Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE UFUNGUZI WA MAONESHO YA 41 YA BIASHARA YA KIMATAIFA YA DAR ES SALAAM VIWANJA VYA MWALIMU J. K. NYERERE, TAREHE 02 JULAI, 2017

Wednesday 23rd August 2017

Mheshimiwa Charles Mwijage (Mb),

         Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji;

Mheshimiwa Amina Salum Ali, Waziri wa Viwanda,

Biashara na Masoko wa Serikali ya Zanzibar;

Waheshimiwa Mawaziri mliopo;

Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;

Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa

         Taasisi za Kimataifa;

Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza

la Wawakilishi;

Mheshimiwa Isaya Mwita, Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam;

Mheshimiwa Mhandisi Christopher Chiza,

         Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANTRADE,

Ndugu Edwin Rutageruka, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE;

Viongozi wa Ngazi Mbalimbali wa Serikali, Vyama vya Siasa

         Pamoja na Dini mliopo;

Waheshimiwa Washiriki wa Maonesho;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha kufika siku hii ya leo. Aidha, napenda nitoe shukran zangu nyingi kwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mheshimiwa Mwijage, pamoja na uongozi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kwa kunialika kuwa Mgeni Rasmi wa Maonesho haya ya 41 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar Es Salaam. Kama mnavyofahamu, hii ni mara yangu ya kwanza kuwa Mgeni Rasmi wa Maonesho haya. Mwaka jana nilikuja hapa kumsindikiza aliyekuwa Mgeni Rasmi, Mheshimiwa Rais Kagame.  Hivyo basi, nawashukuru sana kwa kunipa heshima hii kubwa mwaka huu.

 

Kabla sijaendelea zaidi, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza waandaaji kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuboresha Maonesho haya. Tumeelezwa hivi punde kuwa idadi ya washiriki wa Maonesho haya kila mwaka inaongezeka. Mwaka huu, idadi ya makampuni ya Kitanzania yanayoshiriki ni 2,520, wakati makampuni ya nje ni 515 kutoka mataifa 30. Zaidi ya hapo, tumearifiwa kuwa Shirikisho la Maonesho ya Biashara ya Kimataifa (The Global Association of the Exhibition Industry - UFI) limeyataja Maonesho haya kuwa ni makubwa na bora zaidi katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki na Kati. Huu ni uthibitisho tosha kuwa maonesho haya ni makubwa. Hivyo basi, napenda kwa dhati kabisa, kuwapongeza waandaaji, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara, kwa jitihada kubwa mnazozifanya.

 

Mheshimiwa Waziri;

Ndugu Washiriki, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

         Hakuna shaka yoyote kuwa Maonesho ya Biashara ni nyenzo muhimu ya kutangaza biashara. Ni kweli kuwa katika dunia ya sasa zipo njia nyingi za kutangaza biashara, ikiwemo vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, mabango, n.k. Hata hivyo, jambo lililo dhahiri ni kwamba maonesho ya biashara yamebaki kuwa njia kuu inayoaminika duniani kote katika kutangaza biashara. Hii ni kwa sababu Maonesho ya Biashara yana faida nyingi. Kwa ajili ya ufinyu wa muda, nitataja faida chache za Maonesho ya Biashara.

 

         Kwanza kabisa, tofauti na njia nyingine za kutangaza biashara, Maonesho ya Biashara yanampa fursa mzalishaji wa bidhaa au mtoa huduma kukutana ana kwa ana na mteja wake. Hii humwezesha mzalishaji kupata mrejesho kuhusu namna bidhaa yake (hasa bidhaa mpya) inavyokubalika kwenye soko, mapungufu ya bidhaa hiyo na nini kinahitajika kuboreshwa. Mathalan, katika maonesho haya nina uhakika kuwa yapo makampuni yamekuja kutangaza bidhaa zao mpya. Na kupitia mrejesho watakaoupata kutoka kwa wateja wao, makampuni hayo yatafanya uamuzi wa ama kuendelea na uzalishaji wa bidhaa husika, au kuiboresha ama kuachana nayo.

