamuhabwa, Makamu Mkuu wa Chuo cha Afya

         na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili;

 

Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi

za Kimataifa mliopo;

 

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Maprofesa pamoja na

Wana-Jumuiya wote wa Chuo Kikuu cha Afya na

Sayansi Shirikishi Muhimbili;

 

Viongozi wengine wa Serikali, Vyama vya Siasa

pamoja na Viongozi wa Dini mliopo;

 

Ndugu Wananchi wa Mloganzila na maeneo jirani;

Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana:

 

Napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa uzima na kutuwezesha kukutana hapa leo. Aidha, namshukuru Mkuu wa Chuo, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi, pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, kwa kunialika kwenye tukio hili la ufunguzi wa Hospitali hii ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili, hapa Mloganzila. Hili ni tukio muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu; hivyo basi, ninawashukuru sana kwa kunialika.

 

Napenda pia kutumia fursa hii kuwashukuru Wana-Jumuiya wa Hospitali hii pamoja na wananchi wa hapa Mloganzila na maeneo jirani, kwanza, kwa kujitokeza kwenu kwa wingi kushuhudia tukio hili. Lakini pili, kwa mapokezi yenu mazuri.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Afya njema ni msingi mkubwa wa maendeleo katika Taifa. Nchi ambayo wananchi wake hawana afya njema kamwe haiwezi kupata maendeleo. Hii ni kwa sababu mwananchi asiye na afya njema hawezi kushiriki kwenye shughuli za ujenzi wa Taifa, kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi, biashara, lakini pia kufanya kazi ofisini, viwandani, migodini, n.k.; na kama atashiriki, basi mchango wake utakuwa mdogo sana.

 

Hii, bila shaka, ndio sababu Awamu zote za Uongozi wa nchi yetu, kuanzia Awamu ya Kwanza hadi sasa, zimekuwa zikiweka mkazo mkubwa katika kuboresha huduma za afya hapa nchini. Na mimi leo nafurahi kuja hapa Mloganzila kufungua Hospitali hii ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili. Kama ambavyo mmesikia, Hospitali hii, ambayo ilianza kujengwa mwezi Machi 2014 na kukamilika mwezi Agosti 2016, ni kubwa na pia ya kisasa. Ina uwezo wa kulaza wagonjwa 571 na kuhudumia wagonjwa wengine wa nje. Ujenzi wake pamoja na vifaa umegharimu takriban Dola za Marekani milioni 94.5, sawa na Shilingi za Tanzania bilioni 206.7.  Kati ya fedha hizo, Serikali yetu ilitoa Dola za Marekani milioni 18 sawa na takriban shilingi bilioni 39.4; na kiasi kingine, Dola za Marekani 76.5, sawa na takriban shilingi bilioni 167.3 ni mkopo wa masharti nafuu kutoka kwa marafiki zetu wa Korea Kusini.

 

Napenda kutumia fursa hii, kuishukuru sana Serikali ya Korea Kusini kwa kutupatia mkopo wa masharti nafuu uliotuwezesha kujenga hospitali hii. Korea Kusini ni marafiki zetu. Wametekeleza miradi mbalimbali nchini. Aidha, hivi karibu, Serikali ya Korea inatarajia kufadhili  ujenzi wa Daraja la kupita Juu ya Bahari kutoka Aga Khan hadi ufukwe wa Coco Beach umbali wa takriban kilometa 7.1. Kama hiyo haitoshi, kampuni kutoka Korea Kusini itaanza ujenzi wa meli kwa ajili ya kutoa huduma kwenye Ziwa Victoria. Hivyo, tunawashukuru sana marafiki kwa kukuza ushirikiano. Na nimefurahi Balozi wa Korea Kusini, Mheshimiwa Song Yong yupo hapa. Tafadhali, naomba sana utufikishie shukrani zetu nyingi kwa Serikali pamoja na wananchi wa Korea Kusini. Lakini niseme tu kwamba katika kukuza na kuimarisha zaidi uhusiano wetu na Korea Kusini na sisi tumefungua Ubalozi nchini humo hivi karibuni.

