Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Tovuti Rasmi ya Rais

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tovuti Rasmi ya Rais
Ofisi ya Rais - Ikulu

HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE HAFLA YA KUWEKA JIWE LA MSINGI LA MRADI WA KUBORESHA BANDARI YA DAR ES SALAAM DAR ES SALAAM, TAREHE 2 JULAI, 2017

Wednesday 23rd August 2017

Mheshimiwa Prof. Makame Mbarawa, Waziri wa Ujenzi,

Uchukuzi na Mawasiliano;

 

Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Waziri mliopo;

 

Mheshimiwa Balozi John Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi;

 

Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;

 

Mheshimiwa Dkt. Noman Sigala King, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu;

 

Mheshimiwa Hawa Ghasia, Mwenyekiti wa Kamati ya

Kudumu ya Bunge ya Bajeti;

 

Mheshimiwa Sarah Cooke, Balozi wa Uingereza nchini;

 

Mheshimiwa Mama Bella Bird, Mwakilishi wa Benki ya Dunia;

 

Mwakilishi wa Trade Mark East Africa;

 

Waheshimiwa Wabunge mliopo na Mstahiki Meya wa Dar es Salaam;

 

Waheshimiwa Makatibu Wakuu mliopo hapa;

 

Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania;

 

 

Ndugu Mkurugenzi Mkuu na Wafanyakazi wa Mamlaka

ya Bandari Tanzania;

 

Waheshimiwa Wageni wote Waalikwa, Mabibi na Mabwana:

Nianze kwa kuungana na wote walionitangulia kuzungumza katika kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na kutuwezesha kushuhudia tukio hili. Aidha, napenda nitoe shukrani zangu nyingi kwa Mheshimiwa Waziri, Prof. Mbarawa, pamoja na uongozi mzima wa Mamlaka ya Bandari Tanzania kwa kunipa heshima ya kuwa Mgeni Rasmi katika hafla hii ya kuweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Kuboresha Bandari ya Dar es Salaam. Ahsanteni sana.

 

Mbele yangu hapa nawaona wageni. Namwona Mheshimiwa Balozi Cooke wa Uingereza; Mama Bird, Mwakilishi wa Benki ya Dunia nchini; pamoja na wawakilishi wa Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID) na Trade Mark East Africa, ambao kwa pamoja wametoa mchango wao katika kufadhili mradi huu. Tunawashukuru sana kwa ujio wenu lakini pia kwa kutuunga mkono katika kuutekeleza mradi huu muhimu.

 

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

         Tukio hili la uwekaji Jiwe la Msingi la mradi wa kuboresha Bandari ya Dar es Salaam ni muhimu sana kwa maendeleo na ustawi wa nchi yetu. Ni muhimu kwa sababu Bandari ya Dar es Salaam ni lango kuu la biashara na pia ni kitovu cha uchumi sio tu kwa nchi yetu bali pia kwa baadhi ya nchi jirani. Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 90 ya shehena za mizigo inayoingia na kutoka hapa nchini inapita kwenye Bandari hii. Aidha, nchi takriban 6 hupitisha mizigo yao katika Bandari hii. Nchi hizo ni Burundi, DRC, Malawi, Rwanda, Uganda na Zambia.  Lakini kama hiyo haitoshi, hivi majuzi tu tumeanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (standard gauge). Ufanisi na manufaa ya reli hiyo yatategemea sana utendaji kazi mzuri wa Bandari hii.

 

Kwa kuzingatia mambo hayo yote, ni dhahiri kuwa uboreshaji huu ni umuhimu kwa nchi yetu pamoja na nchi nyingine jirani zinazotumia Bandari hii. Uboreshaji huu utaongeza shehena ya mizigo inayopita katika Bandari hii na hivyo kuipatia Serikali yetu mapato mengi kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na pia kuboresha huduma za jamii. Hivyo basi, napenda nitoe pongezi nyingi kwa Wizara pamoja na Mamlaka ya Bandari Tanzania kwa kuanza kutekeleza mradi huu.

 

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Kama mlivyosikia hivi punde, mradi huu utatekelezwa kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza, ambayo leo tunaweka jiwe la msingi, itahusisha uboreshaji wa Gati Na. 1-7 na Gati la kuhudumia magari (Roll-on-Roll off Berth –RORO). Awamu ya pili ya mradi huu, itahusisha kuongeza kina na kupanua lango la kuingilia Bandarini, mzunguko wa kugeuzia meli (Turning Basin), pamoja na kujenga kujenga Gati mpya Na. 12-15.

 

Gharama za utekelezaji wa mradi huu kwa awamu zote mbili ni Dola za Marekani milioni 421, sawa na takriban Shilingi za Tanzania bilioni 926.2. Kati ya fedha hizo, Serikali ya Tanzania itatoa Dola za Marekani 63.4; Benki ya Dunia itatoa Dola za Marekani milioni 345.2; na Serikali ya Uingereza kupitia Shirika lake la Maendeleo (DFID) itatoa Dola za Marekani milioni 12.4. Hivyo basi, napenda kurudia tena kuwashukuru washirika wetu hawa ambao wamekubali kutuunga mkono katika kutekeleza mradi huu muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu.  

