Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA UWEKAJI JIWE LA MSINGI LA MRADI WA BOMBA LA MAFUTA KUTOKA HOIMA NCHINI UGANDA HADI BANDARI YA TANGA, CHONGOLEANI, TANGA, TAREHE 5 AGOSTI, 2017

Wednesday 23rd August 2017

Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Uganda;

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa

         Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri

         ya Muungano wa Tannzania;

 

Mheshimiwa Dkt. Ali Kirunda Kivejinja,

Naibu Waziri Mkuu wa Uganda;

 

Mheshimiwa Tulia Ackson, Naibu Spika wa Bunge la Tanzania;

Mheshimiwa Abdulrahaman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM;

Waheshimiwa Spika Mstaafu na Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania,

Mama Anna Makinda na Mzee Othman Chande;

 

Waheshimiwa Mawaziri kutoka Tanzania na Uganda;

Mheshimiwa Martin Shigela, Mkuu wa Mkoa wa Tanga;

Wawakilishi wa Makampuni ya Wawekezaji wa Mradi huu;

Waheshimiwa Wabunge mliopo;

Waheshimiwa Makatibu Wakuu na Manaibu mliopo;

Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi

wa Taasisi za Kimataifa;

 

Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa mliopo;

Viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;

Waheshimiwa Viongozi Wengine wa Serikali mliopo;

Viongozi Vyama vya Siasa na Dini mliopo;

Wageni Waalikwa, Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana:

         Napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na kutuwezesha kushuhudia tukio hili muhimu katika historia ya uhusiano wa Tanzania na Uganda. Aidha, kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya Serikali na Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda nimkaribishe Mheshimiwa Rais Yoweri Kaguta Museveni pamoja na ujumbe wake hapa Chongoleani. Namshukuru sana kwa kukubali kushiriki nasi katika hafla hii ya kuweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Bomba wa Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi hapa Tanga.

 

Hii ni mara yangu ya kwanza kuja Tanga tangu nimechaguliwa kuwa Rais wa nchi yetu. Hivyo basi, kabla sijazungumzia tukio lililotuleta hapa, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru wana-Tanga kwa kunichagua. Binafsi, sina cha kuwalipa zaidi ya kuwaahidi kuwa mimi pamoja na wenzangu Serikalini tutawatumikia kwa bidii na kamwe hatutawaangusha.

 

Wageni Waalikwa, Mababi na Mabwana:

Mkoa wa Tanga una historia ndefu na umetoa mchango mkubwa kwa nchi yetu. Enzi za kupigania uhuru, mwaka 1958, Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kabla hajaenda Tabora kwenye Mkutano Mkuu wa TANU, ambao uligubikwa na mgawanyiko, alikuja Tanga. Akiwa Tanga, alikutana na wazee na kupanga nao mikakati ya kudhibiti mgawanyiko uliokuwepo, ambao ulitokana na uamuzi wa Serikali ya Kikoloni kuanzisha utaratibu wa kura tatu. Baada ya kupanga mikakati, Wazee wa Tanga walimsomea dua ndipo akaelekea Tabora kwenye Mkutano, ambao ulihitimishwa kwa kupitisha Azimio la Tabora, maarufu kama “Uamuzi wa Busara”. Azimio hili lilisaidia sana kuharakisha kupatikana kwa uhuru wa nchi yetu.

 

Lakini mbali na kutoa mchango huo mkubwa kwa nchi yetu, Mheshimiwa Rais Museveni ameeleza hivi punde kuwa silaha zake za kwanza wakati akielekea Uganda kuanzisha mapambano, alizipitishia huku Tanga pale Horohoro. Huu ni uthibitisho kuwa Mkoa huu sio tu umetoa mchango kwa nchi yetu bali pia kwa nchi nyingine. Na mimi naamini hata jina la Tanganyika huenda lilitokea huku Tanga.