 

Sambamba na kuishukuru Serikali ya Korea kwa ufadhili wao, napenda, kwa namna ya pekee kabisa, kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Awamu wa Nne kwa kuridhia kuanza kwa ujenzi wa Hospitali hii wakati wa uongozi wake. Mimi nataka niwaeleze ukweli, bila Rais mstaafu Kikwete, Hospitali hii isingejengwa. Yeye ndio aliyeasisi wazo la kujengwa kwa Hospitali hii. Sisi wengine tulikuwa tunatekeleza maelekezo yake. Nakumbuka nikiwa Waziri wa Ardhi alinipa maelekezo ya kufuatilia upatikanaji wa eneo hili. Aidha, nikiwa Waziri wa Ujenzi aliniagiza kujenga barabara ya kuja hadi hapa. Nafurahi niliweza kutekeleza maelekezo yake. Eneo hili lenye ukubwa wa ekari 3,800 lilipatikana na barabara ilijengwa na kukamilika. Lakini, nasema kwa dhati kabisa kuwa, sifa zote kuhusiana na ujenzi wa Hospitali hii ziende kwa Mheshimiwa Kikwete. Napenda pia kuwashukuru na kuwapongeza Mkandarasi, Kampuni ya Kolon Global Corporation ya Korea Kusini, pamoja na Wasimamizi wa mradi kwa kukamilisha ujenzi wa Hospitali hii.

 

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Kama ambavyo Mheshimiwa Ndalichako ameeleza, Hospitali imejengwa kwa madhumuni makubwa matatu. Kwanza, kufundishia wataalam wa masuala ya afya kwa ngazi ya stashahada, shahada, pamoja na shahada za uzamili na uzamivu. Pili, kutoa huduma za afya za kibingwa kwa magonjwa mbalimbali. Na tatu, kufanya tafiti kuhusu namna ya kuboresha tiba na huduma za kinga. Hospitali tayari imekamilika, hivyo, hatua inayofuata sasa ni kuanza ujenzi wa miundombinu ya kufundishia, hususan kumbi za mihadhara (lecture halls), maktaba, maabara, hosteli na cafeteria.   

 

Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali imedhamiria kwa dhati kuhakikisha miundombinu hiyo inajengwa ili kuifanya Hospitali hii itekeleze majukumu yake ipasavyo. Nimeambiwa kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo utagharimu shilingi bilioni 13.32. Na kama alivyosema Mheshimiwa Waziri Ndalichako tayari Mkandarasi, Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA), amelipwa malipo ya awali kiasi cha shilingi bilioni 3.9. Hivyo, natoa wito TBA kuanza mara moja ujenzi wa mradi miundombinu inayohitajika ili kukiwezesha Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili kudahili wanafunzi wengi zaidi, kutoka 3,000 wa sasa hadi kufikia 15,000; na hivyo kupunguza tatizo la uhaba wa watumishi wa afya katika hospitali zetu.

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Kukamilishwa na kufunguliwa rasmi kwa Hospitali hii ya Mloganzila ni sehemu tu ya jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano za kuboresha huduma za afya hapa nchini. Tangu tumeingia madarakani miaka miwili iliyopita, tumejenga na kuboresha miundombinu mbalimbali kwa ajili ya kutoa huduma za afya. Tumejenga vituo vipya vya kutoa huduma za afya vipatavyo 268 na hivyo kufanya nchi yetu kuwa na vituo vya kutoa huduma za afya vipatavyo 7,284. Vituo vingine vya kutoa huduma za afya vinaendelea kujengwa sehemu mbalimbali nchini, ikiwemo ujenzi wa Hospitali za Mikoa mipya ya Njombe, Geita, Katavi na Simiyu. Sambamba na ujenzi wa vituo hivyo vipya, hivi sasa tunaviboresha vituo vya afya 170 kwa gharama ya shilingi bilioni 161.9 ili kuviwezesha kutoa huduma ya uzazi wa dharura. Lengo la uboreshaji huu ni kupunguza vifo vya mama na mtoto kutoka wastani wa vifo 556 katika kila vizazi hai 100,000 vya sasa hadi kufikia angalau vifo 292 mwaka 2020. Tumekamilisha pia ujenzi wa nyumba 220 kwa ajili ya watumishi wa afya.