 

Pili, Maonesho ya Biashara hutoa fursa ya kuyakutanisha makampuni mengi yanayojihusisha na uzalishaji bidhaa au utoaji huduma zinazofanana. Makampuni hayo yanaweza kuwa yanatoka mataifa tofauti au kwenye nchi moja. Hii huyawezesha makampuni hayo kujifunza kutoka makampuni mengine kwa kubadilishana uzoefu, utaalamu na ujuzi wa kutengeneza bidhaa husika kulingana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

 

Sababu ya tatu, ambayo kimsingi inaendana kwa karibu na sababu mbili za mwanzo, ni kwamba Maonesho ya Biashara yanarahisha kuanzisha uhusiano wa kibiashara kati ya makampuni au kati ya kampuni na wateja wake. Mathalan, katika Maonesho haya nina imani kubwa kuwa makubaliano mbalimbali ya kibiashara au mauziano ya bidhaa yatafikiwa kati ya makampuni au makampuni na wateja wao. Kama isingekuwa Maonesho haya, huenda ingechukua muda mrefu na gharama kubwa kuweza kufikia makubaliano hayo.

 

Kutokana na sababu hizi na nyingine nyingi ambazo sikuzitaja, napenda kurudia tena kutoa pongezi kwa waandaaji wa maonesho haya. Lakini zaidi, napenda kuyashukuru na kuyapongeza makampuni ya ndani na ya nje ambayo yamejitokeza kushiriki kwenye Maonesho yetu ya 41 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam.

 

Wageni Waalikwa, Ndugu Washiriki, Mabibi na Mabwana;

Maonesho haya, mbali na kutumika kutangaza bidhaa, yanafungua milango kwa washiriki, hususan kutoka nje, kuweza kufahamu fursa nyingine za kiuchumi zilizo hapa nchini. Na katika hili, ningependa kusema kuwa nchi yetu ina fursa nyingi za kiuchumi. Hivyo basi, nawakaribisha washiriki wa ndani na pia kutoka nje kutumia Maonesho haya kutafuta  fursa nyingine za kiuchumi, ikiwemo kuwekeza kwenye sekta ya viwanda ili kwenda sambamba na kaulimbiu ya Maonesho haya inayosema “Kukuza Biashara kwa Maendeleo ya Viwanda”

 

Kama mnavyofahamu, hivi sasa tumejipanga kuhakikisha nchi yetu inakuwa ya uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025. Ili kufikia azma hiyo, tumeanza kuchukua hatua za kuondoa vikwazo na kero mbalimbali zilizokuwa zikiwakwamisha wawekezaji kuwekeza kwenye sekta hii ya viwanda hapa nchini. Tumeondoa baadhi ya kodi. Na hivi sasa tumeweka mkazo katika kushughulikia tatizo la uhaba wa umeme. Hakuna shaka, ukosefu wa umeme wa uhakika ndio kikwazo kikubwa kinachokwamisha ustawi wa viwanda hapa nchini. Hivi sasa tunazalisha umeme usiozidi Megawati 1,500. Hiki ni kiwango kidogo sana kwa nchi yenye nia ya kujenga uchumi wa viwanda.

 

Hivyo basi, tumeamua kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme. Tunapanua mradi wa umeme wa Kinyerezi I ili uweze kuzalisha Megawati 325 kutoka Megawati 150 za sasa. Aidha, tunatekeleza mradi wa Kinyerezi II, ambao utazalisha Megawati 240.  Aidha, tumeanza maandalizi ya kutekeleza miradi ya Kinyerezi III na IV, ambayo kwa pamoja inatarajiwa kuzalisha Megawati 600. Miradi hii yote ya Kinyerezi itazalisha umeme kwa kutumia gesi asilia.

