Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JOHN POMBE MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA YA KUKABIDHI UENYEKITI WA JUMUIYA YA AFRIKA KWENYE MKUTANO WA 18 WA WAKUU WA NCHI WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI DAR ES SALAAM, TANZANIA, TAREHE 20 MEI, 2017

Wednesday 23rd August 2017

Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda;

 

Mheshimiwa William Ruto, Makamu Rais wa Jamhuri ya Kenya;

 

Mheshimiwa Joseph Butore, Makamu wa Pili

wa Rais wa Jamhuri ya  Burundi;

 

Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar

na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;

 

Waheshimiwa Wawakilishi wa Marais wa Rwanda na Sudan Kusini;

 

Mheshimiwa Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya;

 

Waheshimiwa Mawaziri mliopo hapa;

 

Mheshimiwa Spika wa Bunge la Afrika Mashariki;

 

Mheshimiwa Jaji Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki;

 

Mheshimiwa Balozi Liberat Mfumukeko, Katibu Mkuu wa Jumuiya;

 

Waheshimiwa Makatibu Wakuu Wastaafu wa Jumuiya;

 

Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa;

 

Wageni Wote Waalikwa;

 

Mabibi na Mabwana;

 

Naomba mniruhusu nianze kwa kuwakaribisha washiriki wote katika Mkutano huu 18 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lakini kwa namna ya pekee kabisa, napenda niwakaribishe Wakuu wa Nchi wenzangu pamoja na viongozi mbalimbali mnaoziwakilisha nchi zenu kwenye Mkutano huu hapa Tanzania, hususan katika Jiji letu la Dar es Salaam. Nikiwa Rais, nafahamu mnayo majukumu mengi, hata hivyo, mmeweza kutenga muda wa kuja kuhudhuria Mkutano huu muhimu. Hii ni ishara ya dhamira kubwa tuliyonayo sisi viongozi wa Jumuiya katika kutekeleza ajenda yetu ya utangamano.

 

Napenda pia kutumia fursa hii kutoa shukrani zangu nyingi kwa Baraza la Mawaziri pamoja na Sekretarieti yetu ya Jumuiya, chini ya uongozi wa Balozi Liberat Mfumukeko kwa maandalizi mazuri ya Mkutano huu.  Mmeturahisishia sana kazi yetu sisi viongozi. Na nina imani, kutokana na maandalizi mazuri yaliyofanyika, Mkutano huu utakuwa wa mafanikio makubwa.

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Viongozi wetu, wakati wa kuanzisha Jumuiya hii, na ninafurahi Mheshimiwa Rais Museveni tupo naye hapa, walikuwa na dhamira moja kubwa. Dhamira ya kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi pamoja na utangamano wa nchi za ukanda huu. Aidha, walikuwa na dhamira ya kujenga Jumuiya imara ambayo itazifanya nchi za ukanda wetu zishiriki kikamilifu kwenye masuala ya kimataifa. Walifahamu kuwa, kutokana na udogo na uchanga wa mataifa yao, ingewawia vigumu kushindana na mataifa mengine makubwa, ambayo yameendelea.

 

 Inatia faraja kuona kuwa, tangu kufufuliwa kwa Jumuiya yetu mwaka 2000, mafanikio mengi makubwa ambayo yanakwenda sambamba na dhamira ya waanzilishi wa Jumuiya hii, yamepatikana. Umoja na mshikamano miongoni mwa wana-Afrika Mashariki unazidi kukua. Utangamano wetu unaimarika kila kukicha na unazinufaisha nchi zetu na watu wake. Tumefanikiwa kuanzisha Umoja wa Forodha (Customs Union); hivi sasa tupo kwenye utekelezaji wa Mkataba wa Soko la Pamoja (Common Market Protocol); na hatua za kuanzisha Ushirikiano katika Masuala ya Kifedha (Monetary Union) umeanza. Jumuiya yetu nayo inazidi kuimarika na imebaki kuwa mfano wa kuigwa Barani Afrika na duniani kwa ujumla. Haya ni mafanikio makubwa na napenda niwapongeze wote walioshiriki katika kuyapata.