 

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Kama mlivyosikia, awamu ya kwanza ya mradi huu, awali, ilipangwa kutekelezwa kwa miezi 36. Lakini baada ya mashauriano yaliyofanyika, Mkandarasi, Kampuni ya China Harbour Construction kutoka China, amekubali kukamilisha mradi huu kwa kipindi cha miezi 28. Hili ni jambo jema sana. Sidhani kama kulikwa na  sababu za msingi za kufanya mradi huu uchukue muda mwingi kiasi hicho kuutekeleza. Kampuni iliyopewa kandarasi ya kuutekeleza ni kubwa; lakini fedha pia zipo. Hivyo, nimefurahi kusikia muda wa kutekeleza mradi huu umepunguzwa.

 

Kukamilika mapema kwa mradi huu kutaiwezesha Bandari ya Dar es Salaam kupokea meli nyingi na kubwa; na hivyo kupunguza ucheleweshaji. Hii pia itasaidia Bandari yetu kushindana na Bandari nyingine katika Ukanda wetu. Kama mnavyofahamu, katika siku za hivi karibuni, zimekuwepo taarifa zakupungua mizigo katika Bandari hii. Moja ya sababu zinazochangia hali hiyo ni kwamba kina cha Bandari yetu ni kidogo. Hii inafanya meli kubwa zishindwe kuja au zilazimike kutumia muda mrefu kusubiri. Bila shaka, nyote hapa mnafahamu, katika dunia ya sasa ya ushidani, hakuna mfanyabiashara aliye tayari kupotezewa muda. Hivyo, mradi huu utakapokamilika, utaondoa tatizo la ucheweleshaji katika Bandari yetu. Kama utatokea, basi labda usababishwe na watendaji wetu, ambao ningependa tu kusema kuwa Serikali kamwe haitawavumilia.

 

Lakini mbali na kuondoa tatizo la ucheleweshaji, mradi huu utakuza biashara na shughuli nyingine za kiuchumi kati yetu na nchi nyingine. Kama nilivyosema awali, Bandari hii inatumiwa na mataifa jirani takriban saba. Na mnafahamu pia kuwa nchi yetu ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ambazo kwa pamoja zina watu wapatao milioni 600.  Hivyo, mradi huu utakapokamilika, utakuza biashara kati yetu sio tu na mataifa yanayotumia Bandari yetu bali pia na nchi zote wanachama wa EAC na SADC. Hii ni kwa sababu, Bandari ni kichocheo muhimu cha kukuza biashara miongoni mwa mataifa.  Takriban asilimia 90 ya shehena ya mizigo duniani husafirishwa kwa usafiri wa majini, ambapo Bandari ni kiungo muhimu.

 

 

 

Ndugu Viongozi mliopo;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Jukumu langu leo ni kuweka Jiwe la Msingi la Awamu ya Kwanza ya Mradi wa Upanuzi na Uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam. Hivyo basi, sitapenda kuwachosha kwa hotuba ndefu sana. Hata hivyo, kabla sijahitimisha hotuba yangu, napenda nizungumze masuala manne ya mwisho.

 

Kwanza kabisa, napenda kuwahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kwa dhati kabisa kuboresha na kuimarisha miundombinu ya usafiri hapa nchini. Mbali na kuboresha Bandari ya Dar es Salaam, tunaboresha na kupanua Bandari zetu za Mtwara na Tanga na halikadhalika kwenye Maziwa Makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa. Tunaendelea pia na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege na barabara. Tunafanya hivyo kwa vile tunatambua kuwa huduma na miundombinu imara ya usafiri na usafirishaji ni muhimu sio tu katika kukuza biashara bali pia katika ukuaji wa sekta nyingine za uchumi, ikiwemo kilimo, viwanda, utalii, ufugaji, uvuvi, n.k.

 

Suala la pili ni kwa ndugu zangu wa Mamlaka ya Bandari na Bodi yake. Nawapongeza kwa hatua mnazochukua katika kuboresha na kuongeza ufanisi wa Bandari yetu. Lakini hamna budi kuzidisha juhudi hasa katika usimamizi wa Bandari Kavu Binafsi (ICDs). Bandari hizi kavu zilianzishwa kwa makusudi ya kusaidia pale mizigo inapozidi hapa Bandarini. Lakini kwa taarifa nilizonazo ni kwamba, siku hizi hata kabla ya mizigo kujaa hapa Bandarini, inapelekwa kwenye Bandari hizo Kavu, ambako kuna dalili za ukwepaji kodi. Nimeambiwa pia kwamba mara nyingi mizigo inayopelekwa huko husemekana kuwa inasafirishwa kwenda nje lakini mingi hushushwa hapa hapa nchini. Nitoe wito kwa Mamlaka ya Bandari, Mamlaka ya Mapato pamoja na vyombo vingine husika kushughulikia suala hili la Bandari Kavu na pia ukwepaji wa kodi unaofanyika kupitia Bandari kavu hizo.