 

 Mbali na ujenzi wa miundombinu, tumeendelea na uimarishaji wa huduma za kibingwa kwenye Hospitali zetu za Rufaa za Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Taasisi ya Mifupa (MOI), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (na napenda nimhakikishie Mheshimiwa Waziri wa Afya kuwa tutampatia fedha kwa ajili ya kununua Scan aliyoomba)  pamoja na hospitali za rufaa za Bugando, Mbeya na KCMC. Uboreshaji huu ni pamoja kuanzisha huduma za kupandikiza vifaa vya kuongeza usikivu (cochlea implant). Tumeziongezea pia vifaa, vifaa tiba na vitendanishi. Mathalan, kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tumeongeza vitanda vya ICU kutoka 21 hadi kufikia 75, na vitanda kwa ajili ya wagonjwa wa kusafisha figo vimeongezeka kutoka 27 hadi 42. Tumeongeza pia vyumba vya upasuaji kutoka 13 hadi kufikia 20. Kwa upande wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road tumeiongezea vifaa na vitanda vya wagonjwa kutoka 40 hadi 100; wakati Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete hivi sasa ina uwezo wa kufanya upasuaji wa wagonjwa watatu kwa siku kutoka mmoja hapo awali.

 

Sambamba na hatua hizo, Serikali imeongeza bajeti ya dawa na vifaa tiba, kutoka shilingi bilioni 31 kwenye Mwaka wa Fedha 2015/2016 hadi kufikia shilingi bilioni 251 mwaka 2016/2017; na Mwaka huu wa Fedha Serikali imetenga shilingi bilioni 269 kwa ajili hiyo. Matokeo yake upatikanaji wa dawa muhimu katika Bohari Kuu ya Dawa na vituo vya Serikali vya kutoa huduma za afya umeongezeka. Jambo la kutia moyo zaidi ni kwamba bei ya dawa na vifaa nayo imeanza kupungua, hususan kufuatia uamuzi wa Serikali wa kuanza kununua moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji badala ya kupitia kwa madalali. Mathalan, bei ya dawa ya chanjo ya homa ya ini (hepatitis B Vaccine) imepungua kutoka shilingi 22,000 hadi shilingi 5,300; dawa ya kupambana na maambukizi ya bacteria (Amoxicillin/clavulanic Acid Potassium 625 mg) yenye vidonge 15 bei yake imepungua kutoka shilingi 9,800 hadi shilingi 4,000. Aidha, bei ya shuka za hospitalini imepungua kutoka shilingi 22,200 hadi shilingi 11,100. Hii ni mifano michache tu.

 

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Licha ya hatua tunazozichukua, na ambazo zinatia moyo, natambua kuwa bado sekta yetu ya afya inakabiliwa na matatizo kadhaa. Moja ya matatizo hayo, ni uhaba wa watumishi wa afya. Na tatizo hili kimsingi lina sura kubwa mbili. Sura ya kwanza, ni uhaba wa watumishi wenyewe. Nchi yetu bado ina mahitaji makubwa ya watumishi wa afya. Tulionao ni 89,842 kati ya 184,901 wanaohitajika.  Hivyo, tuna upungufu wa watumishi wa afya takriban 95,059. Serikali inalifahamu hili ndio maana tayari tumetoa vibali vya ajira zipatazo 3,410 (madaktari 258 na wataalam wa kada mbalimbali za afya 3,152) ili kupunguza pengo la watumishi wa afya lililopo, na hasa baada ya kuondolewa watumishi wenye vyeti vya kughushi. Aidha, tumevifanyia ukarabati na upanuzi vyuo vyetu vya uuguzi na ukunga vya Nzega, Mirembe, Mtwara na Tanga pamoja vyuo vya maafisa tabibu Musoma na Mpanda. Matokeo yake udahili wa wanafunzi wa afya imeongezeka hadi kufikia 13,632 na hivyo kuvuka lengo lililowekwa la kudahili wanafunzi 10,000 ifikapo mwaka 2017. Aidha, hivi sasa Serikali inatoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 54.26 kwa wanafunzi wanaosomea masuala ya afya wapatao 10,189. Lakini sio kwamba tunataka kuongeza idadi tu. Hapana. Tunahimiza pia ubora wa wataalam wanaozalishwa kwenye vyuo vyetu. Hii ndio sababu Serikali iliamua kuvisimamisha baadhi ya vyuo kudahili wanafunzi kwa mwaka huu baada ya kujiridhisha kuwa havina uwezo.