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Licha ya mafanikio yaliyopatikana, bado tuna safari ndefu ya kufikia kule ambako waanzilishi wetu walitamani Jumuiya yetu ifike. Jitihada kubwa bado zinahitajika katika kuboresha na kuimarisha Jumuiya na Utangamano wetu. Ni dhahiri kuwa kazi ya kuimarisha Jumuiya yetu sio rahisi, lakini hatuna budi sote kushirikiana katika kuifanya. Na katika hilo, nafurahi kuuarifu Mkutano huu kuwa, katika kipindi ambacho Tanzania ilipewa jukumu la kuongoza Jumuiya yetu, jitihada kubwa zimefanyika za kuboresha na kuimarisha Jumuiya yetu. Natambua muda mfupi ujao, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri atawasilisha Ripoti ambayo imeeleza kwa kirefu mambo yaliyofanyika, lakini naomba nitaje machache:

 

Kwanza, ni kuhusu utekelezaji wa ajenga ya utangamano: Kama mnavyofahamu, utekelezaji wa Eneo Moja la Ushuru wa Forodha (Single Customs Union Territory) unaendelea vizuri. Jitihada za kushughulikia vikwazo vya biashara visivyo vya kodi (Non Tariff Barriers), zimeendelea vizuri. Katika kipindi chetu cha uongozi, tuliweza pia kusimamia utekelezaji wa baadhi ya masuala yanayohusu Soko la Pamoja (Common Market), ambapo baadhi ya sekta zimeanza kutekeleza, wakiwepo wanasheria na wahandisi. Kuhusu Ushirikiano wa Kifedha, tumeweza kufanikisha uandaaji wa miswada miwili ambayo ipo tayari kupelekwa kwenye Bunge letu la Afrika Mashariki kwa ajili ya kujadiliwa. Mswada wa kwanza unahusu uanzishaji wa Taasisi ya Fedha ya Jumuiya (East African Monetary Institute Bill), ambayo itakuwa taasisi ya mpito kuelekea kuanzishwa kwa Benki Kuu ya Afrika Mashariki; na mswada wa pili unahusu Tume ya Jumuiya ya Ufuatiliaji na Usimamizi (the East African Surveillance, Compliance and Enforcement Commission Bill).

 

Pili, Maendeleo ya Miundombinu: Kama mnavyofahamu, ujenzi wa miundombinu, hususan ya usafiri, ni nguzo muhimu katika ustawi wa ushirikiano baina ya mataifa. Hivyo basi, nafurahi kuarifu kuwa, katika kipindi chetu cha Uenyekiti, miradi kadhaa ya miundombinu ya usafiri imeweza kufikia hatua nzuri ya utekelezaji. Mradi wa ujenzi wa Barabara ya Arusha – Holili/Taveta – Voi tayari umeanza. Upembuzi wa mradi wa Barabara ya Malindi – Lunga Lunga/Tanga – Bagamoyo umekamilika na kwa sasa unasubiri fedha ili uanze kutekelezwa. Aidha, miradi ya Barabara za Lusahuga – Rusumo – Kigali na ile ya Nyakanazi – Kasulu – Rumoge – Bujumbura ipo kwenye hatua mbalimbali za usanifu. Utekelezaji wa miundombinu hiyo ya usafiri, umeenda sambamba na ujenzi wa vituo vya pamoja vya mpakani (One-Stop Border Posts). Vituo vya Mpakani 9 kati  ya 15 tayari vimeanza kazi, kikiwemo Kituo cha Rusumo kwenye Mpaka wa Tanzania na Rwanda, ambacho mimi na mwezangu Rais Kagame tulikizindua mwezi Aprili mwaka jana.