 

Ni kutokana na sababu hizo zote, nimefurahi sana leo kuwepo hapa kushuhudia uwekaji wa Jiwe la Msingi la Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga. Kama ambavyo mmesikia, Mradi huu ni mkubwa na wa kihistoria kwa mataifa yetu mawili. Bomba litakalojengwa litakuwa na urefu wa kilometa kilometa 1445, na litakuwa bomba refu zaidi duniani linalotumia teknolojia ya kupasha joto (longest heated pipeline in the world). Tumesikia pia kuwa mradi huu utagharimu Dola za Marekani bilioni 3.5, sawa na takriban Shilingi za Tanzania trilioni 8. Hiki ni kiasi kikubwa sana cha fedha. Hivyo basi, natoa pongezi nyingi sana kwenu wana-Tanga, Watanzania wenzangu, ndugu zetu wa Uganda pamoja na wana-Jumuiya Afrika Mashariki wote kwa kuanza kutekeleza mradi huu mkubwa.

 

Wageni Waalikwa, Mababi na Mabwana:

Leo tupo hapa kuweka Jiwe la Msingi la Mradi huu. Lakini niwe mkweli, hatua hii haikufikiwa kirahisi. Tulikumbana na changamoto nyingi. Walijitokeza watu wengi tu waliojaribu kuzuia Bomba hili kujengwa upande wa Tanzania. Na hata majadiliano hayakuwa mepesi. Kuna nyakati ilitulazimu mimi na mwenzangu Mheshimiwa Rais Museveni kuingilia kati. Na napenda kutumia fursa hii kusema hapa hadharani kuwa Mheshimiwa Rais Museveni ni rafiki wa kweli wa Watanzania. Licha ya baadhi ya watu kumshawishi Bomba hili lisijengwe Tanzania, tulishirikiana naye kwa karibu katika kuwahimiza watendaji wetu kuendelea na majadiliano hadi hatimaye tukaweza kufikia makubaliano ya kujenga Bomba hili upande wa Tanzania.

 

Hivyo basi, namshukuru sana Mheshimiwa Rais Museveni, Serikali pamoja na wananchi wa Uganda kwa kukubali Bomba hili kujengwa Tanzania. Aidha, nawashukuru na kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri, watendaji na wataalam wa Serikali zote mbili ambao walishiriki na kufanikisha majadiliano yetu. Napenda kuwahakikishia ndugu zetu wa Uganda pamoja na wawekezaji kuwa hamjafanya makosa kuichagua Tanzania. Mbali na amani na usalama tulionao pamoja na mazingira mazuri kwa ajili ya kusafirisha mafuta, sisi tuna uzoefu katika kutekeleza, kusimamia na kuendesha miradi kama hii. Tunayo mabomba makubwa ya kusafirisha mafuta na gesi. Mwaka 1968 tulishirikiana na wenzetu wa Zambia kujenga na kukamilisha ujenzi wake Bomba la Mafuta lenye urefu wa kilometa 1,710 kutoka Dar es Salaam hadi Ndola. Na hivi karibuni tumejenga mabomba mengine ya kusafirisha gesi asilia kutoka Songo Songo na Mnazi Bay, kusini mwa nchi yetu, kwenda Dar es Salaam. Huu ni uthibitisho tosha kuwa tuna uzoefu wa kutosha kwenye miradi kama hii.

 

Ndugu Watanzania wenzangu,

Wageni Waalikwa, Mababi na Mabwana:

Katika kuhakikisha kuwa mradi huu unakuja Tanzania, ilitulazimu kujitolea baadhi ya mambo, ikiwemo kusamehe baadhi ya kodi na tozo, kama ambavyo Mheshimiwa Rais Museveni amezitaja kwenye hotuba yake. Tulifanya hivyo kwa kutambua kuwa Mradi huu utakuwa na manufaa makubwa kwa nchi zetu mbili. Bomba litakapokamilika litakuwa linasafirisha takriban lita 200,000 za mafuta ghafi kwa siku, ambapo nchi yetu italipwa Dola za Marekani 12.5 kwa kila pipa. Mbali na hilo, mradi huu utatoa ajira nyingi za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, wakati na baada ya ujenzi kukamilika. Baadhi ya ajira ni hizi ambazo tunazishuhudia hivi leo, ambapo watu wanauza bidhaa zao mbalimbali: chakula; maji, juisi n.k. Lakini wakulima nao watanufaika; na hata wafanyabiashara na wenye viwanda nao watanufaika. Mathalan, Mheshimiwa Rais Museveni ameeleza kuwa ujenzi wa Bomba hili utahitaji saruji nyingi. Hivyo, viwanda vya saruji vitanufaika. Na kwa bahati nzuri, maandalizi ya kujenga kiwanda cha saruji hapa Tanga, ambacho kitakuwa kikubwa zaidi katika Ukanda wetu wa Afrika Mashariki na Kati, yanaendelea vizuri.

 

Sambamba na faida hizo, mradi huu unatarajiwa kuweka misingi ya ushirikiano kwenye sekta ya mafuta na gesi kati ya mataifa yetu. Mathalan, kwa kuwa mafuta kutoka Uganda yatasafirishwa kupitia hapa Tanga, ni dhahiri kuwa sisi nasi tutaweza kuyanunua na hivyo kupunguza gharama za kuagiza bidhaa hiyo kutoka mataifa ya mbali. Aidha, kwa vile mafuta kutoka Uganda yatakuwa ghafi, ni fursa kwa wafanyabiashara wetu na wawekezaji kujenga viwanda vya kuyasafisha. Na kama mlivyomsikia Rais Museveni, hydrocarbons zinazalisha bidhaa nyingi. Mbali na mafuta ya petrol, dizeli, mafuta ya ndege na taa; zinatumika pia kutengeneza plastiki.

 

Kama hiyo haitoshi, bila shaka, baadhi yenu hapa mnafahamu kuwa katika nchi yetu, hususan kwenye maeneo ya Ziwa Tanganyika na Eyasi, zimeonekana dalili za hydrocarbons ambazo zinaashiria uwepo wa mafuta. Kwa kuwa ugunduzi wa mafuta nchini Uganda kwa kiasi kikubwa ulifanywa na wataalam wa nchi hiyo, tumewaomba ndugu zetu wa Uganda nao wamekubali, kushirikiana nasi katika kuendeleza utafiti wa mafuta katika maeneo hayo. Na mafuta yakipatikana, tutayasafirisha kupitia Bomba hili. Zaidi ya hapo, mmemsikia Mheshimiwa Rais Museveni akisema kuwa angependa kuona tunajenga bomba jingine kutoka Tanzania kwenda Uganda kwa ajili ya kusafirisha gesi yetu. Ni dhahiri kuwa mambo haya yote yakifanyika, ushirikiano wetu utaimarika lakini pia tutaufungua kiuchumi Ushoroba wa Kaskazini (Northern Corridor), ambao unahusisha nchi za Burundi, DRC, Rwanda na Sudan Kusini. Hivyo basi, niwaombe wana-Tanga na Watanzania wenzangu kwa ujumla, kujipanga vizuri katika kutumia fursa zitakazoletwa na mradi huu.  

 

Nafahamu kuwa ili kutekeleza mradi huu, baadhi ya wananchi wameanza kulipwa fidia zao. Napenda kuhakikishia kuwa watu wote wenye kustahili, watalipwa fidia zao kwa mujibu wa sheria za nchi yetu. Bahati nzuri, kama mlivyosikia, kati ya kilometa 1445 za Bomba hili, kilometa 1,100 zitakuwa upande wa Tanzania; na litapita katika mikoa minane. Napenda niwahakikishie kuwa watu wote wenye kustahili, kulipwa fidia kwenye Mikoa yote 8, watalipwa fidia zao.  Hakuna hata mtu mmoja atakayedhulumiwa. Lakini nitoe ushauri kwa watu ambao, baada ya kusikia Bomba hili linajengwa, wameanza kuendeleza maeneo ambayo wamepata fununu kuwa Bomba litapita. Waachane kabisa na mpango huo. Wamechelewa. Tulikwishachukua picha za satellite. Tunayafahamu maeneo yote ambayo tunatarajia Bomba hilo litapita. Hivyo, ukianza kujenga sasa, ujue “umeula wa chuya”.

