Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE SHEREHE ZA UZINDUZI WA MFUMO WA KUKUSANYA MAPATO KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI ZILIZOFANYIKA KWENYE KITUO CHA KUTUNZA KUMBUKUMBU KIJITONYAMA DAR ES SALAAM, TAREHE 1 JUNI, 2017

Wednesday 23rd August 2017

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais

wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

 

Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein, Rais wa Zanzibar

na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;

 

Waheshimiwa Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano

wa Tanzania pamoja na Serikali ya Zanzibar mliopo;

 

Waheshimiwa Makatibu Wakuu mliopo;

 

Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;

 

Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;

 

Viongozi Wengine wa Serikali mliopo;

 

Watendaji wa Makampuni mbalimbali mliopo;

 

Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa na Dini mliopo;

 

Wageni wote Waalikwa, Mabibi na Mabwana:

 

Kwanza kabisa, napenda niungane na walionitangulia kuzungumza katika kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, kwa kutupa uhai na kutuwezesha kukutana hapa hivi leo. Aidha, nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri, Prof. Mbarawa na Dkt. Mpango, kwa kunialika ili nami nishiriki katika tukio hili muhimu kwa nchi yetu. Ahsante sana.

 

Vilevile, napenda nitumie fursa hii niwashukuru wageni wote waalikwa na wananchi kwa ujumla kwa kujitokeza kwenu kwa wingi kwenye tukio hili. Hakuna shaka, uwepo wenu mahali hapa leo ni uthibitisho tosha kwamba mnatambua umuhimu wa tukio hili kwa ustawi na maendeleo ya nchi yetu.

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Napenda nikiri kuwa leo nina furaha sana. Furaha yangu inatokana na ukweli kwamba muda mfupi tu uliopita, nimetoka kutembelea Kituo cha Kutunza Taarifa au Kumbukumbu (Data Centre) hapa Kijitonyama. Nimejionea miundombinu ya Kituo hicho na kupata maelezo ya namna kinavyofanya kazi. Kwa hakika nimeridhika na kile nilichokiona na kukisia kutoka kwa wataalam. Nimeshuhudia miundombinu na mitambo ya kisasa na nimefarijika zaidi kusikia kuwa Kituo hiki kina ubora wa kimataifa na ni cha pili kwa ukubwa kwa nchi za Bara la Afrika zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara. Cha kwanza kilichopo nchini Afrika Kusini. Haya ni mafanikio makubwa kwa nchi yetu.

 

Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza sana wote walioshiriki katika kubuni na kufanikisha ujenzi wa kituo hiki, ambacho ni muhimu kwa ustawi na maendeleo ya nchi yetu. Kama mnavyofahamu, Serikali yetu iliamua kujenga Kituo hiki kwa makusudi makubwa mawili. Kusudi la kwanza ni kuhakikisha usalama wa taarifa za taasisi za Serikali na Makampuni binafsi yanayoendesha shughuli zake hapa nchini. Taasisi za Serikali na Makampuni binafsi yatakayotunza taarifa zao katika Kituo hiki yatakuwa na uhakika wa usalama wa taarifa zao, endapo ajali au uhalifu ukitokea kwenye taasisi au makampuni yao.

 

Kusudi la pili ambalo limeifanya Serikali ijenge kituo hiki ni dhamira yake ya kutaka kuimarisha na kukuza sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano nchini. Kama mnavyofahamu, sekta hii inakua kwa kasi na ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi sio tu hapa nchini bali duniani kote. Nchi zote ambazo zimepiga hatua kubwa na kupata mafanikio makubwa katika sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano zimejenga vituo  vya kutunza taarifa (Data Centre) kama hiki. Hivyo basi, uwepo wa Kituo cha Kutunza Taarifa hapa nchini sio tu unatufanya twende sambamba na nchi zilizoendelea kwenye sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano bali pia itasaidia kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa nchi yetu. Hii ni kwa sababu, sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano ni mhimili muhimu wa maendeleo kwenye sekta zote, ikiwemo viwanda, utalii, ujenzi, elimu, afya, kilimo, uvuvi, ufugaji, n.k.

 

 

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Katika maelezo niliyopata leo nimeambiwa kuwa Kituo cha Kutunza Kumbukumbu kilianza kazi tangu mwezi Oktoba 2016. Hata hivyo, mwitikio wa taasisi za Serikali na Makampuni binafsi kujiunga sio mkubwa sana. Ni taasisi na makampuni machache tu ndiyo tayari yamejiunga. Sio zaidi ya taasisi na makampuni kumi (10). Hivyo basi, napenda kutumia fursa hii kuhimiza taasisi za Serikali na makampuni binafsi kujiunga na Kituo kilichojengwa na Serikali. Kama nilivyosema hapo awali, Kituo chetu ni kikubwa sana. Kina uwezo wa kutunza kumbukumbu sio tu za taasisi na makampuni yote ya hapa nchini bali pia taasisi na makampuni ya nje ya nchi. Ubora wake ni wa daraja la juu kabisa (Tier Three). Hivyo, nazikaribisha taasisi na makampuni ya ndani na nje ya nchi kutunza kumbukumbu/taarifa zao kwenye kituo hiki.