 

Sura ya pili ya tatizo la uhaba wa watumishi wa afya hapa nchini, linatokana na mgawanyo usio mzuri wa watumishi wenyewe. Mathalan, nimeambiwa kuwa takriban asilimia 60 ya madaktari wote nchini, wapo hapa Dar es Salaam. Na ni asilimia 40 tu ndio wapo Mikoani. Nafahamu kuwa tatizo hili linasababishwa na mambo mengi, ikiwa ni pamoja na hospitali nyingi kubwa kuwepo hapa Dar es Salaam lakini kuwepo na mazingira mazuri ya kufanyia kazi. Hata hivyo, natambua pia kuwa suala la Wizara ya Afya kusimamia Hospitali za Kibingwa na Maalum pekee, na hospitali nyingine kuanzia ngazi ya mkoa kuwa chini ya TAMISEMI nalo linachangia kuwepo kwa mgawanyo usiowiana wa madaktari kati ya hapa Dar es Salaam na Mikoani; na halikadhalika kati ya Hospitali za Kibingwa na zisiso za Kibingwa.

 

Napenda nitoe mifano michache. Hospitali ya Taifa ya Muhimbili yenye takriban vitanda 1,600, ina jumla ya madaktari bingwa, madaktari wanafunzi na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Muhimbili wapatao 532. Hii maana yake ni kwamba kila daktari anahudumia vitanda vitatu.  Lakini katika Mkoa wa Tabora daktari 1 alikuwa akihudumia wagonjwa 208,329, kwa mujibu wa Sensa ya Mwaka 2012. Mfano mwingine ni wa hapa hapa Dar es Salaam. Hospitali ya Manispaa ya Temeke yenye kuhudumia wastani wa wajawazito wanaojifungua 100 kwa siku ina madaktari bingwa wa akinamama wawili. Lakini Hospitali ya Taifa ya Muhimbili yenye kuhudumia wastani wa akinamama wanaojifungua kati ya 40 hadi 50 kwa siku, ina madaktari bingwa 40; ukiachilia mbali madaktari wanafunzi waliopo. Hii inadhihirisha kuwa hakuna mgawanyo mzuri wa madaktari wachache tulionao. Ni kweli, tunahitaji kuwa na madaktari bingwa wengi katika hospitali zetu. Lakini, haina maana kuwa na madaktari wengi kwenye Hospitali za Kibingwa wakati hospitali nyingine za kawaida, zenye kuhudumia watu wengi, hazina madaktari. Tukiruhusu hali hii kuendelea, wananchi wengi wataendelea kukosa huduma za afya; na hata wakipewa rufaa kwenda hospitali za rufaa au kibingwa wanakuwa tayari wamechelewa na watashindwa kutibika.

 

Hivyo, niziombe Mamlaka husika kulitafakari suala hili kwa kina, ikiwezekana, kuangalia uwezekano wa Hospitali za Mikoa nazo ziwe chini ya Wizara ya Afya. TAMISEMI ibaki kusimamia hospitali za Wilaya, vituo vya afya na zahanati. Nina imani kuwa hii itasaidia kuboresha huduma katika Hospitali za Rufaa za Mikoa na hivyo kuipunguzia mzigo Hospitali  ya Taifa ya Muhimbili. Lakini, sambamba na hilo, niwaombe madaktari nao kuwa wazalendo pindi wakipangiwa kwenda kufanya kazi Mikoani na Wilayani. Serikali imeanza kuboresha maslahi ya watumishi wa afya wanaofanya kazi kwenye Hospitali za Mikoa na Wilaya, ambapo, mathalan, katika Hospitali za Rufaa za Mikoa, daktari bingwa alikuwa akilipwa shilingi 2,000 kwa ajili ya kumuona mgonjwa ambaye ni mwanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima, lakini sasa analipwa shilingi 15,000. Daktari wa kawaida alikuwa akilipwa shilingi 2,000 lakini sasa analipwa shilingi 7,000. Katika Hospitali za Wilaya, daktari alikuwa akilipwa shilingi 1,000 lakini sasa analipwa shilingi 7,000. Tumefanya hivyo ili kuwavutia madaktari kwenda kufanya kazi katika Hospitali za Mikoa na Wilaya nchini.