 

Sambamba na miradi hiyo, tumeanza maandalizi ya kutekeleza mradi mkubwa wa umeme wa maji wa Stiglier’s Gorge, ambao umekuwa katika maandishi tangu enzi za Baba wa Taifa. Mradi huu utazalisha takriban Megawati 2,100. Nafahamu baadhi ya watu wameanza kuupinga mradi huu kwa kisingizio cha kuharibu mazingira na makazi ya viumbe hai kwenye Hifadhi ya Selou. Napenda niwahakikishie mradi huu tutautekeleza. Sababu zinazotolewa na wanaopinga mradi huu hazina nguvu.  Mradi huu tumepanga utatekelezwa katika eneo lisilozidi asilimia 3 ya eneo zima la Hifadhi ya Selou. Hivyo, hoja kwamba utaharibu mazingiza na makazi ya viumbe hazina mashiko. Badala yake, mbali na kuzalisha umeme, mradi huu utawanufaisha viumbe hai kwenye eneo hilo na pia kukuza sekta za uvuvi na kilimo. Hivyo basi, napenda kurudia kusema kuwa mradi huu tutautekeleza. Na nina imani washirika wetu wa maendeleo watatuunga mkono.

 

Wageni Waalikwa, Ndugu Washiriki, Mabibi na Mabwana;

Katika hotuba yake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania, Mheshimiwa Mhandisi Chiza, ameeleza kuwa Mamlaka ina mpango wa kufanya maboresho makubwa katika viwanja hivi. Amesema kuwa mmejipanga kubomoa mabanda yaliyopo ili kujenga mapya pamoja na kujenga hoteli na kumbi za mikutano za kisasa.

 

Jambo hili ni jema. Lakini mimi nina mawazo tofauti kidogo. Kwa mtazamo wangu, mimi naona badala ya ninyi kutumia fedha kujenga majengo haya, mngeweza kuingia makubaliano ya aina fulani na makampuni au taasisi zinazoonesha bidhaa hapa kujenga na kuboresha majengo yao. Na ninyi fedha zenu mzitumie kwenye shughuli nyingine, angalau kujenga kiwanda cha mfano ili kuitikia wito wa Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga Tanzania ya Viwanda. Naamini, kiwanda kitakuwa na faida nyingi kuliko majengo mliyopanga kuyajenga kwenye viwanja hivi. Hii ni kwa sababu, kupitia kiwanda hicho, watanzania wengi zaidi watapata ajira za kudumu lakini pia Serikali itapata kodi hasa katika kipindi hiki ambacho Watanzania wengi wameanza kuhamasika kulipa kodi. Hayo ndio mawazo yangu, hivyo, kama mtaona yanafaa, mnaweza kuyatafakari.

 

Waheshimiwa Mawaziri;

Ndugu Washiriki, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Jukumu langu leo ni kufungua Maonesho ya 41 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam. Kwa sababu hiyo, sitapenda kuwachosha kwa hotuba ndefu. Lakini kabla sijahitimisha, napenda kurudia tena kuwashukuru waandaaji kwa kunikaribisha. Aidha, nawapongeza kwa kuendelea kuyaboresha Maonesho haya. Lakini nitoe kwenu, kama mtaona inafaa, muangalie uwezekano wa kuyaongezea muda kidogo Maonesho haya. Nasema hivyo kwa sababu, mara nyingi, Maonesho haya yamekuwa yakifungwa wakati ambapo yanaanza kuchangamka na wananchi wanaanza kuhamasika kuhudhuria. Hivyo, kama itawapendeza, mnaweza kuongeza hata siku tano hivi.

 

Napenda pia kutumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza washiriki wote. Binafsi ningetamani sana kutembelea mabanda yote lakini kwa sababu ya muda, itaniwia vigumu. Itoshe tu kusema kuwa nawashukuru na kuwapongeza sana kwa kushiriki kwenu kwenye Maonesho haya.   Kwa washiriki wa Tanzania, nawasihi sana myatumie vizuri Maonesho haya katika kujifunza na kuboresha bidhaa na huduma mnazozalisha. Mwisho lakini sio kwa umuhimu, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Mabalozi mnaowakilisha nchi mbalimbali hapa nchini kwa kuja kushiriki nasi katika shughuli hii ya Ufunguzi wa Maonesho ya 41 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam. Tunaahidi tutaendelea kushirikiana nanyi katika masuala mbalimbali.

 

  Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kutamka kuwa Maonyesho ya 41 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yamefunguliwa rasmi.

 

Mungu Yabariki Maonesho Yetu ya Saba Saba!

Mungu Wabariki Washiriki wa Maonesho Haya!

Mungu Ibariki Tanzania!

“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”