 

Ninazo taarifa kuwa, licha ya Serikali kuingia gharama kubwa ya kujenga Kituo kikubwa cha Kutunza Taarifa, zipo taasisi za Serikali ambazo zinaendelea na taratibu za kujenga vituo vyao wenyewe. Sasa naziagiza taasisi zote za Serikali zenye nia ya kujenga vituo vyao vya kutunza kumbukumbu kuachana na mipango hiyo. Tunzeni taarifa zenu kwenye Kituo hiki ambacho kimejengwa na Serikali. Nasema hivyo kwa sababu nina uhakika, hata kama mkijenga, vituo hivyo havitakuwa na ubora kama wa kituo hiki.

 

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Waheshimiwa Viongozi,

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Jambo la pili lililonifanya leo nifurahi ni kwamba, mbali na kushuhudia Kituo hiki cha Kutunza Kumbukumbu, muda mfupi ujao nitazindua Mfumo wa Ukusanyaji Mapato ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na Ushuru wa Bidhaa (Excise Duty) kwa njia ya kielektroniki, yaani Electronic Revenue Collection System (e-RCS). Mfumo huu nao ni muhimu kwa ustawi na maendeleo ya nchi yetu. Kama mnavyofahamu, kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, shughuli nyingi za kiuchumi na kifedha kwa sasa zinafanyika kwa njia ya kielektroniki. Mathalan, makampuni ya simu, mabenki, televisheni pamoja na taasisi za serikali na makampuni binafsi yamekuwa yakifanya miamala mingi ya kifedha kwa njia ya kielektroniki.

 

Licha ya maendeleo hayo, ni bahati mbaya kuwa kwa muda mrefu, nchi yetu imekuwa haina mfumo mahsusi wa kutambua miamala inayofanyika na kukokotoa kodi. Mara nyingi, tumekuwa tukikusanya kodi kwa kukadiria au wakati mwingine imetubidi tupokee kile tunachoambiwa au kuletewa na makampuni husika. Kwa maneno mengine, tulitegemea zaidi uaminifu wa walipa kodi na wakadiria kodi wetu. Lakini sasa tumepata mwarobaini. Mfumo huu utawezesha kuona miamala yote kadri inavyofanyika. Hii itawezesha Serikali kukusanya kodi inayostahili tena kwa wakati. Mualama ukifanyika tu, muda huo Serikali inapata kodi yake. Zaidi ya hapo, Mfumo huu utapunguza kama sio kuondoa kabisa malalamiko ya wafanyabiashara wetu kuhusu kubambikiwa kodi kubwa na wakadiriaji.

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Kamishna Mkuu wa TRA, ameeleza hivi punde kuwa Mfumo huu umepangwa kutekelezwa kwa awamu tatu. Awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa mfumo na kuunganisha Makampuni nane (8) ya Mawasiliano ya simu yaliyopo nchini ambayo ni Vodacom, Tigo, Zantel, TTCL, Halotel, Smart, Smile na Airtel. Awamu ya pili itahusu kuunganisha mfumo huu na mifumo ya taasisi za kifedha na Kibenki. Na awamu ya tatu itahusisha uunganishaji wa mfumo wa e-RCS na mifumo yote ya taasisi na makampuni yanayotoa huduma za malipo kwa njia ya kielektroniki.

 

Ametueleza pia kuwa katika awamu ya kwanza ya utekelezaji, Makampuni matatu (3) ya Halotel, TTCL na Smart tayari yameunganishwa kwenye mfumo; na kampuni ya Smile ipo katika hatua za mwisho kuunganishwa. Nayapongeza makampuni hayo. Aidha, nayahimiza makampuni mengine ya simu kujiunga kwenye mfumo huo ili kuiwezesha Serikali kukusanya kodi yake kama inavyostahili. Nimefurahi leo katika shughuli hii tunao watendaji wakuu wa makampuni karibu yote ya simu, mabenki pamoja na taasisi nyingine. Ni imani yangu kuwa wameusikia na wataufanyia kazi wito wangu wa kujiunga na mfumo huu wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki.