 

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Ukiachilia mbali suala la uhaba wa watumishi wa afya, nchi yetu bado ina upungufu wa miundombinu ya kutolea huduma za afya, hususan zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, nyumba za watumishi, n.k. Kama nilivyoeleza hapo awali, Serikali inaendelea na jitihada za kujenga miundombinu hiyo. Lakini nawakaribisha watu binafsi, makampuni na mashirika ya dini kuendelea kuunga mkono jitihada hizo. 

 

Tatizo la tatu ambalo mimi naliona lenye kuikabili sekta yetu ya afya ni kukosekana kwa viwanda vya kuzalisha madawa hapa nchini. Dawa nyingi tunaagiza kutoka nje kwa gharama za juu. Kama tungekuwa na viwanda vingi vya kuzalisha dawa hapa nchini, nina uhakika bei ya dawa ingekuwa chini zaidi na hospitali zetu zingekuwa na dawa za kutosha. Hivyo basi, napenda kurudia wito wangu kwa wafanyabiashara, makampuni na mashirika mbalimbali kuwekeza kwenye viwanda vya madawa na vifaa tiba hapa nchini. Soko lipo, tena ni kubwa. Mmesikia kuwa tumeongeza bajeti ya dawa, lakini pia washirika wetu mbalimbali wameendelea kutufadhili kwa kutupatia fedha za kununulia dawa. Mathalan, Global Fund wametupatia takriban Dola za Marekani milioni 300 kwa ajili hiyo. Lakini sambamba na hayo, mnafahamu kuwa sisi ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ambazo zina takriban nchi 18. Kama hiyo haitoshi, hivi karibuni taasisi yetu ya Bohari Kuu ya Madawa imekabidhiwa jukumu la kununua dawa kwa niaba ya nchi zote za SADC. Hivyo, soko lipo. Kilichobaki ni kwa wafanyabiashara na wataalam wetu kujipanga vizuri katika kutumia fursa hiyo ya kuwa na soko kubwa la dawa. Nimefurahi kusikia kuwa Hospitali hii ya Mloganzila imetenga eneo mahususi kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya dawa. Na nina imani mtakuwa mmetenga pia eneo maalum kwa ajili ya kulima mimea mbalimbali kwa ajili ya kufanya utafiti wa madawa, ambayo yalikuwa ndio mawazo ya Mzee Kikwete. Napenda pia kutumia fursa hii kuushauri Mfuko wa Bima ya Afya kujielekeza katika mwelekeo huo wa ujenzi wa viwanda vya madawa.

 

Tatizo jingine ambalo naliona ni wananchi wetu wengi kushindwa kujiunga na Mifuko ya Bima ya Afya. Kama mnavyofahamu, gharama za afya huwa ni kubwa na ugonjwa mara nyingi hutokea bila kutarajia. Hali hii inafanya wananchi wengi kushindwa kumudu gharama za matibabu, licha ya kwamba Serikali imejitahidi sana kupunguza gharama za matibabu. Mifuko ya Bima ya Afya (NHIF na CHF) ina nafasi kubwa ya kuwasaidia wananchi kupunguza gharama za matibabu. Lakini kwa bahati mbaya, idadi ya wananchi waliojiunga na mifuko hii ni ndogo. Hivyo basi, nitumie fursa hii kuwaomba wananchi kote nchini kujiunga na Mifuko ya Bima ya Afya ili iwasaidie pindi wanapokumbwa na magonjwa au kuuguliwa na ndugu au jamaa. Gharama za kujiunga na mifuko ya bima ya afya sio kubwa, ni ndogo.

 

 

 

 

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Nimeeleza masuala mengi. Lakini kabla sijahitimisha hotuba yangu, ninayo masuala mengine madogo ya kueleza. Jambo la kwanza, ni kuhusu utunzaji wa miundombinu hii. Kama mlivyosikia, ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa vifaa kwa ajili ya Hospitali hii hapa Mloganzila umegharimu fedha nyingi. Hivyo basi, nawasihi sana wafanyakazi na watumishi wa hapa muitunze. Na niziombe mamlaka husika za hospitali zote nchini kuhakikisha vifaa kwenye Hospitali za Serikali vinatunzwa. Kitunze kidumu.