 

Tatu, Masuala ya Amani na Usalama: Katika kipindi chetu pia, tumefanya jitihada za kutafuta ufumbuzi wa migogoro iliyopo kwenye Ukanda wetu, hususan nchini Burundi na pia Sudan Kusini, ambako Jumuiya ya IGAD inashughulikia kwa karibu. Jitihada zilizofanyika, kwa kiasi fulani, zimesaidia kupunguza uhasama miongoni mwa pande zinazopingana. Napenda kutumia fursa hii kupongeza jitihada kubwa zinazofanywa na Msuluhishi wa Mgogoro wa Burundi, Mheshimiwa Rais Museveni wa Uganda pamoja na Mpatanishi wa Mgogoro huo, Rais Mstaafu wa Tanzania, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa. Wamefanya kazi kubwa sana. Lakini niziombe pande husika kwenye migogoro niliyoitaja kuweka nyuma maslahi yao binafsi na kutanguliza mbele maslahi ya mataifa yao ili kuwezesha migogoro hiyo kumalizika kwa haraka. Wafahamu kuwa, kurejea kwa amani ya kudumu katika nchi hizo, kwa kiasi kikubwa kunawategemea wao.

 

Nne, Masuala ya Utawala Bora na Demokrasia: Hakuna shaka, ukanda wetu umepiga hatua kubwa katika eneo hili. Utawala Bora na masuala ya demokrasia yameimarika katika Mataifa Wanachama yote. Mathalan, mwaka huu pekee, mataifa mawili ya Kenya na Rwanda yanatarajiwa kufanya Uchaguzi Mkuu.  Na napenda nitumie fursa hii, nizitakie heri nchi hizi mbili wanachama katika kutekeleza hatua hiyo muhimu. Chaguzi zifanyike kwa utulivu na amani ili tuioneshe tena dunia kuwa demokrasia imeimarika na kuota mizizi katika ukanda wetu.

 

Tano, Kuimarisha na kukuza mahusiano na Washirika wetu wa Maendeleo. Katika kipindi chetu cha Uenyekiti, Jumuiya yetu imesaini makubaliano ya kifedha na Serikali ya Marekani, kupitia Shirika lake la misaada la USAID; Serikali ya Ujeruma kupitia shirika lake la KfW; Umoja wa Ulaya; Benki ya Dunia pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Makubaliano hayo yana thamani ya takriban Dola za Marekani milioni 300.  

 

Sita, Kubana Matumizi ya Jumuiya.  Kwenye hotuba yangu ya kupokea Uenyekiti wa Jumuiya yetu mwezi Machi mwaka jana niliahidi kusimamia matumizi ya fedha ya Jumuiya yetu. Leo nafurahi kuripoti kuwa, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, tumeweza kupunguza matumizi ya Jumuiya, hususan Sekretarieti, kutoka Dola za Marekani milioni 12.6 hadi kufikia Dola za Marekani milioni 9.1. Nampongeza Katibu Mkuu Dkt. Mfumukeko kwa kusimamia jambo hili vizuri. Nina matumaini makubwa kuwa Mwenyekiti Mpya naye ataendeleza suala hili la usimamizi mzuri wa rasilimali ili fedha nyingi zitumike kwenye shughuli za maendeleo.

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Haya niliyoyataja ni baadhi tu ya mafanikio. Yapo mengine mengi ambayo yamepatikana. Hivyo, napenda nitumie fursa hii kuwashukuru Viongozi wenzangu kwa heshima kubwa waliyoipa Tanzania kuongoza Jumuiya yetu kwa kipindi cha takriba miaka miwili na ushee. Kama mnavyofahamu, awali tulipewa jukumu hili mwezi Februari 2015, lakini mwezi Machi 2016 tuliongezewa tena mwaka mmoja kuendelea kuongoza Jumuiya hii. Kwa maana hiyo, tumeongoza kwa miaka miwili na zaidi. Hii ilikuwa ni heshima kubwa sana kwa nchi yetu. Lakini napenda niwashukuru Waheshimiwa Viongozi kwa imani kubwa mliyoionesha kwangu mimi binafsi. Kama mtakumbuka, mwaka jana wakati nakabidhiwa jukumu la kuwa Mwenyekiti, nilikuwa na kama miezi minne tu tangu niingie madarakani. Lakini licha ya uchanga wangu, mliniamini. Nawashukuru sana.