 

Waheshimiwa Viongozi, Mabibi na Mabwana;

Kama nilivyosema hapo awali, Serikali imeamua kutengeneza Mfumo huu kwa ajili ya kuongeza ukusanyaji mapato ili kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo hapa nchini. Baadhi yenu mtakumbuka kuwa, takriban miezi miwili iliyopita, nchi yetu ilipata bahati ya kutembelewa na Waziri Mkuu wa Ethiopia. Katika mazungumzo yetu, alinieleza kuwa nchini mwake kuna Kampuni moja tu la simu, Ethio Telecom, ambalo linamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100. Mwaka jana Shirika hilo lilipata mapato ya takriban Dola za Marekani bilioni 1.5, na mwaka huu linatarajiwa kukusanya takriban Dola bilioni 2. Makusanyo hayo makubwa ndio yamechangia kuiwezesha Serikali ya Ethiopia kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa reli.

 

Sisi pia, hapo zamani, tulikuwa na shirika moja tu la simu la TTCL. Nimeambiwa kuwa mwaka 1992, Shirika hilo lilitoa gawio lake kwa Serikali kiasi cha takriban shilingi bilioni moja. Baadaye, kutokana na dhamira nzuri ya Serikali ya kutaka kuliongezea ufanisi Shirika hili, iliamuliwa libinafsishwe. Jambo la kusikitisha ni kwamba, baada ya kubinafsishwa, shirika hilo likaanza kujiendesha kwa hasara na halikuwahi kutoa gawio kwa Serikali hadi ikailazimu mwaka jana tulichukue tena. Kwa sasa nchi yetu ina mashirika mengi ya simu, lakini kiasi cha kodi tunachopata, bado ni kidogo. Ni kutokana na ukweli huo, tumeamua kutengeneza mfumo huu wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kieletroniki.

 

Hivyo basi, napenda kurudia tena wito wangu kwa makampuni ya simu nchini kujiunga na mfumo huu. Sambamba na hilo, nayakumbusha na kuyahimiza tena Makampuni ya Simu kujisajili kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam, ambako nako nimearifiwa kuwa kuna kusuasua katika kujisajili. Fanyeni hivyo kwa hiari. Lakini mkiendelea kukaidi, hatutasita kuchukua hatua kali.  Na katika hili naviagiza vyombo vyote husika, hususan TCRA, kuchukua hatua kali dhidi ya kampuni ya simu itakayoshindwa kujiunga na mfumo huu wa kodi wa kieletroniki na pia kujisajili kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam; ikiwezekana kampuni hiyo ifungiwe kabisa kuendesha shughuli zake hapa nchini. Nakuomba Mheshimiwa Makamu wa Rais pamoja na Mawaziri husika kusimamia suala hili.

 

Nasisitiza jambo hili sio kwa sababu tunayachukia makampuni ya simu, bali kwa sababu tunataka shughuli za makampuni haya ziwanufaishe pia Watanzania na nchi yetu kwa ujumla. Wengi wenu hapa mnafahamu kuwa nchi yetu imekuwa ikipoteza mapato mengi ya kodi. Sio tu kwenye makampuni haya ya simu bali pia kwenye shughuli za uchimbaji madini pamoja na shughuli nyingine. Mathalan, hivi sasa tumekuwa tukihangaishana na wamachinga katika kulipa kodi. Lakini naamini kama tungeamua kuwarasimisha wamachinga kwa kuwatengenezea vitambulisho ambavyo watavilipia kwa kiasi kidogo cha fedha, Serikali ingepata mapato mengi. Hata kwenye kodi ya majengo ni hivyo hivyo. Kama kodi ingekuwa ndogo, watu wengi wangeimudu na kuilipa kwa hiari na hivyo kuipatia Serikali mapato makubwa.

 

Waheshimiwa Viongozi,

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

         Nimeeleza mengi niliyotaka kueleza.  Hivyo, napenda niishie hapa. Lakini kabla sijahitimisha hotuba yangu, napenda nitumie fursa hii kutoa pongezi zangu nyingi kwa taasisi zote zilizoshiriki katika kubuni na kutengeza Kituo chetu cha Kutunzia Kumbukumbu pamoja na Mfumo wa Ukusanyaji Kodi na Mapato kwa Njia ya Kieletroniki. Nimefarijika sana kusikia kuwa Mfumo huu Ukusanyaji wa Mapato umetengenezwa na sisi Watanzania wenyewe tena kwa gharama nafuu sana. Hili na jambo zuri na huu ni uthibitisho mwingine kuwa sisi Watanzania, tukiamua, tunaweza.  

 

Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kufanya uzinduzi rasmi wa Mfumo wa Ukusanyaji Kodi na Mapato kwa njia ya kielektroniki.

 

Mungu Ibariki Tanzania!

Mugu Wabariki Watanzania!

 

“Ahsanteni Sana kwa Kunisikiliza”