 

Jambo la pili linaihusu Hospitali hii. Hospitali hii inakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo uhaba wa watumishi. Wanaohitajika ni takriban 950, lakini waliopo ni wachache kutokana na vibali vichache vya ajira na uhaba wa watumishi wenyewe wa afya. Hata hivyo, kwa taarifa nilizonazo ni kuwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ukijumuisha Taasisi ya Moi pamoja na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, ina takriban vitanda 1,940. Aidha, madaktari na watumishi kwa pamoja idadi yao inafikia 3,812. Wodi ya Mwaisela peke yake ina vitanda 244 na kuhudumia wagonjwa wa nje wapatao 400. Wodi hii pia imekuwa ikihudumiwa na madaktari bingwa wapatao 75, wakisaidiwa na madaktari wanafunzi takriban 20 na wauguzi wapatao 69. Lakini, kama nilivyosema, Hospitali hii ya Mloganzila ina vitanda 571, ambavyo havina wagonjwa na inakabiliwa na changamoto ya watumishi.

 

Nimekuwa nikijiuliza kama Hospitali ya Taifa ya Muhimbili yenye kukabiliwa na ufinyu wa nafasi za kulaza wagonjwa ina watumishi wengi kama nilivyoeleza, kwanini basi tusiwahamishe baadhi ya madaktari na wagonjwa kutoka Muhimbili kuja hapa, na hivyo kuweza kupiga ndege wawili kwa jiwe moja. Kwanza, kupunguza uhaba wa watumishi katika Hospitali hii ya Mloganzila. Na pili kupunguza mrundikano wa wagojwa kwenye Hospitali yetu ya Taifa ya Muhimbili. Vilevile, Hospitali hii itaweza kuhudumia watu wengi zaidi kuliko sasa na wanafunzi pia wataweza kujifunza vizuri zaidi. Halikadhalika, tutaipunguzia Serikali gharama kwa vile watumishi watakaohamishiwa hapa kutoka Muhimbili tayari ni waajiriwa wa Serikali; na kwa kuwa Hospitali hii ipo hapa Dar es Salaam hata gharama za uhamisho hazitakuwepo. Hivyo basi, nitoe wito kwa wahusika wote, hususan Wizara ya Elimu na Chuo cha Muhimbili, Wizara ya Afya na Hospitali ya Muhimbili, Taasisi za Moi na ya Moyo ya Jakaya Kikwete pamoja na wahusika wengine, kukutana na kulitafakari suala hili vizuri ili uwekezaji huu ulete manufaa yaliyokusudiwa.

 

Suala jingine lenye kufanana na hili nililotoka kulizungumzia ni kuhusu ushirikiano miongoni mwa taasisi zenye kusimamia Hospitali hii. Kama nilivyoeleza hapo awali, Hospitali hii ina jukumu la kufundisha wataalam wa afya na pia kutoa huduma za afya, hususan za kibingwa kwa wananchi. Inafahamika kuwa jukumu la kusimamia sekta ya afya lipo Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu inashughulikia sekta ya elimu. Kwa maana hiyo, ili Hospitali hii iweze kutekeleza majukumu yake yote mawili ipasavyo ni lazima Wizara hizi mbili pamoja na watendaji wake zifanye kazi kwa karibu na kwa ushirikiano. Nimefurahi kusikia kuwa Waheshimiwa Mawaziri wa Afya na Elimu wanashirikiana; japo sina hakika kama hali iko hivyo hadi kwa watendaji wao. Endapo hapatakuwa na ushirikiano, upo uwezekano wa Hospitali hii kushindwa kutekeleza majukumu yake, ikajikita kwenye jukumu moja, mathalan la kufundisha wataalam na kuacha jukumu la kutoa huduma za afya kutokana na ama utashi wa viongozi wa Hospitali wenyewe au kwa kukosa bajeti ya kutoa huduma ya afya kutoka Wizara ya Afya. Hivyo basi, natoa changamoto kwa wahusika wote kuhakikisha washirikiana ili Hospitali hii itekeleze majukumu yake yote mawili ipasavyo; jukumu la kufundisha wataalam na jukumu la kutoa huduma za afya kwa wananchi. Wizara ya Elimu itoe bajeti ya kufundishia kwa Hospitali hii Wizara ya Afya itenge bajeti itakayoiwezesha Hospitali hii kutoa huduma za afya kwa wananchi, kwa sababu wao ndio wenye jukumu la kusimamia sekta ya afya. Huu ndio wito wangu kwa mamlaka zenye kusimamia Hospitali hii.