Mheshimiwa Rais Museveni;

Ndugu Watanzania wenzangu;

Wageni Waalikwa, Mababi na Mabwana:

Tumekutana hapa kwa ajili ya kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Bomba la Mafuta. Lakini kama nilivyokwishatangulia kusema, hii ni mara yangu ya kwanza kuja Tanga tangu nimekuwa Rais. Kwa sababu hiyo, naomba mniruhusu, japo kwa kifupi, nieleze utekelezaji wa ahadi pamoja na mipango ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa nchi yetu. Na kwa kuwa nipo Tanga, nitaeleza yale tu yanayowahusu wana-Tanga.

 

Kama mtakavyokumbuka, ahadi yetu kubwa wakati wa kampeni ilikuwa ujenzi wa viwanda. Ninyi wana-Tanga mnafahamu kuwa kuna wakati Mkoa wenu ulikuwa na viwanda vingi. Lakini hapo katikati mkaviua. Lakini nimefurahi kusikia kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wenu kuwa hivi sasa viwanda vingi vinajengwa hapa Tanga.  Na kesho amenialika kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwenye baadhi ya viwanda hivyo. Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kwa dhati ya kujenga uchumi wa viwanda, na kwa hapa Tanga tumejipanga kurejesha hadhi ya Tanga, kwa kujenga viwanda vipya na kuvifufua vya zamani vilivyotelekezwa.

 

Suala la pili ni kuhusu ardhi. Nafahamu kuwa moja ya matatizo makubwa yanayowasumbua wana-Tanga hivi sasa ni ukosefu wa ardhi kwa ajili ya kuendesha shughuli mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo kilimo. Maeneo mengi ya ardhi yanamilikiwa na watu wachache ambao wameshindwa kuyaendeleza.  Nilitoa maelekezo kwa Wizara ya Ardhi pamoja na uongozi wa Mkoa kupitia mashamba 72 makubwa yaliyopo katika Mkoa huu. Kufuatia uchambuzi uliofanyika, tayari tumeyachukua mashamba makubwa matano kule Muheza yenye ukubwa wa takriban hekta 14,000, na tumeagiza sehemu ya ardhi hiyo igawiwe kwa wananchi bure na itakayobaki itumike kwa ajili ya shughuli nyingine za maendeleo, ikiwemo kutenga maeneo ya viwanda. Aidha, tumewaandikia barua (notice) wamiliki wa mashamba mengine 12 tukitaka watueleze kwanini tusiwafutie umiliki wao kwa kushindwa kuyaendeleza. Napenda kuwaahidi kuwa zoezi hili ni endelevu. Tutaendelea  kuwanyang’anya watu walihodhi ardhi bila ya kuiendeleza na kuwagawia kwa wananchi. Lakini na ninyi wananchi mkipewa, hakikisheni mnaiendeleza. Kinyume chake, nanyi tutawanyang’anya na kuwapa wengine.

 

Napenda pia kutumia fursa hii kuwaarifu wana-Tanga kuwa hivi karibuni tunatarajia kuanza ujenzi wa barabara ya lami kutoka hapa Tanga hadi Bagamoyo yenye urefu wa takriban kilometa 175. Barabara hii, ambayo itapugunza umbali wa kutoka Tanga kwenda Dar es Salaam pamoja na kuiunganisha nchi yetu na majirani zetu wa Kenya, ni moja ya miradi iliyopo chini ya  Jumuiya ya Afrika Mashariki na itajengwa kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika.