 

Suala la tatu, napenda kuihimiza Mamlaka ya Bandari kuimarisha ulinzi na usalama wa hapa Bandarini, hususan kuhusu mizigo inayoteremshwa. Nimearifiwa kuwa hivi majuzi vimeshushwa vichwa vya treni vipatavyo 15 lakini mpaka sasa havijulikani mmiliki wake.  Shirika la Reli limevikana. Sasa mimi najiuliza inawezekanaje vichwa vya treni viletwe na kushushwa hapa bila kufahamika mmiliki wake. Na kama hilo limewezekana, je haitawezekana pia kwa watu wenye nia mbaya na nchi yetu kuleta vitu vyenye kuhatarisha usalama wetu? Hivyo basi, niwaombe Mamlaka ya Bandari kuimarisha usalama wa Bandari yetu. Na kuhusu tukio hili la vichwa vya treni, niviombe vyombo vya dola kulichunguza ili kuweza kumbaini mmiliki wake.  

 

Suala la nne na la mwisho ni kuhusu wana-siasa wenzangu, ambao wamekuwa wakiibuka kuzungumzia mambo wasiofahamu undani wake. Mathalan, hivi karibuni kuna wanasiasa wamejitokeza kujaribu kuwatetea watu wanaoshikiliwa kwa makosa ya kuhatarisha amani na usalama wa taifa letu. Nawasihi wanasiasa wa namna hiyo kuacha kutafuta sifa na umaarufu usio na tija. Ninyi ndugu zangu hapa nyote ni mashahidi kuwa katika muda mfupi uliopita, nchi yetu imewapoteza askari pamoja na wananchi wasio na hatia zaidi ya 30. Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba wanasiasa hao hawakuwahi kulaani na kukemea mauaji hayo; lakini badala yake wanaibuka kuwatetea watu ambao inaaminika kuwa wanahusika na vitendo hivyo vya mauaji. Hii inatia mashaka kuwa huenda hata wanasiasa hao pia wanahusika, hasa kwa kuzingatia kuwa ukiondoa askari, walengwa wa mauji hayo ni watu kutoka chama kimoja tu. Nitoe wito kwa wanasiasa wenzangu tuchunge ndimi na kauli zetu. Amani ya nchi yetu ni muhimu sana. Tusiichezee. Maendeleo haya tunayoyaona na kuyatamani leo kamwe hayawezi kupatikana kama amani itapotea. Hivyo, tuiache Serikali itekeleze majukumu yake. Kinyume na hapo, hatutawavumilia  wanasiasa wa namna hiyo.  Nilichaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, na hivyo nawajibika kulinda amani na usalama wa nchi yetu kwa nguvu zangu zote. Naviomba vya ulinzi na usalama visiwaogope au kuwaonea aibu wanasiasa wa namna hiyo. Lakini zaidi,  nawaomba  Watanzania wote, bila kujali tofauti zetu za dini, kabila au vyama, kuilinda amani yetu na pia kuweka mbele maslahi ya taifa letu.

 

 

Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi;

Waheshimiwa Viongozi mliopo;

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;

Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote, lakini hasa Wabunge wa Kamati za Miundombinu na Bajeti kwa kuiunga mkono Serikali. Upauzi na uboreshaji wa Bandari hii umezungumzwa kwa muda mrefu, hata hivyo, utekelezaji wake ulikuwa ukikwama kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa fedha. Lakini baada ya Kamati hizi mbili kuupitisha mradi huu pamoja na bajeti yake, sasa tunautekeleza. Nazipongeza sana Kamati hizi mbili kwa uamuzi wenu huo wa kijasiri.

 

Naomba pia mniruhusu kuwashukuru tena washirika wetu katika mradi huu kwa kutuunga mkono. Aidha, nawashukuru Mabalozi wote mliojitokeza kuhudhuria shughuli. Hii inadhihirisha kuwa mnatambua umuhimu wa mradi huu. Tunawashukuru sana na napenda niwaahidi kuwa tutaendelea kushirikiana nanyi kwa karibu.

 

Mwisho lakini sio kwa umuhimu, napenda kuwashukuru tena viongozi wa Wizara pamoja na Mamlaka ya Bandari kwa kunialika kwenye tukio hili. Aidha, nawapongezeni kwa kazi nzuri mnayoifanya. Endeleeni kujituma. Ongezeni mapambano dhidi ya rushwa. Vitendo vya rushwa na wizi viwe mwiko katika Bandari. Zaidi ya hapo zingatieni muda. Msiwacheleweshe wateja wenu. Mkiyafanya hayo, nina imani kuwa Bandari hii itatoa huduma bora na kuchangia maendeleo ya nchi yetu; na hata maslahi ya wafanyakazi wake pia yataboreshwa.

 

Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kutekeleza shughuli iliyonileta ya kuweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Kuboresha Bandari ya Dar es Salaam.

 

Mungu Ibariki Bandari ya Dar es Salaam!

Mungu Zibariki Bandari Zetu Zote!

Mungu Ibariki Tanzania!

 

“Ahsanteni sana kwa kunisikiliza”