 

Suala la tatu linahusu ulipaji wa fidia kwa wananchi waliokuwa wakiishi katika eneo hili. Historia ya eneo hili ipo wazi. Kabla ya kumilikishwa kwenye Hospitali hii, eneo hili, tangu mwaka 1946 lilikuwa chini ya milki ya Serikali, kupitia kwanza Tanganyika Packers na baadaye Kampuni ya Biashara ya Mifugo Tanzania (KABIMITA) chini ya Wizara ya Maji na Maendeleo ya Mifugo. Eneo hili lilitumika kwa ajili ya kufuga, kutunza na kunenepesha mifugo (holding ground) kabla ya kuuzwa au kuchinjwa. Wakati huo hapakuwa na wananchi waliokuwa wakiishi. Baada ya KABIMITA kuacha kulitumia, wananchi walianza kuishi na kuliendeleza, na hatimaye likasajiliwa vijiji vya ujamaa vya Kwembe (1980) na Mloganzila (1993); lakini umilki ardhi ulibaki kuwa Serikalini ndio maana tulipotaka kujenga Hospitali hii, hatukupata taabu kulichukua. Hata hivyo, kwa busara na huruma ya Serikali iliamua kuwa wananchi waliokuwa wakiishi hapa walipwe fidia ya mandelezo waliyoyafanya. Kiasi cha takriban shilingi bilioni 8.07 kililipwa kwa watu 1,919 waliofanyiwa tathmini kati ya mwaka 2008 – 2010. Aidha, mwaka 2011 Serikali iliwalipa fidia wananchi wengine 619 kiasi cha shilingi bilioni 1.61. Hivyo basi, nitumie fursa hii kusema kuwa Serikali haitalipa tena fidia kwenye eneo hili. Na wala wasipite watu kuwadanganya kuwa kuna fidia nyingine. Kama nilivyosema, fidia tayari ilishalipwa.   Lakini nafahamu kuwa wapo wakazi wawili waligomea malipo yao, lakini hundi zao zipo; wakati wowote wakiwa tayari wanaweza kuzifuata kwenye Wizara husika. Fidia iliyotolewa ni kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi yetu.

 

 

 

 

Mheshimiwa Rais Mstaafu Mzee Mwinyi;

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Napenda kuhitimisha kwa kuwashukuru tena viongozi wa Hospitali hii pamoja na Wizara husika kwa kunikaribisha kwenye shughuli hii. Nawashukuru pia Mheshimiwa Makamu wa Rais Mstaafu, Dkt. Bilal pamoja na Waziri Mkuu Mstaafu Mzee Mizengo Pinda, ambao kwa kushirikiana na Rais Mstaafu Mzee Kikwete walifanikisha ujenzi wa Hospitali. Aidha, namshukuru pia Mheshimiwa Mama Anna Makinda, Spika Mstaafu ambaye Bunge aliloliongoza ndilo lilipitisha bajeti ya kujenga Hospitali hii. Na narudia tena kuishukuru Serikali ya Korea Kusini ambao walitupatia mkopo wa ujenzi wa Hospitali hii ya kisasa; pamoja na wengine wote waliofanikisha. Napenda kuwahakikishia viongozi wa Hospitali hii pamoja na wananchi kwa ujumla kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kufanya kila jitihada kuhakikisha hospitali hii ya kisasa inakuwa bora sio tu hapa nchini bali Barani Afrika.

 

La mwisho kabisa, hususan kwa wananchi wa maeneo haya, hivi karibuni Serikali imeanza maandalizi kwa ajili ya ujenzi wa barabara kutoka Ubungo hadi Kibaha. Ili kutekeleza mradi huo, nyumba zilizokuwa zimejengwa kwenye hifadhi ya barabara zimebomolewa kwa mujibu wa sheria. Ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 16 utaanza wakati wowote kuanzia sasa.

Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kutekeleza jukumu lililonileta hapa Mloganzila la kuifungua rasmi Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili.

 

Mungu Ibariki Hospitali Hii!

Mungu Wabariki Wana-Mloganzila!

Mungu Ibariki Tanzania!

 

“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”