 

Sambamba na hayo, hivi punde Mkuu wa Mkoa wenu amewasilisha ombi kuhusu kupauliwa na kuongezwa kina Bandari ya Tanga. Niseme tu kwamba nimelipokea ombi hilo. Ni jambo lililo wazi kuwa kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanyika hapa Tanga hivi sasa, ni lazima tuipanue Bandari hii ili iweze kuhudumia meli kubwa. Hii itasaidia kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam. Mizigo inayokuja Tanga na maeneo ya jirani, ikiwemo mafuta, itashushwa hapa na hivyo kuwapunguzia wananchi gharama. Hivyo basi, napenda kuwahakikishia kuwa Bandari yenu itapanuliwa.  Na kwa bahati nzuri, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mheshimiwa Prof. Mbarawa, yupo hapa. Bila shaka, amesikia na ataliweka suala hili katika mipango ya Wizara yake.

 

Mheshimiwa Rais Museveni;

Ndugu Watanzania wenzangu;

Wageni Waalikwa, Mababi na Mabwana:

Siwezi kuhitimisha hotuba yangu bila ya kuwashukuru na kuwapongeza wawekezaji wa mradi huu, kampuni za Total, Tullow na CNOOC, kwa kukubali kuwekeza katika mradi huu mkubwa. Napenda kuwahakikishia kuwa Tanzania itatoa ushirikiano wote unaohitajika katika kutekeleza mradi huu, kulingana na masharti ya Mkataba.

 

Lakini niwaombe jambo moja. Na ninyi mjitahidi kukamilisha mradi huu mapema. Mwaka 2020 ni mbali sana. Mimi sioni kwanini mradi huu uchukue muda mrefu kiasi hicho kutekelezwa. Makampuni yaliyopewa dhamana ya kujenga Bomba ni makubwa na yana uzoefu wa kutosha. Fedha mmesema mnazo. Na wafanyakazi pia wapo. Hivyo, nawasihi sana mjitahidi kukamilisha mradi huu mapema. Watanzania na bila shaka wananachi wa Uganda pamoja na wana-Afrika Mashariki kwa ujumla wanausubiri kwa hamu mradi huu.

 

Mheshimiwa Rais Museveni;

Waheshimiwa Viongozi;

Wageni Waalikwa, Mababi na Mabwana:

Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kumshukuru tena Mheshimiwa Rais Museveni kwa kuja kushiriki kwenye tukio hili. Namuahidi kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi yake. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuahidi kuwa kwenye sherehe za kuweka Jiwe la Msingi kama hili kule Hoima, nami nitashiriki.

 

Nawashukuru tena wana-Tanga kwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hili. Aidha, nawashukuru kwa kunichagua kuwa Rais wenu. Nawaahidi kuwa Serikali ninayoingoza itawatumikia bila kuwabagua kwa misingi ya dini, kabila au vyama. Utekelezaji wa mradi huu ni kielelezo kuwa Serikali ninayoingoza haina ubaguzi. Bomba hili lingeweza kujenngwa mahali popote nchini, lakini tumeamua kulileta hapa Tanga, ambako Mbunge wake hatokani na Chama tawala. Tumefanya hivyo kwa vile maendeleo hayana chama.

 

Mwisho lakini sio kwa umuhimu, navishukuru na kuvipongeza vikundi vya burudani vilivyotuburudisha kwa nyimbo zao nzuri, hususan zinazotukumbusha sisi Watanzania kuimarisha uzalendo. Navishukuru pia vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri wanayoifanya kwa nchi yetu. Aidha, napenda kuwashukuru na kuwapongeza wana-habari kutoka vyombo vyote kwa kuuhabarisha umma kuhusu tukio hili kubwa na muhimu kwa nchi zetu mbili. 

 

Baada ya kusema hayo, mimi pamoja na Mheshimiwa Rais Museveni tupo tayari kuweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga.

 

Mungu Ubariki Uhusiano kati ya Tanzania na Uganda!

Mungu Ibariki Jumuiya ya Afrika Mashariki!

 

“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”