 

 Napenda pia nitumie fursa hii kuwashukuru kwa ushirikiano na  msaada mkubwa mliutoa kwangu mimi binafsi na kwa nchi yangu katika kipindi chote tulichokuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hii. Hivi punde, nimetoka kueleza baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chetu cha Uenyekiti. Mafanikio hayo yasingepatikana kama msingetupa ushirikiano wa kutosha. Hivyo, nawashukuru sana kwa ushirikiano wenu mkubwa mliotupa.

 

Waheshimiwa Wakuu wa Nchi;

Waheshimiwa Viongozi mnaowakilisha nchi zetu;

Waheshimiwa Mawaziri;

Mheshimiwa Katibu Mkuu wa Jumuiya;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Jukumu langu kubwa leo lilikuwa kuwakaribisha na kukabidhi majukumu ya Uenyekiti wa Jumuiya kwa Mzee wetu, Mheshimiwa Rais Yoweri Museveni wa Uganda. Tayari nimewakaribisha. Sasa nimebakiza jukumu moja la kukabidhi madaraka. Lakini kabla ya kutekeleza jukumu hilo la pili, naomba mniruhusu nitoe shukrani zangu nyingi kwa Katibu Mkuu wa Jumuiya Balozi Mfumukeko, Naibu wake Dkt. Enos Bukuku, wafanyakazi wote wa Jumuiya pamoja na washirika wetu mbalimbali wa maendeleo kwa ushirikiano mkubwa walionipa katika kipindi chote cha Uenyekiti. Niwaombe tu ushirikiano huo muuendeleze pia kwa Mwenyekiti mpya.

 

Natambua Naibu Katibu Mkuu Dkt. Bukuku anamaliza muda wa kutumikia Jumuiya yetu hivi karibuni. Hivyo basi, napenda nitumie fursa hii kumshukuru kwa mchango aliotoa katika Jumuiya yetu; na namtakia kila la heri mahali popote atakapokuwa baada ya kumaliza majukumu haya. Niruhusuni pia nitangulize pongezi zangu kwa Naibu Katibu Mkuu Mteule na Jaji Mteule wa Mahakama ya Jumuiya kutoka Sudan Kusini. Nina imani Mkutano huu utawapitisha, hivyo, napenda niwatakie kila la heri wakati watakapoanza kutekeleza majukumu yao mapya.

 

Mabibi na Mabwana, kwa hakika, ilikuwa ni heshima kubwa kwangu mimi binafsi na kwa nchi yangu kushika wadhifa wa Uenyekiti wa Jumuiya hii, lakini sasa wakati umewadia wa kukabidhi madaraka hayo kwa Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda. Kama mnavyofahamu, Mheshimiwa Rais Museveni ni mzoefu katika masuala ya Jumuiya yetu. Yeye ni miongoni mwa watu walioshiriki kikamilifu katika kuifufua Jumuiya yetu. Hivyo basi, nina matumaini makubwa kuwa, kutokana na uzoefu wake mkubwa, Jumuiya yetu  itazidi kuimarika wakati wa uongozi. Na hata yale masuala ambayo hatukuweza kuyamaliza wakati wa uongozi wetu, hususan suala la migogoro ya Burundi na Sudan Kusini pamoja na Mkataba wa Ubia wa Kiuchumi kati ya Jumuiya yetu na Umoja wa Ulaya, yatapata ufumbuzi.   Napenda nihitimishe kwa kuahidi kuwa Tanzania itatoa ushirikiano wa kutosha kwa Mwenyekiti mpya ili hatimaye tuweze kufikia malengo ya kuanzishwa kwa Jumuiya hii.

 

Mungu Ibariki Jumuiya Yetu!

Mungu Ibariki Afrika!

“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”